Yoshua 23:14-16
Yoshua 23:14-16 Biblia Habari Njema (BHN)
“Sasa, wakati wangu wa kufariki dunia kama ilivyo kawaida ya walimwengu wote umekaribia. Lakini nyinyi nyote mnajua wazi mioyoni na rohoni mwenu kwamba katika mambo yote mema ambayo Mwenyezi-Mungu Mungu wenu aliwaahidi, hakuna hata moja ambalo halikutimia. Yote yametimia kama vile alivyoahidi. Lakini kama vile Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, alivyotimiza mambo yote mema aliyowaahidi, vivyo hivyo anaweza kuwaletea maovu yote mpaka awaangamize nyote kutoka nchi hii nzuri ambayo amewapeni. Kama mkivunja agano lake Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, ambalo aliwaamuru mlishike, mkaenda kuitumikia miungu mingine na kuisujudia, basi, hasira ya Mwenyezi-Mungu itawaka juu yenu, nanyi mtaangamia mara moja kutoka nchi hii nzuri ambayo amewapeni.”
Yoshua 23:14-16 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Angalieni, mimi leo ninakwenda njia ile waendayo watu wote wa ulimwengu; nanyi nyote mnajua mioyoni mwenu, na rohoni mwenu, ya kuwa halikuwapungukia ninyi hata neno moja katika mambo hayo mema yote aliyoyanena BWANA, Mungu wenu, katika habari zenu; yote yametimia kwenu hapana neno lolote mlilopungukiwa. Kisha itakuwa, kama yalivyowafikia yale mambo mema yote, BWANA, Mungu wenu, aliyowaahidia ninyi, kadhalika BWANA atawafikilizia mabaya yote, hata atakapokuwa amewaangamiza katika nchi hii njema, BWANA Mungu wenu, aliyowapa. Hapo mtakapolivunja agano la BWANA, Mungu wenu, alilowaamuru, na kwenda kuitumikia miungu mingine, na kujiinamisha mbele yao, ndipo hasira ya BWANA itakapowaka juu yenu, nanyi mtaangamia upesi katika nchi hii njema aliyowapa.
Yoshua 23:14-16 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Angalieni, mimi leo ninakwenda njia ile waendayo watu wote wa ulimwengu; nanyi nyote mnajua mioyoni mwenu, na rohoni mwenu, ya kuwa halikuwapungukia ninyi hata neno moja katika mambo hayo mema yote aliyoyanena BWANA, Mungu wenu, katika habari zenu; yote yametimia kwenu hapana neno lo lote mlilopungukiwa. Kisha itakuwa, kama yalivyowafikilia yale mambo mema yote, BWANA, Mungu wenu, aliyowaahidia ninyi, kadhalika BWANA atawafikilizia mabaya yote, hata atakapokuwa amewaangamiza katika nchi hii njema, BWANA Mungu wenu, aliyowapa. Hapo mtakapolivunja agano la BWANA, Mungu wenu, alilowaamuru, na kwenda kuitumikia miungu mingine, na kujiinamisha mbele yao, ndipo hasira ya BWANA itakapowaka juu yenu, nanyi mtaangamia upesi katika nchi hii njema aliyowapa.
Yoshua 23:14-16 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
“Sasa mimi ninakaribia kwenda katika njia ya watu wote wa dunia. Mnajua kwa mioyo yenu na roho zenu kwamba hakuna ahadi zozote njema BWANA Mungu wenu alizowaahidia, ambazo hazikutimia. Kila ahadi imetimizwa, hakuna hata moja ambayo haikutimia. Lakini kama vile kila ahadi njema ya BWANA Mungu wenu imekuwa kweli, vivyo hivyo BWANA ataleta maovu yote kama alivyo onya, mpaka awe amewaangamiza kutoka nchi hii nzuri aliyowapa. Kama mkilivunja agano la BWANA Mungu wenu, ambalo aliwaamuru ninyi, mkaenda na kuitumikia miungu mingine na kuisujudia, hasira ya BWANA itawaka dhidi yenu, nanyi mtaangamia kutoka nchi nzuri aliyowapa ninyi.”