Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Walawi 13:1-59

Walawi 13:1-59 Biblia Habari Njema (BHN)

Mwenyezi-Mungu aliwaambia Mose na Aroni, “Iwapo mtu yeyote atakuwa na uvimbe au upele au kipaku mwilini mwake, ikadhihirika kwamba ni ukoma, basi, ataletwa kwa kuhani Aroni au mmoja wa wanawe aliye kuhani. Kuhani atapakagua mahali palipo na ugonjwa na ikiwa nywele za mahali hapo zimebadilika kuwa nyeupe na ugonjwa wenyewe ukionekana kuwa uko ndani zaidi ya ngozi ya mwili wake, basi, huo ni ukoma. Kuhani akimaliza kumkagua, hivyo atatangaza kuwa mtu huyo ni najisi. Lakini ikiwa kipele hicho, ingawa cheupe hakikuingia ndani sana ya ngozi na wala nywele za mahali hapo hazikubadilika kuwa nyeupe, basi, kuhani atamtenga mtu huyo kwa muda wa siku saba. Siku ya saba, kuhani atamwangalia tena mtu huyo, na ikiwa, kulingana na uchunguzi wa kuhani, ugonjwa huo haujaenea kwenye ngozi yake, basi, kuhani atamtenga mtu huyo kwa siku nyingine saba. “Kuhani atamkagua tena mtu huyo siku ya saba. Kama kulingana na uchunguzi wake, ile sehemu ya ugonjwa imefifia na ugonjwa haujaenea, basi, kuhani atamtangaza mtu huyo kuwa safi; huo ni upele tu. Mtu huyo atafua mavazi yake, naye atakuwa safi. Lakini upele huo ukiwa umeenea kwenye ngozi, baada ya mtu huyo kujionesha kwa kuhani kwa ajili ya kutakaswa kwake, basi, atakuja tena kwa kuhani. Kuhani atamwangalia tena, na kama ule upele umeenea kwenye ngozi, basi, kuhani atamtangaza mtu huyo kuwa najisi; huo ni ukoma. “Kama mtu ameshikwa na ukoma, ataletwa kwa kuhani. Kuhani atamwangalia na kama kuna uvimbe mweupe ambao umezifanya nywele zake ziwe nyeupe na uvimbe huo umegeuka kuwa kidonda kibichi, huo ni ukoma wa muda mrefu. Kuhani atamtangaza mtu huyo kuwa najisi. Hakuna haja ya kumweka mtu huyo kwa uchunguzi kwani yu najisi tayari. Kama ukoma umemshika na umeenea mwili mzima, toka utosini hadi nyayoni kama atakavyoona kuhani, hapo kuhani atamwangalia. Kuhani akiona kuwa ukoma umemwenea mwili mzima, basi, atamtangaza mtu huyo kuwa safi kwa sababu mwili umegeuka kuwa mweupe na hivyo mtu huyo yu safi. Lakini kukionekana mwilini mwa mtu huyo kidonda kibichi, basi, mtu huyo atakuwa najisi. Kuhani ataangalia hicho kidonda kibichi na kumtangaza kuwa ni najisi kwa sababu huo ni ukoma. Lakini hicho kidonda kikigeuka tena kuwa cheupe, mtu huyo atarudi kwa kuhani. Kuhani atamwangalia na akiona kuwa kimegeuka kuwa cheupe, basi, atamtangaza mtu huyo kuwa safi. “Kama mtu ameshikwa na jipu, nalo limepona, lakini mahali pale lilipokuwa jipu pamegeuka kuwa uvimbe mweupe au kuwa pekundu lakini peupe kiasi, ni lazima kumwonesha kuhani. Kuhani atamwangalia huyo mtu. Kuhani akiona pamegeuka kuwa na shimo na nywele za mahali hapo zimegeuka kuwa nyeupe, basi, kuhani atamtangaza mtu huyo kuwa najisi; huo ni ugonjwa wa ukoma ambao umetokana na jipu. Lakini kama kuhani atamwangalia huyo mtu na kuona kuwa nywele za mahali hapo si nyeupe na wala hakuna shimo, ila pamefifia, basi, atamtenga huyo mtu kwa muda wa siku saba. Kama ugonjwa huo utaenea kwenye ngozi, basi, kuhani atamtangaza mtu huyo kuwa najisi; sehemu hiyo ina ugonjwa. Lakini, kama ile sehemu haijaenea, basi, lile ni kovu la jipu tu. Kuhani atamtangaza mtu huyo kuwa safi. “Au, Iwapo kuna mahali palipoungua na ile nyama mbichi imegeuka kuwa nyekundu-nyeupe au ni nyeupe, kuhani atapaangalia. Kama akiona kuwa nywele zimegeuka kuwa nyeupe na pana shimo, basi, huo ni ukoma. Ukoma huo umejitokeza kwa njia ya mahali hapo palipoungua. Kuhani atamtangaza mtu huyo kuwa najisi; kwani anao ugonjwa wa ukoma. Lakini kama kuhani akiona kuwa nywele za mahali hapo si nyeupe na hakuna shimo ila pamefifia, basi, kuhani atamtenga mtu huyo kwa muda wa siku saba. Siku ya saba kuhani atamwangalia. Kama umeenea kwenye ngozi, basi, kuhani atamtangaza mtu huyo kuwa najisi; kwani anao ugonjwa wa ukoma. Lakini, kama ile alama haijaenea, ila imefifia, huo ni uvimbe uliotokana na kuungua; basi, kuhani atamtangaza mtu huyo kuwa safi; kwani hilo ni kovu la kuungua. “Kama mtu yeyote