Yoshua 15:13-19
Yoshua 15:13-19 Biblia Habari Njema (BHN)
Kalebu mwana wa Yefune, alipewa sehemu ya nchi ya Yuda kama Mwenyezi-Mungu alivyomwamuru Yoshua. Alipewa Kiriath-arba au mji wa Arba ambaye alikuwa babu wa Anaki. Mji huo sasa unaitwa Hebroni. Kalebu alizifukuza kutoka mji huo koo tatu za Anaki yaani ukoo wa Sheshai, ukoo wa Ahimani na ukoo wa Talmai. Kutoka Hebroni alikwenda kuwashambulia wakazi wa Debiri, mji ambao hapo awali uliitwa Kiriath-seferi. Kalebu akatangaza kwamba atamwoza binti yake Aksa kwa mwanamume yeyote atakayeuteka mji wa Kiriath-seferi. Basi, Othnieli, mwana wa Kenazi, nduguye Kalebu, akauteka mji huo, naye Kalebu akamwoza bintiye. Katika siku yao ya harusi, Aksa alimwambia Othnieli amwombe Kalebu shamba. Aksa alikuwa amepanda punda, na alipokuwa anashuka chini, Kalebu akamwuliza, “Unataka nikupe nini?” Aksa akamjibu, “Nipe zawadi; nipe sehemu yenye maji kwa kuwa huko Negebu ulikonipa ni kukavu.” Basi, Kalebu akampa chemchemi za maji zilizokuwa kwenye nyanda za juu na za chini.
Yoshua 15:13-19 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Kisha alimpa huyo Kalebu mwana wa Yefune sehemu kati ya wana wa Yuda, kama BWANA alivyomwamuru Yoshua, Kiriath-arba, ndiyo Hebroni (ni huyo Arba aliyekuwa babaye Anaki). Huyo Kalebu aliwafukuza watoke hapo hao wana watatu wa Anaki, nao ni Sheshai, na Ahimani, na Talmai, wazawa wa Anaki. Kisha akakwea kutoka huko ili kuwaendea wenyeji wa Debiri; jina la Debiri hapo kwanza lilikuwa Kiriath-seferi. Kalebu akasema, Yeyote atakayeupiga Kiriath-seferi na kuutwaa, mimi nitampa Aksa binti yangu awe mkewe. Naye Othnieli mwana wa Kenazi, nduguye Kalebu, aliutwaa; basi akampa Aksa binti yake awe mkewe. Kisha ikawa, hapo huyo mwanamke alipokwenda kwa mumewe, akamtaka aombe shamba kwa baba yake; akashuka katika punda wake; Kalebu akamwuliza, Unataka nikupe nini? Huyo mwanamke akasema, Nipe baraka; kwa kuwa umeniweka katika nchi ya kusini, unipe na chemchemi za maji pia. Ndipo akampa chemchemi za maji ya upande wa juu, na chemchemi za maji yaupande wa chini.
Yoshua 15:13-19 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Kisha alimpa huyo Kalebu mwana wa Yefune sehemu kati ya wana wa Yuda, kama BWANA alivyomwamuru Yoshua, maana ni Kiriath-arba, ni huyo Arba aliyekuwa babaye Anaki (huo ndio Hebroni). Huyo Kalebu aliwafukuza watoke hapo hao wana watatu wa Anaki, nao ni Sheshai, na Ahimani, na Talmai, wana wa Anaki. Kisha akakwea kutoka huko ili kuwaendea wenyeji wa Debiri; jina la Debiri hapo kwanza lilikuwa Kiriath-seferi. Kalebu akasema, Yeye atakayeupiga Kiriath-seferi na kuutwaa, mimi nitampa Aksa binti yangu awe mkewe. Naye Othnieli mwana wa Kenazi, nduguye Kalebu, aliutwaa; basi akampa Aksa binti yake awe mkewe. Kisha ikawa, hapo huyo mwanamke alipokwenda kwa mumewe, akamtaka aombe shamba kwa baba yake; akashuka katika punda wake; Kalebu akamwuliza, Wataka nini? Huyo mwanamke akasema, Nipe baraka; kwa kuwa umeniweka katika nchi ya kusini, unipe na chemchemi za maji pia. Ndipo akampa chemchemi za maji ya juu, na chemchemi za maji ya chini.
Yoshua 15:13-19 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Kwa kufuata maagizo ya BWANA kwake, Yoshua alimpa Kalebu mwana wa Yefune sehemu katika Yuda: Kiriath-Arba, yaani Hebroni. (Arba alikuwa baba wa zamani wa Anaki.) Kutoka Hebroni, Kalebu alifukuza hao Waanaki watatu: Sheshai, Ahimani na Talmai, wana wa Anaki. Kutoka hapo akaondoka kupigana dhidi ya watu walioishi Debiri (mji wa Debiri hapo uliitwa Kiriath-Seferi). Kalebu akasema, “Nitamwoza binti yangu Aksa kwa mtu atakayeweza kupigana na kuteka Kiriath-Seferi.” Basi Othnieli mwana wa Kenazi, ndugu yake Kalebu, akauteka; hivyo Kalebu akamtoa Aksa binti yake, akaolewa naye. Siku moja Aksa alipokuja kwa Othnieli, alimsihi Othnieli amwombe baba yake, Kalebu, shamba. Aksa aliposhuka kutoka punda wake, Kalebu akamuuliza, “Je, wataka nikufanyie nini?” Akamjibu, “Naomba unifanyie jambo moja la hisani. Kwa kuwa umenipa ardhi huko Negebu, nipe pia chemchemi za maji.” Basi Kalebu akampa chemchemi za juu na za chini.