Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Walawi 1:1-17

Walawi 1:1-17 Biblia Habari Njema (BHN)

Mwenyezi-Mungu alimwita Mose na kuongea naye katika hema la mkutano, akamwambia, “Waambie Waisraeli kwamba kama mtu anapenda kumtolea Mwenyezi-Mungu sadaka ya mnyama, mnyama huyo atamchagua kutoka kundi lake la ng'ombe, kondoo au mbuzi. “Kama sadaka anayotoa mtu ni ya kuteketezwa, atamchagua mnyama dume asiye na dosari kutoka kundi lake, atamtolea mbele ya mlango wa hema la mkutano ili apate fadhili ya Mwenyezi-Mungu; ataweka mkono wake juu ya kichwa cha mnyama wa sadaka ya kuteketezwa, ambayo itakubaliwa kwa ajili ya kumfanyia huyo mtu upatanisho. Kisha, atamchinja huyo ng'ombe mbele ya Mwenyezi-Mungu. Nao makuhani, wazawa wa Aroni, wataichukua damu na kuinyunyizia madhabahu mlangoni mwa hema la mkutano, pande zake zote. Huyo mtu atamchuna huyo mnyama wa sadaka ya kuteketezwa na kumkata vipandevipande. Hao makuhani wazawa wa Aroni watazipanga kuni juu ya madhabahu na kuwasha moto. Kisha makuhani hao watachukua vile vipande vya nyama, kichwa na mafuta, na kuviweka juu ya kuni juu ya madhabahu. Lakini matumbo na miguu ya mnyama huyo mtu ataviosha kwa maji. Kuhani ataiteketeza sadaka yote juu ya madhabahu. Hiyo ni sadaka ya kuteketezwa kwa moto yenye harufu nzuri ya kumpendeza Mwenyezi-Mungu. “Kama sadaka yake ya kuteketezwa ataitoa katika kundi la kondoo au mbuzi, basi, atachagua dume asiye na dosari. Atamchinjia upande wa kaskazini wa madhabahu, mbele ya Mwenyezi-Mungu, hao makuhani, wazawa wa Aroni watainyunyizia madhabahu damu pande zake zote. Kisha huyo mtu atamkata vipandevipande, akivitenga kichwa pamoja na mafuta yake, na kuhani ataviweka kwenye moto juu ya madhabahu. Lakini matumbo na miguu yake ataviosha kwa maji. Kuhani ataiteketeza yote juu ya madhabahu. Hiyo ni sadaka ya kuteketezwa kwa moto yenye harufu nzuri ya kumpendeza Mwenyezi-Mungu. “Ikiwa anamtolea Mwenyezi-Mungu sadaka ya kuteketezwa ya ndege, basi, ataleta sadaka yake ya hua au kinda la njiwa. Kuhani atamleta ndege huyo kwenye madhabahu, atamkongonyoa kichwa chake na kukiteketeza juu ya madhabahu. Damu yake itanyunyiziwa ubavuni mwa madhabahu. Kibofu chake pamoja na uchafu wake ataviondoa na kutupa upande wa mashariki wa madhabahu ambako majivu huwekwa. Atamshika mabawa na kumpasua, lakini asimkate vipande viwili. Kisha, kuhani atamteketeza kwenye madhabahu, juu ya kuni. Hiyo ni sadaka ya kuteketezwa kwa moto yenye harufu nzuri ya kumpendeza Mwenyezi-Mungu.”

Shirikisha
Soma Walawi 1

Walawi 1:1-17 Swahili Revised Union Version (SRUV)