mwanamume au mwanamke, ana kidonda kichwani au kidevuni, kuhani atauangalia ugonjwa huo. Iwapo kuhani ataona kuwa kuna shimo na nywele ni manjano na nyembamba, basi, atamtangaza mtu huyo kuwa najisi; kwani huo ni upele na ni ukoma wa kichwa au wa kidevu. Kama kuhani ataona kuwa hakuna shimo na nywele si nyeusi, basi kuhani atamtenga mtu huyo kwa muda wa siku saba. Siku ya saba kuhani atakiangalia kile kidonda. Kama kidonda hicho hakijaenea na hakuna nywele zenye rangi ya manjano wala hakuna vipele vyovyote mahali hapo, basi, mtu huyo atanyoa nywele au ndevu zake. Lakini mahali pale penye vipele hatapanyoa. Kisha kuhani atamtenga mtu huyo kwa muda mwingine wa siku saba. Siku ya saba, kuhani ataviangalia vile vipele. Iwapo kuhani ataona kuwa vipele hivyo havikuenea kwenye ngozi na wala havikwenda ndani ya ngozi, basi, atamtangaza mtu huyo kuwa safi. Mtu huyo atafua mavazi yake, naye atakuwa safi. Lakini iwapo vipele hivyo vimeenea baada ya kutakaswa, mtu huyo ataangaliwa na kuhani na ikiwa vimeenea kwenye ngozi, kuhani hatahitaji kutafuta nywele zenye rangi manjano; mtu huyo atakuwa najisi. Lakini iwapo kuhani ataona kuwa vile vipele vimepona na nywele nyeusi zimeota mahali hapo, basi, vidonda hivyo vimepona, basi, mtu huyo ni safi. Kuhani atamtangaza mtu huyo kuwa safi. “Kama mtu yeyote, awe mwanamume au mwanamke, ana alama nyeupe mwilini mwake, kuhani atamwangalia mtu huyo. Iwapo kuhani ataona kuwa alama hizo ni nyeupe kiasi, huo ni upele wa kawaida; mtu huyo ni safi. “Kama mwanamume amepata upara, yeye ni safi kwani ana upara tu. Iwapo upara huo umetanda tangu nyuma mpaka mbele mtu huyo ana upara tu na yu safi. Lakini kama kwenye kichwa penye upara au kwenye paji la uso penye upara kuna alama nyekundu-nyeupe, huo ni ukoma unaotokea kwenye upara wake kichwani au kwenye paji lake. Kuhani atamwangalia. Iwapo kuhani ataona kuwa huo uvimbe ni mwekundu-mweupe kwenye upara au kwenye paji lake na unaonekana kama ukoma kwenye ngozi yake, basi, mtu huyo ana ukoma; yeye ni najisi. Kuhani atamtangaza mtu huyo kuwa najisi. Ugonjwa wake upo kwenye kichwa chake. “Mwenye ukoma yeyote atavaa nguo zilizochanika, nywele zake hatazichana, na mdomo wake wa juu ataufunika na atapaza sauti akisema, ‘Mimi ni najisi, mimi ni najisi.’ Ataendelea kuwa najisi kwa muda wote alio na ugonjwa huo. Yeye ni najisi; naye atakaa peke yake nje ya kambi.” “Kama kuna namna ya upele wa ukoma kwenye vazi, liwe la sufu au kitani, vazi hilo liwe limefumwa au limesokotwa kwa kitani au sufu au ni vazi la ngozi ya aina yoyote ile, iwapo upele huo una rangi ya kijani au nyekundu katika vazi hilo, basi, vazi hilo lina upele. Kwa hiyo ni lazima kumwonesha kuhani. Kuhani atauangalia upele huo na kuliweka vazi hilo kando kwa muda wa siku saba. Siku ya saba atauangalia upele huo. Ikiwa upele huo umeenea katika vazi hilo, liwe ni la kufuma au kusokotwa au la ngozi au la ngozi ya aina yoyote ile, vazi hilo lina upele. Hivyo vazi hilo ni najisi. Kuhani atalichoma moto vazi hilo kwani lina namna ya upele wa ukoma. “Kama kuhani ataona kuwa upele haukuenea katika vazi, basi, ataamuru vazi hilo lifuliwe na kuwekwa kando kwa muda mwingine wa siku saba. Kuhani ataliangalia hilo vazi baada ya kuoshwa. Ikiwa ile alama haijabadilika rangi yake hata ingawa upele haukuenea, basi, vazi hilo ni najisi. Vazi hilo utalichoma moto, iwe alama ya upele ipo nyuma au mbele ya vazi hilo. “Kama kuhani ataona kuwa ile alama imefifia baada ya kufuliwa, basi atararua ile sehemu iliyo na namna ya upele wa ukoma. Kisha, ikiwa hiyo alama inaonekana tena baadaye katika vazi lililofumwa au lililosokotwa au katika kitu chochote cha ngozi, basi upele umeenea. Hapo vazi hilo utalichoma moto. Lakini vazi ambalo upele umetokea baada ya kulifua itabidi lifuliwe mara ya pili na hivyo lipate kuwa safi.” Hiyo ni sheria kuhusu namna ya upele wa ukoma unaotokea katika vazi la sufu au kitani au lililofumwa au lililosokotwa au la ngozi. Kwa njia hiyo mtaweza kupambanua kati ya vazi lisilo najisi na lile lililo najisi.

