Maombolezo 3:1-66
Maombolezo 3:1-66 Biblia Habari Njema (BHN)
Mimi ni mtu niliyepata mateso kwa fimbo ya ghadhabu yake Mungu. Amenichukua akanipeleka mpaka gizani kusiko na mwanga. Amenyosha mkono wake dhidi yangu mimi tu, akanichapa tena na tena mchana kutwa. Amenichakaza ngozi na nyama, mifupa yangu ameivunja. Amenizingira na kunizungushia uchungu na mateso. Amenikalisha gizani kama watu waliokufa zamani. Amenizungushia ukuta nisitoroke, amenifunga kwa minyororo mizito. Ingawa naita na kulilia msaada anaizuia sala yangu isimfikie. Njia zangu ameziziba kwa mawe makubwa amevipotosha vichochoro vyangu. Yeye ni kama dubu anayenivizia; ni kama simba aliyejificha. Alinifukuza njiani mwangu, akanilemaza na kuniacha mkiwa. Aliuvuta upinde wake, akanilenga mshale wake. Alinichoma moyoni kwa mishale, kutoka katika podo lake. Nimekuwa kitu cha dhihaka kwa watu wote, mchana kutwa nimekuwa mtu wa kuzomewa. Amenijaza taabu, akanishibisha uchungu. Amenisagisha meno katika mawe, akanifanya nigaegae majivuni. Moyo wangu haujui tena amani, kwangu furaha ni kitu kigeni. Nimewaza “Nimekata tamaa kabisa, tumaini langu kwa Mwenyezi-Mungu limetoweka.” Kukumbuka taabu na kutangatanga kwangu kwanipa uchungu kama wa nyongo. Nayafikiria hayo daima, nayo roho yangu imejaa majonzi. Lakini nakumbuka jambo hili moja, nami ninalo tumaini: Kwamba fadhili za Mwenyezi-Mungu hazikomi, huruma zake hazina mwisho. Kila kunapokucha ni mpya kabisa, uaminifu wake ni mkuu mno. Mwenyezi-Mungu ndiye hazina yangu hivyo nitamwekea tumaini langu. Mwenyezi-Mungu ni mwema kwa wanaomtegemea, ni mwema kwa wote wanaomtafuta. Ni vema mtu kungojea kwa saburi ukombozi utokao kwa Mwenyezi-Mungu. Ni vema mtu kujifunza uvumilivu tangu wakati wa ujana wake. Heri kukaa peke na kimya, mazito yanapompata kutoka kwa Mungu. Yampasa kuinama na kujinyenyekesha, huenda ikawa tumaini bado lipo. Yampasa kumgeuzia shavu mwenye kumpiga, na kuwa tayari kupokea matusi yake. Mwenyezi-Mungu hatatutupa milele. Ingawa atufanya tuhuzunike, atakuwa na huruma tena kadiri ya wingi wa fadhili zake. Yeye hapendelei kuwatesa wala kuwahuzunisha wanadamu. Wafungwa wote nchini wanapodhulumiwa na kupondwa; haki za binadamu zinapopotoshwa mbele yake Mungu Mkuu, kesi ya mtu inapopotoshwa mahakamani, je, Mwenyezi-Mungu haoni hayo? Nani awezaye kuamuru kitu kifanyike Mwenyezi-Mungu asipopanga iwe hivyo? Maafa na mema hutokea tu kwa amri yake Mungu Mkuu. Kwa nini mtu anung'unike, ikiwa ameadhibiwa kwa dhambi zake? Na tupime na kuchunguza mwenendo wetu, tupate kumrudia Mwenyezi-Mungu. Tumfungulie Mungu huko mbinguni mioyo yetu na kumwomba: “Sisi tulikukosea na kukuasi nawe bado hujatusamehe. “Umejizungushia hasira yako ukatufuatia, ukatuua bila huruma. Umejizungushia wingu zito, sala yeyote isiweze kupenya