Yoshua 6:1-7
Yoshua 6:1-7 Biblia Habari Njema (BHN)
Milango ya kuingilia mjini Yeriko ilikuwa imefungwa imara kwa ndani kuwazuia Waisraeli wasiingie. Hakuna mtu aliyeweza kuingia wala kutoka katika mji huo. Mwenyezi-Mungu akamwambia Yoshua, “Angalia! Mimi nitautia mikononi mwako mji wa Yeriko pamoja na mfalme wake na askari wake shujaa. Wewe na wale watu wenye silaha wote mtauzunguka huo mji mara moja kila siku kwa siku sita. Makuhani saba, kila mmoja akiwa amechukua baragumu yake ya pembe za kondoo dume, watatangulia mbele ya sanduku la agano. Katika siku ya saba mtauzunguka mji huo mara saba, huku makuhani wakipiga mabaragumu. Watakapopiga hayo mabaragumu kwa mlio mkubwa na mara tu mtakaposikia huo mlio, watu wote watapiga kelele kubwa, nazo kuta za mji zitaanguka chini. Ndipo watu watauvamia mji kila mmoja kutoka mahali aliposimama.” Basi, Yoshua, mwana wa Nuni, akawaita makuhani, akawaambia, “Libebeni sanduku la agano na makuhani saba wachukue mabaragumu saba za kondoo dume, watangulie mbele ya sanduku la Mwenyezi-Mungu.” Yoshua akawaambia watu, “Nendeni mbele; uzungukeni mji, nao watu wenye silaha waende mbele ya sanduku la agano la Mwenyezi-Mungu.”
Yoshua 6:1-7 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Basi Yeriko ulikuwa umefungwa kabisa kwa sababu ya Waisraeli; hapana mtu aliyetoka wala hapana mtu aliyeingia. BWANA akamwambia Yoshua, Tazama, nimeutia Yeriko katika mkono wako, na mfalme wake, na mashujaa wake. Nanyi mtauzunguka mji huu, wapiganaji wote, mkiuzunguka mji mara moja. Fanya hivi siku sita. Na makuhani saba watachukua baragumu saba za pembe za kondoo dume, watatangulia mbele za hilo sanduku; na siku ya saba mtauzunguka mji mara saba, nao makuhani watapiga baragumu zao. Kisha itakuwa watakapopiga hizo pembe za kondoo dume kwa nguvu, nanyi mtakaposikia kwa mlio wa baragumu, watu wote watapiga kelele kwa sauti kuu; na ukuta wa mji utaanguka chini pale pale, na hao watu watapanda, kila mtu akiendelea mbele kukabili. Bali Yoshua, mwana wa Nuni, akawaita makuhani, akawaambia, Lichukueni sanduku la Agano, tena makuhani saba na wachukue mabaragumu saba za pembe za kondoo dume watangulie mbele ya sanduku la BWANA. Naye akawaambia watu, Piteni mbele, mkauzunguke mji, na hao watu wenye silaha na watangulie mbele ya sanduku la BWANA.
Yoshua 6:1-7 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Basi Yeriko ulikuwa umefungwa kabisa kwa sababu ya wana wa Israeli; hapana mtu aliyetoka wala hapana mtu aliyeingia. BWANA akamwambia Yoshua, Tazama, nimeutia Yeriko katika mkono wako, na mfalme wake, na mashujaa wake. Nanyi mtauzunguka mji huu, watu wote wa vita, mkiuzunguka mji mara moja. Fanya hivi siku sita. Na makuhani saba watachukua tarumbeta saba za pembe za kondoo waume, mbele ya hilo sanduku; na siku ya saba mtauzunguka mji mara saba, nao makuhani watapiga tarumbeta zao. Kisha itakuwa watakapopiga hizo pembe za kondoo waume kwa nguvu, nanyi mtakaposikia sauti ya tarumbeta, watu wote watapiga kelele kwa sauti kuu; na ukuta wa mji utaanguka chini pale pale, na hao watu watapanda, kila mtu akiendelea mbele kukabili. Bali Yoshua, mwana wa Nuni, akawaita makuhani, akawaambia, Lichukueni sanduku la agano, tena makuhani saba na wachukue tarumbeta saba za pembe za kondoo waume mbele ya sanduku la BWANA. Naye akawaambia watu, Piteni mbele, mkauzunguke mji, na hao watu wenye silaha na watangulie mbele ya sanduku la BWANA.
Yoshua 6:1-7 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Basi malango ya Yeriko yalifungwa kwa uthabiti kwa sababu ya Waisraeli. Hakuna mtu yeyote aliyetoka au kuingia. Kisha BWANA akamwambia Yoshua, “Tazama, nimeitia Yeriko mikononi mwako, pamoja na mfalme wake na wapiganaji wake. Zunguka mji mara moja pamoja na watu wote wenye silaha. Fanya hivi kwa siku sita. Uwe na makuhani saba wakibeba mabaragumu ya pembe za kondoo dume mbele ya Sanduku. Siku ya saba, mzunguke mji mara saba, nao makuhani wakipiga baragumu hizo. Utakapowasikia wamepaliza sauti kubwa ya baragumu, watu wote wapige kelele kwa sauti kuu, kisha ukuta wa mji utaanguka na wapiganaji watapanda, kila mtu akielekea mbele yake.” Ndipo Yoshua mwana wa Nuni akaita makuhani na kuwaambia, “Chukueni Sanduku la Agano la BWANA na makuhani saba wachukue baragumu za pembe za kondoo dume mbele yake.” Naye akawaagiza watu, “Songeni mbele! Mkauzunguke mji, na walinzi wenye silaha watangulie mbele ya Sanduku la BWANA.”