Shirikisha
Soma Walawi 13

Walawi 13:1-59 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Kisha BWANA akanena na Musa na Haruni, na kuwaambia, Mtu atakapokuwa na uvimbe katika ngozi ya mwili wake, au upele, au kipaku king'aacho, nao ukawa ni ugonjwa wa ukoma katika ngozi ya mwili wake, ndipo atakapoletwa kwa Haruni kuhani, au kwa mmojawapo wa wanawe makuhani; na huyo kuhani ataliangalia hilo pigo lililo katika ngozi ya mwili; na nywele zilizoko katika hilo pigo zimegeuka kuwa nyeupe, na hilo pigo kuonekana kwake limeingia ndani kuliko ile ngozi ya mwili wake, ni pigo la ukoma hilo; na ikiwa nywele zilizoko katika sehemu zilizougua zimegeuka rangi na kuwa nyeupe, na hilo pigo kuonekana limeingia ndani kuliko ile ngozi ya mwili, hilo ni pigo la ukoma, Lakini ikiwa kipaku king'aacho katika ngozi ya mwili wake ni cheupe, na kuonekana si shimo la kuingia ndani kuliko ngozi wala nywele hazikugeuka kuwa nyeupe, ndipo kuhani atamweka mahali muda wa siku saba huyo aliye na hilo pigo; kisha kuhani atamwangalia siku ya saba; naye akiona ya kuwa pigo limezuilika, na halikuenea katika ngozi yake, ndipo kuhani atamweka mahali muda wa siku saba tena; kisha siku ya saba kuhani atamwangalia tena; ikiwa hilo pigo limeanza kufifia, wala pigo halikuwa katika ngozi yake ndipo kuhani atasema kuwa ni mzima, ni kipele tu; naye atazifua nguo zake, kisha atakuwa ni safi. Lakini ikiwa kipele kimeenea katika ngozi yake baada ya kujionesha kwa kuhani ili kutakaswa, atamwendea kuhani tena; naye kuhani ataangalia, ikiwa huo upele umeenea katika ngozi, ndipo kuhani atasema kuwa ni najisi; ni ukoma. Mtu atakapopatwa na ugonjwa wa ukoma, ndipo ataletwa kwa kuhani; naye kuhani ataangalia, ikiwa pana uvimbe mweupe katika ngozi yake, na mnywele zimegeuzwa kuwa nyeupe, tena ikiwa panafanyika kidonda katika ule uvimbe, ni ukoma usiopona ulio katika ngozi ya mwili wake, na kuhani atasema kuwa ni najisi; hatamweka mahali, kwa kuwa yeye ana unajisi. Huo ukoma ukitokeza katika ngozi ya mgonjwa, na ukaenea katika ngozi yake yote, kutoka kichwani hadi miguuni, kama kuhani atakavyoweza kuona, ndipo huyo kuhani ataangalia; ikiwa ukoma umemwenea mwili wake wote, atasema kuwa ni safi huyo aliye na hilo pigo, ikiwa ngozi yake yote imegeuka kuwa nyeupe, naye akawa safi. Lakini popote kitakapoonekana kidonda kibichi kwake mtu huyo, atakuwa yu najisi. Kuhani atakiangalia hicho kidonda kibichi, naye atasema kuwa ni najisi; kile kidonda kibichi ni najisi; ni ukoma. Au kama hicho kidonda kibichi kinageuka tena na kuwa cheupe, ndipo atamwendea kuhani, na huyo kuhani atamwangalia; ikiwa hilo pigo limegeuzwa kuwa jeupe, ndipo huyo kuhani atasema kuwa huyo aliyekuwa na pigo ni safi. Tena mwili wa mtu utakapokuwa na jipu katika ngozi yake, nalo limepoa, na mahali palipokuwa na lile jipu pana uvimbe mweupe, au kipaku king'aacho, cheupe lakini chekundu kidogo, ndipo atamwonesha kuhani mahali hapo; na kuhani ataangalia, kama kutaonekana kuingia ndani kuliko ngozi yenyewe, na malaika yakiwa yamegeuka kuwa meupe, ndipo kuhani atasema kwamba ni najisi; ni pigo la ukoma limetokea katika hilo jipu. Lakini kuhani akipaangalia, na iwe hamna nywele nyeupe ndani yake, wala hapakuingia ndani kuliko ile ngozi, lakini paanza kufifia, ndipo kuhani atamweka mahali muda wa siku saba; na kwamba pameenea katika ngozi, ndipo kuhani atasema kwamba ni najisi; hili ni pigo. Lakini ikiwa kipaku hicho king'aacho kimekaa pale pale, wala hakienei, ni kovu ya jipu; na kuhani atasema kwamba yu safi. Au mwili wa mtu ukiwa una mahali palipoungua katika ngozi yake, kisha pakawa kidonda, kikawa kipaku chekundu kidogo, au cheupe; ndipo kuhani atapaangalia; ikiwa nywele iliyo katika kile kipaku imegeuka kuwa nyeupe, na kwamba kumeonekana kuingia ndani kuliko ngozi yenyewe; ni ukoma, umetokea katika mahali palipoungua; na kuhani atasema kuwa ni najisi; hili ni pigo la ukoma. Lakini kuhani akipaangalia, nywele nyeupe hamna katika hicho kipaku king'aacho, nacho hakikuingia ndani kuliko ngozi, lakini chafifia; ndipo kuhani atamweka mahali muda wa siku saba; na kuhani atamwangalia siku ya saba; kama kimeenea katika ngozi, ndipo huyo kuhani atasema kuwa ni najisi; hili ni pigo la ukoma. Na kama hicho kipaku kikibaki pale pale, wala hakikuenea katika ngozi, lakini kimefifia; ni kufura kwake pale penye moto, na kuhani atasema kuwa ni safi; kwa kuwa ni kovu la kuwasha hili. Mwanamume au mwanamke atakapopatwa na maradhi kichani au kidevuni, ndipo kuhani ataliangalia hilo pigo; ikiwa pigo limeingia ndani kuliko ngozi yenyewe, na nywele zilizomo kuwa za rangi ya manjano na nyembamba, ndipo kuhani atasema kwamba ni najisi, maana ni kipwepwe, ni ukoma