Yoshua 4:1-7
Yoshua 4:1-7 Biblia Habari Njema (BHN)
Taifa zima lilipokwisha vuka mto Yordani, Mwenyezi-Mungu akamwambia Yoshua, “Chagua watu kumi na wawili miongoni mwa hao Waisraeli, yaani mtu mmoja kutoka kila kabila, uwaagize hivi, ‘Chukueni mawe kumi na mawili kutoka hapa katikati ya mto Yordani, kutoka hapa ilipo miguu ya makuhani, muyachukue mawe hayo, mkayaweke mahali pale ambapo mtalala leo hii.’” Yoshua akawaita hao watu kumi na wawili ambao alikuwa amewateua miongoni mwa Waisraeli, kila kabila mtu mmoja, akawaambia, “Litangulieni sanduku la agano la Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, mpaka katikati ya mto Yordani. Kila mmoja wenu achukue jiwe begani mwake, jiwe moja kwa ajili ya kila kabila la Israeli. Jambo hilo litakuwa ishara kati yenu; na watoto wenu watakapowauliza siku zijazo ‘Je, mawe haya yana maana gani kwenu?’ Nyinyi mtawaambia, ‘Sanduku la agano la Mwenyezi-Mungu lilipopitishwa mtoni Yordani, maji ya mto huo yalizuiliwa yasitiririke!’ Kwa hiyo mawe haya yatakuwa ukumbusho kwa Waisraeli milele.”
Yoshua 4:1-7 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ikawa, hapo hilo taifa zima lilipokuwa limekwisha vuka Yordani, ndipo BWANA akanena na Yoshua, akamwambia, Haya, twaeni watu wanaume kumi na wawili katika hao watu, kila kabila mtu mmoja, kisha uwaamrishe, kusema, Twaeni mawe kumi na mawili, hapo katikati ya Yordani, mahali hapo miguu ya hao makuhani iliposimama imara, mwende na mawe hayo, mkayaweke mahali pale kambini ambapo mtalala usiku huu. Basi Yoshua akawaita hao watu kumi na wawili, aliokuwa ameteua tangu hapo awali, katika wana wa Israeli, kila kabila mtu mmoja; naye Yoshua akawaambia, Haya, piteni ninyi mtangulie mbele ya sanduku la BWANA, Mungu wenu, mwende pale katikati ya Yordani, mkatwae kila mmoja wenu jiwe moja begani mwake, kwa kadiri ya hesabu ya makabila ya wana wa Israeli; ili kwamba jambo hili liwe ishara kati yenu, hapo watoto wenu watakapowauliza ninyi katika siku zijazo, wakisema, Ni nini maana yake mawe haya? Ndipo mtakapowaambia, Ni kwa sababu maji ya Yordani yaliondoka mbele ya sanduku la Agano la BWANA; hapo lilipovuka Yordani, hayo maji ya Yordani yalisimama; na mawe haya yatakuwa ni ukumbusho kwa wana wa Israeli milele.
Yoshua 4:1-7 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ikawa, hapo hilo taifa zima lilipokuwa limekwisha vuka Yordani, ndipo BWANA akanena na Yoshua, akamwambia, Haya, twaeni watu waume kumi na wawili katika hao watu, kila kabila mtu mmoja, kisha uwaamrishe, kusema, Twaeni mawe kumi na mawili, hapo katikati ya Yordani, mahali hapo miguu ya hao makuhani iliposimama imara, mwende nayo mawe hayo, mkayaweke nchi kambini, hapo mtakapolala usiku huu. Basi Yoshua akawaita hao watu kumi na wawili, aliokuwa amewaweka tayari tangu hapo, katika wana wa Israeli, kila kabila mtu mmoja; naye Yoshua akawaambia, Haya, piteni ninyi mtangulie mbele ya sanduku la BWANA, Mungu wenu, mwende pale katikati ya Yordani, mkatwae kila mtu wenu jiwe moja begani mwake, kwa kadiri ya hesabu ya kabila za wana wa Israeli; ili kwamba jambo hili liwe ishara kati yenu, hapo watoto wenu watakapowauliza ninyi katika siku zijazo, wakisema, Ni nini maana yake mawe haya? Ndipo mtakapowaambia, Ni kwa sababu maji ya Yordani yalitindika mbele ya sanduku la agano la BWANA; hapo lilipovuka Yordani, hayo maji ya Yordani yalitindika; na mawe haya yatakuwa ni ukumbusho kwa wana wa Israeli milele.
Yoshua 4:1-7 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Taifa lote lilipokwisha kuvuka Mto Yordani, BWANA akamwambia Yoshua, “Chagua watu kumi na wawili miongoni mwa watu, kila kabila mtu mmoja, uwaambie wachukue mawe kumi na mbili katikati ya Mto Yordani, pale makuhani waliposimama, wayachukue na kuyaweka mahali mtakapokaa usiku huu.” Basi Yoshua akawaita watu kumi na wawili ambao alikuwa amewachagua miongoni mwa Waisraeli, mtu mmoja kutoka kila kabila, naye akawaambia, “Mtangulie mbele ya Sanduku la BWANA Mungu wenu, mwende katikati ya Mto Yordani. Kila mmoja wenu atainua jiwe begani mwake, kulingana na idadi ya makabila ya Israeli, kuwa ishara miongoni mwenu. Siku zijazo, watoto wenu watakapowauliza, ‘Ni nini maana ya mawe haya?’ waambieni kwamba maji ya Mto Yordani yaliyokuwa yakitiririka, yalitindika mbele ya Sanduku la Agano la BWANA. Sanduku lilipovuka Yordani, maji ya Yordani yalitindika. Mawe haya yatakuwa kumbukumbu kwa watu wa Israeli milele.”