Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Walawi 16:1-19

Walawi 16:1-19 Biblia Habari Njema (BHN)

Mwenyezi-Mungu alizungumza na Mose, baada ya wana wawili wa Aroni kufa wakati ule walipomkaribia. Alimwambia, “Mwambie ndugu yako Aroni asiingie mahali patakatifu nyuma ya pazia wakati usiokubaliwa. Asiingie mahali hapo kwani ndipo nitakapotokea katika wingu juu ya kiti cha rehema. Asipotii, atakufa. Aroni ataingia mahali patakatifu sana akiwa na fahali mchanga kwa ajili ya sadaka ya kuondoa dhambi na kondoo dume kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa. Ataoga mwili wote katika maji, kisha atavaa mavazi matakatifu. Ataingia mahali hapo akiwa amevaa mavazi matakatifu: Joho la kitani baada ya nguo ya ndani ya suruali ya kitani na akiwa amevaa kanzu ya kitani na kujifunga mkanda wa kitani. Atatwaa kutoka jumuiya ya watu wa Israeli beberu wawili kwa ajili ya sadaka ya kuondoa dhambi na kondoo dume mmoja kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa. “Aroni atamtoa huyo fahali sadaka ya kuondoa dhambi kwa ajili yake mwenyewe, na kufanya ibada ya upatanisho kwa ajili yake mwenyewe na jamaa yake. Kisha, wale beberu wawili atawaweka kwenye mlango wa hema la mkutano. Atawapigia kura hao beberu wawili, kura moja kwa ajili ya Mwenyezi-Mungu na nyingine kwa ajili ya Azazeli. Atamleta yule beberu ambaye kura ilimtaka kwa ajili ya Mwenyezi-Mungu na kumtolea sadaka ya kuondoa dhambi. Lakini yule beberu aliyetakiwa na kura kwa ajili ya Azazeli atatolewa mbele ya Mwenyezi-Mungu akiwa hai ili kufanya ibada ya upatanisho kuhani atamwacha aende jangwani kwa Azazeli, ili kuondoa dhambi za jumuiya. “Aroni atamtoa fahali wa sadaka ya kuondoa dhambi kwa ajili yake mwenyewe, na kufanya ibada ya upatanisho kwa ajili yake mwenyewe na kwa ajili ya jamaa yake, kisha atamchinja fahali huyo sadaka ya kuondoa dhambi. Halafu atachukua chetezo na kutwaa makaa madhabahuni mbele ya Mwenyezi-Mungu na ubani konzi mbili uliosagwa vizuri sana. Ili asije akafa, atauleta ubani huo mbele ya Mwenyezi-Mungu na kuutia katika moto ili moshi wa ubani huo ukifunike kifuniko cha sanduku la agano. Atachukua kiasi cha damu ya yule fahali na kunyunyiza kwa kidole chake upande wa mashariki juu ya kiti cha rehema kisha atainyunyizia mbele ya sanduku la agano mara saba kwa kidole chake. “Halafu atamchinja yule beberu wa sadaka ya kuondoa dhambi kwa ajili ya watu wote. Damu ya mbuzi huyo ataileta ndani mahali patakatifu sana na kufanya kama alivyofanya na damu ya yule fahali; atainyunyiza juu ya kiti cha rehema, upande wake wa mbele. Hivyo atafanya ibada ya upatanisho kwa ajili ya mahali patakatifu kwa sababu ya unajisi, makosa na dhambi zote za Waisraeli. Ndivyo atakavyofanya pia kwa ajili ya hema la mkutano lililo miongoni mwa watu hao walio najisi. Wakati Aroni anafanya ibada ya upatanisho kwa ajili yake mwenyewe, jamaa yake na jamii nzima ya Israeli, kamwe asiwepo mtu yeyote ndani ya hema la mkutano hadi atakapokuwa amemaliza na kutoka nje. Kisha atatoka na kwenda kwenye madhabahu iliyo mbele ya Mwenyezi-Mungu na kuifanyia ibada ya upatanisho. Atachukua kiasi cha damu ya yule fahali na ya yule mbuzi na kuzipaka pembe za madhabahu pande zote. Atainyunyizia madhabahu hiyo damu kwa kidole chake mara saba na hivyo kuiweka wakfu na kuitakasa unajisi wote wa watu wa Israeli.

