Yoshua 22:1-34
Yoshua 22:1-34 Biblia Habari Njema (BHN)
Basi, Yoshua akawaita watu wa kabila la Reubeni, la Gadi na watu wa nusu ya kabila la Manase akawaambia, “Nyinyi mmefuata yale yote Mose, mtumishi wa Mwenyezi-Mungu, aliyowaamuru na mmetii maagizo niliyowaamuru. Wala hamkuwaacha ndugu zenu muda huo wote mrefu mpaka leo, bali mmefuata kwa makini amri ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu. Sasa Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu amewapa ndugu zenu amani, kama vile alivyoahidi, basi, rudini kwenu katika nchi ambayo mlipewa na Mose mtumishi wa Mwenyezi-Mungu, iwe mali yenu, yaani ngambo ya mto Yordani. Muwe waangalifu kutii amri na sheria ambazo Mose, mtumishi wa Mwenyezi-Mungu, aliwaamuru: Kumpenda Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, mfuate anachotaka na kushika amri zake; mkae pamoja naye na kumtumikia kwa moyo wote na roho yote.” Basi, Yoshua akawabariki na kuwaruhusu waende zao akawaambia, “Rudini makwenu na utajiri mwingi; ng'ombe wenu wote, fedha, dhahabu, shaba, chuma na mavazi mengi. Gawaneni na ndugu zenu nyara zote mlizoziteka kutoka kwa maadui zenu.” Mose alikuwa ameyapa nusu ya kabila la Manase sehemu yao huko Bashani. Naye Yoshua akaipatia nusu ya pili ya kabila hilo sehemu yao huko magharibi ya mto Yordani kama alivyoyapa makabila yale mengine. Basi, watu wa Reubeni, Gadi na nusu ya kabila la Manase wakaachana na watu wa makabila mengine ya Israeli huko Shilo, nchini Kanaani, wakarudi kwao katika nchi ya Gileadi, nchi yao wenyewe waliyoimiliki kwa amri ya Mwenyezi-Mungu kama alivyomwagiza Mose. Walipofika kwenye mto Yordani wakiwa bado katika nchi ya Kanaani, wakajenga madhabahu kubwa sana karibu na mto huo. Basi, habari zikawafikia watu wa makabila mengine ya Israeli kwamba makabila ya Reubeni, Gadi na nusu ya kabila la Manase yalikuwa yamejenga madhabahu kubwa karibu na mto Yordani katika nchi ya Kanaani, yaani ndani ya eneo lao. Waliposikia hivyo, Waisraeli walikusanyika wote huko Shilo kwenda kupigana vita na hayo makabila ya mashariki. Basi, watu wa Israeli wakamtuma Finehasi, mwanawe kuhani Eleazari, huko Gileadi kwa makabila ya Reubeni, Gadi na nusu ya kabila la Manase. Finehasi akaondoka pamoja na wakuu kumi, kila mmoja akiwa mkuu wa jamaa katika kabila lake. Nao wakawaendea watu wa makabila ya Reubeni, Gadi na nusu ya kabila la Manase huko Gileadi wakawaambia, “Jumuiya nzima ya Mwenyezi-Mungu inauliza hivi: ‘Ni udanganyifu gani huu mmemfanyia Mungu wa Israeli? Mbona mmemwasi Mwenyezi-Mungu kwa kujenga madhabahu hii? Je, dhambi tulizotenda huko Peori hazitoshi? Hamwoni kwamba bado hatujajitakasa na kwamba mateso yake bado yanaisumbua jumuiya ya Mwenyezi-Mungu? Kwa nini, basi, mmeacha kumfuata Mwenyezi-Mungu? Mkimwasi Mwenyezi-Mungu leo, kesho ataikasirikia sana jumuiya nzima ya Israeli. Haya, ikiwa nchi yenu si najisi, njoni katika nchi ya Mwenyezi-Mungu ambako hema yake iko na kujichukulia sehemu huko pamoja nasi; ila tu msimwasi Mwenyezi-Mungu na kutufanya sisi sote waasi kwa kujijengea nyinyi wenyewe madhabahu isiyo ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu. Je, Akani mwana wa Zera alipokosa uaminifu katika vitu vitakatifu, ghadhabu haikuangukia jumuiya nzima ya Israeli? Tena