Yoshua 17:14-18
Yoshua 17:14-18 Biblia Habari Njema (BHN)
Watu wa kabila la Yosefu walimwendea Yoshua, wakamwambia, “Kwa nini umetugawia sehemu moja tu ya nchi sisi ambao Mwenyezi-Mungu ametubariki hata akatufanya tuwe wengi sana?” Yoshua akawajibu, “Kama mmekuwa wengi hivyo, hata nchi ya milima ya Efraimu haiwatoshi tena, basi nendeni msituni katika nchi ya Waperizi na ya Warefai, mkaufyeke msitu huo na kufanya makao yenu huko.” Nao wakamjibu, “Ni kweli kwamba nchi hii ya milima haitutoshi; hata hivyo wale Wakanaani wote wanaokaa kwenye tambarare wana magari ya chuma, vilevile wale wote wanaokaa Beth-sheani pamoja na vijiji vyake, na wale wanaoishi katika Bonde la Yezreeli.” Basi, Yoshua akawaambia wazawa wa Yosefu, yaani kabila la Efraimu na Manase, “Kweli nyinyi mmekuwa wengi na wenye uwezo mkubwa. Haifai mpate sehemu moja tu, bali pia nchi ya milima itakuwa yenu. Ingawa sasa ni msitu, mtaifyeka na kuimiliki yote toka upande huu hadi upande mwingine. Mtawaondoa Wakanaani, hata kama wana magari ya chuma na ni wenye nguvu.”
Yoshua 17:14-18 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Kisha wana wa Yusufu wakanena na Yoshua, wakasema, Kwa nini umenipa mimi sehemu moja tu na fungu moja kuwa ni urithi wangu, kwa kuwa mimi ni taifa kubwa la watu, kwa sababu BWANA amenibariki hata hivi sasa? Yoshua akawaambia, Kwa kuwa wewe u taifa kubwa la watu, haya, kwea uende mwituni, ujikatie mahali hapo kwa ajili ya nafsi yako katika nchi ya Waperizi, na ya hao Warefai; maana hiyo nchi ya vilima ya Efraimu ni nyembamba, haikutoshi. Wana wa Yusufu wakasema, Hiyo nchi ya vilima haitutoshi sisi; lakini Wakanaani wote wakaao katika nchi ya bondeni wana magari ya chuma, hao walio katika Beth-sheani na miji yake, na hao walio katika bonde la Yezreeli pia. Kisha Yoshua alinena na nyumba ya Yusufu, maana, ni Efraimu na Manase, akawaambia, Wewe u taifa kubwa la watu, nawe una uwezo mwingi; hutapata sehemu moja tu; lakini hiyo nchi ya vilima itakuwa ni yako; maana, ijapokuwa sasa ni msitu, wewe utaufyeka, na kuimiliki yote hadi mwisho wake; kwa kuwa wewe utawafukuza hao Wakanaani, wajapokuwa wana magari ya chuma, wajapokuwa ni wenye uwezo.
Yoshua 17:14-18 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Kisha wana wa Yusufu wakanena na Yoshua, wakasema, Kwa nini umenipa mimi kura moja tu na fungu moja kuwa ni urithi wangu, kwa kuwa mimi ni taifa kubwa la watu, kwa sababu BWANA amenibarikia hata hivi sasa? Yoshua akawaambia, Kwamba wewe u taifa kubwa la watu, haya, kwea uende mwituni, ujikatie mahali hapo kwa ajili ya nafsi yako katika nchi ya Waperizi, na ya hao Warefai; ikiwa hiyo nchi ya vilima ya Efraimu ni nyembamba, haikutoshi. Wana wa Yusufu wakasema, Hiyo nchi ya vilima haitutoshi sisi; lakini Wakanaani wote wakaao katika nchi ya bondeni wana magari ya chuma, hao walio katika Bethsheani na miji yake, na hao walio katika bonde la Yezreeli pia. Kisha Yoshua alinena na nyumba ya Yusufu, maana, ni Efraimu na Manase, akawaambia, Wewe u taifa kubwa la watu, nawe una uwezo mwingi; hutapata kura moja tu; lakini hiyo nchi ya vilima itakuwa ni yako; maana, ijapokuwa ni mwitu, wewe utaukata, na matokeo yake yatakuwa ni yako; kwa kuwa wewe utawafukuza hao Wakanaani, wajapokuwa wana magari ya chuma, wajapokuwa ni wenye uwezo.
Yoshua 17:14-18 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Wana wa Yusufu wakamwambia Yoshua, “Kwa nini umetupatia sisi mgawo mmoja tu na sehemu moja tu kuwa urithi? Sisi tu watu wengi sana, na BWANA ametubariki kwa wingi.” Yoshua akajibu, “Kama ninyi ni wengi sana, na kama nchi ya vilima ya Efraimu ni ndogo sana kwenu, pandeni msituni mkafyeke eneo kwa ajili yenu wenyewe huko kwenye nchi ya Waperizi na Warefai.” Wana wa Yusufu wakajibu, “Hiyo nchi ya vilima haitutoshi, nao Wakanaani wote wanaoishi katika tambarare wana magari ya vita ya chuma, yaani wale walio Beth-Shani na makazi yake, na wale walio katika Bonde la Yezreeli.” Lakini Yoshua akanena na nyumba ya Yusufu, yaani Efraimu na Manase: “Ninyi ni wengi sana na wenye nguvu sana. Hamtakuwa na mgawo mmoja tu, bali pia nchi hii ya vilima yenye msitu. Ifyekeni, nayo mipaka yake itakuwa yenu umbali mtakaoweza kufika. Ingawa Wakanaani wana magari ya vita ya chuma, na wana nguvu, mtaweza kuwafukuza humo.”