Yoshua 6:1-25
Yoshua 6:1-25 Biblia Habari Njema (BHN)
Milango ya kuingilia mjini Yeriko ilikuwa imefungwa imara kwa ndani kuwazuia Waisraeli wasiingie. Hakuna mtu aliyeweza kuingia wala kutoka katika mji huo. Mwenyezi-Mungu akamwambia Yoshua, “Angalia! Mimi nitautia mikononi mwako mji wa Yeriko pamoja na mfalme wake na askari wake shujaa. Wewe na wale watu wenye silaha wote mtauzunguka huo mji mara moja kila siku kwa siku sita. Makuhani saba, kila mmoja akiwa amechukua baragumu yake ya pembe za kondoo dume, watatangulia mbele ya sanduku la agano. Katika siku ya saba mtauzunguka mji huo mara saba, huku makuhani wakipiga mabaragumu. Watakapopiga hayo mabaragumu kwa mlio mkubwa na mara tu mtakaposikia huo mlio, watu wote watapiga kelele kubwa, nazo kuta za mji zitaanguka chini. Ndipo watu watauvamia mji kila mmoja kutoka mahali aliposimama.” Basi, Yoshua, mwana wa Nuni, akawaita makuhani, akawaambia, “Libebeni sanduku la agano na makuhani saba wachukue mabaragumu saba za kondoo dume, watangulie mbele ya sanduku la Mwenyezi-Mungu.” Yoshua akawaambia watu, “Nendeni mbele; uzungukeni mji, nao watu wenye silaha waende mbele ya sanduku la agano la Mwenyezi-Mungu.” Kulingana na amri ya Yoshua, wale makuhani saba waliokuwa na mabaragumu saba ya kondoo dume wakaenda mbele ya Mwenyezi-Mungu, wakiwa wanapiga mabaragumu, nyuma yao wakifuatwa na lile sanduku la agano. Wale watu wenye silaha wakawatangulia wale makuhani ambao walikuwa wanapiga mabaragumu, na walinzi wengine wakifuata nyuma ya sanduku hilo, huku mabaragumu yakilia kwa mfululizo. Lakini Yoshua akawaamuru watu, “Msipige kelele au kutoa sauti, wala neno lolote lisitoke vinywani mwenu, mpaka siku ile ambapo nitawaambieni mpige kelele; wakati huo ndipo mtakapopiga kelele.” Basi, Yoshua aliwafanya wale watu wauzunguke mji mara moja kila siku wakiwa wamebeba sanduku la agano la Mwenyezi-Mungu na kurudi kambini kulala usiku. Asubuhi yake Yoshua akaamka alfajiri na mapema, na makuhani wakalibeba lile sanduku la agano la Mwenyezi-Mungu. Wale makuhani saba wenye mabaragumu saba za kondoo dume walitembea mbele ya sanduku la Mwenyezi-Mungu wakipiga mabaragumu mfululizo. Watu wenye silaha walilitangulia sanduku la Mwenyezi-Mungu na walinzi wengine nyuma yake. Mabaragumu yakaendelea kupigwa. Siku ya pili yake waliuzunguka huo mji mara moja; na kurudi tena kambini kwao. Walifanya hivyo kwa muda wa siku sita. Siku ya saba, waliamka alfajiri na mapema, wakauzunguka mji huo mara saba kwa namna ileile. Ilikuwa ni siku hiyo tu ambayo waliuzunguka mji huo mara saba. Ilipofika mara ya saba, wakati makuhani walipokwisha piga mabaragumu, Yoshua akawaambia watu, “Pigeni kelele, kwa kuwa Mwenyezi-Mungu amekwisha wapeni huu mji! Mji huo utaangamizwa na kila kitu kilichomo kwani umewekwa wakfu kwa Mwenyezi-Mungu. Rahabu, yule kahaba, ndiye atakayesalimishwa pamoja na wale ambao wamo nyumbani mwake kwa kuwa aliwaficha wapelelezi wetu. Lakini msichukue chochote ambacho kimewekwa wakfu ili kiangamizwe, mkichukua kitu chochote ambacho kimewekwa wakfu ili kiangamizwe mtaifanya kambi ya Israeli kuwa kitu cha kuangamizwa, na hivyo kuiletea balaa. Lakini fedha yote, dhahabu, vyombo vya shaba na chuma ni vitakatifu kwa Mwenyezi-Mungu; hivyo vitawekwa katika hazina ya Mwenyezi-Mungu.” Basi, watu