Akani hakufa tu yeye peke yake kwa sababu ya uovu wake.’” Hapo watu wa makabila ya Reubeni na Gadi na nusu ya kabila la Manase wakawajibu viongozi wa jamaa za Israeli, “Mungu wa miungu ndiye Mwenyezi-Mungu! Mungu wa miungu ndiye Mwenyezi-Mungu! Yeye anajua kwa nini tumefanya hivyo. Na Waisraeli wote watajua pia! Kama huu ni uasi au ni ukosefu wa imani kwa Mwenyezi-Mungu basi, yeye aache kutuokoa leo. Kama tumemwacha Mwenyezi-Mungu tukajenga madhabahu yetu wenyewe ili tutoe sadaka za kuteketezwa, za nafaka au za amani, basi Mwenyezi-Mungu na atulipize kisasi. Lakini sivyo ilivyo. Tuliijenga kwa kuogopa kwamba huenda katika siku zijazo watoto wenu watawaambia watoto wetu, ‘Nyinyi mna uhusiano gani na Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli? Hamwoni kwamba Mwenyezi-Mungu ameweka mto wa Yordani kuwa mpaka kati yenu na sisi? Nyinyi makabila ya Reubeni na kabila la Gadi hamna fungu lolote lenu kwa Mwenyezi-Mungu.’ Hivyo watoto wenu wangeweza baadaye kusababisha watoto wetu waache kumwabudu Mwenyezi-Mungu. Ndiyo maana tuliamua kujenga madhabahu hii, lakini si kwa ajili ya kutolea juu yake sadaka wala tambiko, bali tulitaka madhabahu hii iwe ushuhuda kati yetu na nyinyi na vizazi vyetu vijavyo kwamba sisi tunayo haki ya kumtumikia Mwenyezi-Mungu kwa sadaka zetu za kuteketezwa na tambiko zetu, na kwa sadaka zetu za amani, ili watoto wenu wasije wakawaambia watoto wetu kwamba hawana fungu lolote lao kwa Mwenyezi-Mungu. Tena tulifikiri kwamba ikiwa jambo kama hilo litasemwa juu yetu au juu ya wazawa wetu katika siku zijazo, tutasema, ‘Tazameni mfano wa madhabahu ya Mwenyezi-Mungu ambayo wazee wetu waliijenga; sio kwa ajili ya kutolea juu yake sadaka au tambiko bali kama ushuhuda kati yetu na nyinyi’. Sisi hatukuwa na nia ya kumwasi sasa Mwenyezi-Mungu hata kidogo na kumwacha kwa kujenga madhabahu ya kutolea sadaka za kuteketezwa au sadaka za unga au za tambiko. Hatupendi kutolea sadaka mahali pengine isipokuwa juu ya madhabahu ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu iliyo mbele ya maskani yake.” Kuhani Finehasi, viongozi wa jumuiya nzima na wakuu wa jamaa za Israeli waliokuwa pamoja naye waliposikia maneno hayo ya watu wa makabila ya Reubeni na Gadi na nusu ya kabila la Manase, wakaridhika. Naye Finehasi mwana wa kuhani Eleazari, akayaambia makabila ya Reubeni na Gadi na nusu ya kabila la Manase, “Leo tumejua kwamba Mwenyezi-Mungu yumo miongoni mwenu maana hamkumfanyia Mungu uasi. Sasa mmewaokoa Waisraeli wasiadhibiwe na Mwenyezi-Mungu.” Basi, Finehasi mwana wa kuhani Eleazari pamoja na viongozi wenzake wakawaaga watu wa makabila ya Reubeni na Gadi wakaondoka nchini Gileadi, wakarudi Kanaani kwa Waisraeli na kuwapa habari hizo. Taarifa hiyo ikawafurahisha Waisraeli, wakamshukuru Mwenyezi-Mungu na kuacha mipango yao ya vita na lengo lao la kuharibu kabisa nchi iliyokuwa ya makabila ya Reubeni na Gadi. Watu wa makabila ya Reubeni na Gadi wakaiita ile madhabahu ya “Ushuhuda,” kwani walisema, “Madhababu hii ni ushahidi wetu kwamba Mwenyezi-Mungu ndiye Mungu.”
