Yoshua 24:14-31
Yoshua 24:14-31 Biblia Habari Njema (BHN)
“Sasa, basi, mcheni Mwenyezi-Mungu na kumtumikia kwa moyo mnyofu na uaminifu. Acheni kabisa miungu ile ambayo wazee wenu waliiabudu ngambo ya mto Eufrate na nchini Misri. Mtumikieni Mwenyezi-Mungu. Kama hamtaki kumtumikia Mwenyezi-Mungu, basi chagueni leo hii ni nani mtakayemtumikia: Kwamba ni miungu ile ambayo wazee wenu waliitumikia ngambo ya mto Eufrate, au miungu ya Waamori ambao sasa mnaishi nchini mwao. Lakini mimi na nyumba yangu, tutamtumikia Mwenyezi-Mungu.” Hapo watu wakamjibu, “Hatutaweza kamwe kumwacha Mwenyezi-Mungu na kuitumikia miungu mingine. Maana, Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, ndiye aliyetutoa sisi pamoja na wazee wetu katika nchi ya Misri tulikokuwa watumwa, tukayaona kwa macho yetu wenyewe matendo ya ajabu aliyotenda. Akatulinda katika safari zetu zote na miongoni mwa watu wote ambao tulipita kati yao. “Mwenyezi-Mungu alituondolea watu wote yaani Waamori wote waliokaa nchini. Kwa hiyo, nasi tutamtumikia Mwenyezi-Mungu, maana ndiye Mungu wetu.” Lakini Yoshua akawaambia, “Nyinyi hamwezi kumtumikia Mwenyezi-Mungu, maana yeye ni Mungu Mtakatifu. Yeye ni Mungu mwenye wivu, naye hatawasamehe makosa na dhambi zenu. Mkimwacha Mwenyezi-Mungu na kuitumikia miungu ya kigeni, atawaadhibu na kuwaangamiza kabisa, hata ingawa amewatendea mema haya yote.” Nao watu wakamwambia Yoshua, “La, hasha! Sisi tutamtumikia Mwenyezi-Mungu tu.” Hapo Yoshua akawaambia, “Nyinyi wenyewe ni mashahidi wa nafsi zenu kwamba mmechagua kumtumikia Mwenyezi-Mungu.” Nao wakamjibu, “Sisi tu mashahidi.” Naye akawaambia, “Basi, ondoeni miungu ya kigeni mliyo nayo, mkamfuate Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, kwa moyo wenu wote.” Nao, wakasema, “Tutamtumikia na kumtii Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu.” Hivyo, Yoshua akafanya agano na Waisraeli huko Shekemu, akawapa masharti na maagizo ya kufuata. Yoshua akayaandika haya yote katika kitabu cha sheria ya Mungu; kisha, akachukua jiwe kubwa na kulisimika chini ya mwaloni katika hema ya Mwenyezi-Mungu. Halafu akawaambia watu wote, “Jiwe hili ndilo litakalokuwa shahidi kwetu, maana limesikia maneno yote ambayo Mwenyezi-Mungu ametuambia. Kwa hiyo, litashuhudia dhidi yenu, ili msije mkamkana Mungu wenu.” Halafu Yoshua akawaruhusu watu waondoke; nao wakaenda kila mmoja kwake. Baada ya mambo hayo, Yoshua, mwana wa Nuni na mtumishi wa Mwenyezi-Mungu, akafariki akiwa na umri wa miaka 110. Nao wakamzika kwenye eneo ambalo alikuwa amegawiwa kuwa sehemu yake, huko Timnath-sera, katika milima ya Efraimu, kaskazini ya mlima wa Gaashi. Waisraeli walimtumikia Mwenyezi-Mungu muda wote wa uhai wa Yoshua, na baada ya kifo chake, waliendelea kumtumikia kwa muda walioishi wale wazee waliokuwa wameona kwa macho yao mambo yale Mwenyezi-Mungu aliyowatendea Waisraeli.
