Yoshua 8:18-29
Yoshua 8:18-29 Biblia Habari Njema (BHN)
Halafu Mwenyezi-Mungu akamwambia Yoshua, “Elekeza mkuki wako huko mjini Ai maana nitautia mji huo mikononi mwako.” Yoshua akaelekeza mkuki wake mjini Ai. Mara Yoshua alipouelekeza mkuki wake kule Ai, kikosi kilichokuwa kikivizia upande mwingine kikatoka na kuingia mjini; kikauteka mji na kuuteketeza kwa moto. Watu wa Ai walipotazama nyuma, wakaona moshi kutoka mjini ukipanda mpaka mbinguni. Nao hawakuwa na uwezo wa kukimbia upande wowote, maana Waisraeli waliwageukia hao waliokuwa wanawafuatia. Yoshua na Waisraeli wote walipoona kuwa kikosi kilichokuwa kinavizia kimeuteka mji, na kwamba moshi ulikuwa unapanda juu, waliwageukia na kuanza kuwaua. Watu waliobaki mjini walitoka, lakini wote wakawa wamezingirwa na Waisraeli; nao wakauawa, asibaki hata mmoja wao. Lakini mfalme wa mji wa Ai walimteka akiwa hai na kumpeleka kwa Yoshua. Waisraeli walipomaliza kabisa kuwaua watu wote wa Ai huko nyikani ambako waliwafuatia wakarudi mjini Ai na kuwaua wote waliosalia humo. Jumla ya watu wa Ai waliouawa siku hiyo, wanaume kwa wanawake, walikuwa 12,000. Yoshua hakuushusha mkono wake aliokuwa ameushikilia mkuki wake kuelekea Ai mpaka alipowaua wakazi wote wa mji huo. Waisraeli waliteka tu wanyama na mali kama Mwenyezi-Mungu alivyomwamuru Yoshua. Basi, Yoshua aliuteketeza mji wa Ai kwa moto na kuufanya magofu hadi hivi leo. Kisha akamtundika mfalme wa Ai mtini mpaka jioni. Lakini jua lilipoanza kutua, Yoshua aliamuru maiti yake iondolewe mtini na kutupwa kwenye lango la mji kisha warundike rundo kubwa la mawe juu ya maiti hiyo; rundo hilo liko huko mpaka leo.
Yoshua 8:18-29 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Kisha BWANA akamwambia Yoshua, Haya, unyoshe huo mkuki ulio nao mkononi mwako, uuelekeze upande wa Ai; kwa kuwa nitautia mkononi mwako. Basi Yoshua akaunyosha huo mkuki uliokuwa mkononi mwake kuuelekea huo mji. Wale watu waliovizia wakainuka upesi kutoka mahali pao, nao wakapiga mbio mara hapo alipokuwa amekwisha unyosha mkono wake, wakaingia ndani ya mji, na kuushika; nao wakafanya haraka kuuteketeza kwa moto huo mji. Kisha hapo hao watu wa Ai walipotazama nyuma yao, wakaona, na tazama, moshi wa huo mji ulikuwa unapaa juu kwenda mawinguni, nao hawakuwa na nguvu za kukimbia huku wala huku; na wale watu waliokuwa wamekimbia kwenda nyikani wakageuka na kuwarudia hao waliokuwa wakiwafuatia. Basi hapo Yoshua na Israeli wote walipoona ya kwamba hao waliovizia wamekwisha kuushika huo mji, na ya kwamba moshi wa mji umepaa juu, ndipo wakageuka tena, na kuwaua watu wa Ai. Tena hao; wengine wakatoka nje ya mji huo kinyume chao; hivyo basi wakawa katikati ya Waisraeli, wengine upande huu na wengine upande ule; nao wakawapiga, hata wasimwache hata mmoja miongoni mwao aliyesalia, wala kupona. Kisha wakamshika mfalme wa Ai akiwa hai, nao wakamleta kwa Yoshua. Kisha ikawa, hapo Israeli walipokuwa wamekwisha kuwaua wenyeji wote wa Ai katika bara, hapo katika nyika walipokuwamo wakiwafuatia, nao walikuwa wamekwisha anguka wote kwa makali ya upanga, hadi walipokuwa wameangamizwa wote, ndipo Israeli wakarejea Ai, na kuupiga huo mji kwa makali ya upanga. Wote walioanguka siku hiyo wanaume kwa wanawake, walikuwa ni elfu kumi na mbili, yaani, watu wote wa mji wa Ai. Kwani huyo Yoshua hakuuzuia mkono wake, huo ulionyosha huo mkuki, hadi hapo alipokuwa amewaangamiza kabisa wenyeji wote wa Ai; Isipokuwa mifugo na nyara za mji Israeli wakatwaa wenyewe kuwa ni mapato yao, sawasawa na hilo neno la BWANA alilomwamuru Yoshua. Basi Yoshua akauteketeza mji wa Ai, na kuufanya kuwa ni rundo la magofu hata milele, kuwa ni ukiwa hata siku hii ya leo. Na huyo mfalme wa Ai akamtundika katika mti hadi wakati wa jioni; kisha hapo jua lilipokuchwa Yoshua akaagiza, nao wakauondoa mzoga wake katika huo mti, na kuutupa hapo penye maingilio ya lango la mji, kisha wakaweka pale juu yake rundo kubwa la mawe, hata hivi leo.