Yoshua 22:1-34 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Wakati huo Yoshua akawaita Wareubeni, na Wagadi, na hiyo nusu ya kabila la Manase, naye akawaambia, Ninyi mmeyafuata hayo yote mliyoamriwa na Musa, mtumishi wa BWANA, nanyi mmeisikia sauti yangu katika yote niliyowaamuru mimi; hamkuwaacha hao ndugu zenu siku hizi nyingi hata hivi leo, lakini mmeyashika maagizo ya amri ya BWANA, Mungu wenu. Na sasa yeye BWANA, Mungu wenu, amewapa ndugu zenu kustarehe, kama alivyowaambia; basi sasa rudini ninyi mwende mahemani kwenu, hata nchi ya milki yenu, ambayo huyo Musa, mtumishi wa BWANA, aliwapa ng'ambo ya pili ya Yordani. Lakini mjibidiishe sana kuzifanya amri na sheria, ambazo Musa, mtumishi wa BWANA, aliwaamuru, kumpenda BWANA, Mungu wenu, na kwenenda katika njia zake zote, na kuzishika amri zake, na kushikamana na yeye, na kumtumikia kwa moyo wenu wote na nafsi yenu yote. Basi Yoshua akawabariki, na kuwapa ruhusa waende zao; nao wakaenda mahemani kwao. Basi Musa alikuwa amewapa hiyo nusu moja ya kabila la Manase urithi katika Bashani; lakini hiyo nusu ya pili Yoshua aliwapa urithi kati ya ndugu zao, ng'ambo ya Yordani upande wa kuelekea magharibi. Zaidi ya hayo Yoshua, hapo alipowaruhusu waende zao mahemani kwao, akawabariki, kisha akanena nao, na kuwaambia, Rudini na mali mengi mahemani kwenu, na ng'ombe wengi sana, na fedha, na dhahabu, na shaba, na chuma, na mavazi mengi sana; mgawane na ndugu zenu hizo nyara za adui zenu. Basi wana wa Reubeni, na wana wa Gadi, na hiyo nusu ya kabila la Manase wakarudi, wakatoka kwa wana wa Israeli katika Shilo, ulioko nchi ya Kanaani, ili waende nchi ya Gileadi, hiyo nchi ya milki yao, waliyokuwa wanaimiliki, sawasawa na amri ya BWANA kwa mkono wa Musa. Nao walipofika pande za Yordani zilizo katika nchi ya Kanaani, hao wana wa Reubeni, na wana wa Gadi, na nusu ya kabila la Manase, wakajenga madhabahu huko karibu na Yordani, iliyoonekana kuwa ni madhabahu kubwa. Wana wa Israeli walisikia ikinenwa, Tazama, wana wa Reubeni, na wana wa Gadi, na hiyo nusu ya kabila la Manase, wamejenga madhabahu huko upande wa mbele wa nchi ya Kanaani, katika nchi iliyo karibu na Yordani, kwa upande huo ulio milki ya wana wa Israeli. Basi, wana wa Israeli waliposikia habari hiyo, mkutano wote wa wana wa Israeli wakakutanika pamoja huko Shilo, ili waende kupigana nao. Kisha wana wa Israeli wakatuma wajumbe waende kwa wana wa Reubeni, na wana wa Gadi, na hiyo nusu ya kabila la Manase, hadi nchi ya Gileadi; nao ni hawa, Finehasi mwana wa Eleazari kuhani; na pamoja naye wakuu kumi, mkuu mmoja wa nyumba ya mababa kutoka kwa kila kabila la Israeli; nao kila mmoja alikuwa ni kichwa cha nyumba ya mababa katika maelfu ya Israeli. Nao wakawafikia hao wana wa Reubeni, na wana wa Gadi, na hiyo nusu ya kabila la Manase, katika nchi ya Gileadi, na wakasema nao, wakinena, Mkutano wote wa BWANA wanena, Ni kosa gani hili mlilolikosa juu ya Mungu wa Israeli, hata mkakengeuka hivi leo na kuacha kumfuata BWANA, katika kujijengea madhabahu, na kuasi hivi leo juu ya BWANA? Je! Ule uovu wa Peori haututoshi, ambao hamjajitakasa nafsi zenu katika huo hata hivi leo, ijapokuwa ilikuja tauni juu ya mkutano wa BWANA, hata ikawa hamna budi hivi leo kugeuka na kuacha kumfuata BWANA? Kisha itakuwa, kwa kuwa ninyi mnamwasi BWANA hivi leo, kwamba kesho yeye atakasirika na mkutano wote wa Israeli. Basi ikiwa hiyo inchi yenu ni najisi, vukeni na kuingia katika