Yoshua 5:1-12
Yoshua 5:1-12 Biblia Habari Njema (BHN)
Wafalme wote wa Waamori walioishi ngambo ya magharibi ya Yordani, na wafalme wote wa Wakanaani waliokuwa pwani ya bahari ya Mediteranea, waliposikia kwamba Mwenyezi-Mungu aliyakausha maji ya mto Yordani kwa ajili ya Waisraeli mpaka walipokwisha vuka, wakafa moyo; wakaishiwa nguvu kabisa kwa kuwaogopa Waisraeli. Wakati huo, Mwenyezi-Mungu akamwambia Yoshua, “Tengeneza visu vya jiwe gumu ili uwatahiri Waisraeli.” Basi, Yoshua akatengeneza visu hivyo vya jiwe gumu na kuwatahiri Waisraeli huko Gibea-haaralothi. Sababu ya kuwatahiri Waisraeli ni hii: Waisraeli wote, wanaume, waliotoka Misri ambao walikuwa na umri wa kwenda vitani, wote walifariki safarini jangwani baada ya kutoka nchini Misri. Hao wote waliotoka Misri walikuwa wametahiriwa, lakini wale wote waliozaliwa safarini huko jangwani baada ya kutoka Misri, walikuwa bado hawajatahiriwa. Waisraeli walisafiri kwa muda wa miaka arubaini nyikani hata wanaume wote waliokuwa na umri wa kwenda vitani wakaangamia kwa kuwa hawakusikiliza aliyosema Mwenyezi-Mungu. Mwenyezi-Mungu alikuwa amewaapia watu hao kwamba hawataiona nchi ile inayotiririka maziwa na asali ambayo yeye aliwaapia baba zao kuwa atawapa. Kwa hiyo ilikuwa ni watoto wa watu hao ambao Mwenyezi-Mungu aliwakuza badala yao, hao ndio Yoshua aliwatahiri, kwani hawakuwa wametahiriwa wakati ule walipokuwa safarini jangwani. Wanaume wote walipokwisha tahiriwa walikaa katika sehemu zao humo kambini mpaka walipopona. Kisha Mwenyezi-Mungu akamwambia Yoshua, “Leo hii nimewaondoleeni ile aibu ya Misri.” Hivyo mahali hapo pakaitwa Gilgali mpaka hivi leo. Waisraeli walipokuwa wamepiga kambi huko Gilgali waliadhimisha sikukuu ya Pasaka jioni ya siku ya kumi na nne ya mwezi katika tambarare za Yeriko. Kesho yake, yaani baada ya Pasaka, walikula mikate isiyotiwa chachu na bisi kutokana na mazao ya nchi ile. Basi, tangu siku hiyo walipokula mazao ya nchi hiyo Waisraeli hawakupata mana tena. Tangu mwaka huo Waisraeli walikula mazao ya nchi ya Kanaani.
Yoshua 5:1-12 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ikawa, wafalme wa Waamori, waliokaa ng'ambo ya Yordani pande za magharibi, na wafalme wote wa Wakanaani, waliokuwa karibu na bahari, waliposikia jinsi BWANA alivyoyakausha maji ya Yordani mbele ya wana wa Israeli, hadi tulipokwisha kuvuka, basi mioyo yao iliyeyuka, wala haikuwamo roho ya nguvu ndani yao tena; kwa ajili ya wana wa Israeli. Wakati huo BWANA akamwambia Yoshua, Haya, jifanyie visu vya mawe ya gumegume, watahiri tena wana wa Israeli mara ya pili. Basi Yoshua akajifanyia visu vya mawe ya gumegume, akawatahiri wana wa Israeli huko Gibea-haaralothi. Na sababu ya Yoshua kutahiri ni hii; watu wote wanaume waliotoka Misri, waliokuwa wapiganaji vita wote walifariki katika safari jangwani baada ya kutoka Misri. Kwa kuwa watu wote waliotoka walikuwa wamekwisha kutahiriwa; lakini watu wote waliozaliwa katika safari jangwani walipokwisha kutoka Misri, hao hawakutahiriwa. Kwa kuwa wana wa Israeli walitembea muda wa miaka arubaini barani, hadi hilo taifa zima, yaani, watu wanaume wapiganaji vita, waliotoka Misri, walipokuwa wameangamia; kwa sababu hawakuisikiza sauti ya BWANA; nao ndio BWANA aliowaapia ya kwamba hatawaacha waione hiyo nchi, ambayo BWANA aliwaapia baba zao kwamba atatupa sisi; nchi itiririkayo maziwa na asali. Na watoto wao, aliowainua badala yao ndio hao aliowatahiri Yoshua; kwa kuwa wao walikuwa hawajatahiriwa, kwa maana hawakuwatahiri njiani. Ilikuwa walipokwisha kutahiriwa taifa zima, wakakaa kila mtu mahali pake kambini, hadi walipopoa. BWANA akamwambia Yoshua, Siku hii ya leo nimeivingirisha hiyo aibu ya Misri iondoke juu yenu. Kwa hiyo jina la mahali pale likaitwa Gilgali, hata hivi leo. Basi wana wa Israeli wakapanga hema zao huko Gilgali; nao wakala sikukuu ya Pasaka siku ya kumi na nne ya mwezi, jioni, katika nchi tambarare za Yeriko. Nao wakala katika mazao ya nchi siku ya pili ya kuiandama hiyo sikukuu ya Pasaka, mikate isiyotiwa chachu, na bisi, siku iyo hiyo. Ndipo ile mana ikakoma siku ya pili yake, baada ya wao kuyala hayo mazao ya nchi; na hao wana wa Israeli hawakuwa na mana tena; lakini wakala mazao ya nchi ya Kanaani mwaka huo.