Yoshua 8:18-29 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Kisha BWANA akamwambia Yoshua, Haya, unyoshe huo mkuki ulio nao mkononi mwako, uuelekeze upande wa Ai; kwa kuwa nitautia mkononi mwako. Basi Yoshua akaunyosha huo mkuki uliokuwa mkononi mwake kuuelekea huo mji. Wale watu waliovizia wakainuka kwa upesi kutoka mahali pao, nao wakapiga mbio mara hapo alipokuwa amekwisha unyosha mkono wake, wakaingia ndani ya mji, na kuushika; nao wakafanya haraka kuuteketeza kwa moto huo mji. Kisha hapo hao watu wa Ai walipotazama nyuma yao, wakaona, na tazama, moshi wa huo mji ulikuwa unapaa juu kwenda mawinguni, nao hawakuwa na nguvu za kukimbia huku wala huku; na wale watu waliokuwa wamekimbia kuenenda nyikani wakageuka na kuwarudia hao waliokuwa wakiwafuatia. Basi hapo Yoshua na Israeli wote walipoona ya kwamba hao waliovizia wamekwisha kuushika huo mji, na ya kwamba moshi wa mji umepaa juu, ndipo wakageuka tena, na kuwaua watu wa Ai. Tena hao; wengine wakatoka nje kuutoka huo mji kinyume chao; basi hivyo walikuwa wa katikati ya Israeli, wengine upande huu na wengine upande huu; nao wakawapiga, hata wasimwache hata mmoja miongoni mwao aliyesalia, wala kupona. Kisha wakamshika mfalme wa Ai ali hai, nao wakamleta kwa Yoshua. Kisha ikawa, hapo Israeli walipokuwa wamekwisha kuwaua wenyeji wote wa Ai katika bara, hapo katika nyika walipokuwamo wakiwafuatia, nao walikuwa wamekwisha anguka wote kwa makali ya upanga, hata walipokuwa wameangamizwa wote, ndipo Israeli wakarejea Ai, na kuupiga huo mji kwa makali ya upanga. Wote walioanguka siku hiyo waume kwa wake, walikuwa ni kumi na mbili elfu, yaani, watu wote wa mji wa Ai. Kwani huyo Yoshua hakuuzuia mkono wake, huo ulionyosha huo mkuki, hata hapo alipokuwa amewaangamiza kabisa wenyeji wote wa Ai. Isipokuwa wanyama wa mji na nyara za mji Israeli wakatwaa wenyewe kuwa ni mapato yao, sawasawa na hilo neno la BWANA alilomwamuru Yoshua. Basi Yoshua akaupiga moto mji wa Ai, na kuufanya kuwa ni chungu ya magofu hata milele, kuwa ni ukiwa hata siku hii ya leo. Na huyo mfalme wa Ai akamtundika katika mti hata wakati wa jioni; kisha hapo jua lilipokuchwa Yoshua akaagiza, nao wakauondoa mzoga wake katika huo mti, na kuutupa hapo penye maingilio ya lango la mji, kisha wakaweka pale juu yake chungu kubwa ya mawe, hata hivi leo.
Yoshua 8:18-29 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Ndipo BWANA akamwambia Yoshua, “Inua huo mkuki ulio mkononi mwako kuuelekeza Ai, kwa kuwa nitautia huo mji mkononi mwako.” Hivyo Yoshua akauelekeza mkuki wake Ai. Mara tu alipofanya hivi, wale watu waliokuwa mafichoni wakaondoka upesi kutoka mahali pao na kukimbia mbele. Wakaingia ndani ya mji, wakauteka na kuutia moto kwa haraka. Wanaume wa Ai wakaangalia nyuma, wakauona moshi wa huo mji ukielekea angani, lakini hawakuwa na nafasi ya kutoroka kwa upande wowote, kwa kuwa wale Waisraeli waliokuwa wakiwakimbia kuelekea jangwani walikuwa wamegeuka nyuma kuwakabili wakimbizaji wao. Basi Yoshua na Waisraeli wote walipoona kwamba waviziaji wameshauteka mji na moshi ulikuwa unapaa juu kwenye mji, wakawageukia wanaume wa Ai na kuwashambulia. Wale waviziaji nao pia wakatoka nje ya mji dhidi yao, hivi kwamba wakashikiwa katikati, Waisraeli wakiwa pande zote mbili. Israeli wakawaua, bila kuwaachia yeyote aliyenusurika wala aliyetoroka. Lakini wakamchukua mfalme wa Ai akiwa hai na kumleta kwa Yoshua. Israeli ilipomaliza kuwaua wanaume wote wa Ai katika mashamba na jangwani walipokuwa wamewafukuzia, na baada ya kila mmoja wao kuuawa kwa upanga, Waisraeli wote wakarudi Ai na kuwaua wale waliokuwa wamebakia mjini. Wanaume na wanawake elfu kumi na mbili waliangamia siku ile, yaani watu wote wa Ai. Kwa maana Yoshua hakuurudisha ule mkono wake uliokuwa umeuinua mkuki hadi alipomaliza kuwaangamiza wote walioishi Ai. Lakini Israeli wakajichukulia mifugo na nyara za mji huu, kama vile BWANA alivyokuwa amemwamuru Yoshua. Kwa hiyo Yoshua akauchoma moto mji wa Ai na kuufanya kuwa lundo la magofu la kudumu, mahali pa ukiwa hadi leo. Akamwangika mfalme wa Ai kwenye mti na kumwacha hapo hadi jioni. Wakati wa jua kutua, Yoshua akawaamuru wautoe mwili wake kwenye mti na kuutupa kwenye ingilio la lango la mji. Kisha wakalundika mawe mengi makubwa juu yake, ambayo yamesalia hadi leo.