Yoshua 14:6-13
Yoshua 14:6-13 Biblia Habari Njema (BHN)
Siku moja watu wa kabila la Yuda walimwendea Yoshua huko Gilgali. Kalebu mwana wa Yefune, ambaye alikuwa Mkenizi, akamwambia Yoshua, “Bila shaka unakumbuka jinsi Mwenyezi-Mungu alivyomwambia Mose, mtu wa Mungu, juu yangu na wewe tulipokuwa Kadesh-barnea: Nilipokuwa na umri wa miaka arubaini, Mose mtumishi wa Mungu, alinituma kutoka Kadesh-barnea, kwenda kuipeleleza nchi. Niliporudi nilimletea habari za mambo ya huko kadiri nilivyoamini moyoni mwangu, hali wale wenzangu waliokwenda pamoja nami waliwavunja watu moyo, lakini mimi nilimfuata Mwenyezi-Mungu, Mungu wangu, kwa uaminifu. Siku hiyo Mose aliniapia, ‘Hakika sehemu ya nchi ile ambayo ulipita itakuwa yako wewe na wazawa wako milele. Kwa sababu ya uaminifu wako kwa Mwenyezi-Mungu, Mungu wako’. Lakini sasa tazama! Ni muda wa miaka arubaini na mitano tangu Mwenyezi-Mungu alipoongea na Mose, wakati Waisraeli walipokuwa wanapitia jangwani. Tangu wakati huo Mwenyezi-Mungu, kama alivyoahidi, amenihifadhi hai mpaka leo, na sasa mimi nina umri wa miaka themanini na mitano. Lakini bado nina nguvu kama nilivyokuwa wakati ule Mose aliponituma. Hata sasa nina nguvu za kuweza kupigana vita au kufanya kazi nyingine yoyote. Sasa naomba unipe nchi hii ya milima ambayo Mwenyezi-Mungu aliniahidi siku ile. Wewe ulisikia siku ile kwamba Waanaki waliishi humo katika miji yenye ngome; huenda Mwenyezi-Mungu atakuwa pamoja nami, nami nitawafukuza kama Mwenyezi-Mungu alivyosema.” Ndipo Yoshua akambariki Kalebu mwana wa Yefune na kumpa mji wa Hebroni kuwa sehemu yake.
Yoshua 14:6-13 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Wakati huo wana wa Yuda walimwendea Yoshua hapo Gilgali; na Kalebu, mwana wa Yefune, huyo Mkenizi, akamwambia, Wewe wajua hilo neno BWANA alilomwambia Musa, huyo mtu wa Mungu, katika habari zangu, na katika habari zako wewe, tulipokuwa katika Kadesh-barnea. Mimi nilikuwa mtu wa miaka arubaini umri wangu, hapo Musa mtumishi wa BWANA aliponituma niende kutoka Kadesh-barnea ili kuipeleleza hiyo nchi; nami nilimletea habari tena, kama ilivyokuwa ndani ya moyo wangu. Lakini wale ndugu zangu waliokwea kwenda pamoja nami waliwavunja watu moyo; ila mimi nilimfuata BWANA, Mungu wangu, kwa utimilifu. Kisha Musa akaniapia siku hiyo, akasema, Hakika hiyo nchi ambayo miguu yako imekanyaga itakuwa ni urithi kwako wewe, na kwa watoto wako milele, kwa sababu wewe umemfuata BWANA, Mungu wako, kwa utimilifu. Sasa basi, angalia, yeye BWANA ameniweka hai, kama alivyosema, miaka hii arubaini na mitano, tangu wakati huo BWANA alipomwambia Musa neno hilo, wakati Israeli walipokuwa wanapitia jangwani; na sasa tazama, hivi leo nimetimiza umri wa miaka themanini na mitano. Hata sasa mimi nina nguvu zangu hivi leo kama nilivyokuwa siku hiyo Musa aliyonituma; kama nguvu zangu zilivyokuwa wakati huo, na nguvu zangu ndivyo zilivyo sasa, kwa vita na kwa kwenda na kurudi. Basi sasa unipe mlima huu, ambao BWANA alinena habari zake siku hiyo; kwani wewe ulisikia siku hiyo jinsi Waanaki walivyokuwa huko, na miji ilivyokuwa mikubwa yenye boma; yumkini yeye BWANA atakuwa pamoja nami, nami nitawafukuza watoke nje, kama BWANA alivyonena. Yoshua akambariki, akampa Kalebu, huyo mwana wa Yefune, Hebroni kuwa urithi wake.
