Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Yoshua 7:1-26

Yoshua 7:1-26 Biblia Habari Njema (BHN)

Lakini Waisraeli hawakuwa waaminifu kuhusu vile vitu vilivyotolewa viangamizwe kwani Akani mwana wa Karmi, mwana wa Zabdi, mwana wa Zera, wa kabila la Yuda, alichukua baadhi ya vitu vilivyoamriwa viteketezwe. Kwa hiyo hasira ya Mwenyezi-Mungu ikawaka dhidi ya Waisraeli. Yoshua akawatuma watu kutoka Yeriko kwenda mji wa Ai, ulio karibu ya Beth-aveni, mashariki ya Betheli, akawaambia, “Nendeni mkaipeleleze nchi.” Nao wakaenda na kuupeleleza mji wa Ai. Waliporudi, wakamwambia Yoshua, “Hakuna haja kupeleka watu wote kuushambulia mji wa Ai, maana wakazi wake ni wachache tu. Watu elfu mbili au tatu watatosha.” Basi, watu kama elfu tatu hivi wakaenda kuushambulia mji wa Ai, lakini wakakimbizwa na wakazi wa mji huo. Watu wa Ai wakawaua Waisraeli thelathini na sita na kuwafukuza wengine kutoka lango la mji mpaka Shebarimu, wakawaua kwenye mteremko. Waisraeli wakafa moyo na kulegea kama maji. Yoshua akayararua mavazi yake, yeye pamoja na wazee wa Israeli. Wakajitupa chini mbele ya sanduku la Mwenyezi-Mungu mpaka jioni; wakajitia mavumbi vichwani mwao. Yoshua akasema, “Ole wetu, ee Bwana Mungu! Kwa nini umetuvusha mto Yordani ili kututia mikononi mwa Waamori watuangamize? Tungaliridhika kubaki ngambo ya mto Yordani! Ee Bwana, niseme nini hali Waisraeli wamewakimbia adui zao? Basi, Wakanaani pamoja na wakazi wote wa nchi hii watakapopata habari hiyo watatuzingira na kutufuta kabisa duniani. Sasa utafanya nini kuonesha ukuu wa jina lako?” Mwenyezi-Mungu akamwambia Yoshua, “Simama! Mbona umejitupa chini hivyo? Waisraeli wametenda dhambi, maana wamelivunja agano langu nililowaamuru washike; wamevichukua baadhi ya vitu vilivyowekwa wakfu viangamizwe; wameviiba na kudanganya, wakaviweka pamoja na vitu vyao. Kwa hiyo Waisraeli hawawezi kuwakabili maadui zao; wanawakimbia adui zao kwa sababu wamejifanya wenyewe kuwa kitu cha kuangamizwa! Sitakuwa pamoja nao tena msipoharibu vitu vilivyomo kati yenu vilivyotolewa viangamizwe. Basi, inuka uwatakase watu, waambie wajitakase na kujitayarisha kwa siku ya kesho, maana mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, nasema hivi: ‘Miongoni mwenu kuna vitu vilivyotolewa viangamizwe; hamwezi kuwakabili adui zenu mpaka vitu hivyo vimeondolewa kati yenu! Kwa hiyo kesho asubuhi wote mtakuja mbele yangu, kabila baada ya kabila. Kabila nitakalolichagua litakwenda mbele, ukoo baada ya ukoo. Ukoo nitakaouchagua utakwenda mbele, jamaa baada ya jamaa. Na jamaa nitakayoichagua itakwenda mbele, mtu mmojammoja. Mtu yeyote atakayepatikana akiwa na vitu vilivyotolewa viangamizwe atateketezwa kwa moto, yeye pamoja na kila kitu chake maana ameliasi agano langu mimi Mwenyezi-Mungu, akatenda jambo la aibu katika Israeli.’” Basi, Yoshua akaamka asubuhi na mapema, akawaleta Waisraeli wote karibu, kabila baada ya kabila; kabila la Yuda likachaguliwa. Akazileta karibu koo za Yuda, ukoo baada ya ukoo; na ukoo wa Zerahi ukachaguliwa. Akazileta karibu jamaa za ukoo wa