nchi ya milki yake BWANA, ambamo maskani ya BWANA inakaa ndani yake, nanyi twaeni milki kati yetu; lakini msimwasi BWANA, wala msituasi sisi, kwa kujijengea madhabahu zaidi ya hiyo madhabahu ya BWANA, Mungu wetu. Je! Huyo Akani mwana wa Zera hakukosa katika vile vitu vilivyowekwa wakfu, na hasira ikauangukia mkutano wote wa Israeli? Kisha mtu huyo hakuangamia peke yake katika uovu wake? Ndipo hapo wana wa Reubeni, na wana wa Gadi, na hiyo nusu ya kabila la Manase, wakajibu, na kuwaambia hao waliokuwa ni vichwa vya maelfu ya Israeli, wakasema, Mungu, Mungu BWANA, naam, Mungu, Mungu BWANA, yeye anajua, na Israeli naye atajua; kama ni katika uasi, au kama ni katika kosa juu ya BWANA, usituokoe hivi leo; kama tumejijengea madhabahu ili kukengeuka na kuacha kumfuata BWANA; au kama ni kusongeza juu yake sadaka ya kuteketezwa, au sadaka ya unga, au kama ni kusongeza sadaka za amani juu yake, yeye BWANA mwenyewe na atulipize kisasi; au kama sisi tumefanya jambo hili kwa hofu kuwa, katika siku zijazo wana wenu huenda wakanena na wana wetu na kusema, Ninyi mna uhusiano gani na BWANA, Mungu wa Israeli? Kwa kuwa yeye BWANA ameufanya huu mto wa Yordani uwe mpaka katikati yetu nanyi, enyi wana wa Reubeni, na wana wa Gadi, hamna fungu katika BWANA; basi hivyo wana wenu wangeweza kuwafanya wana wetu waache kumwabudu BWANA. Kwa ajili ya hayo tulisema, Natujijengee madhabahu, si kwa ajili ya sadaka za kuteketezwa, wala kwa sadaka yoyote; bali iwe ushahidi kati yetu nanyi, tena kati ya vizazi vyetu baada yetu, kwamba sisi tunamhudumia BWANA kwa njia ya sadaka zetu za kuteketezwa, na kwa dhabihu zetu, na kwa sadaka zetu za amani; ili kwamba wana wenu wasiwaambie wana wetu katika siku zijazo, Ninyi hamna fungu katika BWANA. Kwa hiyo tulisema, Itakuwa, hapo watakapotuambia neno kama hilo, au kuwaambia watu wa vizazi vyetu katika siku zijazo neno kama hilo, ndipo sisi tutawaambia, Angalieni huu mfano wa madhabahu ya BWANA, walioufanya baba zetu, si kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa, wala kwa ajili ya dhabihu; lakini ni ushahidi kati yetu nanyi. Mungu na atuzuie tusimwasi BWANA, na kukengeuka hivi leo na kuacha kumfuata BWANA, hata mkajenga madhabahu kwa ajili ya sadaka za kuteketezwa, au sadaka za unga, au dhabihu, mbali na ile madhabahu ya BWANA, Mungu wetu, iliyo huko mbele ya maskani yake. Basi Finehasi kuhani, na wakuu wa mkutano, na hao vichwa vya maelfu ya Israeli waliokuwa pamoja naye, hapo walipoyasikia hayo maneno waliyoyasema hao wana wa Reubeni, na wana wa Gadi, na wana wa Manase, maneno hayo yaliwaridhisha sana. Naye Finehasi, mwana wa Eleazari, kuhani, akawaambia wana wa Reubeni, na wana wa Gadi, na wana wa Manase, akasema, Siku hii ya leo tumejua ya kwamba BWANA yu kati yetu, kwa sababu hamkukosa katika jambo hili mbele ya BWANA; sasa ninyi mmewaokoa wana wa Israeli na mkono wa BWANA. Kisha Finehasi, mwana wa Eleazari, kuhani, na hao wakuu, wakarudi na kuwaacha wana wa Reubeni na wana wa Gadi, wakatoka katika nchi ya Gileadi, na kuingia nchi ya Kanaani; wakawarudia wana wa Israeli, wakawapa habari. Ripoti hiyo ikawaridhisha Waisraeli; nao Waisraeli wakamhimidi Mungu, wala hawakusema tena habari ya kuwaendea ili kupigana nao, wala kuiharibu nchi waliyoikaa wana wa Reubeni, na wana wa Gadi. Basi hao wana wa Reubeni, na wana wa Gadi, wakaiita madhabahu hiyo Edi; wakasema, Kwa kuwa ni ushahidi kati yetu ya kwamba yeye BWANA ndiye Mungu.
