Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Yoshua 6:8-21

Yoshua 6:8-21 Biblia Habari Njema (BHN)

Kulingana na amri ya Yoshua, wale makuhani saba waliokuwa na mabaragumu saba ya kondoo dume wakaenda mbele ya Mwenyezi-Mungu, wakiwa wanapiga mabaragumu, nyuma yao wakifuatwa na lile sanduku la agano. Wale watu wenye silaha wakawatangulia wale makuhani ambao walikuwa wanapiga mabaragumu, na walinzi wengine wakifuata nyuma ya sanduku hilo, huku mabaragumu yakilia kwa mfululizo. Lakini Yoshua akawaamuru watu, “Msipige kelele au kutoa sauti, wala neno lolote lisitoke vinywani mwenu, mpaka siku ile ambapo nitawaambieni mpige kelele; wakati huo ndipo mtakapopiga kelele.” Basi, Yoshua aliwafanya wale watu wauzunguke mji mara moja kila siku wakiwa wamebeba sanduku la agano la Mwenyezi-Mungu na kurudi kambini kulala usiku. Asubuhi yake Yoshua akaamka alfajiri na mapema, na makuhani wakalibeba lile sanduku la agano la Mwenyezi-Mungu. Wale makuhani saba wenye mabaragumu saba za kondoo dume walitembea mbele ya sanduku la Mwenyezi-Mungu wakipiga mabaragumu mfululizo. Watu wenye silaha walilitangulia sanduku la Mwenyezi-Mungu na walinzi wengine nyuma yake. Mabaragumu yakaendelea kupigwa. Siku ya pili yake waliuzunguka huo mji mara moja; na kurudi tena kambini kwao. Walifanya hivyo kwa muda wa siku sita. Siku ya saba, waliamka alfajiri na mapema, wakauzunguka mji huo mara saba kwa namna ileile. Ilikuwa ni siku hiyo tu ambayo waliuzunguka mji huo mara saba. Ilipofika mara ya saba, wakati makuhani walipokwisha piga mabaragumu, Yoshua akawaambia watu, “Pigeni kelele, kwa kuwa Mwenyezi-Mungu amekwisha wapeni huu mji! Mji huo utaangamizwa na kila kitu kilichomo kwani umewekwa wakfu kwa Mwenyezi-Mungu. Rahabu, yule kahaba, ndiye atakayesalimishwa pamoja na wale ambao wamo nyumbani mwake kwa kuwa aliwaficha wapelelezi wetu. Lakini msichukue chochote ambacho kimewekwa wakfu ili kiangamizwe, mkichukua kitu chochote ambacho kimewekwa wakfu ili kiangamizwe mtaifanya kambi ya Israeli kuwa kitu cha kuangamizwa, na hivyo kuiletea balaa. Lakini fedha yote, dhahabu, vyombo vya shaba na chuma ni vitakatifu kwa Mwenyezi-Mungu; hivyo vitawekwa katika hazina ya Mwenyezi-Mungu.” Basi, watu wakapiga kelele huku mabaragumu yanapigwa. Watu waliposikia sauti ya mabaragumu walipiga kelele kubwa, na kuta za mji zikaanguka chini kabisa. Mara watu wakauvamia mji, kila mmoja kutoka mahali aliposimama, wakauteka. Kisha wakaangamiza kila kitu mjini humo na kuwaua kwa upanga: Wanaume na wanawake, vijana na wazee, ng'ombe, kondoo na punda.

