Yoshua 8:1-29
Yoshua 8:1-29 Biblia Habari Njema (BHN)
Mwenyezi-Mungu akamwambia Yoshua, “Usiogope, wala usiwe na wasiwasi wowote; wachukue wanajeshi wako wote uelekee mji wa Ai, kwani mfalme wa Ai nimemtia mikononi mwako, pamoja na watu wake, mji wake na nchi yake. Mtautendea mji wa Ai pamoja na mfalme wake kama vile mlivyoutendea mji wa Yeriko pamoja na mfalme wake. Mali zake pamoja na mifugo yake mtakayoteka itakuwa ni mali yenu. Nendeni mwuvamie mji kutoka upande wa nyuma.” Basi, Yoshua akaondoka, pamoja na wanajeshi wake wote kwenda Ai. Akawachagua watu hodari 30,000 na kuwaambia watangulie wakati wa usiku. Akawaamuru hivi: “Nyinyi mtauvizia mji kutoka upande wa nyuma. Msiende mbali na mji, bali muwe tayari wakati wote. Mimi, pamoja na watu wote walio pamoja nami, tutaukaribia mji. Watu watakapotoka nje kuja kutukabili kama hapo awali, sisi tutawakimbia. Nao wataendelea kutufuatia mpaka wawe mbali na mji wao, maana watafikiri wametutimua kama walivyofanya hapo awali. Sisi tutawaacha watufukuze. Hapo, nyinyi mtatokea kutoka huko mlikokuwa mnavizia na kuuteka mji, maana Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, atautia mji huo mikononi mwenu. Mkishauteka mji mtauteketeza kwa moto, kama vile Mwenyezi-Mungu alivyoamuru. Hayo ndiyo maagizo mtakayofuata.” Basi, Yoshua akawaambia waende mahali pao pa kuvizia; nao wakajiweka magharibi ya mji wa Ai kati ya mji wa Ai na Betheli. Lakini Yoshua alilala usiku huo katika kambi ya Waisraeli. Yoshua akaamka asubuhi na mapema, akawakusanya Waisraeli na kuelekea mjini Ai, akiwa pamoja na wazee. Wanajeshi wote waliofuatana naye walikaribia mji na kupiga kambi kaskazini yake, ngambo ya bonde mkabala wa mji wa Ai. Ndipo akachukua watu wengine 5,000 na kuwaweka wavizie kati ya mji wa Betheli na Ai, magharibi ya mji wa Ai. Kikosi kikubwa kiliwekwa kaskazini mwa mji na wale waliobaki waliwekwa magharibi ya mji. Lakini usiku huo, Yoshua akalala bondeni. Mfalme wa mji wa Ai alipoona hivyo, aliharakisha na kwenda kwenye mteremko wa kuelekea Araba ili akabiliane na Waisraeli vitani. Lakini hakujua kwamba mji wake ulikuwa umeviziwa kutoka nyuma. Kisha Yoshua pamoja na watu wake wakajifanya kana kwamba wanashindwa, wakaanza kukimbia kuelekea jangwani. Watu wote waliokuwa mjini waliitwa wawafuatie Waisraeli; na walipokuwa wanamfuatia Yoshua, walitoka na kwenda mbali na mji wao. Hakuna mtu yeyote aliyebaki mjini Ai, waliuacha mji huo wazi wakaenda kuwafuatia Waisraeli. Halafu Mwenyezi-Mungu akamwambia Yoshua, “Elekeza mkuki wako huko mjini Ai maana nitautia mji huo mikononi mwako.” Yoshua akaelekeza mkuki wake mjini Ai. Mara Yoshua alipouelekeza mkuki wake kule Ai, kikosi kilichokuwa kikivizia upande mwingine kikatoka na kuingia mjini; kikauteka mji na kuuteketeza kwa moto. Watu wa Ai walipotazama nyuma, wakaona moshi kutoka mjini ukipanda mpaka mbinguni. Nao hawakuwa na uwezo wa kukimbia upande wowote, maana Waisraeli waliwageukia hao waliokuwa wanawafuatia. Yoshua na Waisraeli wote walipoona kuwa kikosi kilichokuwa kinavizia