Yoshua 13:1-32
Yoshua 13:1-32 Biblia Habari Njema (BHN)
Wakati huu, Yoshua alikuwa mzee wa miaka mingi. Basi, Mwenyezi-Mungu akamwambia, “Wewe sasa umekuwa mzee wa miaka mingi, na kumebaki bado sehemu kubwa za nchi ambazo hazijatwaliwa. Sehemu hizo ni: Nchi yote ya Wafilisti na nchi yote ya Wageshuri, yaani eneo lijulikanalo kama la Wakanaani, kuanzia kijito cha Shihori mpakani mwa Misri hadi eneo la Ekroni huko kaskazini. Maeneo yote ya watawala watano wa Ufilisti: Gaza, Ashdodi, Ashkeloni, Gathi na Ekroni pamoja na eneo la Avi, upande wa kusini. Hali kadhalika nchi za Wakanaani kuanzia Ara ya Wasidoni mpaka Afeka mpakani mwa Waamori; vilevile eneo la Gebali na Lebanoni mashariki ya Baal-gadi chini ya mlima Hermoni mpaka Lebo-hamathi; pia eneo la milima iliyo kati ya Lebanoni na Misrefoth-maimu ambayo wakazi wake ni Wasidoni. Kadiri Waisraeli watakavyoendelea katika nchi hizo, mimi mwenyewe nitayafukuza mataifa hayo mbele yao. Nawe utawagawia Waisraeli sehemu mbalimbali za nchi hizo kwa kura kama nilivyokuamuru. Utayagawia nchi hizo makabila tisa na nusu ya kabila la Manase ambayo bado hayajapata kitu.” Makabila ya Reubeni, Gadi na nusu nyingine ya kabila la Manase yalikuwa yamepewa nchi iliyo mashariki ya mto Yordani, kama Mwenyezi-Mungu alivyomwamuru Mose, mtumishi wake. Eneo lao lilikuwa kuanzia Aroeri ukingoni mwa bonde la Arnoni na mji ule ulio katikati ya bonde, na nchi ile yote ya tambarare tangu Medeba mpaka Diboni, pamoja na miji ya mfalme Sihoni wa Waamori, aliyetawala huko Heshboni hadi mpakani mwa Waamoni, pamoja na nchi za Gileadi, eneo la Wageshuri na Wamaakathi, mlima wa Hermoni na nchi yote ya Bashani mpaka Saleka; na ufalme wote wa Ogu mmoja wa Warefai waliosalia, ambaye alitawala huko Ashtarothi na Edrei katika Bashani. Mose alikuwa amewashinda hao wote na kuwafukuzia mbali. Hata hivyo, Wageshuri na Wamaaka hawakufukuzwa bali wanaishi miongoni mwa Waisraeli mpaka leo. Mose hakuwapa watu wa kabila la Lawi nchi yoyote. Bali tambiko walizomtolea Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli kwa moto, hizo ndizo zilizokuwa fungu lao, kama Mwenyezi-Mungu alivyomwambia Mose. Sehemu ya nchi ambayo Mose aliwapa watu wa kabila la Reubeni kulingana na jamaa zao, ilikuwa kuanzia Aroeri kando ya bonde la Arnoni na mji uliokuwa katika bonde hilo pamoja na nchi yote ya tambarare ya Medeba. Ilikuwa pia pamoja na Heshboni na miji yake yote iliyo katika sehemu tambarare: Yaani Diboni, Bamoth-baali, Beth-baal-meoni, Yahasa, Kedemothi, Mefaathi, Kiriathaimu, Sibma, Sereth-shahari, huko kilimani bondeni, Beth-peori, miteremko ya mlima Pisga, Beth-yeshimothi na miji yote ya tambarare, nchi yote ya mfalme Sihoni wa Waamori ambaye alitawala huko Heshboni; Mose alikuwa amemshinda huyu Sihoni pamoja na viongozi wa Midiani, Evi, Rekemu, Suri, Huri na Reba, ambao walitawala nchi kwa niaba ya mfalme Sihoni. Balaamu, mtabiri, mwana wa Beori