Yoshua 9:1-26
Yoshua 9:1-26 Biblia Habari Njema (BHN)
Wafalme wote waliokuwa ngambo ya mto Yordani katika nchi ya milimani na kwenye tambarare na eneo lote la pwani ya bahari ya Mediteranea kuelekea Lebanoni, Wahiti, Waamori, Wakanaani, Waperizi, Wahivi na Wayebusi, waliposikia habari za Waisraeli, wakakusanyika pamoja kwa nia moja ili kupigana vita na Yoshua na Waisraeli. Lakini wakazi wa Gibeoni walipopata habari juu ya jinsi Yoshua alivyoitenda miji ya Yeriko na Ai, waliamua kutumia hila. Wakatayarisha vyakula, wakapakiza magunia yaliyochakaa juu ya punda wao, viriba vilivyochakaa na kushonwa; wakavaa viatu, nguo zilizochakaa na vyakula vyao vyote vilikuwa vikavu vilivyoota ukungu. Basi, wakamwendea Yoshua kambini Gilgali, wakamwambia yeye na Waisraeli, “Sisi tumetoka nchi ya mbali; tafadhali tunaomba mfanye agano nasi.” Lakini Waisraeli wakawajibu hao Wahivi, “Tunawezaje kufanya agano nanyi? Labda nyinyi mnaishi karibu nasi.” Nao wakamwambia Yoshua, “Sisi tu watumishi wako.” Naye Yoshua akawauliza, “Nyinyi ni akina nani, na mnatoka wapi?” Wakamjibu, “Sisi, watumishi wako, tumetoka nchi ya mbali na tumekuja kwa maana tumesikia sifa za jina la Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu; tulipata habari za umaarufu wake na yote aliyoyafanya nchini Misri. Tumesikia yote aliyowatenda wafalme wawili wa Waamori waliokuwa ngambo ya mto Yordani, mfalme Sihoni wa Heshboni na mfalme Ogu wa Bashani aliyekaa huko Ashtarothi. Ndipo wazee wetu na wananchi wote wa nchi yetu, wakatuambia, tuchukue posho ya safari, tuje kukutana nanyi na kuwaambia kwamba sisi ni watumishi wenu; tafadhali fanyeni agano nasi. Tazama mikate yetu ambayo ilikuwa bado moto tulipoichukua wakati tulipoondoka kwetu, lakini sasa imekauka na kuota ukungu. Viriba hivi tulivijaza maji vikiwa vipya, lakini sasa vimepasukapasuka. Hata mavazi na viatu vyetu vimechakaa, kwani safari ilikuwa ndefu sana.” Hivyo, Waisraeli wakachukua vyakula vyao, bila ya kumwuliza shauri Mwenyezi-Mungu. Yoshua akafanya nao mkataba wa amani; akafanya agano kwamba atawaruhusu kuishi. Viongozi wa jumuiya ya Israeli wakawaapia kutekeleza mapatano hayo. Siku tatu baada ya kufanya agano nao, Waisraeli wakagundua kwamba watu hao walikuwa jirani zao na waliishi miongoni mwao. Basi, Waisraeli wakafunga safari, baada ya siku ya tatu wakafika katika miji yao. Miji hiyo ilikuwa Gibeoni, Kefira, Beerothi na Kiriath-yearimu. Lakini Waisraeli hawakuwaua, maana viongozi wa jumuiya ya Israeli walikuwa wamewaapia kwa jina la Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli. Hivyo basi, jumuiya yote ikawanungunikia viongozi wao. Lakini viongozi wa Waisraeli wakaiambia jumuiya ya watu wao, “Kwa vile tumewaapia kwa jina la Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, sasa hatuwezi kuwadhuru. Tutawaacha waishi, ili tusije tukaadhibiwa kwa sababu ya kiapo tulichokula. Waacheni waishi.” Hivyo Wagibeoni wakawa wanaitumikia jamii nzima ya Israeli, wakiwakatia kuni na kuwachotea maji, kama viongozi wa Waisraeli walivyosema. Yoshua akawaita Wagibeoni na kuwauliza, “Kwa nini mlitudanganya kwamba mlitoka nchi ya mbali na hali nyinyi mnaishi miongoni mwetu? Sasa, nyinyi mmelaaniwa na baadhi yenu daima mtakuwa watumwa wa kukata kuni na kuchota maji kwa ajili ya nyumba ya Mungu wangu.” Wakamjibu Yoshua, “Tuliambiwa kwamba kwa hakika Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, alimwamuru mtumishi wake Mose awaangamize wakazi wote wa nchi hii na kuwapa nyinyi nchi hii iwe mali yenu. Kwa hivyo, tulihofia maisha yetu na ndipo tukafanya jambo hili. Sasa sisi tumo mikononi mwako, ututendee kama unavyoona inafaa.” Basi, alilowatendea ni kuwaokoa mikononi mwa Waisraeli ili wasiangamizwe; hivyo hawakuwaua.