Yoshua 22:1-34 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Wakati huo Yoshua akawaita Wareubeni, na Wagadi, na hiyo nusu ya kabila ya Manase, naye akawaambia, Ninyi mmeyaandama hayo yote mliyoamriwa na Musa, mtumishi wa BWANA, nanyi mmeisikia sauti yangu katika yote niliyowaamuru mimi; hamkuwaacha hao ndugu zenu siku hizi nyingi hata hivi leo, lakini mmeyashika mausia ya amri ya BWANA, Mungu wenu. Na sasa yeye BWANA, Mungu wenu, amewapa ndugu zenu kustarehe, kama alivyowaambia; basi sasa rudini ninyi mwende mahemani kwenu, hata nchi ya milki yenu, ambayo huyo Musa, mtumishi wa BWANA, aliwapa ng’ambo ya pili ya Yordani. Lakini mjibidiishe sana kuzifanya amri na sheria, ambazo Musa, mtumishi wa BWANA, aliwaamuru, kumpenda BWANA, Mungu wenu, na kwenenda katika njia zake zote, na kuzishika amri zake, na kushikamana na yeye, na kumtumikia kwa moyo wenu wote na nafsi yenu yote. Basi Yoshua akawabarikia, na kuwapa ruhusa waende zao; nao wakaenda mahemani kwao. Basi Musa alikuwa amewapa hiyo nusu moja ya kabila ya Manase urithi katika Bashani; lakini hiyo nusu ya pili Yoshua aliwapa urithi kati ya ndugu zao, ng’ambo ya Yordani upande wa kuelekea magharibi. Zaidi ya hayo Yoshua, hapo alipowapeleka waende zao mahemani kwao, akawabarikia, kisha akanena nao, na kuwaambia, Rudini na mali mengi mahemani kwenu, na ng’ombe wengi sana, na fedha, na dhahabu, na shaba, na chuma, na mavao mengi sana; mzigawanye na ndugu zenu hizo nyara za adui zenu. Basi wana wa Reubeni, na wana wa Gadi, na hiyo nusu ya kabila ya Manase wakarudi, wakatoka kwa wana wa Israeli katika Shilo, ulioko nchi ya Kanaani, ili waende nchi ya Gileadi, hiyo nchi ya milki yao, waliyokuwa wanaimiliki, sawasawa na amri ya BWANA kwa mkono wa Musa. Nao walipofika pande za Yordani, zilizo katika nchi ya Kanaani, hao wana wa Reubeni, na wana wa Gadi, na nusu ya kabila ya Manase, wakajenga madhabahu huko karibu na Yordani, iliyoonekana kuwa ni madhabahu kubwa. Wana wa Israeli walisikia ikinenwa, Tazama, wana wa Reubeni, na wana wa Gadi, na hiyo nusu ya kabila ya Manase, wamejenga madhabahu huko upande wa mbele wa nchi ya Kanaani, katika nchi iliyo karibu na Yordani, kwa upande huo ulio milki ya wana wa Israeli. Basi, wana wa Israeli waliposikia habari hiyo, mkutano wote wa wana wa Israeli wakakutanika pamoja huko Shilo, ili waende kupigana nao. Kisha wana wa Israeli wakatuma wajumbe waende kwa wana wa Reubeni, na wana wa Gadi, na hiyo nusu ya kabila ya Manase, hata nchi ya Gileadi; nao ni hawa, Finehasi mwana wa Eleazari kuhani; na pamoja naye wakuu kumi, mkuu mmoja wa nyumba ya mababa kwa ajili ya kila kabila ya Israeli; nao kila mmoja alikuwa ni kichwa cha nyumba ya mababa katika maelfu ya Israeli. Nao wakawafikilia hao wana wa Reubeni, na wana wa Gadi, na hiyo nusu ya kabila ya Manase, katika nchi ya Gileadi, na wakasema nao, wakinena, Mkutano wote wa BWANA wanena, Ni kosa gani hili mlilolikosa juu ya Mungu wa Israeli, hata mkakengeuka hivi leo na kuacha kumwandama BWANA, katika kujijengea madhabahu, na kuasi hivi leo juu ya