Yoshua 18:1-10
Yoshua 18:1-10 Biblia Habari Njema (BHN)
Baada ya kuishinda ile nchi, jumuiya yote ya Waisraeli ilikusanyika huko Shilo na kulisimika hema la mkutano. Yalikuwa yamebaki kati yao makabila saba ambayo hayakuwa yamegawiwa sehemu yao ya nchi. Kwa hiyo, Yoshua akawaambia Waisraeli, “Je, mtakawia mpaka lini kwenda kuimiliki nchi ile ambayo Mwenyezi-Mungu, Mungu wa babu zenu, amewapeni? Chagueni watu watatu kutoka kila kabila niwatume nchini kote wachunguze na kuchora ramani kulingana na makabila yao, kisha waniletee taarifa. Nao wataigawanya nchi hiyo sehemu saba. Kabila la Yuda litabaki na sehemu yake ya kusini na kabila la Yosefu kaskazini. Tayarisheni maelezo kamili juu ya sehemu zote saba na kuniletea. Hapo, nitapiga kura mbele ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, kuhusu sehemu ya kila kabila lenu. Lakini Walawi hawatapata sehemu yoyote kati yenu, maana sehemu yao ni kuwa makuhani wa kumhudumia Mwenyezi-Mungu. Gadi, Reubeni na nusu ya kabila la Manase walikwisha pata sehemu yao upande wa mashariki wa mto Yordani. Walipewa sehemu hii na Mose, mtumishi wa Mwenyezi-Mungu.” Basi, watu hao wakaanza safari ya kwenda kuichunguza nchi. Kabla hawajaenda, Yoshua akawapa maagizo: “Nendeni nchini kote mkaandike maelezo kamili juu ya hiyo nchi, kisha mrudi mnieleze, nami nitapiga kura mbele ya Mwenyezi-Mungu hapa hapa Shilo kuhusu sehemu mtakayopewa.” Wanaume hao wakazunguka nchini kote, wakachora maelezo kamili juu ya sehemu zake saba pamoja na miji yake, kisha wakarudi kwa Yoshua kule kambini Shilo. Huko Shilo, Yoshua akazipigia kura sehemu hizo mbele ya Mwenyezi-Mungu, akawagawia Waisraeli; kila kabila na sehemu yake.
Yoshua 18:1-10 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Kisha mkutano mzima wa wana wa Israeli walikutana pamoja hapo Shilo, wakasimamisha hema ya kukutania huko; nayo nchi ilikuwa imeshindwa mbele zao. Yalikuwa yamebaki kati yao makabila saba ya wana wa Israeli ambayo yalikuwa hayajagawiwa urithi wao. Yoshua akawauliza wana wa Israeli, akasema, Je! Hata lini mtakuwa walegevu katika kuingia kwenu na kuimiliki hiyo nchi, ambayo yeye BWANA, Mungu wa baba zenu, amewapa? Haya, jichagulieni watu watatu kwa ajili ya kila kabila; nami nitawatuma, nao watainuka waende kati ya hiyo nchi, na kuiandika kama urithi wao ulivyo; kisha watanijia. Watu hao wataigawanya nchi iwe mafungu saba; Yuda atakaa katika mpaka wake huko upande wa kusini, na nyumba ya Yusufu watakaa katika mpaka wao upande wa kaskazini. Nanyi mtaiandika nchi iwe mafungu saba, kisha hayo maandiko yake mtaniletea mimi hapa; nami nitawapigia kura hapa mbele ya BWANA, Mungu wetu. Kwa maana Walawi hawana fungu kati yenu; Kwa kuwa huo ukuhani wa BWANA ndio urithi wao; tena Gadi, na Reubeni, na hiyo nusu ya kabila la Manase, wamekwisha pata urithi wao ng'ambo ya pili ya Yordani upande wa mashariki, ambao walipewa na Musa, mtumishi wa BWANA. Basi watu hao wakainuka wakaenda; Yoshua aliwaagiza wale waliokwenda kuichunguza nchi, akawaambia, Nendeni, mkapite katikati ya nchi, na kuandika habari zake, kisha mnijie tena hapa, nami nitawapigia kura kwa ajili yenu hapo mbele za BWANA huko Shilo. Basi watu hao wakaenda, wakapita katikati ya nchi, wakaandika habari zake katika kitabu, na kuigawanya kwa miji yake, hata iwe mafungu saba, kisha wakamrejea Yoshua kambini huko Shilo. Kisha Yoshua akapiga kura kwa ajili yao hapo mbele za BWANA katika Shilo; huko Yoshua akawagawanyia wana wa Israeli hiyo nchi sawasawa na mafungu yao.