Yoshua 9:1-26 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Kisha ikawa hapo wafalme wote waliokaa ng'ambo ya pili ya Yordani, hapo penye nchi ya vilima, na katika Shefela, na katika upande wa pwani yote ya bahari kubwa kuikabili Lebanoni, yaani, huyo Mhiti, na Mwamori, na Mkanaani, na Mperizi, na Mhivi, na Myebusi, waliposikia habari ya mambo hayo; ndipo walipojikutanisha pamoja wenyewe kwa wenyewe, ili kupigana na Yoshua, na hao Israeli, kwa nia moja. Lakini wenyeji wa Gibeoni waliposikia habari ya hayo yote Yoshua aliyokuwa amewatenda watu wa Yeriko, na wa Ai, wao wakatenda kwa hila, nao wakaenda na kujifanya kama ndio wajumbe, wakaenda na magunia makuukuu juu ya punda zao, na viriba vya mvinyo vilivyokuwa vikuukuu vilivyorarukararuka, na kutiwa viraka; na viatu vilivyotoboka na kushonwashonwa katika miguu yao, na mavazi makuukuu tena mkate wote wa chakula chao ulikuwa umekauka na kuota ukungu. Nao wakamwendea Yoshua hadi kambini huko Gilgali, nao wakamwambia yeye na watu wa Israeli, Sisi tumetoka nchi ya mbali sana; basi kwa hiyo fanyeni agano pamoja nasi. Basi watu wa Israeli wakawaambia hao Wahivi, Labda mnakaa kati yetu; nasi tutawezaje kufanya agano nanyi? Nao wakamwambia Yoshua, Sisi tu watumishi wako. Yoshua akawauliza, Ninyi ni nani? Na mnatoka wapi? Nao wakamwambia, Sisi watumishi wako tunatoka nchi iliyo mbali sana, kwa sababu ya jina la BWANA, Mungu wako; kwa kuwa sisi tumesikia sifa zake, na habari ya hayo yote aliyofanya huko Misri, na habari ya hayo yote aliyowatenda wale wafalme wawili wa Waamori, waliokuwa huko ng'ambo ya pili ya Yordani, maana huyo Sihoni, mfalme wa Heshboni, na Ogu, mfalme wa Bashani, aliyekuwa huko Ashtarothi. Kisha wazee wetu, na wenyeji wote wa nchi yetu, walinena nasi na kutuambia, Chukueni vyakula mkononi mwenu kwa ajili ya safari, mwende mkawalaki watu hao, na kuwaambia, Sisi tu watumishi wenu; basi sasa fanyeni agano nasi. Huu mkate wetu tuliutwaa ukiwa bado moto katika nyumba zetu, siku hiyo tuliyotoka kuja kwenu, uwe chakula chetu; lakini sasa, tazama, umekauka, na kuingia ukungu; na viriba vyetu hivi, tulivyovitia divai, vilikuwa ni vipya; sasa, tazama, vimerarukararuka; na haya mavazi yetu na viatu vyetu vimekuwa vikuukuu kwa vile tulivyokuja safari ya mbali sana. Basi wakuu hao wakatwaa katika vyakula vyao, wala wasitake shauri kinywani mwa BWANA. Naye Yoshua akafanya amani pamoja nao, na kufanya agano nao, ili kwamba waachwe hai; na wakuu wa mkutano wakawaapia. Kisha ikawa, mwisho wa siku ya tatu baada ya kufanya hilo agano nao, walisikia habari ya kuwa watu hao ni jirani zao, na ya kwamba waliketi kati yao. Kisha wana wa Israeli walisafiri, wakaifikia miji ya watu hao siku ya tatu. Basi miji ya watu hao ilikuwa ni hii, Gibeoni, na Kefira, na Beerothi, na Kiriath-yearimu. Wana wa