ambaye Waisraeli walimuua alikuwa mmoja wao. Mpaka wa nchi ya kabila la Reubeni upande wa magharibi ulikuwa mto Yordani. Miji na maeneo yaliyotajwa hapa ndiyo sehemu waliyopewa watu wa koo za kabila la Reubeni. Sehemu ya nchi ambayo Mose aliwapa watu wa kabila la Gadi kulingana na koo zao ilikuwa Yazeri, miji yote ya Gileadi na nusu ya nchi ya Waamoni hadi Aroeri iliyo mashariki ya Raba, vilevile kuanzia Heshboni hadi Ramath-mizpe, Betonimu, na kutoka Mahanaimu mpaka wa Debiri, kadhalika miji iliyokuwa katika bonde la Beth-haramu, Beth-nimra, Sukothi na Zafoni na nchi yote iliyokuwa ya mfalme Sihoni wa Heshboni; eneo hilo lilikuwa upande wa mashariki wa Yordani na kupakana na upande wa kusini wa bahari ya Kinerethi. Miji na vijiji hivyo ndivyo walivyopewa watu wa kabila la Gadi kulingana na koo zao. Tena, Mose alikuwa ameipatia nusu ya kabila la Manase kulingana na koo zake, eneo la nchi kuanzia Mahanaimu hadi kuingia katika nchi yote iliyokuwa ya mfalme Ogu katika Bashani, pamoja na miji sitini ya Yairi, nusu ya Gileadi, Ashtarothi, Edrei, ambayo ilikuwa chini ya himaya ya mfalme Ogu wa Bashani; Eneo hili walipewa nusu ya wazawa wa Makiri mwana wa Manase, kulingana na koo zao. Mose alikuwa amewagawia sehemu hizo mbalimbali za nchi iliyokuwa mashariki ya Yeriko na Yordani, wakati alipokuwa kwenye tambarare za Moabu.
Yoshua 13:1-32 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Basi Yoshua alipokuwa mzee, na miaka yake kwendelea sana, BWANA akamwambia, Wewe umekuwa mzee na miaka yako kwendelea sana, kisha inasalia nchi nyingi sana bado kumilikiwa. Nchi iliyosalia ni hii; nchi zote za Wafilisti, na Wageshuri wote; kutoka Shihori, hicho kijito kilichokabili Misri, hata mpaka wa Ekroni upande wa kaskazini, nchi inayohesabiwa kuwa ni ya hao Wakanaani; watawala watano wa hao Wafilisti; Wagaza, na Waashdodi, na Waashkeloni, na Wagiti, na Waekroni; tena Waavi, upande wa kusini; nchi yote ya Wakanaani na Meara iliyo ya Wasidoni, mpaka Afeka, hata mpaka wa Waamori; na nchi ya Wagebali na Lebanoni yote, upande wa mashariki ya jua, kutoka Baal-gadi ulio chini ya mlima wa Hermoni mpaka kufikia maingilio ya Hamathi; na watu wote wenye kukaa nchi za vilima kutoka Lebanoni hadi Misrefoth-maimu, maana, hao Wasidoni wote; hao wote nitawafukuza watoke mbele ya wana wa Israeli; lakini wewe uwape Israeli kuwa ni urithi wao, kama nilivyokuamuru. Basi sasa gawanya nchi hii, iwe urithi wa hizi kabila tisa, na nusu ya kabila la Manase. Pamoja na yeye, Wareubeni na Wagadi walipata urithi wao, waliopewa na Musa, huko ng'ambo ya Yordani upande wa mashariki, vile vile kama huyo Musa mtumishi wa BWANA alivyowapa; kutoka huko Aroeri, iliyoko pale ukingoni mwa bonde la Amoni, na huo mji ulioko pale katikati ya bonde, na nchi tambarare yote ya Medeba mpaka Diboni; na miji yote ya Sihoni mfalme wa Waamori, aliyetawala katika Heshboni, hata mpaka wa wana wa Amoni; na Gileadi