Walawi 19:1-8
Walawi 19:1-8 Biblia Habari Njema (BHN)
Mwenyezi-Mungu alimwambia Mose, “Iambie jumuiya yote ya watu wa Israeli hivi: Ni lazima muwe watakatifu kwani mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, ni mtakatifu. Kila mmoja wenu ni lazima amheshimu mama yake na baba yake, na kuzishika Sabato zangu. Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu. Msizigeukie sanamu za miungu, wala msijitengenezee sanamu za kusubu za miungu. Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu. “Mnaponitolea mimi Mwenyezi-Mungu sadaka za amani, mtanitolea kama itakiwavyo ili mpate kukubaliwa. Sadaka hiyo ni lazima iliwe siku hiyohiyo inapotolewa au kesho yake. Chochote kinachobaki hadi siku ya tatu ni lazima kiteketezwe kwa moto. Kama sehemu ya nyama yake italiwa siku ya tatu, tendo hilo ni chukizo; na sadaka hiyo haitakubaliwa, naye atakayekula nyama hiyo ni lazima awajibike kwa uovu wake kwa sababu amekitia unajisi kitu kitakatifu cha Mwenyezi-Mungu. Mtu huyo atatengwa na watu wake.
Walawi 19:1-8 Swahili Revised Union Version (SRUV)
BWANA akanena na Musa, akamwambia, Nena na mkutano wote wa wana wa Israeli, uwaambie, Mtakuwa watakatifu; kwa kuwa mimi BWANA, Mungu wenu, ni mtakatifu. Kila mtu na amche mama yake, na baba yake, nanyi mtazitunza Sabato zangu; mimi ndimi BWANA, Mungu wenu. Msigeuke kufuata sanamu, wala msijitengenezee miungu ya kusubu mimi ndimi BWANA, Mungu wenu. Nanyi hapo mtakapomchinjia BWANA sadaka ya amani mtaitoa kwa njia ipasayo ili mpate kukubaliwa. Italiwa siku iyo hiyo mliyoichinja, na siku ya pili yake; na kama kitu chochote katika sadaka hiyo kilisalia hata siku ya tatu kitachomwa moto. Ikiwa sadaka hiyo inaliwa hata kidogo siku ya tatu ni machukizo; haitakubaliwa; lakini kila mtu atakayekula atalipizwa uovu wake mwenyewe, kwa sababu amekinajisi kitu hicho kitakatifu cha BWANA; na mtu huyo atatengwa na watu wake.
Walawi 19:1-8 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
BWANA akanena na Musa, akamwambia, Nena na mkutano wote wa wana wa Israeli, uwaambie, Mtakuwa watakatifu; kwa kuwa mimi BWANA, Mungu wenu, ni mtakatifu. Kila mtu na amche mama yake, na baba yake, nanyi mtazitunza Sabato zangu; mimi ndimi BWANA, Mungu wenu. Msigeuke kuandama sanamu, wala msijifanyizie miungu ya kusubu mimi ndimi BWANA, Mungu wenu. Nanyi hapo mtakapomchinjia BWANA sadaka ya amani mtaisongeza ili kwamba mpate kukubaliwa. Italiwa siku iyo hiyo mliyoichinja, na siku ya pili yake; na kama kitu cho chote katika sadaka hiyo kilisalia hata siku ya tatu kitachomwa moto. Kwamba sadaka hiyo yaliwa hata kidogo siku ya tatu ni machukizo; haitakubaliwa; lakini kila mtu atakayekula atauchukua uovu wake mwenyewe, kwa sababu amekinajisi kitu hicho kitakatifu cha BWANA; na nafsi hiyo itakatiliwa mbali na watu wake.
Walawi 19:1-8 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
BWANA akamwambia Musa, “Sema na kusanyiko lote la Waisraeli, uwaambie: ‘Kuweni watakatifu, kwa kuwa mimi, BWANA Mungu wenu, ni mtakatifu. “ ‘Kila mmoja wenu ni lazima amheshimu mama yake na baba yake, na pia ni lazima kuzishika Sabato zangu. Mimi ndimi BWANA Mungu wenu. “ ‘Msiabudu sanamu, wala msijitengenezee miungu ya kusubu. Mimi ndimi BWANA Mungu wenu. “ ‘Mnapotoa dhabihu ya sadaka ya amani kwa BWANA, toeni kwa namna ambayo itakubaliwa kwa niaba yenu. Sadaka hiyo italiwa siku hiyo hiyo mnayoitoa, au kesho yake; chochote kitakachobaki hadi siku ya tatu lazima kiteketezwe kwa moto. Kama sehemu yoyote ya sadaka hiyo italiwa siku ya tatu, itakuwa si safi, nayo haitakubaliwa. Yeyote atakayekula atawajibishwa, kwa sababu amenajisi kitu kilicho kitakatifu kwa BWANA; mtu huyo lazima akatiliwe mbali na watu wake.