Yoshua 24:14-31 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Basi sasa mcheni BWANA, mkamtumikie kwa unyofu wa moyo na kwa kweli; na kuiweka mbali miungu ambayo baba zenu waliitumikia ng'ambo ya Mto, na huko Misri; mkamtumikie yeye BWANA. Nanyi kama mkiona ni vibaya kumtumikia BWANA, chagueni hivi leo mtakayemtumikia; kwamba ni miungu ile ambayo baba zenu waliitumikia ng'ambo ya Mto, au kwamba ni miungu ya wale Waamori ambao mnakaa katika nchi yao; lakini mimi na nyumba yangu tutamtumikia BWANA. Hao watu wakajibu wakasema, Hasha! Tusimwache BWANA, ili kuitumikia miungu mingine; kwa maana BWANA, Mungu wetu, yeye ndiye aliyetupandisha sisi na baba zetu kutoka nchi ya Misri; kutoka nyumba ya utumwa; naye ndiye aliyezifanya ishara zile kubwa mbele ya macho yetu, na kutulinda katika njia ile yote tuliyoiendea, na kati ya watu wa mataifa yote tuliopita katikati yao. BWANA ndiye aliyewafukuza watu wa mataifa yote watoke mbele yetu, naam, Waamori waliokaa katika nchi hii; basi, kwa sababu hiyo sisi nasi tutamtumikia BWANA, maana yeye ndiye Mungu wetu. Yoshua akawaambia watu, Hamwezi kumtumikia BWANA; kwa kuwa yeye ni Mungu mtakatifu; yeye ni Mungu mwenye wivu; hatawasamehe makosa yenu, wala dhambi zenu. Kama mkimwacha BWANA na kuitumikia miungu migeni, ndipo atageuka na kuwatenda mabaya na kuwaangamiza, baada ya kuwatendea mema. Lakini hao watu wakamwambia Yoshua, La! Lakini tutamtumikia BWANA. Yoshua akawaambia watu, Ninyi mmekuwa mashahidi juu ya nafsi zenu, ya kuwa mmemchagua BWANA, ili kumtumikia yeye. Wakasema, Sisi tu mashahidi. Akasema, Basi sasa, iondoeni miungu migeni iliyo kati yenu, mkaielekeze mioyo yenu kwa BWANA, Mungu wa Israeli. Ndipo hao watu wakamwambia Yoshua, BWANA, Mungu wetu, ndiye tutakayemtumikia; na sauti yake ndiyo tutakayoitii. Basi Yoshua akafanya agano na wale watu siku ile, akawapa amri na agizo huko Shekemu. Yoshua akayaandika maneno haya katika kitabu cha Torati ya Mungu; kisha akatwaa jiwe kubwa, akalisimamisha huko, chini ya ule mwaloni uliokuwa karibu na patakatifu pa BWANA. Yoshua akawaambia watu wote, Tazama, jiwe hili litakuwa shahidi juu yetu; kwa maana limesikia maneno yote ya BWANA aliyotuambia, basi litakuwa shahidi juu yenu, msije mkamkana Mungu wenu. Basi Yoshua akawaruhusu watu, wakaenda zao, kila mtu kwenye urithi wake. Ikawa, baada ya hayo, Yoshua, mwana wa Nuni, mtumishi wa BWANA, akafa, mwenye umri wa miaka mia moja na kumi. Wakamzika katika nchi ya urithi wake, huko Timnath-sera; ulio katika nchi ya vilima ya Efraimu, upande wa kaskazini wa mlima wa Gaashi. Nao Israeli wakamtumikia BWANA siku zote za Yoshua, na siku zote za hao wazee walioishi baada ya kufa kwake Yoshua, hao walioijua kazi yote ya BWANA, aliyowatendea Israeli.
Yoshua 24:14-31 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Basi sasa mcheni BWANA, mkamtumikie kwa unyofu wa moyo na kwa kweli; na kuiweka mbali miungu ambayo baba zenu waliitumikia ng’ambo ya Mto, na huko Misri; mkamtumikie yeye BWANA. Nanyi kama mkiona ni vibaya kumtumikia BWANA, chagueni hivi leo mtakayemtumikia; kwamba ni miungu ile ambayo baba zenu waliitumikia ng’ambo ya Mto, au kwamba ni miungu ya wale Waamori ambao mnakaa katika nchi yao; lakini mimi na nyumba yangu tutamtumikia BWANA. Hao watu wakajibu wakasema, Hasha! Tusimwache BWANA, ili kuitumikia miungu mingine; kwa maana BWANA, Mungu wetu, yeye ndiye aliyetupandisha sisi na baba zetu kutoka nchi ya Misri; kutoka nyumba ya utumwa; naye ndiye aliyezifanya ishara zile kubwa mbele ya macho yetu, na kutulinda katika njia ile yote tuliyoiendea, na kati ya watu wa mataifa yote tuliopita katikati yao. BWANA ndiye aliyewafukuza watu wa mataifa yote watoke mbele yetu, naam, Waamori waliokaa katika nchi hii; basi, kwa sababu hiyo sisi nasi tutamtumikia BWANA, maana yeye ndiye Mungu wetu. Yoshua akawaambia watu, Hamwezi kumtumikia BWANA; kwa kuwa yeye ni Mungu mtakatifu; yeye ni Mungu mwenye wivu; hatawasamehe makosa yenu, wala dhambi zenu. Kama mkimwacha BWANA na kuitumikia miungu migeni, ndipo atageuka na kuwatenda mabaya na kuwaangamiza, baada ya kuwatendea mema. Lakini hao watu wakamwambia Yoshua, La! Lakini tutamtumikia BWANA. Yoshua akawaambia watu, Ninyi mmekuwa mashahidi juu ya nafsi zenu, ya kuwa mmemchagua BWANA, ili kumtumikia yeye. Wakasema, Sisi tu mashahidi. Akasema, Basi sasa, iondoeni miungu migeni iliyo kati yenu, mkaielekeze mioyo yenu kwa BWANA, Mungu wa Israeli. Ndipo hao watu wakamwambia Yoshua, BWANA, Mungu wetu, ndiye tutakayemtumikia; na sauti yake ndiyo tutakayoitii. Basi Yoshua akafanya agano na wale watu siku ile, akawapa amri na agizo huko Shekemu. Yoshua akayaandika maneno haya katika kitabu cha torati ya Mungu; kisha akatwaa jiwe kubwa, akalisimamisha huko, chini ya ule mwaloni uliokuwa karibu na patakatifu pa BWANA. Yoshua akawaambia watu wote, Tazama, jiwe hili litakuwa shahidi juu yetu; kwa maana limesikia maneno yote ya BWANA aliyotuambia, basi litakuwa shahidi juu yenu, msije mkamkana Mungu wenu. Basi Yoshua akawaruhusu watu, wakaenda zao, kila mtu kwenye urithi wake. Ikawa, baada ya hayo, Yoshua, mwana wa Nuni, mtumishi wa BWANA, akafa, mwenye umri wa miaka mia na kumi. Wakamzika katika mpaka wa urithi wake, huko Timnath-sera; ulio katika nchi ya vilima ya Efraimu, upande wa kaskazini wa mlima wa Gaashi. Nao Israeli wakamtumikia BWANA siku zote za Yoshua, na siku zote za hao wazee walioishi baada ya kufa kwake Yoshua, hao walioijua kazi yote ya BWANA, aliyowatendea Israeli.