wa kichwa au wa kindevu. Tena kuhani akiliangalia lile pigo la kipwepwe, ikiwa kumeonekana si kuingia ndani kuliko ngozi yenyewe, wala hamna nywele nyeusi ndani yake, ndipo kuhani atamweka mahali huyo aliye na pigo la kipwepwe muda wa siku saba; na siku ya saba kuhani ataliangalia hilo pigo; na ikiwa hicho kipwepwe hakikuenea, wala hamna nywele za rangi ya manjano ndani yake, na kwamba kipwepwe hakionekani kuingia ndani kuliko ngozi yenyewe, ndipo huyo mtu atanyolewa, lakini hicho kipwepwe hatakinyoa; na kuhani atamweka mahali huyo aliye na kipwepwe muda wa siku saba tena; na siku ya saba kuhani atakiangalia hicho kipwepwe, ikiwa kipwepwe hakikuenea katika ngozi yake, wala hakionekani kuingia ndani kuliko ngozi; ndipo huyo kuhani atasema kwamba ni safi; naye atazifua nguo zake, naye atakuwa ni safi. Lakini hicho kipwepwe kama kikienea katika ngozi yake baada ya kutakasika kwake; ndipo kuhani atamwangalia; na ikiwa hicho kipwepwe kimeenea katika ngozi yake, kuhani hatatafuta hizo nywele za rangi ya manjano; yeye ni najisi. Lakini akiona ya kuwa hicho kipwepwe kimepungua, na nywele nyeusi zimemea humo; hicho kipwepwe kimepoa, naye yu safi, na huyo kuhani atasema kwamba yu safi. Mwanamume au mwanamke, atakapokuwa na vipaku ving'aavyo katika ngozi ya mwili, vipaku ving'aavyo vyeupe; ndipo kuhani ataangalia; ikiwa vile vipaku ving'aavyo vilivyo katika ngozi ya mwili wake ni vyeupe kidogo; ni mba iliyotokeza katika ngozi; yeye ni safi. Kwamba nywele za mtu zimemtoka kichwani mwake, yeye ni mwenye upara, ni safi. Tena kwamba nywele za mtu zimemtoka kichwani upande wa mbele, yeye ni mwenye upara wa kipaji; ni safi. Lakini kwamba katika kile kichwa kilicho na upara, au kile kipaji kilicho na upara, laonekana pigo jeupe kisha jekundu kidogo; ni ukoma, unatokea katika kichwa chake cha upara, au katika kipaji chake cha upara. Ndipo kuhani atamwangalia; kivimbe cha pigo kikiwa cheupe na chekundu chekundu, katika kichwa chake chenye upara, au katika kipaji chake cha upara, kama vile kuonekana kwa ukoma katika ngozi ya mwili; yeye ni mtu mwenye ukoma, ni najisi; na kuhani hana budi atasema kuwa ni najisi; pigo lake liko katika kichwa chake. Mtu mwenye ukoma aliye na pigo ndani yake, atavaa nguo zilizoraruka, na nywele timutimu; na ataufunika mdomo wake wa juu na kusema, “Ni najisi, ni najisi”. Kwa siku zote ambazo pigo litakuwa ndani yake atakuwa najisi, ataishi kwa upweke katika makazi yake, nje ya kambi. Kuhusu mavazi; vazi ambalo pigo la ukoma limo ndani yake, liwe ni vazi la sufu au la katani; likiwa limefumwa, au kusokotwa; likiwa ni la kitani au la sufu; liwe katika ngozi, au kitu chochote kilichofanywa cha ngozi; hilo pigo likiwa la rangi ya kijani au jekundu, katika vazi, au katika ngozi, au katika lililofumwa, au katika lililosokotwa, au katika kitu chochote cha ngozi; ni pigo la ukoma, nalo ataoneshwa kuhani; na kuhani ataliangalia hilo pigo, naye atakiweka mahali kile kilicho na pigo muda wa siku saba; kisha siku ya saba ataliangalia hilo pigo; kama pigo limeenea katika hilo lililofumwa, au katika hilo lililosokotwa, au katika ngozi, ijapokuwa hiyo ngozi ina matumizi yoyote; hilo pigo ni ukoma unaona; vazi hilo ni najisi. Naye ataliteketeza vazi hilo, liwe ni la kufumwa au ni la kusokotwa, kama ni la sufu, au la kitani, au kitu chochote cha ngozi, ambacho kina hilo pigo ndani yake; kwa maana, ni ukoma unaona; vazi hilo litateketezwa; Na kama kuhani akitazama, ikiwa hilo pigo halikuenea katika hilo vazi, wala katika hilo lililofumwa, wala katika hilo lililosokotwa, wala katika kitu chochote cha ngozi; ndipo kuhani ataamuru kwamba wakifue kitu kile kilicho na hilo pigo, naye atakiweka mahali muda wa siku saba tena; kisha kuhani ataangalia, baada ya kuoshwa hilo pigo; ikiwa hilo pigo halikugeuka rangi yake, wala halikuenea, ni najisi; utaliteketeza; ni uharibifu likiwa lina doa ndani au nje. Huyo kuhani ataangalia, ikiwa hilo pigo limeanza kufifia, baada ya kufuliwa kwake, ndipo atalirarua hilo pigo litoke katika vazi, au katika ngozi, au katika lililofumwa, au katika lililosokotwa; kisha, likionekana liko vile vile katika hilo vazi, katika lililofumwa, au katika lililosokotwa, au katika kitu chochote cha ngozi, ni pigo lenye kuenea; nawe vazi hilo lenye pigo utaliteketeza. Na hilo vazi, lililofumwa, au lililosokotwa, au kitu chochote cha ngozi, utakalolifua, kama hilo pigo limetoka na kuliacha, ndipo litafuliwa mara ya pili, nalo litakuwa safi. Na katika pigo la ukoma katika vazi la sufu, au la kitani, kama ni katika lililofumwa, au lililosokotwa, au katika kitu chochote cha ngozi, sheria yake ni hiyo, kusema kwamba ni safi, au kusema kwamba ni najisi.

