Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Walawi 10:1-20

Walawi 10:1-20 Biblia Habari Njema (BHN)

Nao Nadabu na Abihu, wanawe Aroni, walichukua kila mmoja chetezo chake, wakaweka moto na ubani, wakamtolea Mwenyezi-Mungu moto najisi, ambao haukulingana na agizo lake Mwenyezi-Mungu. Basi, moto ukatokea mbele ya Mwenyezi-Mungu, ukawateketeza hao vijana, wakafa mbele yake. Hapo, Mose akamwambia Aroni, “Kwa tukio hili Mwenyezi-Mungu amekuonesha maana ya kile alichosema: ‘Nitajionesha kuwa mtakatifu miongoni mwa wale walio karibu nami; nitatukuzwa mbele ya watu wote!’” Aroni akanyamaza kimya. Basi, Mose akawaita Mishaeli na Elsafani, wanawe Uzieli, baba mdogo wa Aroni, akawaambia waje kuondoa maiti za ndugu zao maskani na kuzipeleka nje ya kambi. Wakachukua maiti za ndugu zao na kuzipeleka nje ya kambi wakiwa wamevaa mavazi yao, kama Mose alivyoamuru. Kisha Mose akamwambia Aroni na wanawe, Eleazari na Ithamari, “Msivuruge nywele zenu na wala msirarue mavazi yenu kuomboleza, la sivyo mtakufa na kuiletea jumuiya yote ghadhabu ya Mwenyezi-Mungu. Lakini ndugu zenu yaani jumuiya yote ya Israeli, wanaweza kuomboleza kwa sababu ya moto huo aliouleta Mwenyezi-Mungu. Msitoke nje ya mlango wa hema la mkutano, la sivyo mtakufa; kwani mafuta ya kupaka ya Mwenyezi-Mungu yangali juu yenu.” Aroni na wanawe wakafanya kama Mose alivyosema. Mwenyezi-Mungu aliongea na Aroni, akasema, “Mnapoingia ndani ya hema la mkutano, wewe na wanao msinywe divai wala kileo chochote, la sivyo mtakufa. Hii itakuwa sheria ya kudumu katika vizazi vyenu vyote. Ni lazima mtofautishe kati ya mambo matakatifu na mambo yasiyo matakatifu, kati ya mambo najisi na yasiyo najisi. Mtawafundisha Waisraeli masharti yote ambayo nimewaambia kwa njia ya Mose.” Mose akamwambia Aroni na wanawe waliosalia: Eleazari na Ithamari, “Chukueni ile sehemu ya sadaka ya nafaka iliyosalia kutoka sadaka anazotolewa Mwenyezi-Mungu kwa moto; muile karibu na madhabahu bila kutiwa chachu kwa sababu ni takatifu kabisa. Mtaila katika mahali patakatifu kwa sababu hiyo ni haki yako na wazawa wako kutoka katika sadaka anazotolewa Mwenyezi-Mungu kwa moto. Hivyo ndivyo nilivyoamriwa. Lakini kidari ambacho hufanywa nacho ishara ya kumtolea Mwenyezi-Mungu na mguu unaotolewa sadaka kama ishara, mnaweza kula mahali popote pasipo najisi. Utakula wewe, na watoto wako wa kiume na wa kike. Vitu hivyo umepewa kama haki yako na ya wazawa wako kutoka sadaka za amani za watu wa Israeli. Ule mguu uliotolewa na kidari cha sadaka ya kufanyia ishara ya kumtolea Mwenyezi-Mungu watavileta pamoja na sadaka za mafuta zitolewazo kwa moto, ili kufanya ishara ya kuvitolea mbele ya Mwenyezi-Mungu, viwe sadaka ya kutolewa kwa ishara. Hivyo vitakuwa vyako pamoja na wanao; ni haki yenu milele kama Mwenyezi-Mungu alivyoamuru.” Basi, Mose alichunguza kwa makini kuhusu mbuzi mmoja aliyetolewa sadaka ya kuondoa dhambi, kumbe akagundua kuwa alikwisha teketezwa. Hivyo akawakasirikia sana Eleazari na Ithamari, wana wa Aroni waliosalia, akawauliza, “Kwa nini hamkumla katika mahali patakatifu kwa vile huyo ni kitu kitakatifu kabisa na mlikuwa mmepewa huyo ili kuondoa hatia ya jumuiya na kuwafanyia ibada ya upatanisho mbele ya Mwenyezi-Mungu? Tena, kwa vile damu yake haikuletwa ndani ya mahali patakatifu, ni dhahiri iliwapasa kumla ndani ya mahali patakatifu kama nilivyoamuru.” Aroni akamwambia Mose, “Tazama, leo wametolea sadaka yao ya kuondoa dhambi na sadaka ya kuteketezwa mbele ya Mwenyezi-Mungu; hata hivyo mambo haya yamenipata! Tena kama ningekula ile sadaka ya kuondoa dhambi hivi leo, je, ingekubalika mbele ya Mwenyezi-Mungu?” Mose aliposikia hayo, akaridhika.