BWANA? Je! Ule uovu wa Peori haututoshi, ambao hamjajitakasa nafsi zenu katika huo hata hivi leo, ijapokuwa ilikuja tauni juu ya mkutano wa BWANA, hata ikawa hamna budi hivi leo kugeuka na kuacha kumwandama BWANA? Kisha itakuwa, kwa kuwa ninyi mwamwasi BWANA hivi leo, kwamba kesho yeye atakasirika na mkutano wote wa Israeli. Basi kwamba hiyo nchi ya milki yenu si tohara, ndipo ninyi vukeni na kuingia nchi ya milki yake BWANA, ambayo maskani ya BWANA inakaa ndani yake, nanyi twaeni milki kati yetu; lakini msimwasi BWANA, wala msituasi sisi, kwa kujijengea madhabahu zaidi ya hiyo madhabahu ya BWANA, Mungu wetu. Je! Huyo Akani mwana wa Zera hakukosa katika vile vitu vilivyowekwa wakfu, na hasira ikauangukia mkutano wote wa Israeli? Kisha mtu huyo hakuangamia peke yake katika uovu wake? Ndipo hapo wana wa Reubeni, na wana wa Gadi, na hiyo nusu ya kabila ya Manase, wakajibu, na kuwaambia hao waliokuwa ni vichwa vya maelfu ya Israeli, wakasema, Mungu, Mungu BWANA, naam, Mungu, Mungu BWANA, yeye yuajua, na Israeli naye atajua; kama ni katika uasi, au kama ni katika kosa juu ya BWANA, (usituokoe hivi leo); sisi kujijengea madhabahu ili kukengeuka na kuacha kumwandama BWANA; au kama ni kusongeza juu yake sadaka ya kuteketezwa, au sadaka ya unga, au kama ni kusongeza sadaka za amani juu yake, yeye BWANA mwenyewe na alitake jambo hili; au kama sisi tumefanya jambo hili kwa hadhari sana, tena makusudi, huku tukisema, Katika siku zijazo wana wenu yamkini wakanena na wana wetu, na kusema, Ninyi mna nini na BWANA, yeye Mungu wa Israeli? Kwa kuwa yeye BWANA ameufanya huu mto wa Yordani uwe mpaka katikati ya sisi na ninyi, enyi wana wa Reubeni, na wana wa Gadi, hamna fungu katika BWANA; basi hivyo wana wenu wangewakomesha wana wetu wasimche BWANA. Kwa ajili ya hayo tulisema, Na tufanye tayari ili kujijengea madhabahu, si kwa ajili ya sadaka za kuteketezwa, wala kwa sadaka yo yote; bali itakuwa ni ushahidi kati ya sisi na ninyi, tena kati ya vizazi vyetu baada yetu, ili kwamba tufanye huo utumishi wa BWANA mbele yake kwa njia ya sadaka zetu za kuteketezwa, na kwa dhabihu zetu, na kwa sadaka zetu za amani; ili kwamba wana wenu wasiwaambie wana wetu katika zamani zijazo, Ninyi hamna fungu katika BWANA. Kwa hiyo tulisema, Itakuwa, hapo watakapotuambia neno kama hilo, au kuwaambia watu wa vizazi vyetu katika zamani zijazo neno kama hilo, ndipo sisi tutawaambia, Angalieni huu mfano wa madhabahu ya BWANA, walioufanya baba zetu, si kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa, wala kwa ajili ya dhabihu; lakini ni ushahidi kati ya sisi na ninyi. Mungu na atuzuie msimwasi BWANA, na kukengeuka hivi leo na kuacha kumwandama BWANA, hata mkajenga madhabahu kwa ajili ya sadaka za kuteketezwa, au sadaka za unga, au dhabihu, mbali na ile madhabahu ya BWANA, Mungu wetu, iliyo huko mbele ya maskani yake. Basi Finehasi kuhani, na wakuu wa mkutano, maana, ni hao waliokuwa vichwa vya maelfu ya Israeli waliokuwa pamoja naye, hapo walipoyasikia hayo maneno waliyoyasema hao wana wa Reubeni, na wana wa Gadi, na wana wa Manase, maneno hayo yaliwaridhia sana. Naye Finehasi, mwana wa Eleazari, kuhani, akawaambia wana wa Reubeni, na wana wa Gadi, na wana wa Manase, akasema, Siku hii ya leo twajua ya kwamba