Yoshua 7:6-9
Yoshua 7:6-9 Biblia Habari Njema (BHN)
Yoshua akayararua mavazi yake, yeye pamoja na wazee wa Israeli. Wakajitupa chini mbele ya sanduku la Mwenyezi-Mungu mpaka jioni; wakajitia mavumbi vichwani mwao. Yoshua akasema, “Ole wetu, ee Bwana Mungu! Kwa nini umetuvusha mto Yordani ili kututia mikononi mwa Waamori watuangamize? Tungaliridhika kubaki ngambo ya mto Yordani! Ee Bwana, niseme nini hali Waisraeli wamewakimbia adui zao? Basi, Wakanaani pamoja na wakazi wote wa nchi hii watakapopata habari hiyo watatuzingira na kutufuta kabisa duniani. Sasa utafanya nini kuonesha ukuu wa jina lako?”
Yoshua 7:6-9 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Yoshua akararua mavazi yake, akaanguka kifudifudi mbele ya sanduku la BWANA hadi jioni, yeye na wazee wa Israeli; wakatia mavumbi vichwani mwao. Yoshua akasema, Ee Bwana MUNGU, kwa nini umewavusha watu hawa mto wa Yordani, ili kututia katika mikono ya Waamori, na kutuangamiza? Laiti tu, tungaliridhika kukaa ng'ambo ya Yordani Ee Bwana, niseme nini baada ya Israeli kuwapa visogo adui zao? Maana Wakanaani na wenyeji wote wa nchi hii watasikia habari hii, nao watatuzingira, na kulifuta jina letu katika nchi. Nawe utafanya nini kwa ajili ya jina lako kuu?
Yoshua 7:6-9 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Yoshua akararua mavazi yake, akaanguka kifudifudi mbele ya sanduku la BWANA hata jioni, yeye na wazee wa Israeli; wakatia mavumbi vichwani mwao. Yoshua akasema, Ee Bwana MUNGU, kwa nini umewavusha watu hawa mto wa Yordani, ili kututia katika mikono ya Waamori, na kutuangamiza? Laiti tungelikuwa radhi kukaa ng’ambo ya Yordani Ee Bwana, niseme nini baada ya Israeli kuwapa visogo adui zao? Maana Wakanaani na wenyeji wote wa nchi hii watasikia habari hii, nao watatuzingira, na kulifuta jina letu katika nchi. Nawe utafanya nini kwa ajili ya jina lako kuu?
Yoshua 7:6-9 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Ndipo Yoshua akayararua mavazi yake, akaanguka kifudifudi mbele ya Sanduku la BWANA, na akabakia hapo hadi jioni. Wazee wa Israeli nao wakafanya vivyo hivyo, wakatia mavumbi vichwani mwao. Yoshua akasema, “Ee BWANA Mwenyezi, kwa nini umewavusha watu hawa ngʼambo ya Yordani ili kututia mikononi mwa Waamori watuangamize? Laiti tungeridhika kukaa ngʼambo ile nyingine ya Yordani! Ee Bwana, niseme nini sasa, ikiwa sasa Israeli ameshafukuzwa na adui zake? Wakanaani na watu wengine wa nchi watasikia habari hii, nao watatuzunguka na kufutilia jina letu duniani. Utafanya nini basi kwa ajili ya jina lako mwenyewe lililo kuu?”