Shirikisha
Soma Walawi 16

Walawi 16:1-19 Swahili Revised Union Version (SRUV)

BWANA akasema na Musa, baada ya kufa kwa hao wana wawili wa Haruni, walipokaribia mbele za BWANA, wakafa; BWANA akamwambia Musa, Mwambie Haruni ndugu yako, kwamba asiingie wakati wowote katika mahali patakatifu ndani ya pazia, mbele ya kiti cha rehema, kilicho juu ya sanduku, asije akafa; maana, mimi nitaonekana katika lile wingu juu ya kiti cha rehema. Haruni ataingia katika patakatifu na vitu hivi; ng'ombe dume mchanga kwa sadaka ya dhambi, na kondoo dume kwa sadaka ya kuteketezwa. Ataivaa ile kanzu takatifu ya kitani, atakuwa na zile suruali za kitani mwilini mwake, atafungwa ule mshipi wa kitani, naye atavaa ile kofia ya kitani; hayo ndiyo mavazi matakatifu, naye ataoga mwili wake majini, na kuyavaa. Kisha atatwaa mikononi mwa mkutano wa Waisraeli mbuzi wawili wa kiume, kwa sadaka ya dhambi; na kondoo dume kwa sadaka ya kuteketezwa. Na Haruni atamtoa yule ng'ombe wa sadaka ya dhambi, aliye kwa ajili ya nafsi yake, na kufanya upatanisho kwa ajili ya nafsi yake mwenyewe, na kwa ajili ya nyumba yake. Kisha atawatwaa wale mbuzi wawili na kuwaweka mbele za BWANA mlangoni pa hema ya kukutania. Na Haruni atapiga kura juu ya wale mbuzi wawili; kura moja kwa ajili ya BWANA; na kura ya pili kwa ajili ya Azazeli. Na Haruni atamleta yule mbuzi aliyeangukiwa na kura kwa ajili ya BWANA, na kumtoa awe sadaka ya dhambi. Bali yule mbuzi aliyeangukiwa na kura kwa ajili ya Azazeli atawekwa hai mbele za BWANA ili kumfanyia upatanisho, ili kumpeleka jangwani kwa ajili ya Azazeli. Na Haruni atamsongeza ng'ombe wa sadaka ya dhambi, aliye kwa ajili ya nafsi yake, na kufanya upatanisho kwa ajili ya nafsi yake mwenyewe, na kwa ajili ya nyumba yake; naye atamchinja yule ng'ombe wa sadaka ya dhambi, aliye kwa ajili ya nafsi yake. Kisha atatwaa chetezo kilichojaa makaa ya moto yatokayo katika madhabahu iliyo mbele za BWANA, na konzi mbili za uvumba mzuri uliopondwa sana, mikononi mwake, naye atauleta ndani ya pazia. Kisha atatia ule uvumba juu ya moto mbele za BWANA, ili moshi wa ule uvumba ukisitiri kiti cha rehema kilicho juu ya ushuhuda, asije akafa. Kisha atatwaa baadhi ya damu ya yule ng'ombe, na kuinyunyiza kwa kidole chake juu ya kiti cha rehema upande wa mashariki; na mbele ya kiti cha rehema atainyunyiza ile damu kwa kidole chake mara saba. Kisha atamchinja yule mbuzi wa sadaka ya dhambi, aliye kwa ajili ya watu, na kuileta damu yake ndani ya pazia, na kwa damu hiyo atafanya kama alivyofanya kwa damu ya ng'ombe, na kuinyunyiza juu ya kiti cha rehema, na mbele ya kiti cha rehema, naye atafanya upatanisho kwa ajili ya mahali patakatifu, kwa sababu ya mambo machafu ya wana wa Israeli, na kwa sababu ya makosa yao, kwa ajili ya dhambi zao zote; naye atafanya vile vile kwa ajili ya hema ya kukutania, ikaayo pamoja nao katikati ya machafu yao. Wala hapatakuwa na mtu katika hema ya kukutania, wakati aingiapo ili kufanya upatanisho katika patakatifu, hata atakapotoka nje, baada ya kufanya upatanisho kwa ajili ya nafsi yake mwenyewe, na kwa ajili ya nyumba yake, na kwa ajili ya mkutano wote wa Israeli. Kisha atatoka na kwenda katika madhabahu iliyo mbele za BWANA na kufanya upatanisho kwa ajili yake; atatwaa baadhi ya damu ya yule ng'ombe, na ya yule mbuzi, na kuitia juu ya pembe za madhabahu pande zote. Tena atanyunyiza baadhi ya damu juu ya madhabahu kwa kidole chake mara saba, na kuitakasa, ili machafu yote ya wana wa Israeli yaitoke.