Israeli hawakuwapiga, kwa sababu wakuu wa mkutano walikuwa wamekwisha kuwaapia kwa BWANA, Mungu wa Israeli. Nao mkutano wote wakawanung'unikia hao wakuu. Lakini wakuu wote waliwaambia mkutano wote, Sisi tumewaapia kwa BWANA, Mungu wa Israeli; basi sasa hatuwezi kuwagusa watu hawa. Tutawafanyia neno hili, kisha tutawaacha wawe hai; hasira isije juu yetu, kwa ajili ya hicho kiapo tulichowaapia. Wakuu waliwaambia, Waacheni wawe hai; basi wakawa wenye kupasua kuni, na wenye kuteka maji, kwa ajili ya mkutano wote; vile vile kama hao wakuu walivyowaambia. Basi Yoshua akawaita, akanena nao, na kuwaambia, Mbona ninyi mmetudanganya, huku mkisema, Sisi tu mbali sana na ninyi; nanyi kumbe! Mnakaa kati yetu? Basi sasa mmelaaniwa kisha hatakosekana kuwapo mtu wa kwenu aliye mtumwa, wenye kupasua kuni, na wenye kuteka maji, kwa ajili ya nyumba ya Mungu wangu. Nao wakamjibu Yoshua, na kusema, Ni kwa sababu ya sisi watumishi wako kuambiwa hakika, jinsi huyo BWANA, Mungu wako alivyomwamuru mtumishi wake Musa kuwapa ninyi nchi hii yote, na kuwaangamiza wenyeji wote wa nchi hii watoke mbele zenu; kwa sababu hii tuliogopa mno kwa ajili ya uhai wetu kwa sababu yenu, nasi tumefanya neno hili. Basi sasa, tazama, sisi tu mkononi mwako; basi kama uonavyo kuwa ni vyema na haki kwako wewe kututenda, tutende hivyo. Naye akawafanyia hivyo, na kuwaokoa na mkono wa wana wa Israeli, ili wasiwaue.
Yoshua 9:1-26 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Kisha ikawa hapo wafalme wote waliokaa ng’ambo ya pili ya Yordani, hapo penye nchi ya vilima, na katika Shefela, na katika upande wa pwani yote ya bahari kubwa kuikabili Lebanoni, yaani, huyo Mhiti, na Mwamori, na Mkanaani, na Mperizi, na Mhivi, na Myebusi, waliposikia habari ya mambo hayo; ndipo walipojikutanisha pamoja wenyewe kwa wenyewe, ili kupigana na Yoshua, na hao Israeli, kwa nia moja. Lakini wenyeji wa Gibeoni waliposikia habari ya hayo yote Yoshua aliyokuwa amewatenda watu wa Yeriko, na wa Ai, wao wakatenda kwa hila, nao wakaenda na kujifanya kama ndio wajumbe, wakaenda na magunia makuukuu juu ya punda zao, na viriba vya mvinyo vilivyokuwa vikuukuu vilivyoraruka-raruka, na kutiwa viraka; na viatu vilivyotoboka na kushonwa-shonwa katika miguu yao, na mavao makuukuu waliyokuwa wanavaa; tena mkate wote wa chakula chao ulikuwa umekauka na kuingia koga. Nao wakamwendea Yoshua hata maragoni huko Gilgali, nao wakamwambia yeye na watu wa Israeli, Sisi tumetoka nchi ya mbali sana; basi kwa hiyo fanyeni agano pamoja nasi. Basi watu wa Israeli wakawaambia hao Wahivi, Labda mwakaa kati yetu; nasi tutawezaje kufanya agano nanyi? Nao wakamwambia Yoshua, Sisi tu watumishi wako. Yoshua akawauliza, Ninyi ni nani? Nanyi mwatoka wapi? Nao wakamwambia, Sisi watumishi wako twatoka nchi iliyo mbali sana, kwa sababu ya jina la