Yoshua 13:1-6
Yoshua 13:1-6 Biblia Habari Njema (BHN)
Wakati huu, Yoshua alikuwa mzee wa miaka mingi. Basi, Mwenyezi-Mungu akamwambia, “Wewe sasa umekuwa mzee wa miaka mingi, na kumebaki bado sehemu kubwa za nchi ambazo hazijatwaliwa. Sehemu hizo ni: Nchi yote ya Wafilisti na nchi yote ya Wageshuri, yaani eneo lijulikanalo kama la Wakanaani, kuanzia kijito cha Shihori mpakani mwa Misri hadi eneo la Ekroni huko kaskazini. Maeneo yote ya watawala watano wa Ufilisti: Gaza, Ashdodi, Ashkeloni, Gathi na Ekroni pamoja na eneo la Avi, upande wa kusini. Hali kadhalika nchi za Wakanaani kuanzia Ara ya Wasidoni mpaka Afeka mpakani mwa Waamori; vilevile eneo la Gebali na Lebanoni mashariki ya Baal-gadi chini ya mlima Hermoni mpaka Lebo-hamathi; pia eneo la milima iliyo kati ya Lebanoni na Misrefoth-maimu ambayo wakazi wake ni Wasidoni. Kadiri Waisraeli watakavyoendelea katika nchi hizo, mimi mwenyewe nitayafukuza mataifa hayo mbele yao. Nawe utawagawia Waisraeli sehemu mbalimbali za nchi hizo kwa kura kama nilivyokuamuru.
Yoshua 13:1-6 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Basi Yoshua alipokuwa mzee, na miaka yake kwendelea sana, BWANA akamwambia, Wewe umekuwa mzee na miaka yako kwendelea sana, kisha inasalia nchi nyingi sana bado kumilikiwa. Nchi iliyosalia ni hii; nchi zote za Wafilisti, na Wageshuri wote; kutoka Shihori, hicho kijito kilichokabili Misri, hata mpaka wa Ekroni upande wa kaskazini, nchi inayohesabiwa kuwa ni ya hao Wakanaani; watawala watano wa hao Wafilisti; Wagaza, na Waashdodi, na Waashkeloni, na Wagiti, na Waekroni; tena Waavi, upande wa kusini; nchi yote ya Wakanaani na Meara iliyo ya Wasidoni, mpaka Afeka, hata mpaka wa Waamori; na nchi ya Wagebali na Lebanoni yote, upande wa mashariki ya jua, kutoka Baal-gadi ulio chini ya mlima wa Hermoni mpaka kufikia maingilio ya Hamathi; na watu wote wenye kukaa nchi za vilima kutoka Lebanoni hadi Misrefoth-maimu, maana, hao Wasidoni wote; hao wote nitawafukuza watoke mbele ya wana wa Israeli; lakini wewe uwape Israeli kuwa ni urithi wao, kama nilivyokuamuru.
Yoshua 13:1-6 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Basi Yoshua alipokuwa mzee, na kwendelea sana miaka yake, BWANA akamwambia, Wewe umekuwa mzee na kwendelea sana miaka yako, kisha inasalia nchi nyingi sana bado kumilikiwa. Nchi iliyosalia ni hii; nchi zote za Wafilisti, na Wageshuri wote; kutoka Shihori, hicho kijito kilichokabili Misri, hata mpaka wa Ekroni upande wa kaskazini, nchi inayohesabiwa kuwa ni ya hao Wakanaani; mashehe matano wa hao Wafilisti; Wagaza, na Waashdodi, na Waashkeloni, na Wagiti, na Waekroni; tena Waavi, upande wa kusini; nchi yote ya Wakanaani na Meara iliyo ya Wasidoni, mpaka Afeka, hata mpaka wa Waamori; na nchi ya Wagebali na Lebanoni yote, upande wa kuelekea maawio ya jua, kutoka Baal-gadi ulio chini ya mlima wa Hermoni mpaka kufikilia maingilio ya Hamathi; na watu wote wenye kuikaa nchi ya vilima kutoka Lebanoni hata Misrefoth-maimu, maana, hao Wasidoni wote; hao wote nitawafukuza watoke mbele ya wana wa Israeli; lakini wewe uwape Israeli kuwa ni urithi wao, kama nilivyokuamuru.
Yoshua 13:1-6 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Yoshua alipokuwa mzee, umri wake ukiwa umesogea sana, BWANA akamwambia, “Wewe ni mzee sana, na bado imesalia sehemu kubwa sana ya nchi ambayo haijatwaliwa. “Nchi iliyosalia ni hii: “maeneo yote ya Wafilisti na Wageshuri: kutoka Mto Shihori ulioko mashariki mwa Misri, kuelekea kaskazini kwenye eneo la Ekroni, ambayo yote ilihesabika kama ya Wakanaani, maeneo yale matano ya watawala wa Wafilisti, ambayo ni Gaza, Ashdodi, Ashkeloni, Gathi na Ekroni; nchi ya Waavi kuanzia kusini; nchi yote ya Wakanaani, kuanzia Ara ambayo ni ya Wasidoni, ikienea hadi Afeki, na eneo la Waamori, eneo la Wagebali; na Lebanoni yote kuelekea mashariki, kuanzia Baal-Gadi chini ya Mlima Hermoni hadi Lebo-Hamathi. “Na kuhusu wakaaji wote katika maeneo ya milima, kuanzia Lebanoni hadi Misrefoth-Maimu, pamoja na eneo lote la Wasidoni, mimi mwenyewe nitawafukuza, niwaondoe kwa ajili ya Waisraeli. Hakikisha umegawa nchi hii kwa Israeli kuwa urithi, kama nilivyokuagiza