Yoshua 14:6-13 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Wakati huo wana wa Yuda walimkaribia Yoshua hapo Gilgali; na Kalebu, mwana wa Yefune, huyo Mkenizi, akamwambia, Wewe wajua hilo neno BWANA alilomwambia Musa, huyo mtu wa Mungu, katika habari zangu, na katika habari zako wewe, tulipokuwa katika Kadesh-barnea. Mimi nilikuwa mtu wa miaka arobaini umri wangu, hapo Musa mtumishi wa BWANA aliponituma niende kutoka Kadesh-barnea ili kuipeleleza hiyo nchi; nami nilimletea habari tena, kama ilivyokuwa ndani ya moyo wangu. Lakini wale ndugu zangu waliokwea kwenda pamoja nami waliiyeyusha mioyo ya watu; ila mimi nilimfuata BWANA, Mungu wangu, kwa utimilifu. Kisha Musa akaniapia siku hiyo, akasema, Hakika hiyo nchi ambayo miguu yako imekanyaga itakuwa ni urithi kwako wewe, na kwa watoto wako milele, kwa sababu wewe umemfuata BWANA, Mungu wako, kwa utimilifu. Sasa basi, angalia, yeye BWANA ameniweka hai, kama alivyosema, miaka hii arobaini na mitano, tangu wakati huo BWANA alipomwambia Musa neno hilo, wakati Israeli waliokuwa wakienenda barani; na sasa tazama, hivi leo nimepata miaka themanini na mitano umri wangu. Hata sasa mimi nina nguvu zangu hivi leo kama nilivyokuwa siku hiyo Musa aliyonituma; kama nguvu zangu zilivyokuwa wakati huo, na nguvu zangu ndivyo zilivyo sasa, kwa vita na kwa kutoka nje na kuingia ndani. Basi sasa unipe mlima huu, ambao BWANA alinena habari zake siku hiyo; kwani wewe ulisikia siku hiyo jinsi Waanaki walivyokuwa huko, na miji ilivyokuwa mikubwa yenye boma; yumkini yeye BWANA atakuwa pamoja nami, nami nitawafukuza watoke nje, kama BWANA alivyonena. Yoshua akambarikia, akampa Kalebu, huyo mwana wa Yefune, Hebroni kuwa urithi wake.
Yoshua 14:6-13 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Kisha watu wa Yuda wakamwendea Yoshua huko Gilgali, naye Kalebu mwana wa Yefune yule Mkenizi, akamwambia, “Unajua jambo ambalo BWANA alimwambia Musa mtu wa Mungu huko Kadesh-Barnea kukuhusu wewe na mimi. Nilikuwa na umri wa miaka arobaini, wakati Musa mtumishi wa BWANA, aliponituma kutoka Kadesh-Barnea kuipeleleza hiyo nchi. Nami nikamletea taarifa kama kulingana na nilivyosadiki moyoni. Lakini ndugu zangu tuliopanda nao waliifanya mioyo ya watu iyeyuke kwa hofu. Bali mimi, nilimfuata BWANA Mungu wangu kwa moyo wote. Hivyo katika siku ile, Musa akaniapia, ‘Nchi ambayo umeikanyaga kwa miguu yako itakuwa urithi wako na wa watoto wako milele, kwa sababu umemfuata BWANA Mungu wangu kwa moyo wote.’ “Sasa basi, kama vile BWANA alivyoahidi, ameniweka hai kwa miaka arobaini na tano tangu alipomwambia Musa jambo hili, Waisraeli walipokuwa wanazunguka jangwani. Hivyo mimi hapa leo nina umri wa miaka themanini na tano! Bado nina nguvu kama siku ile Musa aliponituma; nina nguvu za kwenda vitani sasa kama nilivyokuwa wakati ule. Basi nipe nchi hii ya vilima, ambayo BWANA aliniahidi siku ile. Wewe mwenyewe ulisikia wakati ule kwamba Waanaki walikuwa huko na miji yao ilikuwa mikubwa na yenye ngome, lakini, kwa msaada wa BWANA, nitawafukuza watoke huko kama vile alivyonena.” Ndipo Yoshua akambariki Kalebu mwana wa Yefune, na akampa Hebroni kama urithi wake.