humo. Umetufanya kuwa takataka na uchafu miongoni mwa watu wa mataifa. “Maadui zetu wote wanatuzomea. Kitisho na hofu vimetuandama, tumepatwa na maafa na maangamizi. Macho yangu yabubujika mito ya machozi kwa sababu ya kuangamizwa kwa watu wangu. “Machozi yatanitoka bila kikomo, mpaka Mwenyezi-Mungu kutoka huko mbinguni aangalie chini na kuona. Nalia na kujaa majonzi, kuona yaliyowapata kina mama wa mji wangu. “Nimewindwa kama ndege na hao wanichukiao bila sababu. Walinitupa shimoni nikiwa hai na juu yangu wakarundika mawe. Maji yalianza kunifunika kichwa, nami nikafikiri, ‘Huu ni mwisho wangu.’ “Kutoka chini shimoni nilikulilia ee Mwenyezi-Mungu. Wewe umenisikia nikikulilia: ‘Usiache kusikia kilio changu cha msaada bali unipatie nafuu.’ Nilipokuita ulinijia karibu ukaniambia, ‘Usiogope!’ “Umenitetea katika kisa changu ee Mwenyezi-Mungu, umeyakomboa maisha yangu. Umeuona uovu niliotendewa ee Mwenyezi-Mungu, uniamulie kwa wema kisa changu. Umeuona uovu wa maadui zangu, na mipango yao yote ya hila dhidi yangu. “Umesikia matukano yao ee Mwenyezi-Mungu, na mipango yao yote ya hila dhidi yangu. Maneno na mawazo ya maadui zangu siku nzima ni juu ya kuniangamiza mimi. Wakati wote, wamekaa au wanakwenda, mimi ndiye wanayemzomea. Uwalipize, ee Mwenyezi-Mungu kadiri ya hayo matendo yao, kadiri ya mambo waliyotenda wenyewe. Uipumbaze mioyo yao, na laana yako iwashukie. Uwafuatie kwa hasira, uwaangamize, uwafanye watoweke ulimwenguni.”
Maombolezo 3:1-66 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Mimi ni mtu aliyeona mateso Kwa fimbo ya ghadhabu yake. Ameniongoza na kunipeleka katika giza Wala si katika nuru. Hakika juu yangu augeuza mkono wake Mara kwa mara mchana wote. Amechakaza ngozi yangu na nyama yangu; Ameivunja mifupa yangu. Amejenga boma juu yangu, Na kunizungusha uchungu na uchovu. Amenikalisha penye giza, Kama watu waliokufa zamani. Amenizinga pande zote hata siwezi kutoka; Amenifunga kwa mnyororo mzito. Naam, nikilia na kuomba msaada, Huyapinga maombi yangu. Ameziziba njia zangu kwa mawe yaliyochongwa; Ameyapotosha mapito yangu. Alivyo kwangu ni kama dubu aoteaye, Kama simba aliye mafichoni. Amezigeuza njia zangu, na kuniraruararua; Amenifanya ukiwa. Ameupinda upinde wake, Na kunifanya niwe shabaha kwa mshale. Amenichoma viuno Kwa mishale ya podo lake. Nimekuwa dhihaka kwa watu wangu wote; Wimbo wao mchana kutwa. Amenijaza uchungu, Amenikinaisha kwa pakanga. Amenivunja meno kwa changarawe; Amenifunika majivu. Umeniweka nafsi yangu mbali na amani; Nikasahau kufanikiwa. Nikasema, Nguvu zangu zimepotea, Na tumaini langu kwa BWANA. Kumbuka mateso yangu, na msiba wangu, Pakanga na nyongo. Nafsi yangu ingali ikiyakumbuka hayo, Nayo imeinama ndani yangu. Najikumbusha neno hili, Kwa hiyo nina matumaini. Ni huruma za BWANA kwamba