BWANA akamwita Musa, na kusema naye kutoka katika hema ya kukutania, akamwambia, Nena na wana wa Israeli, uwaambie, Mtu wa kwenu atakapomtolea BWANA matoleo, mtatoa matoleo yenu katika wanyama wa kufugwa, katika ng'ombe, kondoo na mbuzi. Ikawa matoleo yake ni sadaka ya kuteketezwa ya ng'ombe, atatoa ng'ombe dume mkamilifu; ataleta mlangoni pa hema ya kukutania, ili akubaliwe mbele ya BWANA. Kisha ataweka mkono wake juu ya kichwa cha hiyo sadaka ya kuteketezwa; nayo itakubaliwa kwa ajili yake, ili kufanya upatanisho kwa ajili yake. Naye atamchinja huyo ng'ombe mbele ya BWANA; kisha wana wa Haruni, hao makuhani, wataileta karibu hiyo damu, na kuinyunyiza damu yake kandokando katika madhabahu iliyo hapo mlangoni pa hema ya kukutania Kisha atachuna sadaka ya kuteketeza na kuikata vipande vyake. Kisha wana wa Haruni, watatia moto juu ya madhabahu, na kuzipanga kuni juu ya moto, kisha wana wa Haruni, makuhani, watazipanga kuni zilizo juu ya moto uliopo juu ya madhabahu; lakini matumbo yake, na miguu yake, ataiosha kwa maji; na huyo kuhani ataviteketeza vyote juu ya madhabahu, ili iwe sadaka ya kuteketezwa, dhabihu ya kusongezwa kwa njia ya moto, ya harufu ya kupendeza kwa BWANA. Na matoleo yake kwamba ni katika kundi, katika kondoo, au katika mbuzi, kuwa sadaka ya kuteketezwa; atatoa dume asiye na dosari. Naye atamchinja hapo upande wa madhabahu ulioelekea kaskazini mbele za BWANA; na wana wa Haruni, hao makuhani, watainyunyiza damu yake juu ya madhabahu pande zote. Kisha atamkata vipande vyake, pamoja na kichwa chake, na mafuta yake; kisha atavipanga vile vipande juu ya kuni zilizo juu ya madhabahu; lakini matumbo yake, na miguu yake, ataosha kwa maji; na huyo kuhani atavisongeza vyote na kuviteketeza juu ya madhabahu; ni sadaka ya kuteketezwa, dhabihu ya kusongezwa kwa njia ya moto, ya harufu ya kupendeza kwa BWANA. Ikawa matoleo yake atakayomtolea BWANA kuwa sadaka ya kuteketezwa, ni ya ndege, ndipo atakapoleta matoleo yake katika hua au katika makinda ya njiwa. Kisha kuhani atamleta karibu na madhabahu, naye atamkongonyoa kichwa, na kumteketeza kwa moto juu ya madhabahu; na damu yake itachuruzishwa kando ya madhabahu; kisha atakiondoa kile kibofu chake, pamoja na taka zake, na kukitupa kando ya madhabahu upande wa mashariki, mahali pa majivu; kisha atampasua na mabawa yake, lakini asimkate vipande viwili; kisha kuhani atamteketeza juu ya madhabahu, juu ya kuni zilizo juu ya moto; ni sadaka ya kuteketezwa, dhabihu ya kusongezwa kwa njia ya moto, ya harufu ya kupendeza kwa BWANA.

Shirikisha
Soma Walawi 1

Walawi 1:1-17 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

BWANA akamwita Musa, na kusema naye kutoka katika hema ya kukutania, akamwambia, Nena na wana wa Israeli, uwaambie, Mtu wa kwenu atakapomtolea BWANA matoleo, mtatoa matoleo yenu katika wanyama wa mifugo, katika ng’ombe na katika kondoo. Matoleo yake kwamba ni sadaka ya kuteketezwa ya ng’ombe, atatoa ng’ombe mume mkamilifu; ataleta mlangoni pa hema ya kukutania, ili akubaliwe mbele ya BWANA. Kisha ataweka mkono wake juu ya kichwa cha hiyo sadaka ya kuteketezwa; nayo itakubaliwa kwa ajili yake, ili kufanya upatanisho kwa ajili yake. Naye atamchinja huyo ng’ombe mbele ya BWANA; kisha wana wa Haruni, hao makuhani, wataileta karibu hiyo damu, na kuinyunyiza damu yake kando-kando katika madhabahu iliyo hapo mlangoni pa hema ya kukutania Kisha atachuna sadaka ya kuteketeza na kuikata vipande vyake. Kisha wana wa Haruni, watatia moto juu ya madhabahu, na kuzipanga kuni juu ya moto, kisha wana wa Haruni, makuhani, watazipanga kuni zilizo juu ya moto uliopo juu ya madhabahu; lakini matumbo yake, na miguu yake, ataiosha kwa maji; na huyo kuhani ataviteketeza vyote juu ya madhabahu, ili iwe sadaka ya kuteketezwa, dhabihu ya kusongezwa kwa njia ya moto, ya harufu ya kupendeza kwa BWANA. Na matoleo yake kwamba ni katika kundi, katika kondoo, au katika mbuzi, kuwa sadaka ya kuteketezwa; atatoa mume mkamilifu. Naye atamchinja hapo upande wa madhabahu ulioelekea kaskazini mbele za BWANA; na wana wa Haruni, hao makuhani, watainyunyiza damu yake juu ya madhabahu pande zote. Kisha atamkata vipande vyake, pamoja na kichwa chake, na mafuta yake; kisha atavipanga vile vipande juu ya kuni zilizo juu ya madhabahu; lakini matumbo yake, na miguu yake, ataosha kwa maji; na huyo kuhani atavisongeza vyote na kuviteketeza juu ya madhabahu; ni sadaka ya kuteketezwa, dhabihu ya kusongezwa kwa njia ya moto, ya harufu ya kupendeza kwa BWANA. Na matoleo yake atakayomtolea BWANA kuwa sadaka ya kuteketezwa, kwamba ni katika ndege, ndipo atakapoleta matoleo yake katika hua au katika makinda ya njiwa. Kisha kuhani atamleta karibu na madhabahu, naye atamkongonyoa kichwa, na kumteketeza kwa moto juu ya madhabahu; na damu yake itachuruzishwa kando ya madhabahu; kisha atakiondoa kile kibofu chake, pamoja na taka zake, na kukitupa kando ya madhabahu upande wa mashariki, mahali pa majivu; kisha atampasua na mabawa yake, lakini asimkate vipande viwili; kisha kuhani atamteketeza juu ya madhabahu, juu ya kuni zilizo juu ya moto; ni sadaka ya kuteketezwa, dhabihu ya kusongezwa kwa njia ya moto, ya harufu ya kupendeza kwa BWANA.