Shirikisha
Soma Walawi 16

Walawi 16:1-19 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

BWANA akasema na Musa, baada ya kufa kwa hao wana wawili wa Haruni, walipokaribia mbele za BWANA, wakafa; BWANA akamwambia Musa, Sema na Haruni ndugu yako, kwamba asiingie wakati wo wote katika mahali patakatifu ndani ya pazia, mbele ya kiti cha rehema, kilicho juu ya sanduku, asije akafa; maana, mimi nitaonekana katika lile wingu juu ya kiti cha rehema. Haruni ataingia katika patakatifu na vitu hivi; ng’ombe mume mchanga kwa sadaka ya dhambi, na kondoo mume kwa sadaka ya kuteketezwa. Ataivaa ile kanzu takatifu ya kitani, atakuwa na zile suruali za kitani mwilini mwake, atafungwa ule mshipi wa kitani, naye atavaa ile kofia ya kitani; hayo ndiyo mavazi matakatifu, naye ataoga mwili wake majini, na kuyavaa. Kisha atatwaa mikononi mwa mkutano wa Waisraeli mbuzi waume wawili, kwa sadaka ya dhambi; na kondoo mume kwa sadaka ya kuteketezwa. Na Haruni atamtoa yule ng’ombe wa sadaka ya dhambi, aliye kwa ajili ya nafsi yake, na kufanya upatanisho kwa ajili ya nafsi yake mwenyewe, na kwa ajili ya nyumba yake. Kisha atawatwaa wale mbuzi wawili na kuwaweka mbele za BWANA mlangoni pa hema ya kukutania. Na Haruni atapiga kura juu ya wale mbuzi wawili; kura moja kwa ajili ya BWANA; na kura ya pili kwa ajili ya Azazeli. Na Haruni atamleta yule mbuzi aliyeangukiwa na kura kwa ajili ya BWANA, na kumtoa awe sadaka ya dhambi. Bali yule mbuzi aliyeangukiwa na kura kwa ajili ya Azazeli atawekwa hai mbele za BWANA ili kumfanyia upatanisho, ili kumpeleka jangwani kwa ajili ya Azazeli. Na Haruni atamsongeza ng’ombe wa sadaka ya dhambi, aliye kwa ajili ya nafsi yake, na kufanya upatanisho kwa ajili ya nafsi yake mwenyewe, na kwa ajili ya nyumba yake; naye atamchinja yule ng’ombe wa sadaka ya dhambi, aliye kwa ajili ya nafsi yake. Kisha atatwaa chetezo kilichojaa makaa ya moto yatokayo katika madhabahu iliyo mbele za BWANA, na konzi mbili za uvumba mzuri uliopondwa sana, mikononi mwake, naye atauleta ndani ya pazia. Kisha atatia ule uvumba juu ya moto mbele za BWANA, ili moshi wa ule uvumba ukisitiri kiti cha rehema kilicho juu ya ushuhuda, asije akafa. Kisha atatwaa baadhi ya damu ya yule ng’ombe, na kuinyunyiza kwa kidole chake juu ya kiti cha rehema upande wa mashariki; na mbele ya kiti cha rehema atainyunyiza ile damu kwa kidole chake mara saba. Kisha atamchinja yule mbuzi wa sadaka ya dhambi, aliye kwa ajili ya watu, na kuileta damu yake ndani ya pazia, na kwa damu hiyo atafanya vile vile kama alivyofanya kwa damu ya ng’ombe, na kuinyunyiza juu ya kiti cha rehema, na mbele ya kiti cha rehema, naye atafanya upatanisho kwa ajili ya mahali patakatifu, kwa sababu ya mambo machafu ya wana wa Israeli, na kwa sababu ya makosa yao, naam, kwa ajili ya dhambi zao zote; naye atafanya vile vile kwa ajili ya hema ya kukutania, ikaayo pamoja nao katikati ya machafu yao. Wala hapatakuwa na mtu katika hema ya kukutania, wakati aingiapo ili kufanya upatanisho katika patakatifu, hata atakapotoka nje, baada ya kufanya upatanisho kwa ajili ya nafsi yake mwenyewe, na kwa ajili ya nyumba yake, na kwa ajili ya mkutano wote wa Israeli. Kisha atatoka na kuiendea madhabahu iliyo mbele za BWANA na kufanya upatanisho kwa ajili yake; atatwaa baadhi ya damu ya yule ng’ombe, na ya damu ya yule mbuzi, na kuitia juu ya pembe za madhabahu pande zote. Tena atanyunyiza baadhi ya damu juu ya madhabahu kwa kidole chake mara saba, na kuitakasa, ili machafu yote ya wana wa Israeli yaitoke.

