Yuda 1:8-16
Yuda 1:8-16 Biblia Habari Njema (BHN)
Hivyo ndivyo pia walivyo watu hawa. Ndoto zao huwaongoza katika kuichafua miili yao wenyewe, kuyadharau mamlaka ya Mungu na kuvitukana viumbe vitukufu vya huko juu. Hata Mikaeli, malaika mkuu, hakufanya hivyo. Katika ule ubishi kati yake na Ibilisi juu ya mwili wa Mose, Mikaeli hakuthubutu kumhukumu Ibilisi kwa matusi, ila alisema: “Bwana mwenyewe na akukaripie.” Lakini watu hawa hutukana chochote wasichokielewa; wataangamizwa kwa mambo yaleyale wanayoyajua kwa silika kama wajuavyo wanyama wasio na akili. Ole wao! Watu hao wamefuata mwenendo uleule wa Kaini. Kwa ajili ya fedha, wamejiingiza katika mkosi uleule wa Balaamu. Wameasi kama Kora alivyoasi na wameangamizwa kama yeye alivyoangamizwa. Kwa makelele yao yasiyo na adabu, na kwa kujipendelea wao wenyewe, watu hao ni kama madoa machafu kwenye karamu mnazoshiriki kwa upendo. Wako kama mawingu yasiyo na mvua yanayopeperushwa na upepo. Wao ni kama miti iliyopukutika isiyozaa matunda, iliyokufa kabisa, iliyong'olewa. Watu hao ni kama mawimbi makali ya bahari, na matendo yao ya aibu yanatoka kama povu. Wao ni kama nyota zinazotangatanga ambazo zimewekewa milele mahali pa giza kuu. Naye Henoki, ambaye ni babu wa saba tangu Adamu, alibashiri hivi juu ya watu hao: “Sikilizeni! Bwana anakuja pamoja na maelfu ya malaika wake watakatifu kuwahukumu watu wote, na kuwaadhibu wote wasiomcha Mungu kwa ajili ya matendo yao yote maovu waliyotenda bila kumjali Mungu, na kwa ajili ya maneno yote mabaya ambayo watu waovu walimkashifu nayo.” Watu hawa hunung'unika daima, hulalamika, hufuata tamaa zao mbaya, hujigamba na kuwasifu watu wengine mno kwa faida yao wenyewe.
Yuda 1:8-16 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Kadhalika na hawa, katika kuota kwao, huutia mwili uchafu, hukataa kutawaliwa, na kuyatukana matukufu. Lakini Mikaeli, malaika mkuu, aliposhindana na Ibilisi, na kuhojiana naye kwa ajili ya mwili wa Musa, hakuthubutu kumshitaki kwa kumlaumu, bali alisema, Bwana na akukemee. Lakini watu hawa huyatukana mambo wasiyoyajua, na mambo wayatambuayo kwa asili wajiharibu kwayo kama wanyama wasio na akili. Ole wao! Kwa sababu walikwenda katika njia ya Kaini, na kulifuata kosa la Balaamu pasipo kujizuia, kwa ajili ya malipo, nao wameangamia katika maasi ya Kora. Watu hawa ni miamba yenye hatari katika karamu zenu za upendo walapo karamu pamoja nanyi, wakijilisha pasipo hofu; ni mawingu yasiyo na maji, yachukuliwayo na upepo; ni miti iliyopukutika, isiyo na matunda, iliyokufa mara mbili, na kung'olewa kabisa; ni mawimbi ya bahari yasiyozuilika, yakitoa aibu yao wenyewe kama povu; ni nyota zipoteazo, ambao weusi wa giza ndio akiba yao waliowekewa milele. Na Henoko, mtu wa kizazi cha saba toka kwa Adamu, alitoa maneno ya unabii juu ya hao, akisema, Angalia, Bwana yuaja na watakatifu wake, maelfu kwa maelfu, ili afanye hukumu juu ya watu wote, na kuwaadhibu wote wasiomcha Mungu, kwa ajili ya kazi zao zote za upotevu walizozitenda bila kumcha Mungu, na kwa ajili ya maneno yote maovu ambayo hao wenye dhambi wasiomcha Mungu wameyanena juu yake. Watu hawa ni wenye kunung'unika, wenye kulalamika, waendao kwa tamaa zao, na vinywa vyao vyanena maneno makuu mno ya kiburi, wakipendelea watu wenye cheo kwa ajili ya faida.