Shirikisha
Soma Walawi 1

Walawi 1:1-17 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)

BWANA akamwita Musa na kusema naye kutoka Hema la Kukutania, akamwambia, “Sema na Waisraeli, uwaambie, ‘Yeyote miongoni mwenu anayeleta sadaka kwa BWANA, alete mnyama kama sadaka yake kutoka kundi lake la ngʼombe, au la kondoo na mbuzi. “ ‘Ikiwa sadaka hiyo ni sadaka ya kuteketezwa kutoka kundi la ngʼombe, atamtoa ngʼombe dume asiye na dosari. Ni lazima amlete kwenye ingilio la Hema la Kukutania ili aweze kukubalika kwa BWANA. Ataweka mkono wake juu ya kichwa cha sadaka ya kuteketezwa, nayo itakubaliwa kwa niaba yake ili kufanya upatanisho kwa ajili yake. Atamchinja yule fahali mchanga mbele za BWANA, kisha wana wa Haruni walio makuhani wataleta damu na kuinyunyiza pande zote za madhabahu yaliyo penye ingilio la Hema la Kukutania. Ataichuna hiyo sadaka ya kuteketezwa na kuikata vipande vipande. Wana wa Haruni kuhani wataweka moto juu ya madhabahu na kupanga kuni juu ya huo moto. Kisha hao wana wa Haruni walio makuhani watapanga vile vipande vya nyama, pamoja na kichwa na mafuta ya huyo mnyama, juu ya zile kuni zinazowaka juu ya madhabahu. Ataziosha sehemu za ndani za yule mnyama pamoja na miguu yake kwa maji; naye kuhani atavichoma vyote juu ya madhabahu. Hii ni sadaka ya kuteketezwa, sadaka iliyotolewa kwa moto, yenye harufu nzuri ya kumpendeza BWANA. “ ‘Ikiwa sadaka ni sadaka ya kuteketezwa kutoka kundi la kondoo au mbuzi, atamtoa dume asiye na dosari. Atamchinjia upande wa kaskazini wa madhabahu mbele za BWANA, nao wana wa Haruni walio makuhani watanyunyizia damu yake pande zote za madhabahu. Atamkata vipande vipande, naye kuhani atavipanga, pamoja na kichwa na mafuta ya mnyama juu ya zile kuni zinazowaka juu ya madhabahu. Ataosha sehemu za ndani na miguu kwa maji, naye kuhani atavileta vyote na kuvichoma juu ya madhabahu. Hii ni sadaka ya kuteketezwa, sadaka iliyotolewa kwa moto, harufu nzuri ya kumpendeza BWANA. “ ‘Ikiwa sadaka inayotolewa kwa BWANA ni sadaka ya kuteketezwa ya ndege, atamtoa hua au kinda la njiwa. Kuhani atamleta kwenye madhabahu, naye atamvunja shingo na kumnyofoa kichwa na kumchoma juu ya madhabahu. Damu yake itachuruzishwa ubavuni mwa madhabahu. Ataondoa kifuko cha chakula pamoja na uchafu wake na kuvitupa upande wa mashariki wa madhabahu, mahali pale penye majivu. Atampasua na kumweka wazi katika mabawa yake, lakini asimwachanishe kabisa, kisha kuhani ataichoma juu ya zile kuni zinazowaka juu ya madhabahu. Hii ni sadaka ya kuteketezwa, sadaka iliyotolewa kwa moto, harufu nzuri ya kumpendeza BWANA.

Shirikisha
Soma Walawi 1