Zerahi, jamaa baada ya jamaa; na jamaa ya Zabdi ikachaguliwa. Yoshua akaileta jamaa ya Zabdi karibu, nyumba baada ya nyumba; na nyumba ya Akani mwana wa Karmi, mwana wa Zabdi, mwana wa Zera, wa kabila la Yuda, ikachaguliwa. Yoshua akamwambia Akani, “Mwanangu, mtukuze Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, msifu na kisha uniambie yale uliyotenda, wala usinifiche.” Akani akamjibu; “Ni kweli nimetenda dhambi mbele ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli. Na hivi ndivyo nilivyofanya: Nilipoona vazi moja zuri kutoka Shinari kati ya nyara, shekeli 200 za fedha na mchi wa dhahabu wenye uzito wa shekeli 50, nikavitamani na kuvichukua; nimevificha ardhini ndani ya hema langu; na fedha iko chini ya vitu hivyo.” Basi, Yoshua akawatuma wajumbe, nao wakakimbia hemani kwa Akani. Na kumbe, vilikuwa vimefichwa hemani na fedha ikiwa chini yake. Wakavichukua hemani na kuvipeleka kwa Yoshua na watu wote wa Israeli; nao wakaviweka chini, mbele ya Mwenyezi-Mungu. Yoshua pamoja na Waisraeli wote, wakamchukua Akani, mwana wa Zera, pamoja na fedha, vazi, dhahabu, watoto wake wa kiume na binti zake, ng'ombe, punda na kondoo wake, hema lake na kila kitu alichokuwa nacho na kuwapeleka kwenye bonde la Akori. Yoshua akamwuliza Akani, “Kwa nini umetuletea taabu? Mwenyezi-Mungu atakuletea taabu wewe mwenyewe leo.” Waisraeli wote wakampiga Akani kwa mawe mpaka akafa. Kisha wakawapiga jamaa yake yote kwa mawe mpaka wakafa, wakawateketeza wote kwa moto. Halafu wakarundika mawe mengi juu yake, ambayo yako hadi leo. Hapo hasira ya Mwenyezi-Mungu ikapoa; na mahali hapo pakaitwa Bonde la Akori mpaka hivi leo.

Shirikisha
Soma Yoshua 7

Yoshua 7:1-26 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Lakini Waisraeli walifanya dhambi katika kitu kilichowekwa wakfu; maana Akani, mwana wa Karmi, mwana wa Zabdi, mwana wa Zera, wa kabila la Yuda, alitwaa baadhi ya vitu vilivyowekwa wakfu; hasira ya BWANA ikawaka juu ya Waisraeli. Kisha Yoshua akatuma watu kutoka Yeriko mpaka mji wa Ai, ulio karibu na Beth-aveni, upande wa mashariki wa Betheli, akawaambia, akisema, Pandeni juu mkaipeleleze nchi, basi wakapanda juu wakaupeleleza Ai. Wakarejea kwa Yoshua wakamwambia, Wasiende watu wote, ila waende watu kama elfu mbili, tatu, wakaupige Ai; usiwataabishe watu wote kwenda huko maana watu hao ni wachache tu. Basi watu wakaenda huko wapata elfu tatu tu; nao wakakimbizwa na wakazi wa mji wa Ai. Watu wa Ai wakawapiga watu kama thelathini na sita; wakawafuatia kutoka mbele ya mlango mpaka Shebarimu, wakawapiga huko kwenye materemko; mioyo ya watu ikayeyuka, ikawa kama maji. Yoshua akararua mavazi yake, akaanguka kifudifudi mbele ya sanduku la BWANA hadi jioni, yeye na wazee wa Israeli; wakatia mavumbi vichwani mwao. Yoshua akasema, Ee Bwana MUNGU, kwa nini umewavusha watu hawa mto wa Yordani, ili kututia katika mikono ya Waamori, na kutuangamiza? Laiti tu, tungaliridhika kukaa ng'ambo ya Yordani Ee Bwana, niseme nini baada ya Israeli kuwapa visogo adui zao? Maana Wakanaani na wenyeji wote wa nchi hii watasikia