Shirikisha
Soma Yoshua 6

Yoshua 6:8-21 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Basi ikawa Yoshua alipokwisha kusema na watu, wale makuhani saba, wenye kuzichukua baragumu saba za pembe za kondoo dume mbele za BWANA, watatangulia, wakayapiga hayo mabaragumu; nalo sanduku la Agano la BWANA likawafuata. Wale watu wenye silaha walikwenda mbele ya hao makuhani walioyapiga mabaragumu, na wale waliokuwa nyuma wakalifuata hilo sanduku; makuhani wakiyapiga mabaragumu walipokuwa wakienda. Yoshua akawaamuru watu, akasema Msipige kelele, wala sauti zenu zisisikiwe, wala neno lolote lisitoke kinywani mwenu, hadi siku ile nitakapowaamuru kupiga kelele, ndipo mtakapopiga kelele. Basi akalipeleka sanduku la BWANA liuzunguke huo mji, likauzunguka mara moja, kisha wakaenda kambini wakakaa humo kambini. Yoshua akaondoka asubuhi na mapema, nao makuhani wakalichukua sanduku la BWANA. Na wale makuhani saba wakayachukua mabaragumu saba ya pembe za kondoo dume mbele ya sanduku la BWANA, wakaenda huku wakiyapiga mabaragumu; nao watu wenye silaha wakawatangulia, na hao waliokuwa nyuma wakalifuata sanduku la BWANA; huku makuhani wakiyapiga mabaragumu bila kukoma. Siku ya pili wakauzunguka mji mara moja, wakarejea kambini; ndivyo walivyofanya siku sita. Ikawa siku ya saba wakaondoka asubuhi na mapema wakati wa mapambazuko, wakauzunguka mji vivyo hivyo mara saba; ni siku hiyo tu ambapo waliuzunguka huo mji mara saba. Hata mara ya saba makuhani wakayapiga mabaragumu, Yoshua akawaambia watu, Pigeni kelele; kwa maana BWANA amewapeni mji huu. Na mji huu utakuwa wakfu kwa BWANA, mji wenyewe na vitu vyote vilivyomo; isipokuwa Rahabu, yule kahaba, ataishi, yeye na watu wote walio pamoja naye nyumbani, kwa sababu aliwaficha hao wapelelezi tuliowatuma. Na ninyi, msikose kujiepusha na kitu kilichowekwa wakfu; msije mkakitwaa kitu kilichowekwa wakfu, baada ya kukiweka wakfu; nanyi hivyo mtaifanya kambi ya Israeli kuwa imelaaniwa na kuifadhaisha. Lakini fedha yote, na dhahabu, na vyombo vya shaba, na chuma, ni vitakatifu kwa BWANA; vitaletwa katika hazina ya BWANA. Basi watu wakapiga kelele, na makuhani wakazipiga tarumbeta; hata ikawa, hapo watu waliposikia mlio wa mabaragumu hao watu wakapiga kelele kwa sauti kuu sana, na ule ukuta wa mji ukaanguka chini kabisa, hata watu wakapanda juu, wakaingia katika mji, kila mtu akisonga mbele kukabili; wakautwaa huo mji. Basi wakaangamiza kabisa vitu vyote vilivyokuwa ndani ya mji, wanaume, wanawake, watoto na wazee, na ng'ombe, kondoo na punda, kwa upanga.

Shirikisha
Soma Yoshua 6

Yoshua 6:8-21 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Basi ikawa Yoshua alipokwisha kusema na watu, wale makuhani saba, wenye kuzichukua tarumbeta saba za pembe za kondoo waume mbele za BWANA, wakatangulia, wakazipiga hizo tarumbeta; nalo sanduku la agano la BWANA likawafuata. Wale watu wenye silaha walikwenda mbele ya hao makuhani waliozipiga tarumbeta, na wale waliokuwa nyuma wakalifuata hilo sanduku; makuhani wakizipiga tarumbeta walipokuwa wakienda. Yoshua akawaamuru watu, akasema Msipige kelele, wala sauti zenu zisisikiwe, wala neno lo lote lisitoke kinywani mwenu, hata siku ile nitakapowaamuru kupiga kelele, ndipo mtakapopiga kelele. Basi akalipeleka sanduku la BWANA liuzunguke huo mji, likauzunguka mara moja, kisha wakaenda kambini wakakaa kambini. Yoshua akaondoka asubuhi na mapema, nao makuhani wakalichukua sanduku la BWANA. Na wale makuhani saba wakazichukua tarumbeta saba za pembe za kondoo waume mbele ya sanduku la BWANA, wakaendelea wakazipiga tarumbeta; nao watu wenye silaha wakawatangulia, na hao waliokuwa nyuma wakalifuata sanduku la BWANA; makuhani wakizipiga tarumbeta walipokuwa wakienda. Siku ya pili wakauzunguka mji mara moja, wakarejea kambini; ndivyo walivyofanya siku sita. Ikawa siku ya saba wakaondoka asubuhi na mapema wakati wa mapambazuko, wakauzunguka mji vivyo hivyo mara saba; ila siku hiyo waliuzunguka huo mji mara saba. Hata mara ya saba makuhani walipozipiga tarumbeta, Yoshua akawaambia watu, Pigeni kelele; kwa maana BWANA amewapeni mji huu. Na mji huu utakuwa wakfu kwa BWANA, mji wenyewe na vitu vyote vilivyomo; isipokuwa Rahabu, yule kahaba, ataishi, yeye na watu wote walio pamoja naye nyumbani, kwa sababu aliwaficha hao wapelelezi tuliowatuma. Na ninyi, msikose kujiepusha na kitu kilichowekwa wakfu; msije mkakitwaa kitu kilichowekwa wakfu, baada ya kukiweka wakfu; nanyi hivyo mtayafanya matuo ya Israeli kuwa yamelaaniwa na kuyafadhaisha. Lakini fedha yote, na dhahabu, na vyombo vya shaba, na chuma, ni vitakatifu kwa BWANA; vitaletwa katika hazina ya BWANA. Basi watu wakapiga kelele, na makuhani wakazipiga tarumbeta; hata ikawa, hapo watu waliposikia sauti ya tarumbeta hao watu wakapiga kelele kwa sauti kuu sana, na ule ukuta wa mji ukaanguka nchi kabisa, hata watu wakapanda juu, wakaingia katika mji, kila mtu akiendelea kukabili mbele; wakautwaa huo mji. Basi wakaangamiza kabisa vitu vyote vilivyokuwa ndani ya mji, wanaume na wanawake, watoto na wazee, na ng’ombe, na kondoo, na punda, kwa makali ya upanga.

