Walawi 14:1-57
Walawi 14:1-57 Biblia Habari Njema (BHN)
Mwenyezi-Mungu alimwambia Mose, “Ifuatayo ni sheria kumhusu mwenye ukoma katika siku ya kutakaswa kwake. Baada ya kupona ataletwa kwa kuhani. Kuhani atakwenda kumwangalia huyo mtu nje ya kambi. Ikiwa ukoma huo umepona, basi, kuhani ataamuru watu walete ndege wawili safi walio hai, kipande cha mwerezi, sufu ya rangi nyekundu na tawi la husopo kwa ajili ya huyo mtu atakayetakaswa. Kuhani atawaamuru wamchinje ndege mmoja katika chungu chenye maji safi ya chemchemi. Kuhani atamchukua yule ndege mwingine hai, kipande kile cha mwerezi, sufu ya rangi nyekundu na lile tawi la husopo na kuvitumbukiza vyote katika damu ya yule ndege aliyechinjwa. Kisha, atamnyunyizia huyo mwenye kutakaswa ile damu mara saba, halafu atamtangaza mtu huyo kuwa safi. Yule ndege hai atamwacha aende zake mashambani nje ya mji. Huyo mtu atayafua mavazi yake, atanyoa nywele zake, na kuoga; naye atakuwa safi. Baada ya hayo atarudi kambini, lakini atakaa nje ya hema lake kwa muda wa siku saba. Siku ya saba atanyoa nywele zake zote, ndevu na kope za macho yake. Kisha atafua mavazi yake na kuoga, ataoga kwa maji; naye atakuwa safi. “Siku ya nane ataleta wanakondoo madume wawili wasio na dosari, kondoo jike wa mwaka mmoja asiye na dosari, kilo tatu za unga laini uliochanganywa na mafuta kwa ajili ya sadaka ya nafaka pamoja na mafuta theluthi moja ya lita. Kuhani atakayemtakasa mtu huyo atamleta mbele ya Mwenyezi-Mungu karibu na mlango wa hema la mkutano pamoja na vitu alivyoleta. Kuhani atachukua mwanakondoo dume mmoja na kumtolea sadaka ya kuondoa hatia pamoja na yale mafuta theluthi moja ya lita. Atafanya ishara ya kuvitolea mbele ya Mwenyezi-Mungu. Kisha atamchinja huyo mwanakondoo katika mahali patakatifu, wanapochinjia wanyama wa sadaka ya kuondoa dhambi na sadaka ya kuteketezwa. Sadaka hii ya kuondoa hatia, kama ilivyo sadaka ya kuondoa dhambi, ni mali yake kuhani; ni sadaka takatifu kabisa. Kuhani atachukua kiasi cha damu ya sadaka ya kuondoa hatia na kumpaka mtu anayetakaswa katika ncha ya sikio lake la kulia na kidole gumba cha mkono wake wa kulia na kidole gumba cha mguu wake wa kulia. Kisha, kuhani atachukua kiasi cha ile theluthi moja ya mafuta na kuyatia katika kiganja cha mkono wake wa kushoto. Atachovya kidole cha mkono wake wa kulia katika mafuta hayo na kumnyunyizia huyo mtu anayetakaswa mara saba mbele ya Mwenyezi-Mungu. Kiasi cha mafuta yanayobaki katika kiganja chake atampaka huyo mtu anayetakaswa katika ncha ya sikio lake la kulia na kidole gumba cha mkono wake wa kulia na kidole gumba cha mguu wake wa kulia, mahali palepale alipompaka damu ya sadaka ya kuondoa hatia. Yale mafuta yaliyobaki atampaka huyo mtu kichwani. Hivyo kuhani atamfanyia ibada ya upatanisho mbele ya Mwenyezi-Mungu. Kuhani atatolea sadaka ya kuondoa dhambi na kumfanyia huyo mtu anayetakaswa ibada ya upatanisho ili kumwondolea unajisi wake. Kisha atamchinja mwanakondoo wa sadaka ya kuteketezwa. Kuhani atatolea ile sadaka ya kuteketezwa na sadaka ya nafaka juu ya madhabahu. Hivyo kuhani atamfanyia huyo mtu ibada ya upatanisho, naye atakuwa safi. “Lakini ikiwa mtu huyo ni maskini, hana uwezo wa kutoa vitu hivyo, basi ataleta mwanakondoo dume mmoja kuwa fidia ya sadaka ya kuondoa hatia ambaye atafanyiwa ishara ya kutoa sadaka ili kumfanyia huyo mtu ibada ya upatanisho. Ataleta pia kilo moja ya unga laini uliochanganywa na mafuta kwa ajili ya sadaka ya nafaka na mafuta theluthi moja ya lita. Ataleta pia hua wawili au makinda mawili ya njiwa kadiri anavyoweza mmoja atakuwa kwa ajili ya sadaka ya kuondoa dhambi na mwingine kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa. Siku ya nane atamletea kuhani vitu hivyo mbele ya mlango wa hema la mkutano kwa ajili ya utakaso wake mbele ya Mwenyezi-Mungu. Kuhani atamchukua huyo mwanakondoo dume wa sadaka ya kuondoa hatia pamoja na yale mafuta theluthi moja ya lita na kufanya ishara ya kuvitolea mbele ya Mwenyezi-Mungu. Atamchinja huyo mwanakondoo dume wa sadaka ya kuondoa hatia. Kuhani atachukua kiasi cha damu na kumpaka huyo mtu anayetakaswa katika ncha ya sikio lake la kulia, katika kidole