Yoshua 18:1-10 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Kisha mkutano mzima wa wana wa Israeli walikutana pamoja hapo Shilo, wakasimamisha hema ya kukutania kuko; nayo nchi ilikuwa imeshindwa mbele zao. Zilisalia katika wana wa Israeli kabila saba ambazo hazijagawanyiwa bado urithi wao. Yoshua akawauliza wana wa Israeli, akasema, Je! Hata lini mtakuwa walegevu katika kuingia kwenu na kuimiliki hiyo nchi, ambayo yeye BWANA, Mungu wa baba zenu, amewapa? Haya, jichagulieni watu watatu kwa ajili ya kila kabila; nami nitawatuma, nao watainuka waende kati ya hiyo nchi, na kuiandika kama urithi wao ulivyo; kisha watanijilia mimi. Watu hao wataigawanya nchi iwe mafungu saba; Yuda atakaa katika mpaka wake huko upande wa kusini, na nyumba ya Yusufu watakaa katika mpaka wao upande wa kaskazini. Nanyi mtaiandika nchi iwe mafungu saba, kisha hayo maandiko yake mtaniletea mimi hapa; nami nitawapigia kura hapa mbele ya BWANA, Mungu wetu. Kwa maana Walawi hawana fungu kati yenu; Kwa kuwa huo ukuhani wa BWANA ndio urithi wao; tena Gadi, na Reubeni, na hiyo nusu ya kabila ya Manase, wamekwisha pata urithi wao ng’ambo ya pili ya Yordani upande wa mashariki, ambao walipewa na Musa, mtumishi wa BWANA. Basi watu hao wakainuka wakaenda; kisha Yoshua aliwaagiza wale waliokwenda kuiandika nchi, akawaambia, Endeni, mkapite katikati ya nchi, na kuiandika habari zake, kisha mnijie tena hapa, nami nitawapigia kura kwa ajili yenu hapo mbele za BWANA huko Shilo. Basi watu hao wakaenda, wakapita katikati ya nchi, wakaandika habari zake katika chuo, na kuigawanya kwa miji yake, hata iwe mafungu saba, kisha wakamrejea Yoshua maragoni huko Shilo. Kisha Yoshua akapiga kura kwa ajili yao hapo mbele za BWANA katika Shilo; huko Yoshua akawagawanyia wana wa Israeli hiyo nchi sawasawa na mafungu yao.
Yoshua 18:1-10 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Kusanyiko lote la Waisraeli wakakusanyika huko Shilo na kusimamisha Hema la Kukutania. Nchi ikawa chini ya utawala wao, lakini palikuwa bado makabila saba ya Israeli ambayo yalikuwa hayajapokea urithi wao. Hivyo Yoshua akawaambia Waisraeli, “Je, mtasubiri hata lini ili kuingia kumiliki nchi ambayo BWANA, Mungu wa baba zenu, amewapa? Chagueni watu watatu kutoka kila kabila. Nitawatuma kukagua nchi hiyo na kuandika taarifa kuhusu mgawanyo wa urithi wa kila kabila. Kisha watarudi kwangu. Mtaigawanya hiyo nchi katika sehemu saba. Yuda atabaki katika eneo lake upande wa kusini na nyumba ya Yusufu katika nchi yake upande wa kaskazini. Baada ya kuandika maelezo ya hizo sehemu saba za nchi, yaleteni kwangu, nami nitawapigia kura mbele za BWANA Mungu wetu. Hata hivyo, Walawi hawatakuwa na sehemu miongoni mwenu, kwa maana huduma ya ukuhani kwa BWANA ndio urithi wao. Nao Gadi, Reubeni na nusu ya kabila la Manase wameshapata urithi wao upande wa mashariki mwa Yordani, ambako Musa mtumishi wa BWANA aliwapa.” Watu hao walipokuwa wanaondoka kwenda kuikagua hiyo nchi, Yoshua akawaagiza, “Nendeni mkakague hiyo nchi na mwandike maelezo yake. Kisha mrudi kwangu, nami nitawapigia kura hapa Shilo mbele za BWANA.” Ndipo hao watu walipoondoka na kupita katika ile nchi. Wakaandika maelezo yake kwenye kitabu, mji kwa mji, katika sehemu saba na kurudisha taarifa kwa Yoshua huko kambini Shilo. Basi Yoshua akawapigia kura huko Shilo mbele za BWANA, na hapo akawagawia Waisraeli nchi kulingana na makabila yao.