Shirikisha
Soma Yoshua 6

Yoshua 6:8-21 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)

Baada ya Yoshua kuzungumza na watu, wale makuhani saba waliozibeba zile baragumu saba mbele za BWANA, wakatangulia mbele, wakipiga baragumu zao na Sanduku la Agano la BWANA likawafuata. Walinzi waliokuwa na silaha wakaenda mbele ya hao makuhani waliopiga hizo baragumu na hao walinzi wa nyuma wakafuata Sanduku. Wakati wote huu baragumu zilikuwa zikipigwa. Bali Yoshua alikuwa amewaagiza watu, “Msipige ukelele wa vita; msipaze sauti zenu, wala kusema neno lolote hadi siku ile nitakayowaambia mpige kelele. Ndipo mtapiga kelele!” Basi akalipeleka Sanduku la BWANA kuzungushwa huo mji, likizungushwa mara moja. Kisha watu wakarudi kambini kulala. Yoshua akaamka asubuhi na mapema siku iliyofuata, nao makuhani wakalichukua Sanduku la BWANA. Wale Makuhani saba waliobeba zile baragumu saba wakatangulia mbele ya Sanduku la BWANA wakizipiga. Watu wenye silaha wakatangulia mbele yao na walinzi wa nyuma wakalifuata Sanduku la BWANA, huku baragumu hizo zikiendelea kulia. Siku ya pili wakauzunguka mji mara moja na kurudi kambini. Wakafanya hivi kwa siku sita. Siku ya saba, wakaamka asubuhi na mapema wakauzunguka mji kama walivyokuwa wakifanya, isipokuwa siku ile waliuzunguka mji mara saba. Walipouzunguka mara ya saba, makuhani walipiga baragumu kwa sauti kubwa, naye Yoshua akawaamuru watu akisema, “Pigeni kelele! Kwa maana BWANA amewapa mji huu! Mji huu pamoja na vyote vilivyomo utatengewa BWANA kwa ajili ya kuangamizwa. Rahabu yule kahaba atasalimishwa, pamoja na wote walio naye nyumbani mwake, kwa sababu aliwaficha wale wapelelezi tuliowatuma. Lakini mjiepushe na vitu vilivyotengwa kwa ajili ya kuangamizwa, msije mkajiletea maangamizi kwa kuchukua chochote katika hivyo; la sivyo, mtailetea kambi ya Israeli maangamizi na taabu. Fedha yote na dhahabu, vyombo vya shaba na chuma ni vitakatifu kwa BWANA, lazima viletwe katika hazina yake.” Baragumu zilipopigwa, watu walipiga kelele; kwa ile sauti ya baragumu na watu kupaza sauti, ukuta ukaanguka; hivyo kila mtu akapanda akiendelea mbele na kuuteka mji. Wakauweka mji wakfu kwa BWANA, na kila chenye uhai ndani yake walikiangamiza kwa upanga: wanaume na wanawake, vijana kwa wazee, ngʼombe, kondoo na punda.

Shirikisha
Soma Yoshua 6