gumba cha mkono wake wa kulia na kidole gumba cha mguu wake wa kulia. Kuhani atatia kiasi cha mafuta hayo katika kiganja cha mkono wake wa kushoto. Kisha atamnyunyizia huyo mtu kwa kidole chake cha kulia kiasi cha hayo mafuta yaliyomo katika kiganja chake cha kushoto mara saba mbele ya Mwenyezi-Mungu. Kuhani atampaka huyo mtu anayetakaswa mafuta katika ncha ya sikio lake la kulia, katika kidole gumba cha mkono wake wa kulia, na kidole gumba cha mguu wake wa kulia. Atampaka mahali pale ambapo alimpaka ile damu ya sadaka ya kuondoa hatia. Mafuta yanayosalia mkononi mwake atampaka huyo mtu kichwani, ili kumfanyia ibada ya upatanisho mbele ya Mwenyezi-Mungu. Kisha kuhani atamchukua mmoja wa wale hua au njiwa wawili kadiri mtu huyo anavyoweza kuleta. Hua atakuwa kwa ajili ya sadaka ya kuondoa dhambi na mwingine kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa. Pamoja na hao, atatoa sadaka ya nafaka; naye kuhani atamfanyia huyo mtu ibada ya upatanisho mbele ya Mwenyezi-Mungu. Huo ndio mwongozo kuhusu mtu mwenye ukoma asiyeweza kutoa sadaka za kumtakasa.” Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose na Aroni, “Mtakapoingia katika nchi ya Kanaani ambayo ninawapa kuwa milki yenu, nami nikafanya namna ya upele wa ukoma uote katika ukuta wa nyumba fulani katika nchi mtakayoimiliki, basi, mwenye nyumba hiyo ni lazima amwambie kuhani kwamba namna ya upele wa ukoma umeonekana katika nyumba yake. Kuhani ataamuru vitu vyote ndani ya nyumba hiyo vitolewe kabla yeye mwenyewe hajaanza uchunguzi wake; visije vyote kutangazwa kuwa najisi. Kisha kuhani ataingia kuiangalia nyumba hiyo. Atauchunguza upele huo; kama upele huo umeonekana ukutani na umesababisha madoa ya rangi ya kijani kibichi au nyekundu na kuonekana kuwa yamepenya ndani ya kuta, basi, kuhani atatoka nje mlangoni na kuifunga nyumba hiyo kwa muda wa siku saba. Siku ya saba kuhani atarudi na kuiangalia tena nyumba hiyo. Ikiwa upele huo umeenea katika kuta za nyumba hiyo, kuhani ataamuru mawe yaliyoko kwenye sehemu zenye upele yatolewe na kutupwa mahali najisi nje ya mji. Lipu ya nyumba hiyo itabanduliwa na kifusi chake kutupwa mahali najisi nje ya mji. Kisha watachukua mawe mapya na kujenga mahali walipobomoa; nao wataipiga nyumba hiyo lipu upya. “Ikiwa upele huo utatokea tena baada ya kutoa mawe hayo na kukwangua lipu na kuipiga lipu upya, yapasa kuhani aje kuichunguza. Ikiwa upele umeenea katika nyumba hiyo, basi huo ni upele wa kufisha; nyumba hiyo ni najisi. Nyumba hiyo ni lazima ibomolewe na mawe yake, miti yake na lipu vipelekwe mahali najisi nje ya mji. Zaidi ya hayo, yeyote atakayeingia ndani ya nyumba hiyo wakati itakapokuwa imefungwa, atakuwa najisi mpaka jioni. Yeyote anayelala katika nyumba hiyo au kulia chakula ndani yake, lazima ayafue mavazi yake. “Lakini ikiwa baada ya kuikagua nyumba hiyo, kuhani ataona kuwa upele haujaenea baada ya kupigwa lipu, basi, kuhani atatangaza kuwa nyumba hiyo ni safi kwani upele umekwisha. Ili kuitakasa nyumba hiyo, mwenye nyumba ataleta ndege wawili pamoja na kipande cha mwerezi, sufu nyekundu na tawi la husopo. Atamchinja ndege mmoja katika chungu chenye maji safi ya chemchemi. Atachukua kipande cha mwerezi, tawi la husopo na ile sufu nyekundu pamoja na yule ndege mwingine aliye hai na kuvitumbukiza vyote katika damu ya yule ndege aliyechinjwa. Kisha atainyunyizia nyumba hiyo damu mara saba. Hivyo ndivyo atakavyoitakasa nyumba hiyo kwa damu ya ndege, maji safi ya chemchemi, ndege hai, kipande cha mwerezi, tawi la husopo na ile sufu nyekundu. Yule ndege hai atamwacha aende zake mashambani nje ya mji. Hivyo ndivyo atakavyoitakasa nyumba hiyo, nayo itakuwa safi.” Hii ndiyo sheria kuhusu aina yoyote ya namna ya upele wa ukoma; upele katika nguo au nyumba, uvimbe, jipu au kipaku, ili kuonesha ni kitu gani kilicho najisi na kisicho najisi. Hiyo ndiyo sheria kuhusu namna ya upele wa ukoma.