habari hii, nao watatuzingira, na kulifuta jina letu katika nchi. Nawe utafanya nini kwa ajili ya jina lako kuu? BWANA akamwambia Yoshua, Haya! Inuka, mbona umeanguka kifudifudi hivi? Israeli wamefanya dhambi, naam, wamelivunja agano langu nililowaagiza; naam, wametwaa baadhi ya vitu vilivyowekwa wakfu; tena wameiba, tena wameficha na kuvitia pamoja na vitu vyao wenyewe. Ndiposa wana wa Israeli hawawezi kusimama mbele ya adui zao; wakawapa visogo adui zao, kwa sababu wamelaaniwa; mimi sitakuwa pamoja nanyi tena, msipokiharibu kitu kile mlicho nacho kilichowekwa wakfu. Haya! Inuka, uwatakase watu, ukaseme, Jitakaseni, muwe tayari kesho; maana BWANA, Mungu wa Israeli, asema hivi; Kitu kilichowekwa wakfu kiko katikati yako, Ee Israeli; huwezi kusimama mbele ya adui zako, hata mtakapokiondoa kile mlicho nacho kilichowekwa wakfu. Basi asubuhi mtaletwa karibu nami kabila kwa kabila; kisha itakuwa ya kwamba kabila ile atakayoitwaa BWANA itakaribia jamaa kwa jamaa; na jamaa ile atakayoitwaa BWANA itakaribia nyumba kwa nyumba; na nyumba ile atakayoitwaa BWANA itakaribia mtu kwa mtu. Tena itakuwa ya kwamba yeye atakayetwaliwa, naye anacho kitu kile kilichowekwa wakfu, atateketezwa kwa moto, yeye na vitu vyote alivyo navyo; kwa sababu amelivunja agano la BWANA, na kwa sababu ametenda upumbavu katika Israeli. Basi Yoshua akaondoka asubuhi na mapema, akawasongeza Israeli kabila kwa kabila; kabila la Yuda likatwaliwa. Akazisongeza jamaa za Yuda, akaitwaa jamaa ya Wazera; akaisongeza jamaa ya Wazera mtu kwa mtu; Zabdi akatwaliwa. Akawasongeza watu wa nyumba yake mmoja mmoja; na Akani, mwana wa Karmi, mwana wa Zabdi, mwana wa Zera, wa kabila la Yuda akatwaliwa. Yoshua akamwambia Akani, Mwanangu, nakusihi, umtukuze BWANA, Mungu wa Israeli, ukaungame kwake; uniambie sasa ulilolitenda; usinifiche. Akani akamjibu Yoshua, akasema, Kweli nimefanya dhambi juu ya BWANA, Mungu wa Israeli, nami nimefanya mambo haya na haya. Nilipoona katika nyara joho zuri ya Babeli, na shekeli mia mbili za fedha, na kabari ya dhahabu, uzani wake shekeli hamsini, basi nilivitamani nikavitwaa; tazama, vimefichwa mchangani katikati ya hema yangu, na ile fedha chini yake. Basi Yoshua akatuma wajumbe wakapiga mbio mpaka hemani; na tazama, vile vitu vilikuwa vimefichwa hemani mwake, na ile fedha chini yake. Wakavitoa kutoka hapo katikati ya hema, wakavileta kwa Yoshua, na kwa wana wa Israeli wote, nao wakaviweka chini mbele za BWANA. Kisha Yoshua, na Israeli wote pamoja naye, wakamtwaa Akani, mwana wa Zera, na ile fedha, na Lile joho, na ile kabari ya dhahabu, na wanawe, na binti zake, na ng'ombe wake, punda wake na kondoo wake, hema yake na vitu vyote alivyokuwa navyo, wakavileta juu hadi bonde la Akori. Yoshua akasema, Mbona umetufadhaisha hivi? BWANA atakufadhaisha wewe leo. Ndipo Israeli wote wakampiga kwa mawe, kisha wakawateketeza kwa moto, na kuwapiga kwa mawe. Kisha wakakusanya juu yake rundo kubwa la mawe hata leo; naye BWANA akauacha ukali wa hasira yake. Kwa sababu hiyo jina la mahali pale likaitwa, Bonde la Akori, hata leo.