BWANA yu kati yetu, kwa sababu hamkukosa katika jambo hili mbele ya BWANA; sasa ninyi mmewaokoa wana wa Israeli na mkono wa BWANA. Kisha Finehasi, mwana wa Eleazari, kuhani, na hao wakuu, wakarudi na kuwaacha wana wa Reubeni, na wana wa Gadi, wakatoka katika nchi ya Gileadi, na kuingia nchi ya Kanaani; wakawarudia wana wa Israeli, wakawapa habari. Wana wa Israeli nao wakaliridhia jambo hilo; nao wana wa Israeli wakamhimidi Mungu, wala hawakusema tena habari ya kuwaendea juu yao kupigana nao, wala kuiharibu nchi waliyoikaa wana wa Reubeni, na wana wa Gadi. Basi hao wana wa Reubeni, na wana wa Gadi, wakaiita madhabahu hiyo Edi; wakasema, Kwa kuwa ni ushahidi kati yetu ya kwamba yeye BWANA ndiye Mungu.
Yoshua 22:1-34 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Ndipo Yoshua akawaita Wareubeni, Wagadi na nusu ya kabila la Manase, naye akawaambia, “Mmeshafanya yale yote Musa mtumishi wa BWANA aliyowaamuru, nanyi mmenitii kwa kila jambo nililowaamuru. Kwa muda mrefu sasa, hadi siku hii ya leo, hamkuwaacha ndugu zenu, bali ninyi mmetimiza ile kazi BWANA Mungu wenu aliyowapa. Sasa kwa kuwa BWANA Mungu wenu amewapa ndugu zenu pumziko kama alivyoahidi, rudini nyumbani mwenu katika nchi ambayo Musa mtumishi wa BWANA aliwapa ngʼambo ya Yordani. Lakini mwe waangalifu sana kushika amri na sheria ambazo Musa mtumishi wa BWANA aliwapa: yaani kumpenda BWANA Mungu wenu na kuenenda katika njia zake zote, kutii amri zake, kushikamana naye kwa uthabiti na kumtumikia kwa moyo wote na roho yote.” Ndipo Yoshua akawabariki na kuwaaga waende zao, nao wakaenda nyumbani kwao. (Kwa nusu ya kabila la Manase, Musa alikuwa amewapa eneo katika Bashani na ile nusu nyingine ya hilo kabila Yoshua aliwapa eneo upande wa magharibi mwa Yordani pamoja na ndugu zao.) Yoshua alipowaaga waende zao nyumbani, aliwabariki, akisema, “Rudini nyumbani kwenu na utajiri wenu mwingi, yaani makundi makubwa ya mifugo, mkiwa na fedha, dhahabu, shaba na chuma, pia mavazi mengi; nanyi mkagawane na ndugu zenu hizo nyara zilizotoka kwa adui zenu.” Kwa hiyo Wareubeni, Wagadi na nusu ya kabila la Manase wakawaacha Waisraeli huko Shilo katika nchi ya Kanaani ili kurudi Gileadi, nchi yao wenyewe waliyoipata sawasawa na agizo la BWANA kupitia Musa. Walipofika Gelilothi karibu na Yordani, katika nchi ya Kanaani, Wareubeni, Wagadi na nusu ya kabila la Manase wakajenga madhabahu ya fahari kubwa huko kando ya Yordani. Waisraeli hao wengine waliposikia kwamba Wareubeni, Wagadi na nusu ya kabila la Manase walikuwa wamejenga madhabahu kwenye mpaka wa Kanaani huko Gelilothi karibu na Yordani kwenye upande wa Israeli, Waisraeli hao wengine walikusanyika huko Shilo ili wapigane nao. Kwa hiyo Waisraeli wengine wakamtuma Finehasi, mwana wa kuhani Eleazari, aende katika nchi ya Gileadi kwa Wareubeni, Wagadi na nusu ya kabila la Manase. Wakatuma viongozi kumi pamoja naye, mmoja kutoka kwa kila kabila la Israeli, kila mmoja akiwa kiongozi katika jamaa miongoni mwa koo za Israeli. Walipofika Gileadi, kwa Wareubeni, Wagadi na nusu ya kabila la Manase, wakawaambia: “Kusanyiko lote la BWANA wasema hivi: ‘Je, mmewezaje kuacha kumwamini Mungu wa Israeli jinsi hii? Mmewezaje kumwacha BWANA na kujijengea madhabahu dhidi yake na kumwasi? Je, dhambi