Shirikisha
Soma Walawi 13

Walawi 13:1-59 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Kisha BWANA akanena na Musa na Haruni, na kuwaambia, Mtu atakapokuwa na kivimbe katika ngozi ya mwili wake, au kikoko, au kipaku king’aacho, nalo likawa pigo la ukoma katika ngozi ya mwili wake, ndipo atakapoletwa kwa Haruni kuhani, au kwa wanawe, makuhani mmojawapo; na huyo kuhani ataliangalia hilo pigo lililo katika ngozi ya mwili; na kwamba malaika yaliyo katika hilo pigo yamegeuka kuwa meupe, na hilo pigo kuonekana kwake limeingia ndani kuliko ile ngozi ya mwili wake, ni pigo la ukoma hilo; na kuhani atamwangalia na kusema kuwa yu mwenye unajisi. Na hicho kipaku king’aacho, kwamba ni cheupe katika ngozi ya mwili wake, na kuonekana kwake si shimo la kuingia ndani kuliko ngozi, na malaika hayakugeuka kuwa meupe, ndipo kuhani atamweka mahali muda wa siku saba huyo aliye na hilo pigo; kisha kuhani atamwangalia siku ya saba; naye akiona ya kuwa pigo limeshangaa, na pigo halikwendelea mbele katika ngozi yake, ndipo kuhani atamweka mahali muda wa siku saba tena; kisha siku ya saba kuhani atamwangalia tena; na tazama, ikiwa hilo pigo limeanza kufifia, wala pigo halikwendelea mbele katika ngozi yake, ndipo kuhani atasema kuwa yu safi; ni kikoko; naye atazifua nguo zake, kisha atakuwa yu safi. Lakini kwamba kikoko kimeenea katika ngozi yake baada ya kuonyesha nafsi yake kwa kuhani kwa kupata kutakaswa kwake ataonyesha nafsi yake tena kwa kuhani; na kuhani ataangalia, na tazama ikiwa hicho kikoko kimeenea katika ngozi, ndipo kuhani atasema kuwa yu najisi; ni ukoma. Pigo la ukoma litakapokuwa katika mtu, ndipo ataletwa kwa kuhani; na kuhani ataangalia, na tazama, ikiwa pana kivimbe cheupe katika ngozi yake, na malaika yamegeuzwa kuwa meupe, tena ikiwa pana nyama mbichi iliyomea katika kile kivimbe, ni ukoma wa zamani ulio katika ngozi ya mwili wake, na kuhani atasema kuwa yu najisi; hatamweka mahali, kwa kuwa yeye yuna unajisi. Tena kwamba huo ukoma ukitokeza katika ngozi yake, na ukoma ukamwenea ngozi yote, tangu kichwa hata miguuni, kama aonavyo kuhani; ndipo huyo kuhani ataangalia; na tazama, ikiwa ukoma umemwenea mwili wake wote, atasema kuwa yu safi huyo aliye na hilo pigo umegeuka kuwa mweupe wote; yeye ni safi. Lakini po pote itakapoonekana nyama mbichi kwake mtu huyo, atakuwa yu najisi. Kuhani ataiangalia hiyo nyama mbichi, naye atasema kuwa yu najisi; ile nyama mbichi ni najisi; ni ukoma. Au kama hiyo nyama mbichi iligeuka tena, na kugeuzwa kuwa nyeupe, ndipo atamwendea kuhani, na huyo kuhani atamwangalia; na tazama, ikiwa hilo pigo limegeuzwa kuwa jeupe, ndipo huyo kuhani atasema kuwa yu safi huyo aliyekuwa na pigo; yeye yu safi. Tena mwili wa mtu utakapokuwa na jipu katika ngozi yake, nalo limepoa, na mahali palipokuwa na lile jipu pana kivimbe cheupe, au kipaku king’aacho, cheupe lakini chekundu kidogo, ndipo atamwonyesha kuhani mahali hapo; na kuhani ataangalia, na tazama, kwamba kumeonekana kuingia ndani kuliko ngozi yenyewe, na malaika yakiwa yamegeuka kuwa meupe, ndipo kuhani atasema kwamba yu najisi; ni pigo la ukoma limetokea katika hilo jipu. Lakini kuhani akipaangalia, na tazama hamna malaika meupe ndani yake, wala hapana pa kuingia ndani kuliko ile ngozi, lakini paanza kufifia, ndipo kuhani atamweka mahali muda wa siku saba; na kwamba pameenea katika ngozi, ndipo kuhani atasema kwamba yu najisi; hili ni pigo. Lakini ikiwa kipaku hicho king’aacho kimeshangaa pale pale, wala hakienei, ni kovu ya jipu; na kuhani atasema kwamba yu safi. Au mwili wa mtu ukiwa una mahali katika ngozi yake penye moto, na hiyo nyama iliyomea pale penye moto, kama kikiwa kipaku chekundu kidogo, au cheupe; ndipo kuhani atapaangalia; na tazama, yakiwa malaika yaliyo katika kile kipaku yamegeuka kuwa meupe, na kwamba kumeonekana kuingia ndani kuliko ngozi yenyewe; ni ukoma, umetokea katika mahali penye moto; na kuhani atasema kwamba yu najisi; hili ni pigo la ukoma. Lakini kuhani akipaangalia, na tazama, malaika meupe hamna katika hicho kipaku king’aacho, nacho hakikuingia ndani kuliko ngozi, lakini chafifia; ndipo kuhani atamweka mahali muda wa siku saba; na kuhani atamwangalia siku ya saba; kama kimeenea katika ngozi, ndipo huyo kuhani atasema kwamba yu najisi; hili ni pigo la ukoma. Na kama hicho kipaku kikishangaa pale pale, wala hakikuenea katika ngozi, lakini kimefifia; ni kufura kwake pale penye moto, na kuhani atasema kwamba yu safi; kwa kuwa ni kovu la kuwasha hili. Tena mtu, mume au mke, akiwa na pigo juu ya kichwa, au katika ndevu zake, ndipo kuhani ataliangalia hilo pigo; na tazama, kwamba kumeonekana kuingia ndani kuliko ngozi yenyewe, tena zikiwamo nywele za rangi ya manjano kisha nyembamba, ndipo kuhani atasema kwamba yu najisi, maana, ni kipwepwe, ni ukoma wa kichwa, au wa ndevu. Tena