Walawi 14:1-57 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Kisha BWANA akanena na Musa, na kumwambia, Hii ndiyo sheria ya mwenye ukoma, katika siku ya kutakaswa kwake; ataletwa kwa kuhani, na huyo kuhani atatoka aende nje ya kambi; na kuhani ataangalia, ikiwa pigo la ukoma limepoa kwake huyo mwenye ukoma; ndipo huyo kuhani ataagiza kwamba watwae kwa ajili yake atakayetakaswa ndege wawili walio hai, ambao ni safi, na mti wa mwerezi, na sufu nyekundu, na hisopo; kisha kuhani ataagiza ndege mmoja achinjwe katika chombo cha udongo kilicho juu ya maji ya mtoni; kisha huyo ndege aliye hai atamshika, na huo mti wa mwerezi, na hiyo sufu nyekundu, na hisopo, naye atavichovya, pamoja na yule ndege aliye hai, katika damu ya huyo ndege aliyechinjwa juu ya maji ya mtoni; kisha atamnyunyizia huyo atakayetakaswa na ukoma mara saba, naye atasema kwamba ni safi, kisha atamwacha yule ndege aliye hai aende zake nyikani. Naye huyo atakayetakaswa atazifua nguo zake, na kunyoa nywele zake zote, na kuoga katika maji, naye atakuwa safi; baada ya hayo ataingia ndani ya kambi, lakini ataketi nje ya hema yake muda wa siku saba. Kisha siku ya saba atanyoa nywele zote za kichwani mwake, na ndevu zake, na nyusi zake, nywele zake zote pia atazinyoa; kisha atazifua nguo zake, na kuoga mwili wake majini, naye atakuwa safi. Kisha siku ya nane atachukua wana-kondoo wawili wa kiume wasio na dosari, na mwana-kondoo mmoja wa kike wa mwaka wa kwanza asiye na dosari, na sehemu tatu za kumi za efa moja ya unga mwembamba kuwa sadaka ya unga, kuchanganywa na mafuta, na logi moja ya mafuta. Kisha kuhani atakayemtakasa atamsimamisha huyo mtu atakayetakaswa, pamoja na vitu vile vyote, mbele za BWANA, mlangoni pa hema ya kukutania; kisha kuhani atamshika mmoja kati ya hao wana-kondoo wa kiume, na kumsongeza awe sadaka ya hatia, pamoja na hiyo logi ya mafuta, kisha atavitikisa kuwa ni sadaka ya kutikiswa mbele za BWANA; kisha atamchinja huyo mwana-kondoo mahali hapo wachinjiapo sadaka ya dhambi na sadaka ya kuteketezwa, ndani ya mahali patakatifu; kwa kuwa kama hiyo sadaka ya dhambi ilivyo ya kuhani, ndivyo ilivyo sadaka ya hatia; ni takatifu sana; kisha huyo kuhani atatwaa baadhi ya hiyo damu ya sadaka ya hatia, naye kuhani ataitia katika ncha ya sikio la kulia la huyo atakayetakaswa, na katika kidole cha gumba cha mkono wake wa kulia, na katika kidole kikuu cha mguu wake wa kulia; kisha kuhani atatwaa katika hiyo logi ya mafuta, na kuyamimina katika kitanga cha mkono wake mwenyewe wa kushoto; kisha kuhani atatia kidole cha mkono wa kulia katika hayo mafuta, yaliyo katika mkono wake wa kushoto, naye atayanyunyiza hayo mafuta kwa kidole chake mara saba mbele za BWANA; na katika yale mafuta yaliyobaki mkononi mwake kuhani atayatia katika ncha ya sikio la kulia la huyo atakayetakaswa, na katika kidole cha gumba cha mkono wake wa kulia, na katika kidole kikuu cha mguu wake wa kulia, juu ya damu ya sadaka ya hatia; na mafuta yaliyobaki, yaliyo katika mkono wa kuhani, atayatia juu ya kichwa cha huyo atakayetakaswa; na kuhani atafanya upatanisho kwa ajili yake, mbele za BWANA. Kisha kuhani atasongeza sadaka ya dhambi, na kufanya upatanisho kwa ajili yake huyo atakayetakaswa kwa sababu ya unajisi wake; kisha baadaye ataichinja sadaka ya kuteketezwa; kisha kuhani ataisongeza hiyo sadaka ya kuteketezwa, na sadaka ya unga, juu ya madhabahu na kuhani atafanya upatanisho kwa ajili yake, naye atakuwa safi. Lakini akiwa ni maskini, naye hawezi kupata kiasi hicho, ndipo atatwaa mwana-kondoo mmoja wa kiume, awe sadaka ya hatia ya kutikiswa, ili kufanya upatanisho kwa ajili yake, na sehemu ya kumi ya efa ya unga mwembamba, uliochanganywa na mafuta kuwa sadaka ya unga, na logi ya mafuta; na hua wawili, au makinda mawili ya njiwa, kama awezavyo kuwapata; huyo mmoja atakuwa sadaka ya dhambi, na wa pili atakuwa sadaka ya kuteketezwa. Hata siku ya nane atawaleta kwa kuhani, mlangoni pa hema ya kukutania mbele za BWANA, kwa ajili ya kutakaswa kwake. Na kuhani atamtwaa huyo mwana-kondoo wa sadaka ya hatia, na hiyo logi ya mafuta, naye kuhani atavitikisa viwe sadaka ya kutikiswa mbele za BWANA; kisha atamchinja mwana-kondoo wa sadaka ya hatia, na kuhani atatwaa katika damu ya sadaka ya hatia, na kuitia katika ncha ya sikio la kulia la huyo atakayetakaswa, na katika kidole cha gumba cha mkono wake wa kulia, na katika kidole kikuu cha mguu wake wa