Yoshua 5:10-15
Yoshua 5:10-15 Biblia Habari Njema (BHN)
Waisraeli walipokuwa wamepiga kambi huko Gilgali waliadhimisha sikukuu ya Pasaka jioni ya siku ya kumi na nne ya mwezi katika tambarare za Yeriko. Kesho yake, yaani baada ya Pasaka, walikula mikate isiyotiwa chachu na bisi kutokana na mazao ya nchi ile. Basi, tangu siku hiyo walipokula mazao ya nchi hiyo Waisraeli hawakupata mana tena. Tangu mwaka huo Waisraeli walikula mazao ya nchi ya Kanaani. Siku moja Yoshua alipokuwa karibu na mji wa Yeriko, ghafla aliona mtu mmoja amesimama mbele yake na upanga uliofutwa mkononi mwake. Yoshua akamwendea, akamwuliza, “Je, wewe ni wetu au ni wa adui zetu?” Naye akamjibu; “Wala wenu wala wa adui zenu! Ila mimi ni kamanda wa jeshi la Mwenyezi-Mungu, na sasa nimewasili.” Yoshua akainama chini akasujudu, kisha akamwuliza, “Bwana wangu, mimi mtumishi wako, unataka nifanye nini?” Huyo kamanda wa jeshi la Mwenyezi-Mungu akamwambia, “Vua viatu vyako kwa maana mahali unaposimama ni patakatifu.” Yoshua akafanya hivyo.
Yoshua 5:10-15 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Basi wana wa Israeli wakapanga hema zao huko Gilgali; nao wakala sikukuu ya Pasaka siku ya kumi na nne ya mwezi, jioni, katika nchi tambarare za Yeriko. Nao wakala katika mazao ya nchi siku ya pili ya kuiandama hiyo sikukuu ya Pasaka, mikate isiyotiwa chachu, na bisi, siku iyo hiyo. Ndipo ile mana ikakoma siku ya pili yake, baada ya wao kuyala hayo mazao ya nchi; na hao wana wa Israeli hawakuwa na mana tena; lakini wakala mazao ya nchi ya Kanaani mwaka huo. Ikawa hapo Yoshua alipokuwa karibu na mji wa Yeriko, akainua macho yake na kuangalia juu, akaona ghafla mtu mmoja, mwanamume amesimama amemkabili naye alikuwa na upanga uliofutwa mkononi mwake; Yoshua akamwendea, na kumwambia, Je! Wewe u upande wetu, au upande wa adui zetu? Akasema, La, lakini mimi ni kamanda wa jeshi la BWANA, nimekuja sasa. Yoshua akainama chini hadi nchi, akasujudu, akamwuliza, Bwana wangu aniambia nini mimi mtumishi wake? Huyo kamanda wa jeshi la BWANA akamwambia Yoshua, Vua viatu vyako miguuni mwako; kwa kuwa mahali hapo usimamapo ni patakatifu. Yoshua akafanya hivyo.
Yoshua 5:10-15 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Basi wana wa Israeli wakapanga hema zao huko Gilgali; nao wakala sikukuu ya pasaka siku ya kumi na nne ya mwezi, jioni, katika nchi tambarare za Yeriko. Nao wakala katika mazao ya nchi siku ya pili ya kuiandama hiyo sikukuu ya pasaka, mikate isiyotiwa chachu, na bisi, siku iyo hiyo. Ndipo ile mana ikakoma siku ya pili yake, baada ya wao kuyala hayo mazao ya nchi; na hao wana wa Israeli hawakuwa na mana tena; lakini wakala katika viliwa vya nchi ya Kanaani mwaka huo. Ikawa hapo Yoshua alipokuwa karibu na mji wa Yeriko, akavua macho yake na kuangalia, na tazama, mtu mume akasimama kumkabili mbele yake, naye alikuwa na upanga wazi mkononi mwake; Yoshua akamwendea, na kumwambia, Je! Wewe u upande wetu, au upande wa adui zetu? Akasema, La, lakini nimekuja sasa, nili amiri wa jeshi la BWANA. Yoshua akapomoka kiusouso hata nchi, naye akasujudu, akamwuliza, Bwana wangu aniambia nini mimi mtumishi wake? Huyo amiri wa jeshi la BWANA akamwambia Yoshua, Vua viatu vyako miguuni mwako; kwa kuwa mahali hapo usimamapo ni patakatifu. Yoshua akafanya vivyo.
Yoshua 5:10-15 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Jioni ya siku ya kumi na nne ya mwezi, wakiwa wamepiga kambi huko Gilgali kwenye nchi tambarare za Yeriko, Waisraeli wakaadhimisha Pasaka. Siku iliyofuata Pasaka, katika siku ile ile, wakala mazao ya nchi: mikate isiyotiwa chachu na nafaka za kukaanga. Mana ilikoma siku iliyofuata baada ya Waisraeli kula chakula kilichotoka katika nchi; hapakuwa na mana tena kwa ajili ya Waisraeli, ila mwaka huo walikula mazao ya nchi ya Kanaani. BWANA Basi Yoshua alipokuwa karibu na Yeriko, akainua macho, akaona mtu aliyesimama mbele yake, akiwa na upanga mkononi. Yoshua akamwendea na kumuuliza, “Je, wewe uko upande wetu au upande wa adui zetu?” Akajibu, “La, siko upande wowote, lakini mimi nimekuja nikiwa jemadari wa jeshi la BWANA.” Yoshua akasujudu, uso wake ukigusa chini, akamuuliza, “Je, Bwana, una ujumbe gani kwa mtumishi wako?” Jemadari wa jeshi la BWANA akajibu, “Vua viatu vyako, kwa maana mahali uliposimama ni patakatifu.” Naye Yoshua akafanya hivyo.