hatuangamii, Kwa kuwa rehema zake hazikomi. Ni mpya kila siku asubuhi; Uaminifu wako ni mkuu. BWANA ndiye fungu langu, husema nafsi yangu, Kwa hiyo nitamtumaini yeye. BWANA ni mwema kwa hao wamngojeao, Kwa hiyo nafsi imtafutayo. Ni vema mtu autarajie wokovu wa BWANA Na kumngojea kwa utulivu. Ni vema mwanadamu aichukue nira Wakati wa ujana wake. Na akae peke yake na kunyamaza kimya; Kwa sababu Bwana ameweka hayo juu yake. Na atie kinywa chake mavumbini; Ikiwa yamkini liko tumaini. Na amwelekezee yule ampigaye shavu lake; Ashibishwe mashutumu. Kwa kuwa Bwana hatamtupa mtu Hata milele. Maana ajapomhuzunisha atamrehemu, Kwa kadiri ya wingi wa huruma zake. Maana moyo wake hapendi kuwatesa wanadamu. Wala kuwahuzunisha. Wafungwa wote wa duniani Kupondwa chini kwa miguu, Kuipotosha hukumu ya mtu Mbele zake Aliye Juu, Na kumnyima mtu haki yake, Hayo Bwana hayaridhii kabisa. Ni nani asemaye neno nalo likafanyika, Ikiwa Bwana hakuliagiza? Je! Katika kinywa chake Aliye Juu Hayatoki maovu na mema? Mbona anung'unika mwanadamu aliye hai Mtu akiadhibiwa kwa dhambi zake? Na tuchunguze njia zetu na kuzijaribu, Na kumrudia BWANA tena. Na tumwinulie Mungu aliye mbinguni Mioyo yetu na mikono. Sisi tumekosa na kuasi; Wewe hukusamehe. Umetufunika kwa hasira na kutufuatia; Umeua, wala hukuona huruma. Umejifunika nafsi yako kwa wingu, Maombi yetu yasipite. Umetufanya kuwa takataka, na vifusi Katikati ya mataifa. Juu yetu adui zetu wote Wametupanulia vinywa vyao. Hofu imetujilia na shimo, Ukiwa na uharibifu. Jicho langu lachuruzika mito ya machozi Kwa sababu ya kuharibiwa kwa binti zangu. Jicho langu latoka machozi lisikome, Wala haliachi; Hata BWANA atakapoangalia Na kutazama toka mbinguni. Jicho langu lanitia huzuni nafsini mwangu, Kwa ajili ya kuangamizwa kwa binti wa watu wangu. Walio adui zangu bila sababu Wameniwinda sana kama ndege; Wameukatilia mbali uhai wangu gerezani, Na kutupa jiwe juu yangu. Maji mengi yalipita juu ya kichwa changu, Nikasema, Nimekatiliwa mbali. Nililiitia jina lako, BWANA, kutoka lile shimo Liendalo chini kabisa. Ukaisikia sauti yangu; usifiche sikio lako Ili usisikie pumzi yangu, kwa kilio changu. Ulinikaribia siku ile nilipokulilia; Ukasema, Usiogope. Ee BWANA umenitetea katika kisa cha nafsi yangu; Umeukomboa uhai wangu. Umekuona kudhulumiwa kwangu, Ee BWANA; Unihukumie neno langu. Umekiona kisasi chao chote, Na mashauri yao yote juu yangu. Ee BWANA, umeyasikia matukano yao, Na mashauri yao yote juu yangu; Midomo yao walioinuka juu yangu Na maazimio yao juu yangu mchana kutwa. Uangalie kuketi kwao, na kuinuka kwao; Wimbo wao ndio mimi. Utawalipa malipo, Ee BWANA, Sawasawa na kazi ya mikono yao. Utawapa ushupavu wa moyo; Laana yako juu yao. Utawafuatia kwa hasira, na kuwaangamiza Wasiwe tena chini ya mbingu za BWANA.