Yuda 1:8-16 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Kadhalika na hawa, katika kuota kwao, huutia mwili uchafu, hukataa kutawaliwa, na kuyatukana matukufu. Lakini Mikaeli, malaika mkuu, aliposhindana na Ibilisi, na kuhojiana naye kwa ajili ya mwili wa Musa, hakuthubutu kumshitaki kwa kumlaumu, bali alisema, Bwana na akukemee. Lakini watu hawa huyatukana mambo wasiyoyajua, na mambo wayatambuayo kwa asili wajiharibu kwayo kama wanyama wasio na akili. Ole wao! Kwa sababu walikwenda katika njia ya Kaini, na kulifuata kosa la Balaamu pasipo kujizuia, kwa ajili ya ujira, nao wameangamia katika maasi ya Kora. Watu hawa ni miamba yenye hatari katika karamu zenu za upendo walapo karamu pamoja nanyi, wakijilisha pasipo hofu; ni mawingu yasiyo na maji, yachukuliwayo na upepo; ni miti iliyopukutika, isiyo na matunda, iliyokufa mara mbili, na kung’olewa kabisa; ni mawimbi ya bahari yasiyozuilika, yakitoa aibu yao wenyewe kama povu; ni nyota zipoteazo, ambao weusi wa giza ndio akiba yao waliowekewa milele. Na Henoko, mtu wa saba baada ya Adamu, alitoa maneno ya unabii juu ya hao, akisema, Angalia, Bwana alikuja na watakatifu wake, maelfu maelfu, ili afanye hukumu juu ya watu wote, na kuwaadhibisha wote wasiomcha Mungu, kwa ajili ya kazi zao zote za upotevu walizozitenda bila kumcha Mungu, na kwa ajili ya maneno magumu yote ambayo hao wenye dhambi wasiomcha Mungu wameyanena juu yake. Watu hawa ni wenye kunung’unika, wenye kulalamika, waendao kwa tamaa zao, na vinywa vyao vyanena maneno makuu mno ya kiburi, wakipendelea watu wenye cheo kwa ajili ya faida.
Yuda 1:8-16 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Vivyo hivyo, hawa waotao ndoto huutia mwili unajisi, hukataa kuwa chini ya mamlaka na kunena mabaya juu ya wenye mamlaka. Lakini hata malaika mkuu Mikaeli alipokuwa anashindana na ibilisi kuhusu mwili wa Musa, hakuthubutu kumlaumu, bali alimwambia, “Bwana na akukemee!” Lakini watu hawa hunena mabaya dhidi ya mambo wasiyoyafahamu. Na katika mambo yale wanayoyafahamu kwa hisia kama wanyama wasio na akili, hayo ndiyo hasa yatakayowaangamiza. Ole wao! Kwa kuwa wanaifuata njia ya Kaini, wamekimbilia faida katika kosa la Balaamu na kuangamia katika uasi wa Kora. Watu hawa ni dosari katika karamu zenu za upendo, wakila pamoja nanyi bila hofu, wakijilisha wenyewe tu. Wao ni mawingu yasiyokuwa na maji, yakichukuliwa na upepo, miti isiyo na matunda wakati wa mapukutiko, ambayo hunyauka, iliyokufa mara mbili na kungʼolewa kabisa. Wao ni mawimbi makali ya bahari, yakitoa povu la aibu yao wenyewe, ni nyota zipoteazo, ambao weusi wa giza ndio akiba waliowekewa milele. Henoko, mtu wa saba kuanzia Adamu, alitoa unabii kuhusu watu hawa, akisema: “Tazama, Bwana anakuja pamoja na maelfu kwa maelfu ya watakatifu wake, ili kumhukumu kila mmoja na kuwapatiliza wote wasiomcha Mungu kwa matendo yao yote ya uasi waliyoyatenda, pamoja na maneno yote ya kuchukiza ambayo wenye dhambi wamesema dhidi yake.” Watu hawa ni wenye kunungʼunika na wenye kutafuta makosa; wao hufuata tamaa zao mbovu; hujisifu kwa maneno makuu, na kuwasifu mno watu wengine kwa faida yao wenyewe.