wakapiga kelele huku mabaragumu yanapigwa. Watu waliposikia sauti ya mabaragumu walipiga kelele kubwa, na kuta za mji zikaanguka chini kabisa. Mara watu wakauvamia mji, kila mmoja kutoka mahali aliposimama, wakauteka. Kisha wakaangamiza kila kitu mjini humo na kuwaua kwa upanga: Wanaume na wanawake, vijana na wazee, ng'ombe, kondoo na punda. Yoshua akawaambia wale wapelelezi wawili walioipeleleza nchi hiyo, “Nendeni katika nyumba ya yule kahaba; mkamlete yule mwanamke na wale wote ambao ni ndugu zake kama mlivyomwapia.” Basi, wale vijana wapelelezi wakaenda; wakamleta Rahabu, baba yake na mama yake, ndugu zake na watu wote wa jamaa yake, wakawaweka nje ya kambi ya Israeli. Kisha, wakauchoma moto mji wa Yeriko na kila kitu kilichokuwako isipokuwa fedha, dhahabu, vyombo vya shaba na vya chuma; hivyo viliwekwa katika hazina ya nyumba ya Mwenyezi-Mungu. Lakini yule kahaba Rahabu pamoja na watu wote wa nyumba ya baba yake, Yoshua aliyaokoa maisha yao. Rahabu akaishi miongoni mwa Waisraeli hadi leo, kwa kuwa aliwaficha wajumbe ambao Yoshua aliwatuma kwenda kuupeleleza mji wa Yeriko.
Yoshua 6:1-25 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Basi Yeriko ulikuwa umefungwa kabisa kwa sababu ya Waisraeli; hapana mtu aliyetoka wala hapana mtu aliyeingia. BWANA akamwambia Yoshua, Tazama, nimeutia Yeriko katika mkono wako, na mfalme wake, na mashujaa wake. Nanyi mtauzunguka mji huu, wapiganaji wote, mkiuzunguka mji mara moja. Fanya hivi siku sita. Na makuhani saba watachukua baragumu saba za pembe za kondoo dume, watatangulia mbele za hilo sanduku; na siku ya saba mtauzunguka mji mara saba, nao makuhani watapiga baragumu zao. Kisha itakuwa watakapopiga hizo pembe za kondoo dume kwa nguvu, nanyi mtakaposikia kwa mlio wa baragumu, watu wote watapiga kelele kwa sauti kuu; na ukuta wa mji utaanguka chini pale pale, na hao watu watapanda, kila mtu akiendelea mbele kukabili. Bali Yoshua, mwana wa Nuni, akawaita makuhani, akawaambia, Lichukueni sanduku la Agano, tena makuhani saba na wachukue mabaragumu saba za pembe za kondoo dume watangulie mbele ya sanduku la BWANA. Naye akawaambia watu, Piteni mbele, mkauzunguke mji, na hao watu wenye silaha na watangulie mbele ya sanduku la BWANA. Basi ikawa Yoshua alipokwisha kusema na watu, wale makuhani saba, wenye kuzichukua baragumu saba za pembe za kondoo dume mbele za BWANA, watatangulia, wakayapiga hayo mabaragumu; nalo sanduku la Agano la BWANA likawafuata. Wale watu wenye silaha walikwenda mbele ya hao makuhani walioyapiga mabaragumu, na wale waliokuwa nyuma wakalifuata hilo sanduku; makuhani wakiyapiga mabaragumu walipokuwa wakienda. Yoshua akawaamuru watu, akasema Msipige kelele, wala sauti zenu zisisikiwe, wala neno lolote lisitoke kinywani mwenu, hadi siku ile nitakapowaamuru kupiga kelele, ndipo mtakapopiga kelele. Basi akalipeleka sanduku la BWANA liuzunguke huo mji, likauzunguka mara moja, kisha wakaenda kambini wakakaa humo kambini. Yoshua akaondoka asubuhi na mapema, nao makuhani wakalichukua sanduku la BWANA. Na wale makuhani saba wakayachukua mabaragumu saba ya pembe za kondoo dume mbele ya sanduku la BWANA, wakaenda huku wakiyapiga mabaragumu; nao watu wenye silaha wakawatangulia, na hao waliokuwa nyuma wakalifuata sanduku la BWANA; huku