Maombolezo 3:1-66 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Mimi ni mtu aliyeona mateso Kwa fimbo ya ghadhabu yake. Ameniongoza na kuniendesha katika giza Wala si katika nuru. Hakika juu yangu augeuza mkono wake Mara kwa mara mchana wote. Amechakaza nyama yangu na ngozi yangu; Ameivunja mifupa yangu. Amejenga boma juu yangu, Na kunizungusha uchungu na uchovu. Amenikalisha penye giza, Kama watu waliokufa zamani. Amenizinga pande zote hata siwezi kutoka; Ameufanya mnyororo wangu mzito. Naam, nikilia na kuomba msaada, Huyapinga maombi yangu. Ameziziba njia zangu kwa mawe yaliyochongwa; Ameyapotosha mapito yangu. Alivyo kwangu ni kama dubu aoteaye, Kama simba aliye mafichoni. Amezigeuza njia zangu, na kunirarua-rarua; Amenifanya ukiwa. Ameupinda upinde wake, Na kunifanya niwe shabaha kwa mshale. Amenichoma viuno Kwa mishale ya podo lake. Nimekuwa dhihaka kwa watu wangu wote; Wimbo wao mchana kutwa. Amenijaza uchungu, Amenikinaisha kwa pakanga. Amenivunja meno kwa changarawe; Amenifunika majivu. Umeniweka nafsi yangu mbali na amani; Nikasahau kufanikiwa. Nikasema, Nguvu zangu zimepotea, Na tumaini langu kwa BWANA. Kumbuka mateso yangu, na msiba wangu, Pakanga na nyongo. Nafsi yangu ikali ikiyakumbuka hayo, Nayo imeinama ndani yangu. Najikumbusha neno hili, Kwa hiyo nina matumaini. Ni huruma za BWANA kwamba hatuangamii, Kwa kuwa rehema zake hazikomi. Ni mpya kila siku asubuhi; Uaminifu wako ni mkuu. BWANA ndiye fungu langu, husema nafsi yangu, Kwa hiyo nitamtumaini yeye. BWANA ni mwema kwa hao wamngojeao, Kwa hiyo nafsi imtafutayo. Ni vema mtu autarajie wokovu wa BWANA Na kumngojea kwa utulivu. Ni vema mwanadamu aichukue nira Wakati wa ujana wake. Na akae peke yake na kunyamaza kimya; Kwa sababu Bwana ameweka hayo juu yake. Na atie kinywa chake mavumbini; Ikiwa yamkini liko tumaini. Na amwelekezee yule ampigaye shavu lake; Ashibishwe mashutumu. Kwa kuwa Bwana hatamtupa mtu Hata milele. Maana ajapomhuzunisha atamrehemu, Kwa kadiri ya wingi wa huruma zake. Maana moyo wake hapendi kuwatesa wanadamu. Wala kuwahuzunisha. Kuwaseta chini kwa miguu Wafungwa wote wa duniani, Kuipotosha hukumu ya mtu Mbele zake Aliye juu, Na kumnyima mtu haki yake, Hayo Bwana hayaridhii kabisa. Ni nani asemaye neno nalo likafanyika, Ikiwa Bwana hakuliagiza? Je! Katika kinywa chake Aliye juu Hayatoki maovu na mema? Mbona anung’unika mwanadamu aliye hai Mtu akiadhibiwa kwa dhambi zake? Na tuchunguze njia zetu na kuzijaribu, Na kumrudia BWANA tena. Na tumwinulie Mungu aliye mbinguni Mioyo yetu na mikono. Sisi tumekosa na kuasi; Wewe hukusamehe. Umetufunika kwa hasira na kutufuatia; Umeua, wala hukuona huruma. Umejifunika nafsi yako kwa wingu, Maombi yetu yasipite. Umetufanya kuwa takataka, na vifusi Katikati ya mataifa. Juu yetu adui zetu wote Wametupanulia vinywa vyao. Hofu imetujilia na