Shirikisha
Soma Walawi 10

Walawi 10:1-20 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Na Nadabu na Abihu, wana wa Haruni, wakatwaa kila mtu chetezo chake, wakatia moto ndani yake, wakatia na uvumba, nao wakatoa moto najisi mbele ya BWANA, ambao yeye hakuwaagiza. Kisha moto ukatoka hapo mbele za BWANA, na ukawateketeza, nao wakafa mbele za BWANA. Ndipo Musa akamwambia Haruni, Jambo hili ni hilo BWANA alilolinena, akisema, Nitatakaswa mimi katika hao wanikaribiao, nami nitatukuzwa mbele ya watu hao wote. Haruni akanyamaza kimya. Musa akawaita Mishaeli na Elisafani, wana wa Uzieli mjombaye Haruni, na kuwaambia, Njoni karibu, mwachukue hawa ndugu zenu, mkawaondoe hapa mbele ya maskani, mwende nao nje ya kambi. Basi wakaja karibu, na kuwachukua, wakiwa wamevaa nguo zao, wakawachukua nje ya kambi; kama Musa alivyosema. Kisha Musa akamwambia Haruni na wanawe Eleazari na Ithamari, Msiache wazi nywele za vichwani mwenu, wala msiyararue mavazi yenu; ili kwamba msife, tena asiukasirikie mkutano wote; lakini ndugu zenu, nyumba yote ya Israeli, na waomboleze kwa ajili ya waliochomwa na moto wa BWANA. Wala hamtatoka nje mlangoni mwa hema ya kukutania, msije mkafa; kwa sababu mafuta ya kutiwa ya BWANA yako juu yenu. Nao wakafanya kama hilo neno la Musa. Kisha BWANA akanena na Haruni, na kumwambia, Usinywe divai wala kileo chochote, wewe, wala wanao pamoja nawe, hapo mwingiapo ndani ya hema ya kukutania, ili kwamba msife; amri hii itakuwa ni amri ya milele katika vizazi vyenu; kisha, mpate kupambanua kati ya yaliyo matakatifu na hayo yaliyo ya siku zote, na kati ya yaliyo najisi na hayo yaliyo safi; tena mpate kuwafundisha wana wa Israeli amri hizi zote ambazo BWANA amewaambia kwa mkono wa Musa. Kisha Musa akanena na Haruni, na Eleazari, na Ithamari, hao wanawe waliobaki, Twaeni hiyo sadaka ya unga iliyosalia katika kafara za BWANA zilizotolewa kwa moto, mkaile pasipo kutiwa chachu, pale karibu na madhabahu; kwa kuwa ni takatifu sana; nanyi mtaila katika mahali patakatifu, kwa sababu ni haki yako, na haki ya wanao, katika hizo kafara zisongezwazo kwa BWANA kwa moto; kwani niliagizwa hivyo. Na kidari cha kutikiswa, na mguu wa kuinuliwa, mtavila katika mahali palipo safi; wewe, na wanao, na binti zako pamoja nawe; kwa maana vimetolewa kuwa ni haki yako, na haki ya wanao, katika zile kafara za sadaka za amani za wana wa Israeli. Mguu wa kuinuliwa, na kidari cha kutikiswa, Watavileta pamoja na dhabihu zisongezwazo kwa njia ya moto, za hayo mafuta ili kuvitikisa viwe sadaka ya kutikiswa mbele za BWANA; kisha vitakuwa ni vyako wewe, na vya wanao pamoja nawe, ni haki yenu milele, kama BWANA alivyoagiza. Kisha Musa akamtafuta sana huyo mbuzi wa sadaka ya dhambi, naye, tazama, alikuwa amekwisha kuteketezwa; naye akawakasirikia hao Eleazari na Ithamari, wana wa Haruni, hao waliobaki, akawaambia, Kwa nini hamkula hiyo sadaka ya dhambi katika mahali patakatifu, kwa kuwa ni takatifu sana, naye amewapa ninyi ili kuuchukua uovu wa mkutano, na kuwafanyia upatanisho mbele za BWANA? Angalieni, hiyo damu yake haikuletwa ndani ya mahali patakatifu; iliwapasa kuila ndani ya mahali patakatifu, kama nilivyowaagiza. Haruni akamwambia Musa, Angalia, hivi leo wamesongeza sadaka yao ya dhambi, na sadaka yao ya kuteketezwa, mbele za BWANA; kisha mambo kama haya yamenipata; tena kama ningalikula hiyo sadaka ya dhambi hivi leo, je! Lingekuwa ni jambo la kupendeza mbele za macho ya BWANA? Naye Musa aliposikia hayo, akaridhika.