kimeuteka mji, na kwamba moshi ulikuwa unapanda juu, waliwageukia na kuanza kuwaua. Watu waliobaki mjini walitoka, lakini wote wakawa wamezingirwa na Waisraeli; nao wakauawa, asibaki hata mmoja wao. Lakini mfalme wa mji wa Ai walimteka akiwa hai na kumpeleka kwa Yoshua. Waisraeli walipomaliza kabisa kuwaua watu wote wa Ai huko nyikani ambako waliwafuatia wakarudi mjini Ai na kuwaua wote waliosalia humo. Jumla ya watu wa Ai waliouawa siku hiyo, wanaume kwa wanawake, walikuwa 12,000. Yoshua hakuushusha mkono wake aliokuwa ameushikilia mkuki wake kuelekea Ai mpaka alipowaua wakazi wote wa mji huo. Waisraeli waliteka tu wanyama na mali kama Mwenyezi-Mungu alivyomwamuru Yoshua. Basi, Yoshua aliuteketeza mji wa Ai kwa moto na kuufanya magofu hadi hivi leo. Kisha akamtundika mfalme wa Ai mtini mpaka jioni. Lakini jua lilipoanza kutua, Yoshua aliamuru maiti yake iondolewe mtini na kutupwa kwenye lango la mji kisha warundike rundo kubwa la mawe juu ya maiti hiyo; rundo hilo liko huko mpaka leo.
Yoshua 8:1-29 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Kisha BWANA akamwambia Yoshua, Usiogope, wala usifadhaike; wachukue wanajeshi wako wote waende pamoja nawe, nanyi inukeni, mwende Ai, angalia, mimi nimemtia mkononi mwako huyo mfalme wa Ai, na watu wake, na mji wake, na nchi yake; nawe utautenda mji wa Ai na mfalme wake kama ulivyoutenda mji wa Yeriko na mfalme wake; lakini nyara zake na wanyama wake wa mji mtavitwaa kuwa mateka yenu wenyewe; huo mji uuwekee waoteaji upande wa nyuma. Basi Yoshua akainuka, na watu wote wa vita pamoja naye, ili waende Ai; Yoshua akachagua watu elfu thelathini, watu mashujaa wenye uwezo, akawatuma wakati wa usiku. Akawaagiza, akasema, Angalieni, mtaotea kuuvizia ule mji, upande wa nyuma wa mji; msiende mbali sana na mji, lakini kaeni tayari nyote; na mimi, na watu wote walio pamoja nami, tutaukaribia mji; kisha itakuwa, hapo watakapotoka nje kupigana nasi, kama walivyofanya hapo kwanza, sisi tutakimbia mbele yao; nao watatoka nje watufuate, hadi tuwavute waende mbali na mji wao; kwa kuwa watasema, Wakimbia mbele yetu, kama walivyofanya kwanza; nasi tutakimbia mbele yao; basi ninyi mtainuka mtoke hapo mwoteapo, na kuushika mji; kwa kuwa BWANA, Mungu wenu, atautia mikononi mwenu. Kisha itakuwa, mtakapoushika mji, ndipo mtauteketeza mji kwa moto; sawasawa na hilo neno la BWANA; angalieni, nimewaagiza. Basi Yoshua akawatuma; nao wakaenda hadi hapo watakapootea, wakakaa kati ya Betheli na Ai, upande wa magharibi wa Ai; lakini Yoshua akalala usiku huo kati ya watu. Yoshua akaamka asubuhi na mapema, akawakutanisha watu, kisha akatangulia kukwea kwenda Ai mbele ya hao watu, yeye na wazee wa Israeli. Watu wote, hao wa vita, waliokuwa pamoja naye, wakaenda wakakaribia, na kufika mbele ya mji, wakatua upande wa kaskazini wa Ai; napo palikuwa na bonde kati yao na Ai. Kisha akatwaa watu kama elfu tano, akawaweka kuotea kati ya Betheli na Ai, upande wa magharibi wa huo mji. Basi wakawaweka hao watu, jeshi zima lililokuwa upande wa kaskazini wa mji, na