shimo, Ukiwa na uharibifu. Jicho langu lachuruzika mito ya maji Kwa ajili ya uvunjifu wa binti ya watu wangu. Jicho langu latoka machozi lisikome, Wala haliachi; Hata BWANA atakapoangalia Na kutazama toka mbinguni. Jicho langu lanitia huzuni nafsini mwangu, Kwa sababu ya binti zote za mji wangu. Walio adui zangu bila sababu Wameniwinda sana kama ndege; Wameukatilia mbali uhai wangu gerezani, Na kutupa jiwe juu yangu. Maji mengi yalipita juu ya kichwa changu, Nikasema, Nimekatiliwa mbali. Naliliitia jina lako, BWANA, kutoka lile shimo Liendalo chini kabisa. Ukaisikia sauti yangu; usifiche sikio lako Ili usisikie pumzi yangu, kwa kilio changu. Ulinikaribia siku ile nilipokulilia; Ukasema, Usiogope. Ee BWANA umenitetea mateto ya nafsi yangu; Umeukomboa uhai wangu. Umekuona kudhulumiwa kwangu, Ee BWANA; Unihukumie neno langu. Umekiona kisasi chao chote, Na mashauri yao yote juu yangu. Ee BWANA, umeyasikia matukano yao, Na mashauri yao yote juu yangu; Midomo yao walioinuka juu yangu Na maazimio yao juu yangu mchana kutwa. Uangalie kuketi kwao, na kuinuka kwao; Wimbo wao ndio mimi. Utawalipa malipo, Ee BWANA, Sawasawa na kazi ya mikono yao. Utawapa ushupavu wa moyo; Laana yako juu yao. Utawafuatia kwa hasira, na kuwaangamiza Wasiwe tena chini ya mbingu za BWANA.
Maombolezo 3:1-66 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Mimi ndiye mtu aliyeona mateso kwa fimbo ya ghadhabu yake. Amenifukuzia mbali na kunifanya nitembee gizani wala si katika nuru; hakika, amegeuza mkono wake dhidi yangu tena na tena, mchana kutwa. Amefanya ngozi yangu na nyama yangu kuchakaa na ameivunja mifupa yangu. Amenizingira na kunizunguka kwa uchungu na taabu. Amenifanya niishi gizani kama wale waliokufa. Amenizungushia ukuta ili nisiweze kutoroka, amenifunga kwa minyororo mizito. Hata ninapoita au kulia ili kuomba msaada, anakataa kupokea maombi yangu. Ameizuia njia yangu kwa mapande ya mawe, amepotosha njia zangu. Kama dubu aviziaye, kama simba mafichoni, ameniburuta kutoka njiani, akanirarua na kuniacha bila msaada. Amevuta upinde wake na kunifanya mimi niwe lengo kwa ajili ya mishale yake. Alinichoma moyo wangu kwa mishale iliyotoka kwenye podo lake. Nimekuwa kichekesho kwa watu wangu wote, wananidhihaki kwa wimbo mchana kutwa. Amenijaza kwa majani machungu na kunishibisha kwa nyongo. Amevunja meno yangu kwa changarawe, amenikanyagia mavumbini. Amani yangu imeondolewa, nimesahau kufanikiwa ni nini. Kwa hiyo nasema, “Fahari yangu imeondoka na yale yote niliyokuwa nimetarajia kutoka kwa BWANA.” Nayakumbuka mateso yangu na kutangatanga kwangu, uchungu na nyongo. Ninayakumbuka vyema, nayo nafsi yangu imezimia ndani yangu. Hata hivyo najikumbusha neno hili na kwa hiyo ninalo tumaini. Kwa sababu ya upendo mkuu wa BWANA, hatuangamii, kwa kuwa huruma zake hazikomi kamwe. Ni mpya kila asubuhi, uaminifu