Shirikisha
Soma Yoshua 7

Yoshua 7:1-26 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Lakini wana wa Israeli walifanya dhambi katika kitu kilichowekwa wakfu; maana Akani, mwana wa Karmi, mwana wa Zabdi, mwana wa Zera, wa kabila ya Yuda, alitwaa baadhi ya vitu vilivyowekwa wakfu; hasira ya BWANA ikawaka juu ya wana wa Israeli. Kisha Yoshua akatuma watu kutoka Yeriko mpaka mji wa Ai, ulio karibu na Bethaveni, upande wa mashariki wa Betheli, akawaambia, akisema, Pandeni juu mkaipeleleze nchi, basi wakapanda juu wakaupeleleza Ai. Wakarejea kwa Yoshua wakamwambia, Wasiende watu wote, ila waende watu kama elfu mbili, tatu, wakaupige Ai; usiwataabishe watu wote kwa kuwaendesha huko; maana watu hao ni wachache tu. Basi watu wakaenda huko wapata elfu tatu tu; nao wakakimbia mbele ya watu wa Ai. Watu wa Ai wakawapiga watu kama thelathini na sita; wakawafuatia kutoka mbele ya mlango mpaka Shebarimu, wakawapiga huko kwenye matelemko; mioyo ya watu ikayeyuka, ikawa kama maji. Yoshua akararua mavazi yake, akaanguka kifudifudi mbele ya sanduku la BWANA hata jioni, yeye na wazee wa Israeli; wakatia mavumbi vichwani mwao. Yoshua akasema, Ee Bwana MUNGU, kwa nini umewavusha watu hawa mto wa Yordani, ili kututia katika mikono ya Waamori, na kutuangamiza? Laiti tungelikuwa radhi kukaa ng’ambo ya Yordani Ee Bwana, niseme nini baada ya Israeli kuwapa visogo adui zao? Maana Wakanaani na wenyeji wote wa nchi hii watasikia habari hii, nao watatuzingira, na kulifuta jina letu katika nchi. Nawe utafanya nini kwa ajili ya jina lako kuu? BWANA akamwambia Yoshua, Haya! Inuka, mbona umeanguka kifudifudi hivi? Israeli wamefanya dhambi, naam, wamelivunja agano langu nililowaagiza; naam, wametwaa baadhi ya vitu vilivyowekwa wakfu; tena wameiba, tena wameficha na kuvitia pamoja na vitu vyao wenyewe. Ndiposa wana wa Israeli hawawezi kusimama mbele ya adui zao; wakawapa visogo adui zao, kwa sababu wamelaaniwa; mimi sitakuwa pamoja nanyi tena, msipokiharibu kitu kile mlicho nacho kilichowekwa wakfu. Haya! Inuka, uwatakase watu, ukaseme, Jitakaseni, mwe tayari kesho; maana BWANA, Mungu wa Israeli, asema hivi; Kitu kilichowekwa wakfu kiko katikati yako, Ee Israeli; huwezi kusimama mbele ya adui zako, hata mtakapokiondoa kile mlicho nacho kilichowekwa wakfu. Basi asubuhi mtaletwa karibu nami kabila kwa kabila; kisha itakuwa ya kwamba kabila ile atakayoitwaa BWANA itakaribia jamaa kwa jamaa; na jamaa ile atakayoitwaa BWANA itakaribia nyumba kwa nyumba; na nyumba ile atakayoitwaa BWANA itakaribia mtu kwa mtu. Tena itakuwa ya kwamba yeye atakayetwaliwa, naye anacho kitu kile kilichowekwa wakfu, atateketezwa kwa moto, yeye na vitu vyote alivyo navyo; kwa sababu amelivunja agano la BWANA, na kwa sababu ametenda upumbavu katika Israeli. Basi Yoshua akaondoka asubuhi na mapema, akawasogeza Israeli kabila kwa kabila; kabila ya Yuda ikatwaliwa. Akazisogeza jamaa za Yuda, akaitwaa jamaa ya Wazera; akaisogeza jamaa ya Wazera mtu kwa mtu; Zabdi akatwaliwa. Akawasogeza watu wa nyumba yake mmoja mmoja; na Akani, mwana wa