Shirikisha
Soma Walawi 16

Walawi 16:1-19 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)

BWANA akasema na Musa baada ya kifo cha wale wana wawili wa Haruni waliokufa walipokaribia mbele za BWANA. BWANA akamwambia Musa: “Mwambie ndugu yako Haruni asije wakati wowote anaotaka ndani ya Patakatifu pa Patakatifu, nyuma ya pazia pale mbele ya kiti cha rehema kile kilicho juu ya Sanduku la Agano, la sivyo atakufa, kwa sababu huwa ninatokea ndani ya wingu juu ya kile kiti cha rehema. “Hivi ndivyo Haruni atakavyoingia katika mahali patakatifu: atachukua fahali mchanga kwa ajili ya sadaka ya dhambi, na kondoo dume kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa. Atavaa koti takatifu la kitani, pamoja na nguo za ndani za kitani; atafunga mshipi wa kitani kiunoni, na kuvaa kilemba cha kitani. Haya ni mavazi matakatifu, kwa hiyo ni lazima aoge kwa maji kabla ya kuyavaa mavazi hayo. Atachukua beberu wawili kutoka kwa jumuiya ya Israeli kwa ajili ya sadaka ya dhambi, na kondoo dume kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa. “Haruni atamtoa huyo fahali kwa ajili ya sadaka yake ya dhambi ili afanye upatanisho kwa ajili yake mwenyewe na nyumba yake. Kisha atawachukua wale beberu wawili na kuwaleta mbele za BWANA kwenye ingilio la Hema la Kukutania. Haruni atapiga kura kwa ajili ya hao mbuzi wawili, mmoja kwa ajili ya BWANA na mwingine kwa ajili ya kubebeshwa dhambi za Israeli. Haruni atamleta yule mbuzi ambaye kura ya BWANA imemwangukia na kumtoa dhabihu kwa ajili ya sadaka ya dhambi. Lakini mbuzi aliyechaguliwa kwa kura kuwa wa kubebeshwa dhambi atatolewa akiwa hai mbele za BWANA, atumike kwa kufanya upatanisho kwa kumwacha aende jangwani akiwa amebebeshwa dhambi. “Haruni atamleta yule fahali kwa ajili ya sadaka ya dhambi yake mwenyewe, ili kufanya upatanisho kwa ajili yake na nyumba yake, naye atamchinja huyo fahali kwa ajili ya sadaka ya dhambi yake mwenyewe. Atachukua chetezo kilichojaa makaa yanayowaka kutoka madhabahuni mbele za BWANA, na konzi mbili za uvumba laini uliosagwa vizuri wenye harufu, na kuvipeleka nyuma ya pazia. Ataweka uvumba juu ya moto mbele za BWANA, na moshi wa uvumba utafunika kile kiti cha rehema kilicho juu ya Ushuhuda, ili asife. Atachukua sehemu ya damu ya fahali, na kwa kidole chake atanyunyiza sehemu ya mbele ya kiti cha rehema; kisha atanyunyiza sehemu ya hiyo damu kwa kidole chake mara saba mbele ya kiti cha rehema. “Kisha atamchinja mbuzi wa sadaka ya dhambi kwa ajili ya watu, na kuichukua damu yake nyuma ya pazia, na aifanyie kama alivyofanya kwa damu ya fahali: Atanyunyiza juu ya kiti cha rehema na mbele yake. Kwa njia hii atafanya upatanisho kwa ajili ya Patakatifu pa Patakatifu kwa sababu ya unajisi na uasi wa Waisraeli, kwa dhambi zao zozote. Atafanya hivyo kwa ajili ya Hema la Kukutania, ambalo liko miongoni mwao katikati ya unajisi wao. Mtu yeyote haruhusiwi kuwa ndani ya Hema la Kukutania, kuanzia wakati Haruni anapoingia kufanya upatanisho katika Patakatifu pa Patakatifu, hadi atakapotoka nje, baada ya kujifanyia upatanisho yeye mwenyewe na nyumba yake, pamoja na jumuiya yote ya Israeli. “Kisha atatoka aje kwenye madhabahu yaliyo mbele za BWANA na kufanya upatanisho kwa ajili yake. Atachukua sehemu ya damu ya fahali na sehemu ya damu ya mbuzi, na kuiweka kwenye pembe za madhabahu. Atanyunyiza sehemu ya hiyo damu juu ya madhabahu kwa kidole chake mara saba, ili kuitakasa na kuiweka wakfu kutokana na unajisi wa Waisraeli.

Shirikisha
Soma Walawi 16