Yoshua 20:1-9
Yoshua 20:1-9 Biblia Habari Njema (BHN)
Kisha Mwenyezi-Mungu akamwambia Yoshua, awaambie Waisraeli hivi: “Jichagulieni miji ambamo mtu aweza kukimbilia usalama ambayo nilimwambia Mose akueleze. Mtu yeyote akimuua mtu bila kukusudia anaweza kukimbilia katika mji mmojawapo na hivyo kumkwepa yule mtu aliye na jukumu la kulipiza kisasi cha damu. Mwuaji atakimbilia katika mji mmojawapo na kusimama mlangoni mwa mji na kuwaeleza wazee wa mji huo kesi yake. Wazee watampokea ndani na kumpa mahali pa kuishi pamoja nao. Yule mwenye kulipiza kisasi akimwandama mpaka mjini, wazee wa mji huo hawaruhusiwi kumtoa mwuaji huyo kwa yule mwenye kulipiza kisasi, maana alimuua mwenzake kwa bahati mbaya, kwa vile hapakuwa na uadui kati yao hapo awali. Mwuaji ataendelea kuishi humo mpaka hapo atakapohukumiwa mbele ya jumuiya nzima ya Israeli na pia mpaka hapo yule kuhani mkuu ambaye alikuwa na madaraka wakati huo amefariki. Baada ya hapo mtu huyo ataweza kurudi nyumbani kwake katika mji ule alikotoroka.” Basi, kwa ajili hiyo wakaitenga miji ya Kedeshi katika Galilaya kwenye milima ya Naftali, Shekemu katika milima ya Efraimu na Kiriath-arba (yaani Hebroni) katika nchi ya milima ya Yuda. Katika ngambo ya mto Yordani, mashariki ya mji wa Yeriko, walichagua mji wa Bezeri ulio kwenye nyika tambarare na ambao mji wenyewe ni wa eneo la kabila la Reubeni. Pia walichagua Ramothi huko Gileadi ambao ni mji wa kabila la Gadi na Golani huko Bashani katika eneo la kabila la Manase. Hii ndiyo miji iliyotengwa kwa ajili ya watu wote wa Israeli na wageni walioishi miongoni mwao, ili mtu yeyote atakayemuua mwenzake bila kukusudia akimbilie huko asije akauawa na mwenye jukumu la kulipiza kisasi cha damu, hadi hapo atakapohukumiwa mbele ya jumuiya nzima.
Yoshua 20:1-9 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Kisha BWANA akanena na Yoshua, na kumwambia, Nena wewe na wana wa Israeli, uwaambie, Haya, toeni hiyo miji ya makimbilio, ambayo niliwaambia habari zake kwa mkono wa Musa; ili kwamba mwenye kuua mtu, aliyemwua mtu yeyote pasipo kukusudia, na pasipo kujua, apate kukimbilia huko; nayo itakuwa ni mahali pa kukimbilia kwenu, kumkimbia huyo ajilipizaye kisasi cha damu. Naye ataikimbilia miji hiyo mmojawapo, naye atasimama hapo penye maingilio ya lango la huo mji, kisha atanena neno lake masikioni mwa wazee wa mji; nao watamtia kwao ndani ya mji, na kumpa mahali, ili apate kukaa kati yao. Na kama huyo mwenye kujilipiza kisasi cha damu akimfuatia, ndipo hawatamtoa huyo mwuaji kumtia mkononi mwake huyo; kwa sababu alimpiga mwenziwe naye hakujua, wala hakumchukia tangu hapo. Naye atakaa katika mji huo, hadi hapo atakaposimama mbele ya mkutano kuhukumiwa, hadi kifo chake kuhani mkuu mwenye kuwapo siku hizo; ndipo yule mwuaji atarudi, na kuuendea mji wake mwenyewe, na nyumba yake mwenyewe, hadi mji huo alioutoka hapo alipokimbia. Nao wakaweka Kedeshi katika Galilaya katika nchi ya vilima ya Naftali, na Shekemu katika nchi ya vilima ya Efraimu, na Kiriath-arba (ndio Hebroni) katika nchi ya vilima ya Yuda. Tena ng'ambo ya pili ya Yordani pande za Yeriko upande wa kuelekea mashariki wakaweka Bezeri ulioko nyikani, katika nchi tambarare ya kabila la Reubeni, na Ramothi katika Gileadi katika kabila la Gadi, na Golani katika Bashani katika kabila la Manase. Miji hiyo ndiyo miji iliyoamriwa kwa ajili ya wana wa Israeli wote, na kwa ajili ya mgeni akaaye kati yao ugenini, ili kwamba mtu yeyote atakayemwua mtu pasipo kukusudia apate kimbilia huko, asife kwa mkono wa mwenye kujilipiza kisasi cha damu, hadi hapo atakapokuwa amekwisha simama mbele ya mkutano.