kulia; kisha kuhani atajimiminia baadhi ya mafuta hayo katika kitanga cha mkono wake wa kushoto; kisha kuhani atanyunyiza baadhi ya hayo mafuta yaliyo katika mkono wake wa kushoto, kwa kidole chake cha mkono wa kulia mara saba mbele za BWANA; kisha kuhani atatia mengine katika hayo mafuta yaliyo mkononi mwake katika ncha ya sikio la kulia la huyo atakayetakaswa, na katika kidole cha gumba cha mkono wake wa kulia, na katika kidole kikuu cha mguu wake wa kulia, juu ya mahali pale penye damu ya sadaka ya hatia; na mafuta yaliyobaki katika mkono wa kuhani atayatia juu ya kichwa cha huyo atakayetakaswa, ili kufanya upatanisho kwa ajili yake mbele za BWANA. Kisha atasongeza hao hua mmojawapo, au hao makinda ya njiwa mmojawapo, kadiri ya awezao kuwapata; hata kadiri aliyoweza, mmoja kuwa sadaka ya dhambi, na wa pili kuwa sadaka ya kuteketezwa, pamoja na sadaka ya unga; na huyo kuhani atafanya upatanisho kwa ajili yake huyo atakayetakaswa mbele za BWANA. Huyo ambaye ndani yake mna pigo la ukoma, ambaye hawezi kukipata hicho kipasacho kutakaswa kwake, sheria yake ni hiyo. BWANA akanena na Musa na Haruni, na kuwaambia, Hapo mtakapoingia nchi ya Kanaani, ambayo nawapa kuwa ni milki yenu, nami nitakapolitia pigo la ukoma katika nyumba ya nchi hiyo ya milki yenu; ndipo mwenye nyumba hiyo atakwenda na kumwambia kuhani, akisema, Naona mimi ya kwamba pana kama pigo katika nyumba yangu; ndipo kuhani ataagiza kwamba watoe vyote vilivyomo nyumbani, kabla kuhani hajaingia ndani kuliangalia hilo pigo, ili vyote vilivyomo nyumbani visiwe najisi, kisha baadaye kuhani ataingia ndani ya nyumba hiyo aikague; naye ataliangalia hilo pigo, na tazama, likiwa pigo limo ndani ya kuta za nyumba, nalo lina mashimo-mashimo, rangi ya majani, au mekundu, na kuonekana kuingia ndani kuliko huo ukuta; ndipo kuhani atatoka katika nyumba hiyo mpaka mlangoni pa nyumba, na kuifunga hiyo nyumba muda wa siku saba; siku ya saba kuhani atakwenda tena, naye ataangalia; na tazama, likiwa pigo limeenea katika kuta za nyumba; ndipo kuhani atawaambia wayatoe hayo mawe, yaliyo na pigo, na kuyatupa mahali penye uchafu nje ya mji; naye atafanya kwamba hiyo nyumba ikwanguliwe ndani pande zote, na chokaa watakayokwangua wataimwaga nje ya mji mahali palipo na uchafu; kisha watatwaa mawe mengine, na kuyatia mahali pa mawe hayo; naye atatwaa chokaa nyingine, na kuipaka chokaa hiyo nyumba. Na kama hilo pigo likirudi tena, na kutokea ndani ya nyumba, baada ya yeye kuyatoa hayo mawe, na baada ya kuikwangua nyumba, na baada ya kupakwa chokaa, ndipo kuhani ataingia ndani na kuangalia, likiwa pigo limeenea ndani ya hiyo nyumba, ni ukoma unaodhuru hiyo nyumba; ni unajisi. Naye ataibomoa nyumba, mawe yake, na miti yake, na chokaa yote ya hiyo nyumba; naye atavichukua vyote nje ya mji hadi mahali palipo na uchafu. Tena mtu atakayeingia ndani ya hiyo nyumba wakati huo wote iliofungwa, atakuwa najisi hadi jioni. Na mtu alalaye ndani ya nyumba hiyo atazifua nguo zake, naye alaye chakula ndani ya nyumba hiyo atazifua nguo zake. Kisha kuhani akiingia ndani kukagua na kuona kuwa pigo halikuenea katika hiyo nyumba baada ya nyumba kupakwa chokaa; ndipo kuhani atatangaza kuwa nyumba hiyo ni safi, maana pigo limepoa. Naye atatwaa ndege wawili, na mti wa mwerezi, na sufu nyekundu, na hisopo, kwa kuitakasa hiyo nyumba; naye atamchinja mmojawapo wa ndege hao katika chombo cha udongo kilicho juu ya maji ya mtoni; kisha atatwaa huo mti wa mwerezi, na hisopo, na sufu nyekundu, pamoja na huyo ndege aliye hai, na kuvichovya vyote katika damu ya huyo ndege aliyechinjwa, na katika hayo maji ya mtoni, na kuinyunyizia nyumba mara saba; naye ataitakasa hiyo nyumba kwa damu ya ndege, na kwa maji ya mtoni, na kwa huyo ndege aliye hai, na kwa mti wa mwerezi, na kwa hisopo, na kwa sufu nyekundu; lakini ndege aliye hai atamwacha atoke mle mjini aende nyikani; ndivyo atakavyofanya upatanisho kwa ajili ya hiyo nyumba; nayo itakuwa safi. Hiyo ndiyo sheria ya pigo la ukoma ya kila aina, na ya kipwepwe; na ya ukoma wa vazi, na ukoma wa nyumba; na kivimbe, na kikoko na kipaku king'aacho; ili kufunza itakapokuwa ni unajisi, na itakapokuwa ni safi; hiyo ndiyo sheria ya ukoma.