Yoshua 24:14-31 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
“Sasa basi mcheni BWANA na kumtumikia kwa uaminifu wote. Itupeni mbali miungu ambayo baba zenu waliiabudu huko ngʼambo ya Mto na huko Misri, nanyi mtumikieni BWANA. Lakini msipoona vyema kumtumikia BWANA, chagueni hivi leo mtakayemtumikia, kama ni miungu ile baba zenu waliitumikia ngʼambo ya Frati, au miungu ya Waamori, ambao mnakaa katika nchi yao. Lakini mimi na nyumba yangu, tutamtumikia BWANA.” Ndipo hao watu wakajibu, “Hili jambo liwe mbali nasi la kumsahau BWANA na kuitumikia miungu mingine! BWANA Mungu wetu mwenyewe ndiye alitutoa sisi na baba zetu akatupandisha kutoka Misri, kutoka nchi ile ya utumwa, na kutenda zile ishara kubwa mbele ya macho yetu. Ndiye aliyetulinda katika safari yetu yote na kutokana na mataifa yote ambayo tulipita katikati yao. BWANA akayafukuza mbele yetu mataifa yote pamoja na Waamori, walioishi katika nchi hii. Hivyo sisi nasi tutamtumikia BWANA kwa kuwa yeye ndiye Mungu wetu.” Yoshua akawaambia watu, “Hamwezi kumtumikia BWANA. Yeye ni Mungu Mtakatifu, ni Mungu mwenye wivu. Hatasamehe uasi wenu na dhambi zenu. Ikiwa mkimwacha BWANA na kuitumikia miungu migeni, atageuka na kuwaleteeni maafa na kuwaangamiza, baada ya kuwa mwema kwenu.” Lakini watu wakamwambia Yoshua, “Sivyo! Sisi tutamtumikia BWANA.” Ndipo Yoshua akawaambia, “Ninyi mmekuwa mashahidi juu yenu wenyewe kuwa mmechagua kumtumikia BWANA.” Nao wakajibu, “Ndiyo, tu mashahidi.” Yoshua akawaambia, “Sasa basi, itupeni mbali hiyo miungu migeni mliyo nayo, nanyi mtoleeni BWANA, Mungu wa Israeli, mioyo yenu.” Nao watu wakamwambia Yoshua, “Tutamtumikia BWANA Mungu wetu na kumtii yeye.” Siku ile Yoshua akafanya agano kwa ajili ya watu na hapo Shekemu ndipo alipowaandikia amri na sheria. Naye Yoshua akayaandika mambo haya katika Kitabu cha Sheria ya Mungu. Ndipo akalitwaa jiwe kubwa, akalisimamisha huko chini ya mwaloni, karibu na mahali patakatifu pa BWANA. Yoshua akawaambia watu wote, “Tazameni! Jiwe hili litakuwa shahidi juu yetu. Limesikia maneno yote BWANA aliyotuambia. Litakuwa shahidi juu yenu kama mtakuwa waongo kwa Mungu wenu.” Basi Yoshua akawatuma watu kila mmoja aende katika urithi wake mwenyewe. Baada ya mambo haya, Yoshua mwana wa Nuni, mtumishi wa BWANA akafa akiwa na umri wa miaka mia moja na kumi. Nao wakamzika katika nchi ya urithi wake, huko Timnath-Sera katika nchi ya vilima ya Efraimu, kaskazini mwa Mlima Gaashi. Israeli wakamtumikia BWANA siku zote za maisha ya Yoshua, na za hao wazee walioishi baada ya Yoshua kufa, ambao waliona kila kitu BWANA alichowatendea Israeli.