kuhani akiliangalia lile pigo la kipwepwe, na tazama, kwamba kumeonekana si kuingia ndani kuliko ngozi yenyewe, wala hamna nywele nyeusi ndani yake, ndipo kuhani atamweka mahali huyo aliye na pigo la kipwepwe muda wa siku saba; na siku ya saba kuhani ataliangalia hilo pigo; na ikiwa hicho kipwepwe hakikuenea, wala hamna nywele za rangi ya manjano ndani yake, na kwamba kipwepwe hakionekani kuingia ndani kuliko ngozi yenyewe, ndipo huyo mtu atanyolewa, lakini hicho kipwepwe hatakinyoa; na kuhani atamweka mahali huyo aliye na kipwepwe muda wa siku saba tena; na siku ya saba kuhani atakiangalia hicho kipwepwe, na tazama, ikiwa kipwepwe hakikuenea katika ngozi yake, wala hakionekani kuingia ndani kuliko ngozi; ndipo huyo kuhani atasema kwamba yu safi; naye atazifua nguo zake, naye atakuwa yu safi. Lakini hicho kipwepwe kama kikienea katika ngozi yake baada ya kutakasika kwake; ndipo kuhani atamwangalia; na ikiwa hicho kipwepwe kimeenea katika ngozi yake, kuhani hatatafuta hizo nywele za rangi ya manjano; yeye yu najisi. Lakini akiona ya kuwa hicho kipwepwe kimeshangaa, na nywele nyeusi zimemea humo; hicho kipwepwe kimepoa, naye yu safi, na huyo kuhani atasema kwamba yu safi. Mtu, mume au mke, atakapokuwa na vipaku ving’aavyo katika ngozi ya mwili, vipaku ving’aavyo vyeupe; ndipo kuhani ataangalia; na tazama, ikiwa vile vipaku ving’aavyo vilivyo katika ngozi ya mwili wake ni vyeupe kidogo; ni mba hivyo, imetokea katika ngozi; yeye yu safi. Kwamba nywele za mtu zimemtoka kichwani mwake, yeye ni mwenye upaa, yu safi. Tena kwamba nywele za mtu zimemtoka kichwani upande wa mbele, yeye ni mwenye upaa wa kipaji; yu safi. Lakini kwamba katika kile kichwa kilicho na upaa, au kile kipaji kilicho na upaa, laonekana pigo jeupe kisha jekundu kidogo; ni ukoma, unatokea katika kichwa chake cha upaa, au katika kipaji chake cha upaa. Ndipo kuhani atamwangalia; na tazama, kivimbe cha pigo kikiwa cheupe na chekundu-chekundu, katika kichwa chake chenye upaa, au katika kipaji chake cha upaa, kama vile kuonekana kwa ukoma katika ngozi ya mwili; yeye ni mtu mwenye ukoma, yu najisi; na kuhani hana budi atasema kuwa yu najisi; pigo lake li katika kichwa chake. Kisha mwenye ukoma aliye na pigo ndani yake, nguo zake zitararuliwa, na nywele za kichwa chake zitaachwa wazi, naye atafunika mdomo wake wa juu, naye atapiga kelele, Ni najisi, ni najisi. Siku zote ambazo pigo li ndani yake, yeye atakuwa mwenye unajisi; yeye yu najisi; atakaa peke yake; makazi yake yatakuwa nje ya marago. Tena, vazi nalo ambalo pigo la ukoma li ndani yake, kwamba ni vazi la sufu, au kwamba ni la kitani; likiwa limefumwa, au kusokotwa; likiwa ni la kitani au la sufu; kwamba ni katika ngozi, au kitu cho chote kilichofanywa cha ngozi; hilo pigo likiwa la rangi ya majani au jekundu, katika vazi, au katika ngozi, au katika lililofumwa, au katika lililosokotwa, au katika kitu cho chote cha ngozi; ni pigo la ukoma, nalo ataonyeshwa kuhani; na kuhani ataliangalia hilo pigo, naye atakiweka mahali kile kilicho na pigo muda wa siku saba; kisha siku ya saba ataliangalia hilo pigo; kama pigo limeenea katika hilo lililofumwa, au katika hilo lililosokotwa, au katika ngozi, ijapokuwa hiyo ngozi ina matumizi yo yote; hilo pigo ni ukoma unaokula; vazi hilo ni najisi. Naye atalichoma moto vazi hilo, kwamba ni lililofumwa au kwamba ni lililosokotwa, kama ni la sufu, au la kitani, au kitu cho chote cha ngozi, ambacho kina hilo pigo ndani yake; kwa maana, ni ukoma unaokula; vazi hilo litachomwa moto; Na kama kuhani akitazama, na tazama, ikiwa hilo pigo halikuenea katika hilo vazi, wala katika hilo lililofumwa, wala katika hilo lililosokotwa, wala katika kitu cho chote cha ngozi; ndipo kuhani ataamuru kwamba wakifue kitu kile kilicho na hilo pigo, naye atakiweka mahali muda wa siku saba tena; kisha kuhani ataangalia, baada ya kuoshwa hilo pigo; na tazama, ikiwa hilo pigo halikugeuka rangi yake, wala halikuenea, li najisi; utakichoma moto; ni uharibifu likiwa lina upaa ndani au nje. Huyo kuhani akiangalia, na tazama, ikiwa hilo pigo limeanza kufifia, baada ya kufuliwa kwake, ndipo atalirarua hilo pigo litoke katika vazi, au katika ngozi, au katika lililofumwa, au katika lililosokotwa; kisha, likionekana li vivyo katika hilo vazi, katika lililofumwa, au katika lililosokotwa, au katika kitu cho chote cha ngozi, ni pigo lenye kuenea; nawe vazi hilo lenye pigo utalichoma moto. Na hilo vazi, lililofumwa, au lililosokotwa, au kitu cho chote cha ngozi, utakalolifua, kama hilo pigo limetoka na kuliacha, ndipo litafuliwa mara ya pili, nalo litakuwa safi. Na katika pigo la ukoma katika vazi la sufu, au la kitani, kama ni katika lililofumwa, au lililosokotwa, au katika kitu cho chote cha ngozi, sheria yake ni hiyo, kusema kwamba ni safi, au kusema kwamba ni najisi.