ya Peori haikutosha? Hata ingawa kulikuja tauni juu ya kusanyiko la BWANA, hadi leo hatujatakasika kutokana na dhambi hiyo! Je, sasa ndiyo mnamwacha BWANA? “ ‘Mkimwasi BWANA leo, kesho atawakasirikia kusanyiko lote la Israeli. Ikiwa nchi mnayomiliki imenajisika, vukeni mje katika nchi ya BWANA, mahali Maskani ya BWANA ilipo, nanyi mkajitwalie sehemu miongoni mwetu, lakini msije mkaasi dhidi ya BWANA wala dhidi yetu sisi kwa kujijengea madhabahu, isipokuwa madhabahu ya BWANA Mungu wetu. Akani mwana wa Zera alipokosa uaminifu kwa vitu vilivyotengwa kwa ajili ya kuangamizwa, je, ghadhabu haikuwapata kusanyiko lote la Israeli? Si yeye pekee aliyekufa kwa ajili ya dhambi yake.’ ” Ndipo Wareubeni, Wagadi na nusu ya kabila la Manase walipowajibu viongozi wa koo za Israeli, wakisema: “Yeye Mwenye Nguvu, Mungu, BWANA! Yeye Mwenye Nguvu, Mungu, BWANA! Yeye anajua! Israeli na wajue! Kama huu umekuwa ni uasi au kukosa utii kwa BWANA, msituache hai siku hii ya leo. Kama tumejijengea madhabahu yetu wenyewe ili kumwacha BWANA, na kutoa sadaka za kuteketezwa na sadaka za nafaka, au kutoa sadaka za amani juu yake, BWANA mwenyewe na atupatilize leo. “Sivyo! Tulifanya hivyo kwa hofu kwamba siku zijazo wazao wenu wanaweza wakawaambia wazao wetu, ‘Mna uhusiano gani na BWANA, Mungu wa Israeli? BWANA ameifanya Yordani kuwa mpaka kati yetu na ninyi, ninyi Wareubeni na Wagadi! Hamna fungu kwa BWANA.’ Kwa hiyo wazao wenu wanaweza wakawasababisha wazao wetu wakaacha kumcha BWANA. “Hii ndiyo sababu tulisema, ‘Tujiweke tayari na tujenge madhabahu, lakini si kwa ajili ya sadaka za kuteketezwa au dhabihu.’ Badala yake, itakuwa ni ushahidi kati yetu na ninyi na vizazi vijavyo, kwamba tutamwabudu BWANA katika mahali patakatifu pake pamoja na sadaka zetu za kuteketezwa, dhabihu na sadaka za amani. Ndipo katika siku zijazo, wazao wenu hawataweza kuwaambia wazao wetu, ‘Ninyi hamna fungu katika BWANA.’ “Nasi tulisema, ‘Wakati wowote wakituambia hilo, au kuwaambia uzao wetu, tutawajibu hivi: Angalieni nakala hii ya madhabahu ya BWANA, ambayo baba zetu waliijenga, si kwa ajili ya sadaka za kuteketezwa na dhabihu, bali kama ushahidi kati yetu na ninyi.’ “Hili jambo la kumwasi BWANA na kumwacha siku hii ya leo kwa kujenga madhabahu kwa ajili ya sadaka za kuteketezwa, sadaka za nafaka na dhabihu, isipokuwa madhabahu ya BWANA Mungu wetu iliyo mbele ya Maskani yake na liwe mbali nasi.” Kuhani Finehasi na viongozi wa kusanyiko, hao wakuu wa koo za Israeli, waliposikia hayo waliyosema Wareubeni, Wagadi na Manase, wakaridhika. Naye Finehasi mwana wa kuhani Eleazari, akawaambia Wareubeni, Wagadi na Manase, “Leo tunajua kwamba BWANA yuko pamoja nasi, kwa sababu hamkukosa uaminifu kwa BWANA katika jambo hili. Sasa mmewaokoa Waisraeli kutoka kwa mkono wa BWANA.” Ndipo Finehasi, mwana wa kuhani Eleazari, na viongozi wakarudi Kanaani kutoka mkutano wao na Wareubeni na Wagadi huko Gileadi, nao wakatoa taarifa kwa Waisraeli. Walifurahi kusikia taarifa hiyo, na wakamhimidi Mungu. Wala hawakuzungumza tena habari za kupigana vita dhidi yao ili kuharibu nchi ambayo Wareubeni na Wagadi waliishi. Nao Wareubeni na Wagadi wakaita madhabahu hayo Edi: kwa kuwa itakuwa shahidi kati yetu na ninyi kwamba BWANA ndiye Mungu.