Karmi, mwana wa Zabdi, mwana wa Zera, wa kabila ya Yuda akatwaliwa. Yoshua akamwambia Akani, Mwanangu, nakusihi, umtukuze BWANA, Mungu wa Israeli, ukaungame kwake; uniambie sasa ulilolitenda; usinifiche. Akani akamjibu Yoshua, akasema, Kweli nimefanya dhambi juu ya BWANA, Mungu wa Israeli, nami nimefanya mambo haya na haya. Nilipoona katika nyara joho nzuri ya Babeli, na shekeli mia mbili za fedha, na kabari ya dhahabu, uzani wake shekeli hamsini, basi nalivitamani nikavitwaa; tazama, vimefichwa mchangani katikati ya hema yangu, na ile fedha chini yake. Basi Yoshua akatuma wajumbe wakapiga mbio mpaka hemani; na tazama, vile vitu vilikuwa vimefichwa hemani mwake, na ile fedha chini yake. Wakavitoa kutoka hapo katikati ya hema, wakavileta kwa Yoshua, na kwa wana wa Israeli wote, nao wakaviweka chini mbele za BWANA. Kisha Yoshua, na Israeli wote pamoja naye, wakamtwaa Akani, mwana wa Zera, na ile fedha, na Lile joho, na ile kabari ya dhahabu, na wanawe, na binti zake, na ng’ombe zake, na punda zake, na kondoo zake, na hema yake, na vitu vyote alivyokuwa navyo, wakavileta juu hata bonde la Akori. Yoshua akasema, Mbona umetufadhaisha hivi? BWANA atakufadhaisha wewe leo. Ndipo Israeli wote wakampiga kwa mawe, kisha wakawateketeza kwa moto, na kuwapiga kwa mawe. Kisha wakakusanya juu yake chungu kubwa ya mawe hata leo; naye BWANA akauacha ukali wa hasira yake. Kwa sababu hiyo jina la mahali pale likaitwa, Bonde la Akori, hata hivi leo.

Shirikisha
Soma Yoshua 7

Yoshua 7:1-26 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)

Lakini Waisraeli hawakuwa waaminifu kuhusu vile vitu vilivyotengwa kwa ajili ya kuangamizwa; Akani mwana wa Karmi, mwana wa Zabdi, mwana wa Zera, wa kabila la Yuda, alivichukua baadhi ya hivyo vitu. Hasira ya BWANA ikawaka dhidi ya Israeli. Basi Yoshua akatuma watu kutoka Yeriko waende Ai, karibu na Beth-Aveni mashariki mwa Betheli, akawaambia, “Pandeni mkaipeleleze nchi.” Basi wale watu wakapanda wakaipeleleza Ai. Waliporudi kwa Yoshua, wakasema, “Si lazima watu wote waende kupigana na Ai. Watume watu elfu mbili au tatu wakauteke huo mji. Usiwachoshe watu wote, kwa sababu huko kuna watu wachache tu.” Basi wakapanda kama wanaume elfu tatu tu, lakini wakashambuliwa na wanaume wa Ai, ambao waliwaua wanaume kama thelathini na sita miongoni mwao. Wakawafukuza Waisraeli kutoka lango la mji hadi Shebarimu, nao wakawauwa huko kwenye miteremko. Kutokana na hili mioyo ya watu ikayeyuka kwa hofu, ikawa kama maji. Ndipo Yoshua akayararua mavazi yake, akaanguka kifudifudi mbele ya Sanduku la BWANA, na akabakia hapo hadi jioni. Wazee wa Israeli nao wakafanya vivyo hivyo, wakatia mavumbi vichwani mwao. Yoshua akasema, “Ee BWANA Mwenyezi, kwa nini umewavusha watu hawa ngʼambo ya Yordani ili kututia mikononi mwa Waamori watuangamize? Laiti tungeridhika kukaa ngʼambo ile nyingine ya Yordani! Ee Bwana, niseme nini sasa, ikiwa sasa Israeli ameshafukuzwa na adui zake? Wakanaani na watu wengine wa nchi watasikia habari hii, nao watatuzunguka na kufutilia jina letu duniani. Utafanya nini