makuhani wakiyapiga mabaragumu bila kukoma. Siku ya pili wakauzunguka mji mara moja, wakarejea kambini; ndivyo walivyofanya siku sita. Ikawa siku ya saba wakaondoka asubuhi na mapema wakati wa mapambazuko, wakauzunguka mji vivyo hivyo mara saba; ni siku hiyo tu ambapo waliuzunguka huo mji mara saba. Hata mara ya saba makuhani wakayapiga mabaragumu, Yoshua akawaambia watu, Pigeni kelele; kwa maana BWANA amewapeni mji huu. Na mji huu utakuwa wakfu kwa BWANA, mji wenyewe na vitu vyote vilivyomo; isipokuwa Rahabu, yule kahaba, ataishi, yeye na watu wote walio pamoja naye nyumbani, kwa sababu aliwaficha hao wapelelezi tuliowatuma. Na ninyi, msikose kujiepusha na kitu kilichowekwa wakfu; msije mkakitwaa kitu kilichowekwa wakfu, baada ya kukiweka wakfu; nanyi hivyo mtaifanya kambi ya Israeli kuwa imelaaniwa na kuifadhaisha. Lakini fedha yote, na dhahabu, na vyombo vya shaba, na chuma, ni vitakatifu kwa BWANA; vitaletwa katika hazina ya BWANA. Basi watu wakapiga kelele, na makuhani wakazipiga tarumbeta; hata ikawa, hapo watu waliposikia mlio wa mabaragumu hao watu wakapiga kelele kwa sauti kuu sana, na ule ukuta wa mji ukaanguka chini kabisa, hata watu wakapanda juu, wakaingia katika mji, kila mtu akisonga mbele kukabili; wakautwaa huo mji. Basi wakaangamiza kabisa vitu vyote vilivyokuwa ndani ya mji, wanaume, wanawake, watoto na wazee, na ng'ombe, kondoo na punda, kwa upanga. Naye Yoshua akawaambia wale wanaume wawili walioipeleleza nchi, Ingieni katika nyumba ya yule kahaba, mkamtoe huyo mwanamke mwenyewe na vitu vyote alivyo navyo, kama mlivyomwapia. Basi wale vijana wapelelezi wakaingia, wakamtoa Rahabu, na baba yake, na mama yake, na ndugu zake, na vitu vyote walivyokuwa navyo, wakawatoa na jamaa zake wote pia; wakawaweka nje ya kambi ya Israeli. Kisha wakauteketeza mji kwa moto, na vitu vyote vilivyokuwa ndani yake; bali fedha, na dhahabu, na vyombo vya shaba, na vya chuma, wakavitia katika hazina ya nyumba ya BWANA. Lakini Yoshua akamhifadhi Rahabu, yule kahaba, na watu wa nyumba ya baba yake, na vitu vyote alivyokuwa navyo; naye akakaa kati ya Israeli hata leo; kwa sababu aliwaficha wale wajumbe aliowatuma Yoshua ili kuupeleleza mji wa Yeriko.
Yoshua 6:1-25 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Basi Yeriko ulikuwa umefungwa kabisa kwa sababu ya wana wa Israeli; hapana mtu aliyetoka wala hapana mtu aliyeingia. BWANA akamwambia Yoshua, Tazama, nimeutia Yeriko katika mkono wako, na mfalme wake, na mashujaa wake. Nanyi mtauzunguka mji huu, watu wote wa vita, mkiuzunguka mji mara moja. Fanya hivi siku sita. Na makuhani saba watachukua tarumbeta saba za pembe za kondoo waume, mbele ya hilo sanduku; na siku ya saba mtauzunguka mji mara saba, nao makuhani watapiga tarumbeta zao. Kisha itakuwa watakapopiga hizo pembe za kondoo waume kwa nguvu, nanyi mtakaposikia sauti ya tarumbeta, watu wote watapiga kelele kwa sauti kuu; na ukuta wa mji utaanguka chini pale pale, na hao watu watapanda, kila mtu akiendelea mbele kukabili. Bali Yoshua, mwana wa Nuni, akawaita makuhani, akawaambia, Lichukueni sanduku la agano, tena makuhani saba na wachukue tarumbeta saba za pembe za kondoo waume mbele ya sanduku la BWANA. Naye akawaambia watu, Piteni mbele, mkauzunguke mji, na hao watu wenye silaha na