Shirikisha
Soma Walawi 13

Walawi 13:1-59 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)

BWANA akawaambia Musa na Haruni, “Iwapo mtu yeyote atakuwa na uvimbe, au upele, au alama nyeupe juu ya ngozi yake, ambayo yaweza kuwa ugonjwa wa ngozi wa kuambukiza, ni lazima aletwe kwa kuhani Haruni, au kwa mmoja wa wanawe, hao makuhani. Kuhani atachunguza hicho kidonda kilichopo juu ya ngozi yake, na kama nywele za mahali palipo na kidonda zimebadilika kuwa nyeupe, na ikiwa kidonda kimeingia ndani ya ngozi, basi ni ugonjwa wa ngozi wa kuambukiza, yaani ukoma. Kuhani atakapomchunguza, atamtangaza mtu huyo kuwa najisi. Kama alama juu ya ngozi yake ni nyeupe, lakini haionekani kuingia ndani ya ngozi, na nywele kwenye alama hiyo hazijageuka kuwa nyeupe, kuhani atamtenga mtu aliyeambukizwa kwa siku saba. Siku ya saba, kuhani atamchunguza, na kama hakuona badiliko kwenye kile kidonda na hakijaenea juu ya ngozi, atamtenga kwa siku nyingine saba. Siku ya saba kuhani atamchunguza tena, na kama kidonda kimepungua na hakijaenea juu ya ngozi, kuhani atamtangaza mtu huyo kuwa ni safi; ni upele tu. Ni lazima mtu huyo afue mavazi yake, naye atakuwa safi. Lakini ikiwa ule upele utaenea katika ngozi yake baada ya yeye kujionesha kwa kuhani na kutangazwa kuwa safi, ni lazima aende tena kwa kuhani. Kuhani atamchunguza, na kama upele umeenea kwenye ngozi, atamtangaza kuwa najisi, kwani ni ugonjwa wa ngozi wa kuambukiza. “Wakati mtu yeyote ana ugonjwa wa ngozi wa kuambukiza, ni lazima aletwe kwa kuhani. Kuhani atamchunguza na kama kuna uvimbe mweupe katika ngozi ambao umefanya nywele kuwa nyeupe, na kama kuna nyama mbichi ndani ya uvimbe, ni ugonjwa sugu wa ngozi, na kuhani atamtangaza kuwa najisi. Hatamtenga tena kwa sababu ni najisi tayari. “Ikiwa ugonjwa utakuwa umeenea kwenye ngozi yake yote kwa kadiri kuhani atakavyoweza kuona, kwamba umeenea kwenye ngozi yote ya huyo mgonjwa kutoka kichwani hadi wayo, kuhani atamchunguza, na kama ugonjwa umeenea mwili mzima, atamtangaza huyo mtu kuwa safi. Kwa kuwa mwili wote umekuwa mweupe, yeye ni safi. Lakini itokeapo nyama mbichi kwenye ngozi yake, atakuwa najisi. Kuhani atakapoiona hiyo nyama mbichi, atamtangaza mtu huyo kuwa najisi. Hiyo nyama mbichi ni najisi, ana ugonjwa wa kuambukiza. Hiyo nyama mbichi ikigeuka na kuwa nyeupe, ni lazima amwendee kuhani. Kuhani atamchunguza, na kama vidonda vimekuwa vyeupe, kuhani atamtangaza mgonjwa huyo kuwa safi; kisha atakuwa safi. “Wakati mtu ana jipu juu ya ngozi yake nalo likapona, napo mahali palipokuwa na jipu pakatokea uvimbe mweupe, au alama yenye wekundu na weupe, ni lazima akajioneshe kwa kuhani. Kuhani atapachunguza, na kama uvimbe umeingia ndani ya ngozi, na nywele zimegeuka kuwa nyeupe, kuhani atamtangaza mtu huyo kuwa najisi. Ni ugonjwa wa ngozi wa kuambukiza uliojitokeza pale jipu lilipokuwa. Lakini ikiwa kuhani anapopachunguza pakawa hapana nywele nyeupe ndani yake, wala hapakuingia ndani ya ngozi, na pameanza kupungua, basi kuhani atamtenga mtu huyo kwa siku saba. Kama unaenea kwenye ngozi, kuhani atamtangaza kuwa najisi; ni ugonjwa wa ngozi wa kuambukiza. Lakini ikiwa ile alama haijabadilika wala kuenea, ni kovu tu kutokana na jipu, kuhani atamtangaza kuwa safi. “Wakati mtu ameungua kwenye ngozi yake, pakatokea alama yenye wekundu na weupe, au alama nyeupe ikaonekana penye nyama mbichi pale palipoungua, kuhani ataichunguza ile alama, na kama nywele zilizo juu yake zimegeuka kuwa nyeupe, na panaonekana kuingia ndani ya ngozi, basi huo ni ugonjwa wa ngozi wa kuambukiza ambao umetokea katika jeraha la moto. Kuhani atamtangaza kuwa najisi; ni ugonjwa wa ngozi wa kuambukiza. Lakini kuhani akipachunguza na akaona kwamba hakuna nywele nyeupe kwenye alama ile, wala hapakuingia ndani ya ngozi, na pamepungua, basi kuhani atamtenga kwa siku saba. Siku ya saba kuhani atamchunguza tena, na kama unaenea kwenye ngozi, kuhani atamtangaza kuwa najisi; ni ugonjwa wa ngozi wa kuambukiza. Lakini, kama alama ile haikubadilika na wala haijaenea kwenye ngozi, napo pamepungua, ni uvimbe kutokana na jeraha la moto, na kuhani atamtangaza kuwa safi; ni kovu tu kutokana na kuungua. “Ikiwa mwanaume au mwanamke ana kidonda juu ya kichwa au juu ya kidevu, kuhani atakichunguza kile kidonda, na