basi kwa ajili ya jina lako mwenyewe lililo kuu?” BWANA akamwambia Yoshua, “Simama! Unafanya nini ukilala kifudifudi? Israeli ametenda dhambi. Wamekiuka agano langu nililowaamuru kulishika. Wamechukua baadhi ya vitu vilivyotengwa kwa ajili ya kuangamizwa; wameiba, wamesema uongo, na wameviweka pamoja na mali yao. Ndiyo sababu Waisraeli hawawezi kusimama dhidi ya adui zao. Wanawapa visogo na kukimbia kwa kuwa wanastahili maangamizi. Sitakuwa pamoja nanyi tena hadi mwangamize kila kitu miongoni mwenu kilichotengwa kwa maangamizi. “Nenda, ukawatakase watu. Waambie, ‘Jitakaseni mjiandae kwa ajili ya kesho; kwa sababu hili ndilo asemalo BWANA, Mungu wa Israeli: Vitu vilivyotengwa kwa ajili ya kuangamizwa vimo kati yenu, ee Israeli. Hamwezi kusimama dhidi ya adui zenu hadi mtakapoviondoa. “ ‘Asubuhi, mtakuja kabila kwa kabila. Kisha kabila atakalolichagua BWANA watakuja mbele kufuatana na koo zao; nao ukoo atakaouchagua BWANA watakuja mbele jamaa kwa jamaa, nayo jamaa atakayoichagua BWANA watakuja mbele mtu kwa mtu. Yule atakayekutwa na vitu vilivyotengwa kwa ajili ya kuangamizwa, atateketezwa kwa moto pamoja na vitu vyote alivyo navyo. Kwa kuwa amelivunja agano la BWANA na kufanya kitu cha aibu katika Israeli!’ ” Kesho yake asubuhi na mapema Yoshua akaamuru Israeli kuja mbele kabila kwa kabila; na kabila la Yuda likachaguliwa. Koo za Yuda zikaja mbele, naye akawachagua Wazera. Akaamuru ukoo wa Wazera kuja mbele jamaa kwa jamaa, nayo jamaa ya Zabdi ikachaguliwa. Yoshua akaamuru jamaa ya Zabdi kuja mbele mtu kwa mtu, naye Akani mwana wa Karmi, mwana wa Zabdi, mwana wa Zera, wa kabila la Yuda, akachaguliwa. Ndipo Yoshua akamwambia Akani, “Mwanangu, mtukuze BWANA, Mungu wa Israeli, nawe ukiri kwake. Niambie ni nini ulichotenda; usinifiche.” Akani akamjibu Yoshua, “Ni kweli! Nimetenda dhambi dhidi ya BWANA, Mungu wa Israeli. Hili ndilo nililofanya: Nilipoona katika nyara joho zuri la kutoka Babeli, shekeli mia mbili za fedha, na kabari ya dhahabu ya uzito wa shekeli hamsini, nikavitamani na nikavichukua. Tazama, vimefichwa ardhini ndani ya hema langu, pamoja na hiyo fedha chini yake.” Kwa hiyo Yoshua akatuma wajumbe, nao wakakimbia hadi kwenye hema. Tazama, vile vitu vilikuwa vimefichwa kwenye hema lake, pamoja na ile fedha chini yake. Wakavichukua vile vitu toka kwenye hema, wakamletea Yoshua pamoja na Waisraeli wote, wakavitandaza mbele za BWANA. Basi Yoshua, pamoja na Israeli yote, wakamchukua Akani mwana wa Zera, pamoja na ile fedha, lile joho, ile kabari ya dhahabu, wanawe wa kiume na wa kike, ngʼombe, punda na kondoo wake, hema lake pamoja na vitu vyote alivyokuwa navyo, wakavileta katika Bonde la Akori. Yoshua akasema, “Kwa nini umetuletea taabu hii? BWANA atakuletea taabu leo.” Ndipo Israeli yote ikampiga Akani kwa mawe, na baada ya kuwapiga jamaa yake yote kwa mawe, wakawateketeza kwa moto. Wakakusanya lundo la mawe juu ya Akani, ambalo lipo hadi leo. Naye BWANA akageuka kutoka hasira yake kali. Kwa hiyo mahali pale pakaitwa Bonde la Akori tangu siku hiyo.

Shirikisha
Soma Yoshua 7