Walawi 19:1-18
Walawi 19:1-18 Biblia Habari Njema (BHN)
Mwenyezi-Mungu alimwambia Mose, “Iambie jumuiya yote ya watu wa Israeli hivi: Ni lazima muwe watakatifu kwani mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, ni mtakatifu. Kila mmoja wenu ni lazima amheshimu mama yake na baba yake, na kuzishika Sabato zangu. Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu. Msizigeukie sanamu za miungu, wala msijitengenezee sanamu za kusubu za miungu. Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu. “Mnaponitolea mimi Mwenyezi-Mungu sadaka za amani, mtanitolea kama itakiwavyo ili mpate kukubaliwa. Sadaka hiyo ni lazima iliwe siku hiyohiyo inapotolewa au kesho yake. Chochote kinachobaki hadi siku ya tatu ni lazima kiteketezwe kwa moto. Kama sehemu ya nyama yake italiwa siku ya tatu, tendo hilo ni chukizo; na sadaka hiyo haitakubaliwa, naye atakayekula nyama hiyo ni lazima awajibike kwa uovu wake kwa sababu amekitia unajisi kitu kitakatifu cha Mwenyezi-Mungu. Mtu huyo atatengwa na watu wake. “Utakapovuna mavuno ya nchi yako, usivune kabisa hadi mpakani mwa shamba wala usirudi nyuma kukusanya mabaki. Msirudie kukusanya kila kitu katika shamba la mizabibu, wala usiokote zabibu zilizoanguka chini; utawaachia maskini na wageni. Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu. “Msiibe, msidanganye wala kuambiana uongo. Msiape uongo kwa jina langu hata kulikufuru jina la Mungu wenu. Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu. “Usimdhulumu jirani yako wala kumwibia. Mshahara wa mtu aliyeajiriwa usikae kwako usiku kucha hadi asubuhi. Usimlaani kiziwi wala kuweka kizuizi mbele ya kipofu, bali umche Mungu wako. Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu. “Unapotoa hukumu uamue kwa haki; usimpendelee maskini wala kumwogopa mwenye cheo. Bali ni lazima kumwamua jirani kwa haki. Kamwe usipitepite ukiwachongea watu wa jamaa yako. Usiyatie maisha ya jirani yako katika hatari ya kifo kwa maneno yako. Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu. “Usimwekee kisasi ndugu yako moyoni mwako, bali upatane daima na jirani yako ili usije ukatenda dhambi. Usijilipize kisasi au kuwa na kinyongo dhidi ya wazawa wa watu wako bali umpende jirani yako kama unavyojipenda wewe mwenyewe. Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu.
Walawi 19:1-18 Swahili Revised Union Version (SRUV)
BWANA akanena na Musa, akamwambia, Nena na mkutano wote wa wana wa Israeli, uwaambie, Mtakuwa watakatifu; kwa kuwa mimi BWANA, Mungu wenu, ni mtakatifu. Kila mtu na amche mama yake, na baba yake, nanyi mtazitunza Sabato zangu; mimi ndimi BWANA, Mungu wenu. Msigeuke kufuata sanamu, wala msijitengenezee miungu ya kusubu mimi ndimi BWANA, Mungu wenu. Nanyi hapo mtakapomchinjia BWANA sadaka ya amani mtaitoa kwa njia ipasayo ili mpate kukubaliwa. Italiwa siku iyo hiyo mliyoichinja, na siku ya pili yake; na kama kitu chochote katika sadaka hiyo kilisalia hata siku ya tatu kitachomwa moto. Ikiwa sadaka hiyo inaliwa hata kidogo siku ya tatu ni machukizo; haitakubaliwa; lakini kila mtu atakayekula atalipizwa uovu wake mwenyewe, kwa sababu amekinajisi kitu hicho kitakatifu cha BWANA; na mtu huyo atatengwa na watu wake. Na mtakapovuna mavuno ya nchi yenu, usivune kabisa katika pembe za shamba lako, wala usiyakusanye masazo ya mavuno yako; wala usiyakusanye masazo ya mizabibu yako, wala usiyaokote matunda ya mizabibu yako yaliyopukutika; uyaache kwa ajili ya maskini na mgeni; mimi ndimi BWANA, Mungu wenu. Msiibe, wala msidanganye, wala msiambiane uongo. Msiape uongo kwa jina langu, na ukalinajisi jina la Mungu wako; Mimi ndimi BWANA. Usimdhulumu jirani yako, wala kumnyang'anya mali yake; ujira wake aliyeajiriwa usikae kwako usiku kucha hadi asubuhi. Usimlaani kiziwi, wala usitie kwazo mbele ya kipofu, bali umche Mungu wako; Mimi ndimi BWANA. Msitende yasiyo haki katika hukumu, usimpendelee mtu maskini, wala kumstahi mwenye nguvu; bali utamhukumu jirani yako kwa haki. Usiende huku na huko katikati ya watu wako, kama mchongezi; wala usijifaidi kwa damu ya jirani yako; mimi ndimi BWANA. Usimchukie ndugu yako moyoni mwako; ni lazima kumkemea jirani yako, au ulipizwe uovu kwa ajili yake Usifanye kisasi, wala kuwa na kinyongo juu ya wana wa watu wako; bali umpende jirani yako kama nafsi yako; Mimi ndimi BWANA.