na mpaka wa Wageshuri, na Wamaaka, na mlima wa Hermoni wote, na Bashani yote mpaka Saleka; ufalme wote wa Ogu uliokuwa katika Bashani, huyo aliyekuwa akitawala katika Ashtarothi na katika Edrei (huyo alisalia katika mabaki ya wale Warefai); kwa kuwa Musa aliwapiga hao na kuwafukuza. Pamoja na hayo wana wa Israeli hawakuwafukuza Wageshuri, wala Wamaaka; lakini Wageshuri na Wamaaka wamekaa kati ya Israeli, hadi siku hii ya leo. Lakini hakuwapa watu wa kabila la Lawi urithi wowote ule; maana sadaka za BWANA, Mungu wa Israeli, zisongezwazo kwa njia ya moto ndizo urithi wake huyo, kama alivyomwambia. Musa akawapa kabila la wana wa Reubeni kwa kadiri ya jamaa zao. Mpaka wao ulikuwa kutoka hapo Aroeri, iliyo pale ukingoni mwa bonde la Arnoni, na huo mji ulio katikati ya bonde, na nchi tambarare yote iliyo karibu na Medeba; na Heshboni na miji yake yote iliyoko katika bonde; na Diboni, na Bamoth-baali, na Beth-baal-meoni; na Yahasa, na Kedemothi, na Mefaathi; na Kiriathaimu, na Sibma, na Sereth-shahari katika kilima cha hilo bonde; na Beth-peori, na nchi za materemko ya Pisga, na Beth-yeshimothi; na miji yote ya nchi tambarare, na ufalme wote wa Sihoni mfalme wa Waamori, aliyekuwa akitawala katika Heshboni, aliyepigwa na Musa pamoja na hao wakubwa wa Midiani, nao ni Evi, na Rekemu, na Suri, na Huri, na Reba, hao watawala wa Sihoni, waliokuwa katika nchi hiyo. Balaamu naye, huyo mwana wa Beori, huyo mchawi, wana wa Israeli walimwua kwa upanga kati ya hao wengine waliowaua. Na mpaka wa wana wa Reubeni ulikuwa ni mto wa Yordani, na kingo zake. Huo ndio urithi wa wana wa Reubeni sawasawa na jamaa zao, miji yake na vijiji vyake. Musa akawapa kabila la Gadi, hao wana wa Gadi, kwa kadiri ya jamaa zao. Mpaka wao ulikuwa ni Yazeri, na miji hiyo ya Gileadi, na nusu ya nchi ya wana wa Amoni, mpaka Aroeri uliokabili Raba; tena kutoka Heshboni mpaka Ramath-Mizpe, na Betonimu; tena kutoka Mahanaimu hadi mpaka wa Debiri; tena katika bonde, Beth-haramu, na Bethnimira, na Sukothi, na Safoni, hiyo iliyosalia ya ufalme wa Sihoni mfalme wa Heshboni, yaani mto wa Yordani na kingo zake, mpaka mwisho wa bahari ya Kinerethi ng'ambo ya pili ya Yordani upande wa mashariki. Huo ndio urithi wa wana wa Gadi sawasawa na jamaa zao, miji yake na vijiji vyake. Kisha Musa akawapa hao wa nusu ya kabila la Manase urithi wao; ulikuwa ni wa hiyo nusu ya kabila la wana wa Manase sawasawa na jamaa zao. Na mpaka wao ulikuwa kutoka huko Mahanaimu, Bashani yote, na ufalme wote wa Ogu mfalme wa Bashani, na miji yote ya Yairi, iliyo katika Bashani, miji sitini; na nusu ya Gileadi, na Ashtarothi, na Edrei, hiyo miji ya ufalme wa Ogu katika Bashani, ilikuwa ni ya wana wa Makiri mwana wa Manase maana, kwa hiyo nusu ya wana wa Makiri sawasawa na jamaa zao. Hizi ndizo mirathi ambazo Musa alizigawanya katika nchi tambarare za Moabu, ng'ambo ya pili ya Yordani, kukabili Yeriko, upande wa mashariki.