BWANA, Mungu wako; kwa kuwa sisi tumesikia sifa zake, na habari ya hayo yote aliyofanya huko Misri, na habari ya hayo yote aliyowatenda wale wafalme wawili wa Waamori, waliokuwa huko ng’ambo ya pili ya Yordani, maana huyo Sihoni, mfalme wa Heshboni, na Ogu, mfalme wa Bashani, aliyekuwa huko Ashtarothi. Kisha wazee wetu, na wenyeji wote wa nchi yetu, walinena nasi na kutuambia, Chukueni vyakula mkononi mwenu kwa ajili ya safari, mwende mkawalaki watu hao, na kuwaambia, Sisi tu watumishi wenu; basi sasa fanyeni agano nasi. Huu mkate wetu tuliutwaa ukali moto katika nyumba zetu, siku hiyo tuliyotoka kuja kwenu, uwe chakula chetu; lakini sasa, tazama, umekauka, na kuingia koga; na viriba vyetu hivi, tulivyovitia divai, vilikuwa ni vipya; sasa, tazama, vimeraruka-raruka; na haya mavazi yetu na viatu vyetu vimekuwa vikuukuu kwa vile tulivyokuja safari ya mbali sana. Basi hao watu wakatwaa katika vyakula vyao, wala wasitake shauri kinywani mwa BWANA. Naye Yoshua akafanya amani pamoja nao, na kufanya agano nao, ili kwamba waachwe hai; na wakuu wa mkutano wakawaapia. Kisha ikawa, mwisho wa siku ya tatu baada ya kufanya hilo agano nao, walisikia habari ya kuwa watu hao ni jirani zao, na ya kwamba waliketi kati yao. Kisha wana wa Israeli walisafiri, wakaifikilia miji ya watu hao siku ya tatu. Basi miji ya watu hao ilikuwa ni hii, Gibeoni, na Kefira, na Beerothi, na Kiriath-yearimu. Wana wa Israeli hawakuwapiga, kwa sababu wakuu wa mkutano walikuwa wamekwisha kuwaapia kwa BWANA, Mungu wa Israeli. Nao mkutano wote wakawanung’unikia hao wakuu. Lakini wakuu wote waliwaambia mkutano wote, Sisi tumewaapia kwa BWANA, Mungu wa Israeli; basi sasa hatuwezi kuwagusa watu hawa. Tutawafanyia neno hili, kisha tutawaacha wawe hai; hasira isije juu yetu, kwa ajili ya hicho kiapo tulichowaapia. Wakuu waliwaambia, Waacheni wawe hai; basi wakawa wenye kupasua kuni, na wenye kuteka maji, kwa ajili ya mkutano wote; vile vile kama hao wakuu walivyowaambia. Basi Yoshua akawaita, akanena nao, na kuwaambia, Mbona ninyi mmetudanganya, huku mkisema, Sisi tu mbali sana na ninyi; nanyi kumbe! Mwakaa kati yetu? Basi sasa mmelaaniwa kisha hatakosekana kuwapo mtu wa kwenu aliye mtumwa, wenye kupasua kuni, na wenye kuteka maji, kwa ajili ya nyumba ya Mungu wangu. Nao wakamjibu Yoshua, na kusema, Ni kwa sababu ya sisi watumishi wako kuambiwa hakika, jinsi huyo BWANA, Mungu wako alivyomwamuru mtumishi wake Musa kuwapa ninyi nchi hii yote, na kuwaangamiza wenyeji wote wa nchi hii watoke mbele zenu; kwa sababu hii tuliogopa mno kwa ajili ya uhai wetu kwa sababu yenu, nasi tumefanya neno hili. Basi sasa, tazama, sisi tu mkononi mwako; basi kama uonavyo kuwa ni vyema na haki kwako wewe kututenda, tutende vivyo. Naye akawafanyia hivyo, na kuwaokoa na mkono wa wana wa Israeli, ili wasiwaue.