Walawi 19:1-18 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
BWANA akanena na Musa, akamwambia, Nena na mkutano wote wa wana wa Israeli, uwaambie, Mtakuwa watakatifu; kwa kuwa mimi BWANA, Mungu wenu, ni mtakatifu. Kila mtu na amche mama yake, na baba yake, nanyi mtazitunza Sabato zangu; mimi ndimi BWANA, Mungu wenu. Msigeuke kuandama sanamu, wala msijifanyizie miungu ya kusubu mimi ndimi BWANA, Mungu wenu. Nanyi hapo mtakapomchinjia BWANA sadaka ya amani mtaisongeza ili kwamba mpate kukubaliwa. Italiwa siku iyo hiyo mliyoichinja, na siku ya pili yake; na kama kitu cho chote katika sadaka hiyo kilisalia hata siku ya tatu kitachomwa moto. Kwamba sadaka hiyo yaliwa hata kidogo siku ya tatu ni machukizo; haitakubaliwa; lakini kila mtu atakayekula atauchukua uovu wake mwenyewe, kwa sababu amekinajisi kitu hicho kitakatifu cha BWANA; na nafsi hiyo itakatiliwa mbali na watu wake. Na mtakapovuna mavuno ya nchi yenu, usivune kabisa kabisa pembe za shamba lako, wala usiyakusanye masazo ya mavuno yako; wala usiyakusanye masazo ya mizabibu yako, wala usiyaokote matunda ya mizabibu yako yaliyopukutika; uyaache kwa ajili ya maskini na mgeni; mimi ndimi BWANA, Mungu wenu. Msiibe, wala msidanganye, wala msiambiane uongo. Msiape uongo kwa jina langu, hata ukalinajisi jina la Mungu wako; Mimi ndimi BWANA. Usimdhulumu jirani yako, wala kumnyang’anya mali yake; ijara yake aliyeajiriwa isikae kwako usiku kucha hata asubuhi. Usimlaani kiziwi, wala usitie kwazo mbele ya kipofu, bali umche Mungu wako; Mimi ndimi BWANA. Msitende yasiyo haki katika hukumu, usimpendelee mtu maskini, wala kumstahi mwenye nguvu; bali utamhukumu jirani yako kwa haki. Usiende huko na huko katikati ya watu wako, kama mchongezi; wala usisimame kinyume cha damu ya jirani yako; mimi ndimi BWANA. Usimchukie ndugu yako moyoni mwako; ni lazima kumkemea jirani yako, wala usichukue dhambi kwa ajili yake. Usifanye kisasi, wala kuwa na kinyongo juu ya wana wa watu wako; bali umpende jirani yako kama nafsi yako; Mimi ndimi BWANA.
Walawi 19:1-18 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
BWANA akamwambia Musa, “Sema na kusanyiko lote la Waisraeli, uwaambie: ‘Kuweni watakatifu, kwa kuwa mimi, BWANA Mungu wenu, ni mtakatifu. “ ‘Kila mmoja wenu ni lazima amheshimu mama yake na baba yake, na pia ni lazima kuzishika Sabato zangu. Mimi ndimi BWANA Mungu wenu. “ ‘Msiabudu sanamu, wala msijitengenezee miungu ya kusubu. Mimi ndimi BWANA Mungu wenu. “ ‘Mnapotoa dhabihu ya sadaka ya amani kwa BWANA, toeni kwa namna ambayo itakubaliwa kwa niaba yenu. Sadaka hiyo italiwa siku hiyo hiyo mnayoitoa, au kesho yake; chochote kitakachobaki hadi siku ya tatu lazima kiteketezwe kwa moto. Kama sehemu yoyote ya sadaka hiyo italiwa siku ya tatu, itakuwa si safi, nayo haitakubaliwa. Yeyote atakayekula atawajibishwa, kwa sababu amenajisi kitu kilicho kitakatifu kwa BWANA; mtu huyo lazima akatiliwe mbali na watu wake. “ ‘Unapovuna mavuno ya nchi yako, usivune hadi kwenye mipaka ya shamba lako, wala usikusanye mabaki ya mavuno yako. Usirudi mara ya pili katika shamba lako la mizabibu, wala usiokote zabibu zilizoanguka chini. Ziache kwa ajili ya maskini na mgeni. Mimi ndimi BWANA Mungu wako. “ ‘Usiibe. “ ‘Usiseme uongo. “ ‘Msidanganyane. “ ‘Usiape kwa uongo kwa Jina langu, na hivyo kulinajisi jina la Mungu wako. Mimi ndimi BWANA. “ ‘Usimdhulumu wala kumwibia jirani yako. “ ‘Usishikilie mshahara wa kibarua usiku kucha hadi asubuhi. “ ‘Usimlaani kiziwi, wala usiweke kikwazo mbele ya kipofu, lakini umche Mungu wako. Mimi ndimi BWANA. “ ‘Usipotoshe haki; usioneshe kumpendelea maskini, wala upendeleo kwa mwenye cheo, bali mwamulie jirani yako kwa haki. “ ‘Usieneze uchochezi miongoni mwa watu wako. “ ‘Usifanye kitu chochote kile kinachohatarisha maisha ya jirani yako. Mimi ndimi BWANA. “ ‘Usimchukie ndugu yako moyoni mwako. Karipia jirani yako kwa uwazi ili usishiriki hatia yake. “ ‘Usijilipizie kisasi wala kuwa na kinyongo dhidi ya mmoja wa jamaa yako, lakini mpende jirani yako kama unavyojipenda mwenyewe. Mimi ndimi BWANA.