Walawi 14:1-57 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Kisha BWANA akanena na Musa, na kumwambia, Hii ndiyo sheria ya mwenye ukoma, katika siku ya kutakaswa kwake; ataletwa kwa kuhani, na huyo kuhani atatoka aende nje ya marago; na kuhani ataangalia, na tazama, ikiwa pigo la ukoma limepoa kwake huyo mwenye ukoma; ndipo huyo kuhani ataagiza kwamba watwae kwa ajili yake atakayetakaswa ndege wawili walio hai, ambao ni safi, na mti wa mwerezi, na sufu nyekundu, na hisopo; kisha kuhani ataagiza ndege mmoja achinjwe katika chombo cha udongo kilicho juu ya maji ya mtoni; kisha huyo ndege aliye hai atamshika, na huo mti wa mwerezi, na hiyo sufu nyekundu, na hisopo, naye atavichovya hivyo, pamoja na yule ndege aliye hai, katika damu ya huyo ndege aliyechinjwa juu ya maji ya mtoni; kisha atamnyunyizia huyo atakayetakaswa na ukoma mara saba, naye atasema kwamba yu safi, kisha atamwacha yule ndege aliye hai aende zake nyikani. Naye huyo atakayetakaswa atazifua nguo zake, na kunyoa nywele zake zote, na kuoga katika maji, naye atakuwa safi; baada ya hayo ataingia ndani ya marago, lakini ataketi nje ya hema yake muda wa siku saba. Kisha siku ya saba atanyoa nywele zote za kichwani mwake, na ndevu zake, na nyushi zake, nywele zake zote pia atazinyoa; kisha atazifua nguo zake, na kuoga mwili wake majini, naye atakuwa safi. Kisha siku ya nane atachukua wana-kondoo wawili waume wakamilifu, na mwana-kondoo mmoja wa kike wa mwaka wa kwanza mkamilifu, na sehemu tatu za kumi za efa moja ya unga mwembamba kuwa sadaka ya unga, kuchanganywa na mafuta, na logi moja ya mafuta. Kisha kuhani atakayemtakasa atamsimamisha huyo mtu atakayetakaswa, pamoja na vitu vile vyote, mbele za BWANA, mlangoni pa hema ya kukutania; kisha kuhani atamshika mmoja katika hao wana-kondoo waume, na kumsongeza awe sadaka ya hatia, pamoja na hiyo logi ya mafuta, kisha atavitikisa kuwa ni sadaka ya kutikiswa mbele za BWANA; kisha atamchinja huyo mwana-kondoo mahali hapo wachinjapo sadaka ya dhambi na sadaka ya kuteketezwa, ndani ya mahali patakatifu; kwa kuwa kama hiyo sadaka ya dhambi ilivyo ya kuhani, ni vivyo sadaka ya hatia; ni takatifu sana; kisha huyo kuhani atatwaa katika hiyo damu ya sadaka ya hatia, naye kuhani ataitia katika ncha ya sikio la kuume la huyo atakayetakaswa, na katika chanda cha gumba cha mkono wake wa kuume, na katika kidole kikuu cha mguu wake wa kuume; kisha kuhani atatwaa katika hiyo logi ya mafuta, na kuyamimina katika kitanga cha mkono wake mwenyewe wa kushoto; kisha kuhani atatia kidole cha mkono wa kuume katika hayo mafuta, yaliyo katika mkono wake wa kushoto, naye atayanyunyiza hayo mafuta kwa kidole chake mara saba mbele za BWANA; na katika yale mafuta yaliyobaki mkononi mwake kuhani atayatia katika ncha ya sikio la kuume la huyo atakayetakaswa, na katika chanda cha gumba cha mkono wake wa kuume, na katika kidole kikuu cha mguu wake wa kuume, juu ya damu ya sadaka ya hatia; na mafuta yaliyobaki, yaliyo katika mkono wa kuhani, atayatia juu ya kichwa cha huyo atakayetakaswa; na kuhani atafanya upatanisho kwa ajili yake, mbele za BWANA. Kisha kuhani atasongeza sadaka ya dhambi, na kufanya upatanisho kwa ajili yake huyo atakayetakaswa kwa sababu ya unajisi wake; kisha baadaye ataichinja sadaka ya kuteketezwa; kisha kuhani ataisongeza hiyo sadaka ya kuteketezwa, na sadaka ya unga, juu ya madhabahu na kuhani atafanya upatanisho kwa ajili yake, naye atakuwa safi. Tena kwamba ni maskini, naye hawezi kupata kiasi hicho, ndipo atatwaa mwana-kondoo mmoja wa kiume, awe sadaka ya hatia ya kutikiswa, ili kufanya upatanisho kwa ajili yake, na sehemu ya kumi ya efa ya unga mwembamba, uliochanganywa na mafuta kuwa sadaka ya unga, na logi ya mafuta; na hua wawili, au makinda mawili ya njiwa, kama awezavyo kuwapata; huyo mmoja atakuwa sadaka ya dhambi, na wa pili atakuwa sadaka ya kuteketezwa. Hata siku ya nane atawaleta kwa kuhani, mlangoni pa hema ya kukutania mbele za BWANA, kwa ajili ya kutakaswa kwake. Na kuhani atamtwaa huyo mwana-kondoo wa sadaka ya hatia, na hiyo logi ya mafuta, naye kuhani atavitikisa viwe sadaka ya kutikiswa