Yoshua 9:1-26 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Basi ikawa wafalme wote waliokuwa magharibi mwa Yordani waliposikia haya yote, na wale waliokuwa katika nchi ya vilima, na katika Shefela, na katika pwani yote ya Bahari Kuu hadi kufikia Lebanoni (wafalme wa Wahiti, Waamori, Wakanaani, Waperizi, Wahivi na Wayebusi), waliungana ili kupigana vita dhidi ya Yoshua na Israeli. Hata hivyo, watu wa Gibeoni waliposikia kuhusu yote Yoshua aliyowatendea watu wa Yeriko na Ai, waliamua kufanya hila: Wakajifanya kama wajumbe wakiwa na punda waliobebeshwa mizigo ya magunia yaliyochakaa, na viriba vikuukuu vya mvinyo, vyenye nyufa zilizozibwa. Walivaa miguuni mwao viatu vilivyoraruka na kushonwa, kisha wakavaa nguo kuukuu. Chakula chao kilikuwa mkate uliokauka na kuingia koga. Ndipo wakamwendea Yoshua kambini huko Gilgali, wakamwambia yeye pamoja na Waisraeli, “Tumetoka katika nchi ya mbali; fanyeni mkataba nasi.” Basi Waisraeli wakawaambia hao Wahivi, “Lakini huenda mnakaa karibu nasi. Twawezaje basi kufanya mkataba nanyi?” Wakamwambia Yoshua, “Sisi ni watumishi wako.” Yoshua akawauliza, “Ninyi ni nani, na mnatoka wapi?” Nao wakamjibu: “Watumishi wako wametoka nchi ya mbali sana kwa ajili ya umaarufu wa BWANA Mungu wenu. Kwa kuwa tumesikia taarifa zake: hayo yote aliyofanya huko Misri, pia yale yote aliyowatendea wafalme wawili wa Waamori mashariki mwa Yordani; huyo Sihoni mfalme wa Heshboni na Ogu mfalme wa Bashani, aliyetawala huko Ashtarothi. Basi wazee wetu na wale wote wanaoishi katika nchi yetu walituambia, ‘Chukueni chakula cha safari; nendeni mkakutane na watu hao na kuwaambia, “Sisi tu watumishi wenu, fanyeni mapatano nasi.” ’ Mkate huu wetu ulikuwa wa moto tulipoufunga siku tulipoanza safari kuja kwenu, lakini sasa angalia jinsi ulivyokauka na kuota ukungu. Viriba hivi vya mvinyo vilikuwa vipya tulipovijaza, lakini ona jinsi vilivyo na nyufa. Nguo zetu na viatu vimechakaa kwa ajili ya safari ndefu.” Basi Waisraeli wakavikagua vyakula vyao bila kupata shauri kutoka kwa BWANA. Ndipo Yoshua akafanya nao mkataba wa amani ili kuwaacha waishi, na viongozi wa kusanyiko wakauthibitisha kwa kiapo. Siku ya tatu baada ya kufanya mkataba na Wagibeoni, Waisraeli wakapata habari kuwa watu hao ni majirani zao, walioishi karibu nao. Ndipo Waisraeli wakasafiri, na siku ya tatu wakafika kwenye miji yao: yaani Gibeoni, Kefira, Beerothi na Kiriath-Yearimu. Lakini Waisraeli hawakuwashambulia kwa kuwa viongozi wa kusanyiko walikuwa wamewaapia kwa BWANA, Mungu wa Israeli. Kusanyiko lote wakanungʼunika dhidi ya hao viongozi, lakini viongozi wote wakawajibu, “Tumeshawaapia kwa BWANA, Mungu wa Israeli, kwa hiyo hatuwezi kuwagusa sasa. Hivi ndivyo tutakavyowafanyia: Tutawaacha waishi, ili ghadhabu isije juu yetu kwa kuvunja kiapo tulichowaapia.” Wakaendelea kusema, “Waacheni waishi, lakini wawe wapasua kuni na wachota maji kwa ajili ya jamii yote.” Hivyo ahadi waliyoweka viongozi kwao ikawa hivyo. Kisha Yoshua akawaita Wagibeoni na kuwaambia, “Kwa nini mmetudanganya kwa kutuambia, ‘Tunaishi mbali nanyi,’ ilhali mnaishi karibu nasi? Sasa mko chini ya laana: Daima mtakuwa wapasua kuni na wachota maji kwa ajili ya nyumba ya Mungu wangu.” Wakamjibu Yoshua, “Watumwa wako waliambiwa waziwazi jinsi BWANA Mungu wenu alivyomwamuru mtumishi wake Musa kuwapa ninyi nchi hii yote na kuwaangamiza wakazi wake wote toka mbele zenu. Kwa hiyo tuliogopa mno kwa ajili ya uhai wetu kwa sababu yenu, ndiyo maana tukafanya neno hili. Sasa tupo mikononi mwako. Tufanyieni lolote mnaloona kuwa jema na haki kwenu.” Kwa hiyo Yoshua akawaokoa mikononi mwa Waisraeli, nao hawakuwaua.