wale waliokuwa wakiotea upande wa magharibi wa mji; naye Yoshua akaenda usiku huo katikati ya hilo bonde. Kisha ikawa hapo huyo mfalme wa Ai alipoona jambo hilo, ndipo walipofanya haraka, na wakaamka asubuhi na mapema, na wanaume wa mji wakatoka nje waende kupigana na Israeli, yeye na watu wake wote, kwa wakati ulioamriwa, kuikabili Araba; lakini hakujua ya kwamba walikuwako waviziao kinyume chake kwa upande wa nyuma wa mji. Kisha Yoshua na watu wa Israeli wote walifanya kana kwamba wameshindwa mbele yao, wakakimbia kwa njia ya nyika. Watu wote waliokuwa ndani ya mji waliitwa wakusanyike pamoja ili kuwafuatia; nao wakamfuatia Yoshua, wakasongea mbele na kuuacha mji. Hakusalia mtu yeyote ndani ya Ai, au katika Betheli, asiyetoka nje kuwafuatia Israeli; wakauacha mji wazi na kuwafuatia Israeli. Kisha BWANA akamwambia Yoshua, Haya, unyoshe huo mkuki ulio nao mkononi mwako, uuelekeze upande wa Ai; kwa kuwa nitautia mkononi mwako. Basi Yoshua akaunyosha huo mkuki uliokuwa mkononi mwake kuuelekea huo mji. Wale watu waliovizia wakainuka upesi kutoka mahali pao, nao wakapiga mbio mara hapo alipokuwa amekwisha unyosha mkono wake, wakaingia ndani ya mji, na kuushika; nao wakafanya haraka kuuteketeza kwa moto huo mji. Kisha hapo hao watu wa Ai walipotazama nyuma yao, wakaona, na tazama, moshi wa huo mji ulikuwa unapaa juu kwenda mawinguni, nao hawakuwa na nguvu za kukimbia huku wala huku; na wale watu waliokuwa wamekimbia kwenda nyikani wakageuka na kuwarudia hao waliokuwa wakiwafuatia. Basi hapo Yoshua na Israeli wote walipoona ya kwamba hao waliovizia wamekwisha kuushika huo mji, na ya kwamba moshi wa mji umepaa juu, ndipo wakageuka tena, na kuwaua watu wa Ai. Tena hao; wengine wakatoka nje ya mji huo kinyume chao; hivyo basi wakawa katikati ya Waisraeli, wengine upande huu na wengine upande ule; nao wakawapiga, hata wasimwache hata mmoja miongoni mwao aliyesalia, wala kupona. Kisha wakamshika mfalme wa Ai akiwa hai, nao wakamleta kwa Yoshua. Kisha ikawa, hapo Israeli walipokuwa wamekwisha kuwaua wenyeji wote wa Ai katika bara, hapo katika nyika walipokuwamo wakiwafuatia, nao walikuwa wamekwisha anguka wote kwa makali ya upanga, hadi walipokuwa wameangamizwa wote, ndipo Israeli wakarejea Ai, na kuupiga huo mji kwa makali ya upanga. Wote walioanguka siku hiyo wanaume kwa wanawake, walikuwa ni elfu kumi na mbili, yaani, watu wote wa mji wa Ai. Kwani huyo Yoshua hakuuzuia mkono wake, huo ulionyosha huo mkuki, hadi hapo alipokuwa amewaangamiza kabisa wenyeji wote wa Ai; Isipokuwa mifugo na nyara za mji Israeli wakatwaa wenyewe kuwa ni mapato yao, sawasawa na hilo neno la BWANA alilomwamuru Yoshua. Basi Yoshua akauteketeza mji wa Ai, na kuufanya kuwa ni rundo la magofu hata milele, kuwa ni ukiwa hata siku hii ya leo. Na huyo mfalme wa Ai akamtundika katika mti hadi wakati wa jioni; kisha hapo jua lilipokuchwa Yoshua akaagiza, nao wakauondoa mzoga wake katika huo mti, na kuutupa hapo penye maingilio ya lango la mji, kisha wakaweka pale juu yake rundo kubwa la mawe, hata hivi leo.