Yoshua 20:1-9 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Kisha BWANA akanena na Yoshua, na kumwambia, Nena wewe na wana wa Israeli, uwaambie, Haya, toeni hiyo miji ya makimbilio, ambayo niliwaambia habari zake kwa mkono wa Musa; ili kwamba mwenye kuua mtu, aliyemwua mtu awaye yote pasipo kukusudia, na pasipo kujua, apate kukimbilia kuko; nayo itakuwa ni mahali pa kukimbilia kwenu, kumkimbia huyo ajilipizaye kisasi cha damu. Naye ataikimbilia miji hiyo mmojawapo, naye atasimama hapo penye maingilio ya lango la huo mji, kisha atanena neno lake masikioni mwa wazee wa mji; nao watamtia kwao ndani ya mji, na kumpa mahali, ili apate kukaa kati yao. Na kama huyo mwenye kujilipiza kisasi cha damu akimwandamia, ndipo hawatamtoa huyo mwuaji kumtia mkononi mwake huyo; kwa sababu alimpiga mwenziwe naye hakujua, wala hakumchukia tangu hapo. Naye atakaa katika mji huo, hata hapo atakaposimama mbele ya mkutano kuhukumiwa, hata kifo chake kuhani mkuu mwenye kuwapo siku hizo; ndipo yule mwuaji atarudi, na kuuendea mji wake mwenyewe, na nyumba yake mwenyewe, hata mji huo alioutoka hapo alipokimbia. Nao wakaweka Kedeshi katika Galilaya katika nchi ya vilima ya Naftali, na Shekemu katika nchi ya vilima ya Efraimu, na Kiriath-arba (ndio Hebroni) katika nchi ya vilima ya Yuda. Tena ng’ambo ya pili ya Yordani pande za Yeriko upande wa kuelekea mashariki wakaweka Bezeri ulioko nyikani, katika nchi tambarare ya kabila ya Reubeni, na Ramothi katika Gileadi katika kabila ya Gadi, na Golani katika Bashani katika kabila ya Manase. Miji hiyo ndiyo miji iliyoamriwa kwa ajili ya wana wa Israeli wote, na kwa ajili ya mgeni akaaye kati yao ugenini, ili kwamba mtu awaye yote atakayemwua mtu pasipo kukusudia apate kimbilia huko, asife kwa mkono wa mwenye kujilipiza kisasi cha damu, hata hapo atakapokuwa amekwisha simama mbele ya mkutano.
Yoshua 20:1-9 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Ndipo BWANA akamwambia Yoshua, “Waambie Waisraeli, watenge miji ya kukimbilia, kama nilivyokuagiza kupitia Musa, ili mtu yeyote atakayemuua mtu kwa bahati mbaya na pasipo kukusudia aweze kukimbilia huko na kujiepusha na mlipiza kisasi wa damu. “Anapokimbilia mojawapo ya hii miji, atasimama kwenye maingilio ya lango la mji mkuu na kueleza wazee wa mji kuhusu shauri lake. Kisha watampokea katika mji wao na kumpa mahali pa kuishi nao. Kama mlipiza kisasi wa damu akimfuatilia, wasimkabidhi yule mshtakiwa, kwa sababu alimuua jirani yake bila kukusudia, na bila kuwa na nia ya kudhuru. Huyu aliyeua atakaa kwenye mji huo hadi awe amesimama kukabili mashtaka yake mbele ya kusanyiko na hadi kuhani mkuu anayehudumu kwa wakati huo atakapokufa. Ndipo atakapoweza kurudi nyumbani mwake katika mji ambao aliukimbia.” Basi wakatenga Kedeshi katika Galilaya kwenye nchi ya vilima ya Naftali, Shekemu katika nchi ya vilima ya Efraimu, na Kiriath-Arba (yaani Hebroni) kwenye nchi ya vilima ya Yuda. Katika upande wa mashariki mwa Yordani (ngʼambo ya Yeriko) wakatenga Bezeri katika jangwa katika uwanda wa juu katika kabila la Reubeni, Ramothi katika Gileadi katika kabila la Gadi, na Golani huko Bashani katika kabila la Manase. Mwisraeli yeyote au mgeni yeyote aishiye miongoni mwao aliyemuua mtu kwa bahati mbaya, angeweza kukimbilia katika miji hiyo iliyotengwa na asiuawe na mlipiza kisasi wa damu kabla hajasimama kukabili mashtaka mbele ya kusanyiko.