watangulie mbele ya sanduku la BWANA. Basi ikawa Yoshua alipokwisha kusema na watu, wale makuhani saba, wenye kuzichukua tarumbeta saba za pembe za kondoo waume mbele za BWANA, wakatangulia, wakazipiga hizo tarumbeta; nalo sanduku la agano la BWANA likawafuata. Wale watu wenye silaha walikwenda mbele ya hao makuhani waliozipiga tarumbeta, na wale waliokuwa nyuma wakalifuata hilo sanduku; makuhani wakizipiga tarumbeta walipokuwa wakienda. Yoshua akawaamuru watu, akasema Msipige kelele, wala sauti zenu zisisikiwe, wala neno lo lote lisitoke kinywani mwenu, hata siku ile nitakapowaamuru kupiga kelele, ndipo mtakapopiga kelele. Basi akalipeleka sanduku la BWANA liuzunguke huo mji, likauzunguka mara moja, kisha wakaenda kambini wakakaa kambini. Yoshua akaondoka asubuhi na mapema, nao makuhani wakalichukua sanduku la BWANA. Na wale makuhani saba wakazichukua tarumbeta saba za pembe za kondoo waume mbele ya sanduku la BWANA, wakaendelea wakazipiga tarumbeta; nao watu wenye silaha wakawatangulia, na hao waliokuwa nyuma wakalifuata sanduku la BWANA; makuhani wakizipiga tarumbeta walipokuwa wakienda. Siku ya pili wakauzunguka mji mara moja, wakarejea kambini; ndivyo walivyofanya siku sita. Ikawa siku ya saba wakaondoka asubuhi na mapema wakati wa mapambazuko, wakauzunguka mji vivyo hivyo mara saba; ila siku hiyo waliuzunguka huo mji mara saba. Hata mara ya saba makuhani walipozipiga tarumbeta, Yoshua akawaambia watu, Pigeni kelele; kwa maana BWANA amewapeni mji huu. Na mji huu utakuwa wakfu kwa BWANA, mji wenyewe na vitu vyote vilivyomo; isipokuwa Rahabu, yule kahaba, ataishi, yeye na watu wote walio pamoja naye nyumbani, kwa sababu aliwaficha hao wapelelezi tuliowatuma. Na ninyi, msikose kujiepusha na kitu kilichowekwa wakfu; msije mkakitwaa kitu kilichowekwa wakfu, baada ya kukiweka wakfu; nanyi hivyo mtayafanya matuo ya Israeli kuwa yamelaaniwa na kuyafadhaisha. Lakini fedha yote, na dhahabu, na vyombo vya shaba, na chuma, ni vitakatifu kwa BWANA; vitaletwa katika hazina ya BWANA. Basi watu wakapiga kelele, na makuhani wakazipiga tarumbeta; hata ikawa, hapo watu waliposikia sauti ya tarumbeta hao watu wakapiga kelele kwa sauti kuu sana, na ule ukuta wa mji ukaanguka nchi kabisa, hata watu wakapanda juu, wakaingia katika mji, kila mtu akiendelea kukabili mbele; wakautwaa huo mji. Basi wakaangamiza kabisa vitu vyote vilivyokuwa ndani ya mji, wanaume na wanawake, watoto na wazee, na ng’ombe, na kondoo, na punda, kwa makali ya upanga. Naye Yoshua akawaambia wale wanaume wawili walioipeleleza nchi, Ingieni katika nyumba ya yule kahaba, mkamtoe huyo mwanamke mwenyewe na vitu vyote alivyo navyo, kama mlivyomwapia. Basi wale vijana wapelelezi wakaingia, wakamtoa Rahabu, na baba yake, na mama yake, na ndugu zake, na vitu vyote walivyokuwa navyo, wakawatoa na jamaa zake wote pia; wakawaweka nje ya matuo ya Israeli. Kisha wakauteketeza mji kwa moto, na vitu vyote vilivyokuwa ndani yake; bali fedha, na dhahabu, na vyombo vya shaba, na vya chuma, wakavitia katika hazina ya nyumba ya BWANA. Lakini Yoshua akamhifadhi Rahabu, yule kahaba, na watu wa nyumba ya baba yake, na vitu vyote alivyokuwa navyo; naye akakaa kati ya Israeli hata leo; kwa sababu aliwaficha wale wajumbe aliowatuma Yoshua ili kuupeleleza mji wa Yeriko.