Shirikisha
Soma Walawi 10

Walawi 10:1-20 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Na Nadabu na Abihu, wana wa Haruni, wakatwaa kila mtu chetezo chake, wakatia moto ndani yake, wakatia na uvumba, nao wakatoa moto wa kigeni mbele ya BWANA, ambao yeye hakuwaagiza. Kisha moto ukatoka hapo mbele za BWANA, nao ukawala, nao wakafa mbele za BWANA. Ndipo Musa akamwambia Haruni, Jambo hili ni hilo BWANA alilolinena, akisema, Nitatakaswa mimi katika hao wanikaribiao, nami nitatukuzwa mbele ya watu hao wote. Haruni akanyamaza kimya. Musa akawaita Mishaeli na Elisafani, wana wa Uzieli mjombaye Haruni, na kuwaambia, Njoni karibu, mwachukue hawa ndugu zenu, mkawaondoe hapa mbele ya maskani, mwende nao nje ya marago. Basi wakaja karibu, na kuwachukua, hali wamevaa nguo zao, wakawachukua nje ya marago; kama Musa alivyosema. Kisha Musa akamwambia Haruni na wanawe Eleazari na Ithamari, Msiache wazi nywele za vichwani mwenu, wala msiyararue mavao yenu; ili kwamba msife, tena asiukasirikie mkutano wote; lakini ndugu zenu, nyumba yote ya Israeli, na waomboleze kwa ajili ya hicho kichomo alichowasha BWANA. Wala hamtatoka nje mlangoni mwa hema ya kukutania, msije mkafa; kwa sababu mafuta ya kutiwa ya BWANA ya juu yenu. Nao wakafanya kama hilo neno la Musa. Kisha BWANA akanena na Haruni, na kumwambia, Usinywe divai wala kileo cho chote, wewe, wala wanao pamoja nawe, hapo mwingiapo ndani ya hema ya kukutania, ili kwamba msife; amri hii itakuwa ni amri ya milele katika vizazi vyenu; kisha, mpate kupambanua kati ya yaliyo matakatifu na hayo yaliyo ya siku zote, na kati ya yaliyo najisi na hayo yaliyo safi; tena mpate kuwafundisha wana wa Israeli amri hizi zote ambazo BWANA amewaambia kwa mkono wa Musa. Kisha Musa akanena na Haruni, na Eleazari, na Ithamari, hao wanawe waliobaki, Twaeni hiyo sadaka ya unga iliyosalia katika kafara za BWANA zilizotolewa kwa moto, mkaile pasipo kutiwa chachu, pale karibu na madhabahu; kwa kuwa ni takatifu sana; nanyi mtaila katika mahali patakatifu, kwa sababu ni haki yako, na haki ya wanao, katika hizo kafara zisongezwazo kwa BWANA kwa moto; kwani ni hivyo nilivyoagizwa. Na kidari cha kutikiswa, na mguu wa kuinuliwa, mtavila katika mahali palipo safi; wewe, na wanao, na binti zako pamoja nawe; kwa maana vimetolewa kuwa ni haki yako, na haki ya wanao, katika zile kafara za sadaka za amani za wana wa Israeli. Mguu wa kuinuliwa, na kidari cha kutikiswa, Watavileta pamoja na dhabihu zisongezwazo kwa njia ya moto, za hayo mafuta ili kuvitikisa viwe sadaka ya kutikiswa mbele za BWANA; kisha vitakuwa ni vyako wewe, na vya wanao pamoja nawe, ni haki yenu milele, kama BWANA alivyoagiza. Kisha Musa akamtafuta sana huyo mbuzi wa sadaka ya dhambi, naye, tazama, alikuwa amekwisha kuchomwa moto; naye akawakasirikia hao Eleazari na Ithamari, wana wa Haruni, hao waliobaki, akawaambia, Kwa nini hamkula hiyo sadaka ya dhambi katika mahali patakatifu, kwa kuwa ni takatifu sana, naye amewapa ninyi ili kuuchukua uovu wa mkutano, na kuwafanyia upatanisho mbele za BWANA? Angalieni, hiyo damu yake haikuletwa ndani ya mahali patakatifu; iliwapasa kuila ndani ya mahali patakatifu, kama nilivyowaagiza. Haruni akamwambia Musa, Angalia, hivi leo wamesongeza sadaka yao ya dhambi, na sadaka yao ya kuteketezwa, mbele za BWANA; kisha mambo kama haya yamenipata; tena kama ningalikula hiyo sadaka ya dhambi hivi leo, je! Lingekuwa ni jambo la kupendeza mbele za macho ya BWANA? Naye Musa aliposikia hayo, yakampendeza.