kama ataona kuwa kimeingia ndani ya ngozi, na nywele zilizo juu yake ni njano na nyembamba, kuhani atamtangaza mtu huyo kuwa najisi; ni ugonjwa wa ngozi wa kuambukiza wa kichwa au kidevu. Lakini kama kuhani akichunguza aina hii ya kidonda, kionekane kuwa hakijaingia ndani ya ngozi, na hakuna nywele nyeusi juu yake, basi atamtenga mtu huyo kwa siku saba. Siku ya saba kuhani atachunguza kidonda kile, na kama hakijaenea, na hakuna nywele za manjano juu yake, wala haukuingia ndani ya ngozi, mtu huyo ni lazima anyolewe, isipokuwa mahali palipo na ugonjwa, naye kuhani atamtenga kwa siku nyingine saba. Siku ya saba kuhani atachunguza tena kidonda kile; ikiwa hakijaenea kwenye ngozi na hakikuingia ndani ya ngozi, kuhani atamtangaza kuwa safi. Lazima afue nguo zake, naye atakuwa safi. Lakini ikiwa kidonda kitaenea katika ngozi baada ya kutangazwa kuwa safi, kuhani atamchunguza, na kama kidonda kimeenea kwenye ngozi, kuhani hana haja ya kutazama kama kuna nywele za manjano; mtu huyo ni najisi. Hata hivyo, katika uchunguzi wake akiona hapajabadilika, na nywele nyeusi zimeota juu yake, huyo mtu amepona. Yeye si najisi; kuhani atamtangaza kuwa safi. “Ikiwa mwanaume au mwanamke ana alama nyeupe juu ya ngozi yake, kuhani atamchunguza, na kama alama hizo zina weupe uliofifia, ni vipele visivyo na madhara vilivyojitokeza kwenye ngozi; mtu huyo ni safi. “Wakati mwanaume hana nywele naye ana upara, yeye ni safi. Ikiwa hana nywele kwenye ngozi ya kichwa chake, na ana upara kwenye paji, ni safi. Lakini kama ana kidonda chenye wekundu na weupe kwenye kichwa chake chenye upara, au kwenye paji la uso, ni ugonjwa wa ngozi wa kuambukiza unaojitokeza kichwani au kwenye paji lake la uso. Kuhani atamchunguza, na kama kidonda kilichovimba juu ya kichwa chake au kwenye paji la uso ni chekundu au cheupe kama ugonjwa wa ngozi wa kuambukiza, mtu huyo ni mgonjwa, na ni najisi. Kuhani atamtangaza kuwa najisi kwa sababu ya kidonda kwenye kichwa chake. “Mtu mwenye ugonjwa kama huo wa kuambukiza ni lazima avae nguo zilizoraruka, awachilie nywele zake bila kuzichana, afunike sehemu ya chini ya uso wake, na apige kelele, ‘Najisi! Najisi!’ Kwa muda wote atakaokuwa na ugonjwa huo wa kuambukiza atabaki kuwa najisi. Ni lazima aishi peke yake; ni lazima aishi nje ya kambi. “Kuhusu vazi lolote lililoharibiwa na maambukizo ya ukoma, liwe ni vazi la sufu au kitani, vazi lolote lililofumwa au kusokotwa la kitani au sufu, ngozi yoyote au chochote kilichotengenezwa kwa ngozi: ikiwa maambukizo kwenye vazi, ngozi, au vazi lililofumwa au kusokotwa la kitani au sufu, au kitu chochote cha ngozi, ni rangi ya kijani au nyekundu, huo ni ukoma unaoenea, na ni lazima kuhani aoneshwe. Kuhani atachunguza ukoma huo na kulitenga vazi hilo kwa siku saba. Siku ya saba atalichunguza, na kama ukoma umeenea kwenye vazi, au vazi lililofumwa au kusokotwa, au ngozi, kwa vyovyote vile itumikavyo, ni ukoma wa kuangamiza; vazi hilo ni najisi. Ni lazima achome vazi hilo, liwe ni la sufu au kitani kilichofumwa au kusokotwa, au kitu chochote cha ngozi chenye maambukizo; kwa kuwa ni ukoma wa kuangamiza, vazi lote ni lazima lichomwe moto. “Lakini kuhani akilichunguza na akaona kuwa ule ukoma haujaenea kwenye vazi, au vazi lililofumwa au kusokotwa, au kitu cha ngozi, ataagiza kwamba vazi lenye maambukizo lisafishwe. Kisha atalitenga kwa siku nyingine saba. Baada ya vazi lenye maambukizo kusafishwa, kuhani atalichunguza, na kama ukoma haujaonesha badiliko lolote, hata kama haujaenea, ni najisi. Lichome kwa moto, iwe ukoma umeenea upande mmoja au mwingine. Kama kuhani ataona kuwa ile alama imefifia baada ya kuoshwa, basi atararua sehemu iliyoambukizwa ya vazi, au ngozi, au vazi lililofumwa au kusokotwa. Lakini ikijitokeza tena kwenye vazi, au vazi lililofumwa au kusokotwa, ama kitu cha ngozi, ule ni ukoma unaoenea; chochote chenye ukoma ni lazima kichomwe kwa moto. Vazi, au vazi lililofumwa au kusokotwa, au kitu chochote cha ngozi, baada ya kusafishwa na kuondolewa ukoma, ni lazima lioshwe tena, ili liwe safi.” Haya ndio masharti kuhusu maambukizo ya ukoma kwenye mavazi ya sufu au kitani, mavazi yaliyofumwa au kusokotwa, ama kitu chochote cha ngozi, kwa ajili ya kuvitangaza kuwa safi au najisi.

Shirikisha
Soma Walawi 13