Yoshua 6:1-25 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Basi malango ya Yeriko yalifungwa kwa uthabiti kwa sababu ya Waisraeli. Hakuna mtu yeyote aliyetoka au kuingia. Kisha BWANA akamwambia Yoshua, “Tazama, nimeitia Yeriko mikononi mwako, pamoja na mfalme wake na wapiganaji wake. Zunguka mji mara moja pamoja na watu wote wenye silaha. Fanya hivi kwa siku sita. Uwe na makuhani saba wakibeba mabaragumu ya pembe za kondoo dume mbele ya Sanduku. Siku ya saba, mzunguke mji mara saba, nao makuhani wakipiga baragumu hizo. Utakapowasikia wamepaliza sauti kubwa ya baragumu, watu wote wapige kelele kwa sauti kuu, kisha ukuta wa mji utaanguka na wapiganaji watapanda, kila mtu akielekea mbele yake.” Ndipo Yoshua mwana wa Nuni akaita makuhani na kuwaambia, “Chukueni Sanduku la Agano la BWANA na makuhani saba wachukue baragumu za pembe za kondoo dume mbele yake.” Naye akawaagiza watu, “Songeni mbele! Mkauzunguke mji, na walinzi wenye silaha watangulie mbele ya Sanduku la BWANA.” Baada ya Yoshua kuzungumza na watu, wale makuhani saba waliozibeba zile baragumu saba mbele za BWANA, wakatangulia mbele, wakipiga baragumu zao na Sanduku la Agano la BWANA likawafuata. Walinzi waliokuwa na silaha wakaenda mbele ya hao makuhani waliopiga hizo baragumu na hao walinzi wa nyuma wakafuata Sanduku. Wakati wote huu baragumu zilikuwa zikipigwa. Bali Yoshua alikuwa amewaagiza watu, “Msipige ukelele wa vita; msipaze sauti zenu, wala kusema neno lolote hadi siku ile nitakayowaambia mpige kelele. Ndipo mtapiga kelele!” Basi akalipeleka Sanduku la BWANA kuzungushwa huo mji, likizungushwa mara moja. Kisha watu wakarudi kambini kulala. Yoshua akaamka asubuhi na mapema siku iliyofuata, nao makuhani wakalichukua Sanduku la BWANA. Wale Makuhani saba waliobeba zile baragumu saba wakatangulia mbele ya Sanduku la BWANA wakizipiga. Watu wenye silaha wakatangulia mbele yao na walinzi wa nyuma wakalifuata Sanduku la BWANA, huku baragumu hizo zikiendelea kulia. Siku ya pili wakauzunguka mji mara moja na kurudi kambini. Wakafanya hivi kwa siku sita. Siku ya saba, wakaamka asubuhi na mapema wakauzunguka mji kama walivyokuwa wakifanya, isipokuwa siku ile waliuzunguka mji mara saba. Walipouzunguka mara ya saba, makuhani walipiga baragumu kwa sauti kubwa, naye Yoshua akawaamuru watu akisema, “Pigeni kelele! Kwa maana BWANA amewapa mji huu! Mji huu pamoja na vyote vilivyomo utatengewa BWANA kwa ajili ya kuangamizwa. Rahabu yule kahaba atasalimishwa, pamoja na wote walio naye nyumbani mwake, kwa sababu aliwaficha wale wapelelezi tuliowatuma. Lakini mjiepushe na vitu vilivyotengwa kwa ajili ya kuangamizwa, msije mkajiletea maangamizi kwa kuchukua chochote katika hivyo; la sivyo, mtailetea kambi ya Israeli maangamizi na taabu. Fedha yote na dhahabu, vyombo vya shaba na chuma ni vitakatifu kwa BWANA, lazima viletwe katika hazina yake.” Baragumu zilipopigwa, watu walipiga kelele; kwa ile sauti ya baragumu na watu kupaza sauti, ukuta ukaanguka; hivyo kila mtu akapanda akiendelea mbele na kuuteka mji. Wakauweka mji wakfu kwa BWANA, na kila chenye uhai ndani yake walikiangamiza kwa upanga: wanaume na wanawake, vijana kwa wazee, ngʼombe, kondoo na punda. Yoshua akawaambia wale watu wawili waliokuwa wameipeleleza nchi, “Nendeni nyumbani mwa yule kahaba; mleteni pamoja na wote walio nyumbani mwake, kulingana na kiapo chenu kwake.” Basi wale vijana waliofanya upelelezi wakaenda kumleta Rahabu, baba yake na mama yake, na ndugu zake na watu wote waliokuwa pamoja naye. Wakaleta jamaa yake yote na kuwaweka mahali nje ya kambi ya Israeli. Kisha wakauchoma mji wote na kila kitu kilichokuwa ndani yake. Lakini fedha, dhahabu, na vyombo vya shaba na vya chuma wakaviweka katika hazina ya nyumba ya BWANA. Lakini Yoshua akamhifadhi Rahabu yule kahaba, jamaa yake yote na vyote alivyokuwa navyo, kwa sababu aliwaficha watu waliotumwa na Yoshua kuipeleleza Yeriko, naye anaishi miongoni mwa Waisraeli hata leo.