Yoshua 8:1-29 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Kisha BWANA akamwambia Yoshua, Usiche, wala usifadhaike; wachukue watu wote wa vita waende pamoja nawe, nanyi inukeni, mwende Ai, angalia, mimi nimemtia mkononi mwako huyo mfalme wa Ai, na watu wake, na mji wake, na nchi yake; nawe utautenda mji wa Ai na mfalme wake kama ulivyoutenda mji wa Yeriko na mfalme wake; lakini nyara zake na wanyama wake wa mji mtavitwaa kuwa mateka yenu wenyewe; huo mji uuwekee waoteaji upande wa nyuma. Basi Yoshua akainuka, na watu wote wa vita pamoja naye, ili waende Ai; Yoshua akachagua watu thelathini elfu, watu mashujaa wenye uwezo, akawapeleka wakati wa usiku. Akawaagiza, akasema, Angalieni, mtaotea kuuvizia ule mji, upande wa nyuma wa mji; msiende mbali sana na mji, lakini kaeni tayari nyote; na mimi, na watu wote walio pamoja nami, tutaukaribia mji; kisha itakuwa, hapo watakapotoka nje kupigana nasi, kama walivyofanya hapo kwanza, sisi tutakimbia mbele yao; nao watatoka nje watufuate, hata tuwavute waende mbali na mji wao; kwa kuwa watasema, Wakimbia mbele yetu, kama walivyofanya kwanza; nasi tutakimbia mbele yao; basi ninyi mtainuka mtoke hapo mwoteapo, na kuushika mji; kwa kuwa BWANA, Mungu wenu, atautia mikononi mwenu. Kisha itakuwa, mtakapoushika mji, ndipo mtauteketeza mji kwa moto; sawasawa na hilo neno la BWANA; angalieni, nimewaagiza. Basi Yoshua akawatuma; nao wakaenda hata hapo watakapootea, wakakaa kati ya Betheli na Ai, upande wa magharibi wa Ai; lakini Yoshua akalala usiku huo kati ya watu. Yoshua akaamka asubuhi na mapema, akawakutanisha watu, kisha akatangulia kukwea kwenda Ai mbele ya hao watu, yeye na wazee wa Israeli. Watu wote, hao wa vita, waliokuwa pamoja naye, wakaenda wakakaribia, na kufikilia mbele ya mji, wakatua upande wa kaskazini wa Ai; napo palikuwa na bonde kati ya yeye na Ai. Kisha akatwaa watu kama elfu tano, akawaweka kuotea kati ya Betheli na Ai, upande wa magharibi wa huo mji. Basi wakawaweka hao watu, jeshi zima lililokuwa upande wa kaskazini wa mji, na wale waliokuwa waotea upande wa magharibi wa mji; naye Yoshua akaenda usiku huo katikati ya hilo bonde. Kisha ikawa hapo huyo mfalme wa Ai alipoona jambo hilo, ndipo walipofanya haraka, na wakaamka asubuhi na mapema, na watu waume wa mji wakatoka nje waende kupigana na Israeli, yeye na watu wake wote, kwa wakati ulioamriwa, kuikabili Araba; lakini hakujua ya kwamba walikuwako waviziao kinyume chake kwa upande wa nyuma wa mji. Kisha Yoshua na watu wa Israeli wote walifanya kana kwamba wameshindwa mbele yao, wakakimbia kwa njia ya nyika. Watu wote waliokuwa ndani ya mji waliitwa wakusanyike pamoja ili kuwafuatia; nao wakamfuatia Yoshua, wakasongea mbele na kuuacha mji. Hakusalia mtu ye yote ndani ya Ai, au katika Betheli, asiyetoka nje kuwafuatia Israeli; wakauacha mji wazi na kuwafuatia Israeli. Kisha BWANA akamwambia Yoshua, Haya, unyoshe huo mkuki ulio nao mkononi mwako, uuelekeze upande wa Ai; kwa kuwa nitautia mkononi mwako. Basi Yoshua akaunyosha huo mkuki uliokuwa mkononi mwake kuuelekea huo mji. Wale watu waliovizia wakainuka kwa upesi kutoka mahali pao, nao wakapiga mbio mara hapo alipokuwa amekwisha unyosha mkono wake, wakaingia