mbele za BWANA; kisha atamchinja mwana-kondoo wa sadaka ya hatia, na kuhani atatwaa katika damu ya sadaka ya hatia, na kuitia katika ncha ya sikio la kuume la huyo atakayetakaswa, na katika chanda cha gumba cha mkono wake wa kuume, na katika kidole kikuu cha mguu wake wa kuume; kisha kuhani atamimina sehemu ya hayo mafuta katika kitanga cha mkono wake mwenyewe wa kushoto; kisha kuhani atanyunyiza baadhi ya hayo mafuta yaliyo katika mkono wake wa kushoto, kwa kidole chake cha mkono wa kuume mara saba mbele za BWANA; kisha kuhani atatia mengine katika hayo mafuta yaliyo mkononi mwake katika ncha ya sikio la kuume la huyo atakayetakaswa, na katika chanda cha gumba cha mkono wake wa kuume, na katika kidole kikuu cha mguu wake wa kuume, juu ya mahali pale penye damu ya sadaka ya hatia; na mafuta yaliyobaki katika mkono wa kuhani atayatia juu ya kichwa cha huyo atakayetakaswa, ili kufanya upatanisho kwa ajili yake mbele za BWANA. Kisha atasongeza hao hua mmojawapo, au hao makinda ya njiwa mmojawapo, kadiri ya awezao kuwapata; hata kadiri aliyoweza, mmoja kuwa sadaka ya dhambi, na wa pili kuwa sadaka ya kuteketezwa, pamoja na sadaka ya unga; na huyo kuhani atafanya upatanisho kwa ajili yake huyo atakayetakaswa mbele za BWANA. Huyo ambaye ndani yake mna pigo la ukoma, ambaye hawezi kukipata hicho kipasacho kutakaswa kwake, sheria yake ni hiyo. BWANA akanena na Musa na Haruni, na kuwaambia, Hapo mtakapoingia nchi ya Kanaani, ambayo nawapa kuwa ni milki yenu, nami nitakapolitia pigo la ukoma katika nyumba ya nchi hiyo ya milki yenu; ndipo mwenye nyumba hiyo atakwenda na kumwambia kuhani, akisema, Naona mimi ya kwamba pana kama pigo katika nyumba yangu; ndipo kuhani ataagiza kwamba watoe vyote vilivyomo nyumbani, mbele ya kuhani hajaingia ndani kuliangalia hilo pigo, ili kwamba vyote vilivyomo nyumbani visiwekwe kuwa unajisi; kisha baadaye kuhani ataingia ndani ya nyumba hiyo aitazame; naye ataliangalia hilo pigo, na tazama, likiwa pigo limo ndani ya kuta za nyumba, nalo lina mashimo-mashimo, rangi ya majani, au mekundu, na kuonekana kuingia ndani kuliko huo ukuta; ndipo kuhani atatoka katika nyumba hiyo mpaka mlangoni pa nyumba, na kuifunga hiyo nyumba muda wa siku saba; siku ya saba kuhani atakwenda tena, naye ataangalia; na tazama, likiwa pigo limeenea katika kuta za nyumba; ndipo kuhani atawaambia wayatoe hayo mawe, yaliyo na pigo, na kuyatupa mahali penye uchafu nje ya mji; naye atafanya kwamba hiyo nyumba ikwanguwe ndani pande zote, na chokaa watakayokwangua wataimwaga nje ya mji mahali palipo na uchafu; kisha watatwaa mawe mengine, na kuyatia mahali pa mawe hayo; naye atatwaa chokaa nyingine, na kuipaka chokaa hiyo nyumba. Na kama hilo pigo likirudi tena, na kutokea ndani ya nyumba, baada ya yeye kuyatoa hayo mawe, na baada ya kuikwangua nyumba, na baada ya kupakwa chokaa, ndipo kuhani ataingia ndani na kuangalia, na tazama, likiwa pigo limeenea ndani ya hiyo nyumba, ni ukoma unaokula hiyo nyumba; ni katika unajisi. Naye ataibomoa nyumba, mawe yake, na miti yake, na chokaa yote ya hiyo nyumba; naye atavichukua vyote nje ya mji hata mahali palipo na uchafu. Tena mtu atakayeingia ndani ya hiyo nyumba wakati huo wote iliofungwa, atakuwa najisi hata jioni. Na mtu alalaye ndani ya nyumba hiyo atazifua nguo zake, naye alaye chakula ndani ya nyumba hiyo atazifua nguo zake. Tena kwamba kuhani akiingia ndani na kuangalia, na tazama, ikiwa pigo halikuenea katika hiyo nyumba, baada ya nyumba kupakwa chokaa; ndipo kuhani atasema kwamba hiyo nyumba i safi, maana, pigo limepoa. Naye atatwaa ndege wawili, na mti wa mwerezi, na sufu nyekundu, na hisopo, kwa kuitakasa hiyo nyumba; naye atamchinja mmojawapo wa ndege hao katika chombo cha udongo kilicho juu ya maji ya mtoni; kisha atatwaa huo mti wa mwerezi, na hisopo, na sufu nyekundu, pamoja na huyo ndege aliye hai, na kuvichovya vyote katika damu ya huyo ndege aliyechinjwa, na katika hayo maji ya mtoni, na kuinyunyiza nyumba mara saba; naye ataitakasa hiyo nyumba kwa damu ya ndege, na kwa maji ya mtoni, na kwa huyo ndege aliye hai, na kwa mti wa mwerezi, na kwa hisopo, na kwa sufu nyekundu; lakini ndege aliye hai atamwacha atoke mle mjini aende nyikani; ndivyo atakavyofanya upatanisho kwa ajili ya hiyo nyumba; nayo itakuwa safi. Hiyo ndiyo sheria ya pigo la ukoma ya kila aina, na ya kipwepwe; na ya ukoma wa vazi, na ukoma wa nyumba; na kivimbe, na kikoko na kipaku king’aacho; ili kufunza itakapokuwa ni unajisi, na itakapokuwa ni safi; hiyo ndiyo sheria ya ukoma.