Shirikisha
Soma Walawi 10

Walawi 10:1-20 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)

Nadabu na Abihu, wana wa Haruni, wakachukua vyetezo vyao, wakaweka moto ndani yake na kuongeza uvumba; kisha wakamtolea BWANA moto usio halali, kinyume na agizo la Mungu. Hivyo moto ukaja kutoka kwa uwepo wa BWANA na kuwateketeza, nao wakafa mbele za BWANA. Kisha Musa akamwambia Haruni, “Hili ndilo alilonena BWANA, aliposema: “ ‘Miongoni mwa wale watakaonikaribia nitajionesha kuwa mtakatifu; machoni pa watu wote nitaheshimiwa.’ ” Haruni akanyamaza. Musa akawaita Mishaeli na Elisafani, wana wa Uzieli mjomba wake Haruni, akawaambia, “Njooni hapa. Ondoeni miili ya ndugu zenu mbele ya mahali patakatifu, mkaipeleke nje ya kambi.” Hivyo wakaja na kuwaondoa, wakiwa bado wamevalia makoti yao ya ibada, wakawapeleka nje ya kambi, kama Musa alivyoamuru. Ndipo Musa akamwambia Haruni pamoja na wanawe, Eleazari na Ithamari, “Msifunue vichwa vyenu wala msirarue mavazi yenu, la sivyo mtakufa na BWANA ataikasirikia jumuiya nzima. Lakini ndugu zenu, nyumba yote ya Israeli, wanaweza kuwaombolezea wale ambao BWANA amewaangamiza kwa moto. Msitoke nje ya ingilio la Hema la Kukutania, la sivyo mtakufa, kwa sababu mafuta ya BWANA ya upako yako juu yenu.” Hivyo wakafanya kama vile Musa alivyosema. Kisha BWANA akamwambia Haruni, “Wewe na wanao msinywe mvinyo wala kinywaji kingine kilichochachuka wakati mwingiapo katika Hema la Kukutania, la sivyo mtakufa. Hili litakuwa agizo la kudumu kwa vizazi vijavyo. Ni lazima mtenganishe kati ya kilicho kitakatifu na kilicho cha kawaida, kati ya kilicho najisi na kilicho safi, na lazima mwafundishe Waisraeli amri zote ambazo BWANA aliwapa kupitia Musa.” Musa akamwambia Haruni pamoja na wanawe waliosalia, Eleazari na Ithamari, “Chukueni sadaka ya nafaka iliyobaki kutoka kwa sadaka zilizotolewa kwa BWANA kwa moto, muile hapo kando ya madhabahu ikiwa imeandaliwa bila chachu, kwa sababu ni takatifu sana. Mtaila katika mahali patakatifu kwa sababu ni fungu lenu na fungu la wana wenu la sadaka zilizotolewa kwa BWANA kwa moto, kwa maana hivyo ndivyo nilivyoamriwa. Lakini wewe na wanao na binti zako mwaweza kula kidari kile kilichoinuliwa na paja lile lililotolewa. Mtavila katika mahali patakatifu; mmepewa wewe na wanao kuwa fungu lenu la sadaka za amani za Waisraeli. Paja lile lililotolewa na kidari kile kilichoinuliwa lazima viletwe pamoja na sehemu za mafuta ya wanyama wa sadaka za kuteketezwa kwa moto, ili kuinuliwa mbele za BWANA kuwa sadaka ya kuinuliwa. Hili litakuwa fungu lako na wanao milele, kama BWANA alivyoagiza.” Musa alipouliza kuhusu mbuzi aliyetolewa sadaka ya dhambi na kugundua kwamba ameteketezwa, aliwakasirikia Eleazari na Ithamari, wana wa Haruni waliobaki. Akawauliza, “Kwa nini hamkula sadaka ya dhambi katika eneo la mahali patakatifu? Ni takatifu sana. Mlipewa ninyi ili kuondoa hatia ya jumuiya kwa ajili ya kuwafanyia upatanisho mbele za BWANA. Kwa kuwa damu yake haikuletwa ndani ya Mahali Patakatifu, mngemla mbuzi huyo katika sehemu ya mahali patakatifu kama nilivyoagiza.” Haruni akamjibu Musa, “Leo wanangu wametoa sadaka zao za dhambi na sadaka zao za kuteketezwa mbele za BWANA, lakini mambo kama haya yamenitokea mimi. Je, BWANA angependezwa kama ningekuwa nimekula sadaka ya dhambi leo?” Musa aliposikia haya, akaridhika.

Shirikisha
Soma Walawi 10