Yoshua 8:1-8
Yoshua 8:1-8 Biblia Habari Njema (BHN)
Mwenyezi-Mungu akamwambia Yoshua, “Usiogope, wala usiwe na wasiwasi wowote; wachukue wanajeshi wako wote uelekee mji wa Ai, kwani mfalme wa Ai nimemtia mikononi mwako, pamoja na watu wake, mji wake na nchi yake. Mtautendea mji wa Ai pamoja na mfalme wake kama vile mlivyoutendea mji wa Yeriko pamoja na mfalme wake. Mali zake pamoja na mifugo yake mtakayoteka itakuwa ni mali yenu. Nendeni mwuvamie mji kutoka upande wa nyuma.” Basi, Yoshua akaondoka, pamoja na wanajeshi wake wote kwenda Ai. Akawachagua watu hodari 30,000 na kuwaambia watangulie wakati wa usiku. Akawaamuru hivi: “Nyinyi mtauvizia mji kutoka upande wa nyuma. Msiende mbali na mji, bali muwe tayari wakati wote. Mimi, pamoja na watu wote walio pamoja nami, tutaukaribia mji. Watu watakapotoka nje kuja kutukabili kama hapo awali, sisi tutawakimbia. Nao wataendelea kutufuatia mpaka wawe mbali na mji wao, maana watafikiri wametutimua kama walivyofanya hapo awali. Sisi tutawaacha watufukuze. Hapo, nyinyi mtatokea kutoka huko mlikokuwa mnavizia na kuuteka mji, maana Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, atautia mji huo mikononi mwenu. Mkishauteka mji mtauteketeza kwa moto, kama vile Mwenyezi-Mungu alivyoamuru. Hayo ndiyo maagizo mtakayofuata.”
Yoshua 8:1-8 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Kisha BWANA akamwambia Yoshua, Usiogope, wala usifadhaike; wachukue wanajeshi wako wote waende pamoja nawe, nanyi inukeni, mwende Ai, angalia, mimi nimemtia mkononi mwako huyo mfalme wa Ai, na watu wake, na mji wake, na nchi yake; nawe utautenda mji wa Ai na mfalme wake kama ulivyoutenda mji wa Yeriko na mfalme wake; lakini nyara zake na wanyama wake wa mji mtavitwaa kuwa mateka yenu wenyewe; huo mji uuwekee waoteaji upande wa nyuma. Basi Yoshua akainuka, na watu wote wa vita pamoja naye, ili waende Ai; Yoshua akachagua watu elfu thelathini, watu mashujaa wenye uwezo, akawatuma wakati wa usiku. Akawaagiza, akasema, Angalieni, mtaotea kuuvizia ule mji, upande wa nyuma wa mji; msiende mbali sana na mji, lakini kaeni tayari nyote; na mimi, na watu wote walio pamoja nami, tutaukaribia mji; kisha itakuwa, hapo watakapotoka nje kupigana nasi, kama walivyofanya hapo kwanza, sisi tutakimbia mbele yao; nao watatoka nje watufuate, hadi tuwavute waende mbali na mji wao; kwa kuwa watasema, Wakimbia mbele yetu, kama walivyofanya kwanza; nasi tutakimbia mbele yao; basi ninyi mtainuka mtoke hapo mwoteapo, na kuushika mji; kwa kuwa BWANA, Mungu wenu, atautia mikononi mwenu. Kisha itakuwa, mtakapoushika mji, ndipo mtauteketeza mji kwa moto; sawasawa na hilo neno la BWANA; angalieni, nimewaagiza.
Yoshua 8:1-8 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Kisha BWANA akamwambia Yoshua, Usiche, wala usifadhaike; wachukue watu wote wa vita waende pamoja nawe, nanyi inukeni, mwende Ai, angalia, mimi nimemtia mkononi mwako huyo mfalme wa Ai, na watu wake, na mji wake, na nchi yake; nawe utautenda mji wa Ai na mfalme wake kama ulivyoutenda mji wa Yeriko na mfalme wake; lakini nyara zake na wanyama wake wa mji mtavitwaa kuwa mateka yenu wenyewe; huo mji uuwekee waoteaji upande wa nyuma. Basi Yoshua akainuka, na watu wote wa vita pamoja naye, ili waende Ai; Yoshua akachagua watu thelathini elfu, watu mashujaa wenye uwezo, akawapeleka wakati wa usiku. Akawaagiza, akasema, Angalieni, mtaotea kuuvizia ule mji, upande wa nyuma wa mji; msiende mbali sana na mji, lakini kaeni tayari nyote; na mimi, na watu wote walio pamoja nami, tutaukaribia mji; kisha itakuwa, hapo watakapotoka nje kupigana nasi, kama walivyofanya hapo kwanza, sisi tutakimbia mbele yao; nao watatoka nje watufuate, hata tuwavute waende mbali na mji wao; kwa kuwa watasema, Wakimbia mbele yetu, kama walivyofanya kwanza; nasi tutakimbia mbele yao; basi ninyi mtainuka mtoke hapo mwoteapo, na kuushika mji; kwa kuwa BWANA, Mungu wenu, atautia mikononi mwenu. Kisha itakuwa, mtakapoushika mji, ndipo mtauteketeza mji kwa moto; sawasawa na hilo neno la BWANA; angalieni, nimewaagiza.
Yoshua 8:1-8 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Ndipo BWANA akamwambia Yoshua, “Usiogope, wala usivunjike moyo. Chukua jeshi lote la vita uende pamoja nalo kuishambulia Ai. Kwa kuwa nimeshamweka mikononi mwako mfalme wa Ai, pamoja na watu wake, mji wake na nchi yake. Utautendea mji wa Ai na mfalme wake kama ulivyotendea Yeriko na mfalme wake, isipokuwa mnaweza kunyakua mali zao na mifugo yao kuwa nyara zenu. Weka waviziaji upande wa nyuma ya mji.” Basi Yoshua na jeshi lote wakainuka kushambulia Ai. Akachagua mashujaa elfu thelathini walio bora miongoni mwa wapiganaji wake, akawapeleka wakati wa usiku, akiwaagiza: “Sikilizeni kwa makini. Mtavizia nyuma ya mji. Msiende mbali sana na mji. Wote kuweni macho. Mimi na watu walio pamoja nami tutaukabili mji, kisha itakuwa hapo watu watakapotoka nje kupigana nasi, kama walivyofanya hapo awali, sisi tutawakimbia. Watatufuatilia hadi tutakapokuwa tumewavuta mbali na mji kwa kuwa watasema, ‘Wanatukimbia, kama walivyofanya hapo awali.’ Hivyo tutakapowakimbia, ninyi mtainuka mtoke mafichoni na kuuteka mji. BWANA Mungu wenu atautia mkononi mwenu. Mtakapokuwa mmeuteka mji, uteketezeni kwa moto. Fanyeni kama vile BWANA alivyoamuru. Tazameni, nimewaagiza.”