Walawi 14:1-57 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
BWANA akamwambia Musa, “Haya ndio masharti yanayomhusu mtu mgonjwa wakati wa ibada yake ya utakaso, anapoletwa kwa kuhani: Kuhani ataenda kumchunguza nje ya kambi. Kama mtu huyo atakuwa amepona ugonjwa wake wa ngozi wa kuambukiza, kuhani ataagiza vitu vifuatavyo viletwe kwa ajili ya mtu atakayetakaswa: ndege wawili safi walio hai, mti wa mwerezi, kitani nyekundu, na hisopo. Kisha kuhani ataagiza kwamba mmoja wa ndege wale achinjwe kwenye chungu chenye maji safi. Kisha kuhani atamchukua ndege aliye hai na kumtumbukiza pamoja na mti wa mwerezi, kitani nyekundu na hisopo ndani ya damu ya yule ndege aliyechinjiwa kwenye maji safi. Atamnyunyizia yule mwenye ugonjwa wa kuambukiza maji hayo mara saba, na kumtangaza kuwa safi. Kisha atamwachia yule ndege aliye hai aende zake kwenye mashamba. “Huyo mtu atakayetakaswa ni lazima afue nguo zake, anyoe nywele zake zote, na aoge kwa maji; ndipo atakapotakasika. Baada ya hili anaweza kuingia kambini, lakini ni lazima akae nje ya hema lake kwa siku saba. Siku ya saba ni lazima anyoe nywele zake zote; yaani anyoe nywele za kichwa, ndevu zake, kope zake na nywele nyingine zote. Ni lazima afue nguo zake, na aoge kwa maji, naye atakuwa safi. “Siku ya nane, ni lazima alete kondoo dume wawili na kondoo jike mmoja, wote wa mwaka mmoja na wasio na dosari, pamoja na sehemu tatu za kumi ya efa ya unga laini uliochanganywa na mafuta, kwa ajili ya sadaka ya nafaka, na logi moja ya mafuta. Kuhani anayemtangaza kuwa safi atamkabidhi mtu huyo atakayetakaswa pamoja na sadaka zake zote mbele za BWANA katika ingilio la Hema la Kukutania. “Kisha kuhani atamchukua mmoja wa wale kondoo dume na kumtoa kuwa sadaka ya hatia, pamoja na ile logi moja ya mafuta; ataviinua mbele za BWANA kuwa sadaka ya kuinuliwa. Atamchinja huyo kondoo katika mahali patakatifu ambapo sadaka ya dhambi na ile ya kuteketezwa huchinjiwa. Kama ilivyo sadaka ya dhambi, sadaka ya hatia ni ya kuhani; ni takatifu sana. Kuhani atachukua sehemu ya damu ya sadaka ya hatia na kuitia kwenye ncha ya sikio la kuume la yule atakayetakaswa, kwenye kidole gumba cha mkono wake wa kuume, na kidole kikubwa cha mguu wake wa kuume. Kisha kuhani atachukua sehemu ya ile logi ya mafuta, ayamimine kwenye kiganja cha mkono wake mwenyewe wa kushoto, na achovye kidole chake cha shahada cha mkono wake wa kuume kwenye mafuta yaliyo kwenye kiganja chake, na kwa kidole hicho anyunyize mafuta hayo mara saba mbele za BWANA. Kuhani atampaka yule anayetakaswa sehemu ya mafuta yaliyobaki kiganjani kwenye ncha ya sikio lake la kuume, kwenye kidole gumba cha mkono wake wa kuume, na kidole kikubwa cha mguu wake wa kuume, mahali palepale alipompaka damu ya sadaka ya kuondoa hatia. Kuhani atayapaka mafuta yaliyobaki kwenye kiganja chake juu ya kichwa cha yule anayetakaswa, na kufanya upatanisho kwa ajili yake mbele za BWANA. “Kisha kuhani atatoa dhabihu ya sadaka ya dhambi na kufanya upatanisho kwa ajili ya yule atakayetakaswa kutoka unajisi wake. Baada ya hayo, kuhani atachinja sadaka ya kuteketezwa na kuitoa juu ya madhabahu, pamoja na sadaka ya nafaka ili kumfanyia upatanisho, naye atakuwa safi. “Hata hivyo, kama ni maskini na hawezi kupata vitu hivi, lazima achukue mwana-kondoo wa kiume mmoja kuwa sadaka ya hatia ipate kuinuliwa ili kumfanyia upatanisho, pamoja na sehemu ya kumi ya efa ya unga laini uliochanganywa na mafuta kwa ajili ya sadaka ya nafaka, logi moja ya mafuta, na hua wawili au makinda wawili wa njiwa, kile atakachoweza kupata, mmoja kwa sadaka ya dhambi, na mwingine kwa sadaka ya kuteketezwa. “Katika siku ya nane, lazima avilete vitu hivyo kwa kuhani, kwa ajili ya kutakaswa kwake kwenye ingilio la Hema la Kukutania mbele za BWANA. Kuhani atamchukua