ndani ya mji, na kuushika; nao wakafanya haraka kuuteketeza kwa moto huo mji. Kisha hapo hao watu wa Ai walipotazama nyuma yao, wakaona, na tazama, moshi wa huo mji ulikuwa unapaa juu kwenda mawinguni, nao hawakuwa na nguvu za kukimbia huku wala huku; na wale watu waliokuwa wamekimbia kuenenda nyikani wakageuka na kuwarudia hao waliokuwa wakiwafuatia. Basi hapo Yoshua na Israeli wote walipoona ya kwamba hao waliovizia wamekwisha kuushika huo mji, na ya kwamba moshi wa mji umepaa juu, ndipo wakageuka tena, na kuwaua watu wa Ai. Tena hao; wengine wakatoka nje kuutoka huo mji kinyume chao; basi hivyo walikuwa wa katikati ya Israeli, wengine upande huu na wengine upande huu; nao wakawapiga, hata wasimwache hata mmoja miongoni mwao aliyesalia, wala kupona. Kisha wakamshika mfalme wa Ai ali hai, nao wakamleta kwa Yoshua. Kisha ikawa, hapo Israeli walipokuwa wamekwisha kuwaua wenyeji wote wa Ai katika bara, hapo katika nyika walipokuwamo wakiwafuatia, nao walikuwa wamekwisha anguka wote kwa makali ya upanga, hata walipokuwa wameangamizwa wote, ndipo Israeli wakarejea Ai, na kuupiga huo mji kwa makali ya upanga. Wote walioanguka siku hiyo waume kwa wake, walikuwa ni kumi na mbili elfu, yaani, watu wote wa mji wa Ai. Kwani huyo Yoshua hakuuzuia mkono wake, huo ulionyosha huo mkuki, hata hapo alipokuwa amewaangamiza kabisa wenyeji wote wa Ai. Isipokuwa wanyama wa mji na nyara za mji Israeli wakatwaa wenyewe kuwa ni mapato yao, sawasawa na hilo neno la BWANA alilomwamuru Yoshua. Basi Yoshua akaupiga moto mji wa Ai, na kuufanya kuwa ni chungu ya magofu hata milele, kuwa ni ukiwa hata siku hii ya leo. Na huyo mfalme wa Ai akamtundika katika mti hata wakati wa jioni; kisha hapo jua lilipokuchwa Yoshua akaagiza, nao wakauondoa mzoga wake katika huo mti, na kuutupa hapo penye maingilio ya lango la mji, kisha wakaweka pale juu yake chungu kubwa ya mawe, hata hivi leo.
Yoshua 8:1-29 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Ndipo BWANA akamwambia Yoshua, “Usiogope, wala usivunjike moyo. Chukua jeshi lote la vita uende pamoja nalo kuishambulia Ai. Kwa kuwa nimeshamweka mikononi mwako mfalme wa Ai, pamoja na watu wake, mji wake na nchi yake. Utautendea mji wa Ai na mfalme wake kama ulivyotendea Yeriko na mfalme wake, isipokuwa mnaweza kunyakua mali zao na mifugo yao kuwa nyara zenu. Weka waviziaji upande wa nyuma ya mji.” Basi Yoshua na jeshi lote wakainuka kushambulia Ai. Akachagua mashujaa elfu thelathini walio bora miongoni mwa wapiganaji wake, akawapeleka wakati wa usiku, akiwaagiza: “Sikilizeni kwa makini. Mtavizia nyuma ya mji. Msiende mbali sana na mji. Wote kuweni macho. Mimi na watu walio pamoja nami tutaukabili mji, kisha itakuwa hapo watu watakapotoka nje kupigana nasi, kama walivyofanya hapo awali, sisi tutawakimbia. Watatufuatilia hadi tutakapokuwa tumewavuta mbali na mji kwa kuwa watasema, ‘Wanatukimbia, kama walivyofanya hapo awali.’ Hivyo tutakapowakimbia, ninyi mtainuka mtoke mafichoni na kuuteka mji. BWANA Mungu wenu atautia mkononi mwenu. Mtakapokuwa mmeuteka mji, uteketezeni kwa moto. Fanyeni kama vile BWANA alivyoamuru. Tazameni, nimewaagiza.” Ndipo Yoshua akawatuma watu, nao wakaenda mahali pa kujificha, wakawa wanavizia kati ya Betheli na Ai, kuelekea upande wa magharibi wa Ai, lakini Yoshua akalala miongoni mwa watu usiku huo. Asubuhi na mapema siku iliyofuata, Yoshua akakusanya jeshi lake, na yeye na viongozi wa Israeli wakawaongoza kwenda Ai. Wanajeshi wote waliokuwa pamoja na Yoshua walipanda, wakakaribia na kufika mbele ya mji. Wakapiga kambi kaskazini mwa Ai, pakiwa na bonde kati yao na huo mji. Yoshua alikuwa amewachukua watu wapatao elfu tano, akawaweka mafichoni kusubiri kushambulia, kati ya Betheli na Ai, upande wa magharibi wa mji. Wakawaweka askari katika maeneo yao: wale wote waliokuwa kambini wakawa kaskazini ya mji na wale waliokuwa wakivizia wakawa upande wa magharibi. Usiku huo Yoshua akaenda katika lile bonde. Mfalme wa Ai alipoona jambo hili, yeye pamoja na wanaume wote wa mji wakatoka kwa haraka asubuhi na mapema kukutana na Israeli katika vita mahali palipotazamana na Araba. Lakini hakujua kwamba kulikuwa kumewekwa waviziaji dhidi yake nyuma ya mji. Yoshua na Waisraeli wote wakaruhusu kurudishwa nyuma mbele yao, na kuelekea jangwani. Watu wote wa Ai wakaitwa ili kuwafuatia, nao wakavutwa kumfuatia Yoshua mbali na mji. Hakuna hata mwanaume mmoja aliyebakia Ai wala Betheli ambaye hakufuatia Israeli. Wakauacha mji wazi na kuwafuatia Waisraeli. Ndipo BWANA akamwambia Yoshua, “Inua huo mkuki ulio mkononi mwako kuuelekeza Ai, kwa kuwa nitautia huo mji mkononi mwako.” Hivyo Yoshua akauelekeza mkuki wake Ai. Mara tu alipofanya hivi, wale watu waliokuwa mafichoni wakaondoka upesi kutoka mahali pao na kukimbia mbele. Wakaingia ndani ya mji, wakauteka na kuutia moto kwa haraka. Wanaume wa Ai wakaangalia nyuma, wakauona moshi wa huo mji ukielekea angani, lakini hawakuwa na nafasi ya kutoroka kwa upande wowote, kwa kuwa wale Waisraeli waliokuwa wakiwakimbia kuelekea jangwani walikuwa wamegeuka nyuma kuwakabili wakimbizaji wao. Basi Yoshua na Waisraeli wote walipoona kwamba waviziaji wameshauteka mji na moshi ulikuwa unapaa juu kwenye mji, wakawageukia wanaume wa Ai na kuwashambulia. Wale waviziaji nao pia wakatoka nje ya mji dhidi yao, hivi kwamba wakashikiwa katikati, Waisraeli wakiwa pande zote mbili. Israeli wakawaua, bila kuwaachia yeyote aliyenusurika wala aliyetoroka. Lakini wakamchukua mfalme wa Ai akiwa hai na kumleta kwa Yoshua. Israeli ilipomaliza kuwaua wanaume wote wa Ai katika mashamba na jangwani walipokuwa wamewafukuzia, na baada ya kila mmoja wao kuuawa kwa upanga, Waisraeli wote wakarudi Ai na kuwaua wale waliokuwa wamebakia mjini. Wanaume na wanawake elfu kumi na mbili waliangamia siku ile, yaani watu wote wa Ai. Kwa maana Yoshua hakuurudisha ule mkono wake uliokuwa umeuinua mkuki hadi alipomaliza kuwaangamiza wote walioishi Ai. Lakini Israeli wakajichukulia mifugo na nyara za mji huu, kama vile BWANA alivyokuwa amemwamuru Yoshua. Kwa hiyo Yoshua akauchoma moto mji wa Ai na kuufanya kuwa lundo la magofu la kudumu, mahali pa ukiwa hadi leo. Akamwangika mfalme wa Ai kwenye mti na kumwacha hapo hadi jioni. Wakati wa jua kutua, Yoshua akawaamuru wautoe mwili wake kwenye mti na kuutupa kwenye ingilio la lango la mji. Kisha wakalundika mawe mengi makubwa juu yake, ambayo yamesalia hadi leo.