wako ni mkuu. Nimeiambia nafsi yangu, “BWANA ni fungu langu, kwa hiyo nitamngojea.” BWANA ni mwema kwa wale wanaomtumaini, na kwa yule anayemtafuta; ni vyema kungojea kwa utulivu kwa ajili ya wokovu wa BWANA. Ni vyema mtu kuchukua nira bado angali kijana. Na akae peke yake awe kimya, kwa maana BWANA ameiweka juu yake. Hata azike uso wake mavumbini bado tumaini litakuwepo. Na atoe shavu lake kwa yule ampigaye, na ajazwe na aibu. Kwa kuwa watu hawakatiliwi mbali na Bwana milele. Ingawa huleta huzuni, ataonesha huruma, kwa kuwa upendo wake usiokoma ni mkuu. Kwa maana hapendi kuwaletea mateso au huzuni watoto wa wanadamu. Kuwaponda chini ya nyayo wafungwa wote katika nchi, Kumnyima mtu haki zake mbele za Aliye Juu Sana, kumnyima mtu haki: Je, Bwana asione mambo kama haya? Nani awezaye kusema nalo likatendeka kama Bwana hajaamuru? Je, si ni kwenye kinywa cha Aliye Juu Sana ndiko yatokako maafa na mambo mema? Je, mwanadamu yeyote aliye hai aweza kulalamika wakati anapoadhibiwa kwa ajili ya dhambi zake? Tuzichunguze njia zetu na kuzijaribu, na tumrudie BWANA Mungu. Tuinue mioyo yetu pamoja na mikono yetu kwa Mungu mbinguni, na tuseme: “Tumetenda dhambi na kuasi nawe hujasamehe. “Umejifunika mwenyewe kwa hasira na kutufuatilia; umetuchinja bila huruma. Unajifunika mwenyewe kwa wingu, ili pasiwe na ombi litakaloweza kupenya. Umetufanya takataka na uchafu miongoni mwa mataifa. “Adui zetu wote wamefumbua vinywa vyao wazi dhidi yetu. Tumeteseka kwa hofu kuu na shida ya ghafula, uharibifu na maangamizi.” Vijito vya machozi vinatiririka kutoka machoni mwangu, kwa sababu watu wangu wameangamizwa. Macho yangu yatatiririka machozi bila kukoma, bila kupata nafuu, hadi BWANA atazame chini kutoka mbinguni na kuona. Lile ninaloliona huniletea huzuni nafsini kwa sababu ya wanawake wote wa mji wangu. Wale waliokuwa adui zangu bila sababu wameniwinda kama ndege. Walijaribu kukomesha maisha yangu ndani ya shimo na kunitupia mawe; maji yalifunika juu ya kichwa changu, nami nikafikiri nilikuwa karibu kukatiliwa mbali. Nililiitia jina lako, Ee BWANA, kutoka vina vya shimo. Ulisikia ombi langu: “Usikizibie masikio yako kilio changu nikuombapo msaada.” Ulikuja karibu nilipokuita, nawe ukasema, “Usiogope.” Ee Bwana, ulichukua shauri langu, ukaukomboa uhai wangu. Umeona, Ee BWANA, ubaya niliotendewa. Tetea shauri langu! Umeona kina cha kisasi chao, mashauri yao yote mabaya dhidi yangu. Ee BWANA, umesikia matukano yao, mashauri yao yote mabaya dhidi yangu: kile adui zangu wanachonongʼona na kunungʼunikia dhidi yangu mchana kutwa. Watazame! Wakiwa wameketi au wamesimama, wananidhihaki katika nyimbo zao. Uwalipe kile wanachostahili, Ee BWANA, kwa yale ambayo mikono yao imetenda. Weka pazia juu ya mioyo yao, laana yako na iwe juu yao! Wafuatilie katika hasira na uwaangamize chini ya mbingu za BWANA.