mwana-kondoo kwa ajili ya sadaka ya hatia, pamoja na ile logi ya mafuta ya kuinuliwa mbele za BWANA kuwa sadaka ya kuinuliwa. Atamchinja huyo mwana-kondoo kwa ajili ya sadaka ya hatia. Kisha ataichukua sehemu ya damu yake na kuipaka kwenye ncha ya sikio la kuume la yule anayetakaswa, na aipake pia kwenye kidole gumba cha mkono wa kuume wa huyo mtu, na kidole kikubwa cha mguu wake wa kuume. Kuhani atamiminia sehemu ya mafuta kwenye kiganja chake cha mkono wa kushoto, na kwa kidole chake cha shahada cha mkono wa kuume, atamnyunyizia yule anayetakaswa yale mafuta yaliyo kwenye kiganja chake mara saba mbele za BWANA. Atampaka mafuta yaliyobaki kwenye kiganja chake katika sehemu zote, kama alivyompaka damu ya sadaka ya hatia: yaani kwenye ncha ya sikio la kuume la yule anayetakaswa, kwenye kidole gumba cha mkono wake wa kuume, na kidole kikubwa cha mguu wake wa kuume. Kuhani atayapaka mafuta yaliyobaki katika kiganja chake kwenye kichwa cha yule anayetakaswa, na kufanya upatanisho kwa ajili yake mbele za BWANA. Kisha atatoa dhabihu wale hua ama makinda wa njiwa ambao yule mtu ataweza kuwapata, mmoja kwa ajili ya sadaka ya dhambi, na mwingine kuwa sadaka ya kuteketezwa, pamoja na sadaka ya nafaka. Kwa njia hii kuhani atafanya upatanisho mbele za BWANA kwa ajili ya yule anayetakaswa.” Haya ndio masharti kwa mtu yeyote mwenye ugonjwa wa ngozi wa kuambukiza, na ambaye hana uwezo wa kutoa sadaka za kawaida kwa ajili ya kutakaswa kwake. BWANA akawaambia Musa na Haruni, “Mtakapoingia katika nchi ya Kanaani ninayowapa kuwa milki yenu, nami nikaweka ukoma unaoenea kwenye nyumba katika nchi ile, ni lazima mwenye nyumba hiyo akamwambie kuhani, ‘Nimeona kitu fulani kinachofanana na ukoma kwenye nyumba yangu.’ Kuhani ataagiza vitu vyote vitolewe ndani ya nyumba, kabla hajaenda kuchunguza kama ina ukoma huo, ili kitu chochote ndani ya nyumba kisitangazwe kuwa najisi. Baada ya hili, kuhani ataingia ndani na kuikagua hiyo nyumba. Atachunguza ukoma huo katika kuta za nyumba hiyo, nazo kama zina rangi ya kijani kibichi au wekundu, na kuna mibonyeo ndani ya ukuta, kuhani atatoka na kufunga mlango wa nyumba hiyo kwa siku saba. Siku ya saba, kuhani atarudi kuikagua nyumba. Kama ukoma umeenea juu ya kuta, ataagiza kwamba mawe yote yaliyoambukizwa yaondolewe na kutupwa katika eneo lililo najisi nje ya mji. Kuta zote za ndani ya nyumba hiyo ni lazima zikwanguliwe, na kifusi chake kitupwe mahali najisi nje ya mji. Kisha watachukua mawe mengine na kujenga palipobomolewa kwa udongo mpya wa mfinyanzi, na wapake nyumba hiyo chokaa. “Ikiwa ukoma huo utatokea tena ndani ya ile nyumba baada ya mawe kuondolewa, na nyumba kukwanguliwa na kupakwa chokaa, kuhani ataenda kuikagua, na kama ukoma umeenea ndani ya nyumba, basi ni ukoma unaoharibu; nyumba hiyo ni najisi. Ni lazima ibomolewe: mawe yake, mbao na chokaa yote; vyote vikatupwe nje ya mji mahali palipo najisi. “Yeyote atakayeingia katika nyumba hiyo ikiwa imefungwa, atakuwa najisi hadi jioni. Yeyote atakayelala au kula ndani ya nyumba hiyo ni lazima afue nguo zake. “Lakini ikiwa kuhani atakuja kuikagua na kukuta kuwa ukoma haujaenea tena baada ya nyumba kupakwa chokaa, ataitangaza nyumba ile kuwa safi, kwa sababu ukoma umekwisha. Ili kuitakasa nyumba hiyo, mwenye nyumba ataleta ndege wawili, mti wa mwerezi, kitani nyekundu na hisopo. Atamchinja mmoja wa wale ndege kwenye chungu chenye maji safi. Kisha atachukua mti wa mwerezi, hisopo, kitani nyekundu na ndege aliye hai, na kuvitumbukiza ndani ya damu ya ndege aliyechinjwa pamoja na maji safi, na kuinyunyizia nyumba ile mara saba. Ataitakasa nyumba kwa damu ya yule ndege, maji safi, ndege aliye hai, mti wa mwerezi, hisopo na uzi mwekundu. Kisha atamwachia yule ndege aliye hai huru mashambani nje ya mji. Kwa njia hii atafanya upatanisho kwa ajili ya nyumba ile, nayo itakuwa safi.” Haya ndio masharti kuhusu aina yoyote ya ugonjwa wa ngozi wa kuambukiza, kidonda chochote, ukoma katika vazi au ndani ya nyumba, kwa uvimbe, upele, au alama nyeupe katika ngozi, kupambanua wakati kitu fulani ni safi au najisi. Haya ndio masharti kuhusu magonjwa ya ngozi ya kuambukiza na ukoma.