Yoshua 5:1-12 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ikawa, wafalme wa Waamori, waliokaa ng’ambo ya Yordani pande za magharibi, na wafalme wote wa Wakanaani, waliokuwa karibu na bahari, waliposikia jinsi BWANA alivyoyakausha maji ya Yordani mbele ya wana wa Israeli, hata tulipokwisha kuvuka, basi mioyo yao iliyeyuka, wala haikuwamo roho ya nguvu ndani yao tena; kwa ajili ya wana wa Israeli. Wakati huo BWANA akamwambia Yoshua, Haya, jifanyie visu vya mawe ya gumegume, watahiri tena wana wa Israeli mara ya pili. Basi Yoshua akajifanyia visu vya mawe ya gumegume, akawatahiri wana wa Israeli huko Gibea-haaralothi. Na sababu ya Yoshua kutahiri ni hii; watu wote waliotoka Misri, waliokuwa waume, hao watu waume wote waendao vitani walikufa katika bara njiani, baada ya wao kutoka Misri. Kwa kuwa watu wote waliotoka walikuwa wamekwisha kutahiriwa; lakini watu wote waliozaliwa katika bara njiani walipokwisha kutoka Misri, hao hawakutahiriwa. Kwa kuwa wana wa Israeli walitembea muda wa miaka arobaini barani, hata hilo taifa zima, yaani, watu waume waendao vitani, waliotoka Misri, walipokuwa wameangamia; kwa sababu hawakuisikiza sauti ya BWANA; nao ndio BWANA aliowaapia ya kwamba hatawaacha waione hiyo nchi, ambayo BWANA aliwaapia baba zao kwamba atatupa sisi; nchi ijaayo maziwa na asali. Na watoto wao, aliowainua badala yao ndio hao aliowatahiri Yoshua; kwa kuwa wao walikuwa hawakutahiriwa, kwa maana walikuwa hawakuwatahiri njiani. Ilikuwa walipokwisha kutahiriwa taifa zima, wakakaa kila mtu mahali pake maragoni, hata walipopoa. BWANA akamwambia Yoshua, Siku hii ya leo nimeivingirisha hiyo aibu ya Misri iondoke juu yenu. Kwa hiyo jina la mahali pale likaitwa Gilgali, hata hivi leo. Basi wana wa Israeli wakapanga hema zao huko Gilgali; nao wakala sikukuu ya pasaka siku ya kumi na nne ya mwezi, jioni, katika nchi tambarare za Yeriko. Nao wakala katika mazao ya nchi siku ya pili ya kuiandama hiyo sikukuu ya pasaka, mikate isiyotiwa chachu, na bisi, siku iyo hiyo. Ndipo ile mana ikakoma siku ya pili yake, baada ya wao kuyala hayo mazao ya nchi; na hao wana wa Israeli hawakuwa na mana tena; lakini wakala katika viliwa vya nchi ya Kanaani mwaka huo.
Yoshua 5:1-12 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Basi wafalme wote wa Waamori magharibi mwa Yordani na wafalme wote wa Kanaani waliokuwa kwenye pwani waliposikia jinsi BWANA alivyoukausha Mto Yordani mbele ya Waisraeli hata tulipokwisha kuvuka, mioyo yao ikayeyuka kwa hofu, wala hawakuwa na ujasiri tena wa kukabiliana na Waisraeli. Wakati huo BWANA akamwambia Yoshua, “Tengeneza visu vya gumegume na uwatahiri Waisraeli tena.” Kwa hiyo Yoshua akatengeneza visu vya gumegume na kutahiri Waisraeli huko Gibeath-Haaralothi. Hii ndiyo sababu ya Yoshua kufanya hivyo: Wanaume wote waliotoka Misri, wote wenye umri wa kwenda vitani, walikufa jangwani wakiwa njiani baada ya kuondoka Misri. Watu wote waliotoka Misri walikuwa wametahiriwa, lakini watu wote waliozaliwa jangwani wakiwa safarini kutoka Misri hawakuwa wametahiriwa. Waisraeli walitembea jangwani miaka arobaini hadi wanaume wote wale waliokuwa na umri wa kwenda vitani wakati waliondoka Misri walipokwisha kufa, kwa kuwa hawakumtii BWANA. Kwa maana BWANA alikuwa amewaapia kuwa wasingeweza kuona nchi ambayo alikuwa amewaahidi baba zao katika kuapa kutupatia, nchi inayotiririka maziwa na asali. Kwa hiyo akawainua wana wao baada yao na hawa ndio hao ambao Yoshua aliwatahiri. Walikuwa hawajatahiriwa bado kwa sababu walikuwa safarini. Baada ya taifa lote kutahiriwa, waliendelea kukaa kambini hadi walipopona. BWANA akamwambia Yoshua, “Leo nimeiondoa aibu ya Wamisri kutoka kwenu.” Basi mahali pale pakaitwa Gilgali hadi leo. Jioni ya siku ya kumi na nne ya mwezi, wakiwa wamepiga kambi huko Gilgali kwenye nchi tambarare za Yeriko, Waisraeli wakaadhimisha Pasaka. Siku iliyofuata Pasaka, katika siku ile ile, wakala mazao ya nchi: mikate isiyotiwa chachu na nafaka za kukaanga. Mana ilikoma siku iliyofuata baada ya Waisraeli kula chakula kilichotoka katika nchi; hapakuwa na mana tena kwa ajili ya Waisraeli, ila mwaka huo walikula mazao ya nchi ya Kanaani.