Yoshua 13:1-32 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Basi Yoshua alipokuwa mzee, na kwendelea sana miaka yake, BWANA akamwambia, Wewe umekuwa mzee na kwendelea sana miaka yako, kisha inasalia nchi nyingi sana bado kumilikiwa. Nchi iliyosalia ni hii; nchi zote za Wafilisti, na Wageshuri wote; kutoka Shihori, hicho kijito kilichokabili Misri, hata mpaka wa Ekroni upande wa kaskazini, nchi inayohesabiwa kuwa ni ya hao Wakanaani; mashehe matano wa hao Wafilisti; Wagaza, na Waashdodi, na Waashkeloni, na Wagiti, na Waekroni; tena Waavi, upande wa kusini; nchi yote ya Wakanaani na Meara iliyo ya Wasidoni, mpaka Afeka, hata mpaka wa Waamori; na nchi ya Wagebali na Lebanoni yote, upande wa kuelekea maawio ya jua, kutoka Baal-gadi ulio chini ya mlima wa Hermoni mpaka kufikilia maingilio ya Hamathi; na watu wote wenye kuikaa nchi ya vilima kutoka Lebanoni hata Misrefoth-maimu, maana, hao Wasidoni wote; hao wote nitawafukuza watoke mbele ya wana wa Israeli; lakini wewe uwape Israeli kuwa ni urithi wao, kama nilivyokuamuru. Basi sasa gawanya nchi hii, iwe urithi wa hizi kabila kenda, na nusu ya kabila ya Manase. Pamoja na yeye, Wareubeni na Wagadi walipata urithi wao, waliopewa na Musa, huko ng’ambo ya Yordani upande wa mashariki, vile vile kama huyo Musa mtumishi wa BWANA alivyowapa; kutoka huko Aroeri, iliyo pale ukingoni mwa bonde la Amoni, na huo mji ulio pale katikati ya bonde, na nchi tambarare yote ya Medeba mpaka Diboni; na miji yote ya Sihoni mfalme wa Waamori, aliyetawala katika Heshboni, hata mpaka wa wana wa Amoni; na Gileadi na mpaka wa Wageshuri, na Wamaaka, na mlima wa Hermoni wote, na Bashani yote mpaka Saleka; ufalme wote wa Ogu uliokuwa katika Bashani, huyo aliyekuwa akitawala katika Ashtarothi na katika Edrei (huyo alisalia katika mabaki ya wale Warefai); kwa kuwa Musa aliwapiga hao na kuwafukuza. Pamoja na hayo wana wa Israeli hawakuwafukuza Wageshuri, wala Wamaaka; lakini Wageshuri na Wamaaka wamekaa kati ya Israeli, hata siku hii ya leo. Lakini hakuwapa watu wa kabila ya Lawi urithi uwao wote; maana sadaka za BWANA, Mungu wa Israeli, zisongezwazo kwa njia ya moto ndizo urithi wake huyo, kama alivyomwambia. Musa akawapa kabila ya wana wa Reubeni kwa kadiri ya jamaa zao. Mpaka wao ulikuwa kutoka hapo Aroeri, iliyo pale ukingoni mwa bonde la Arnoni, na huo mji ulio katikati ya bonde, na nchi tambarare yote iliyo karibu na Medeba; na Heshboni na miji yake yote iliyoko katika bonde; na Diboni, na Bamoth-baali, na Beth-baal-meoni; na Yahasa, na Kedemothi, na Mefaathi; na Kiriathaimu, na Sibma, na Sereth-shahari katika kilima cha hilo bonde; na Beth-peori, na nchi za matelemko ya Pisga, na Beth-yeshimothi; na miji yote ya nchi tambarare, na ufalme wote wa Sihoni mfalme wa Waamori, aliyekuwa akitawala katika Heshboni, aliyepigwa na Musa pamoja na hao wakubwa wa Midiani, nao ni Evi, na Rekemu, na Suri, na Huri, na Reba, hao mashehe wa Sihoni, waliokuwa katika nchi hiyo. Balaamu naye, huyo mwana wa Beori, huyo mchawi, wana wa Israeli walimwua kwa upanga kati ya hao wengine waliowaua. Na mpaka wa wana wa Reubeni ulikuwa ni mto wa Yordani, na mpaka wake. Huo ndio urithi wa wana wa Reubeni sawasawa na jamaa zao, miji yake na vijiji vyake. Musa akawapa kabila ya Gadi, hao wana wa Gadi, kwa kadiri ya jamaa zao. Mpaka wao ulikuwa ni Yazeri, na miji hiyo ya Gileadi, na nusu ya nchi ya wana wa Amoni, mpaka Aroeri uliokabili Raba; tena kutoka Heshboni mpaka Ramath-Mizpe, na Betonimu; tena kutoka Mahanaimu hata mpaka wa Debiri; tena katika bonde, Beth-haramu, na Bethnimira, na Sukothi, na Safoni, hiyo iliyosalia ya ufalme wa Sihoni mfalme wa Heshboni, yaani mto wa Yordani na mpaka wake, mpaka mwisho wa bahari ya Kinerethi ng’ambo ya pili ya Yordani upande wa mashariki. Huo ndio urithi wa wana wa Gadi sawasawa na jamaa zao, miji yake na vijiji vyake. Kisha Musa akawapa hao wa nusu ya kabila ya Manase urithi wao; ulikuwa ni wa hiyo nusu ya kabila ya wana wa Manase sawasawa na jamaa zao. Na mpaka wao ulikuwa kutoka huko Mahanaimu, Bashani yote, na ufalme wote wa Ogu mfalme wa Bashani, na miji yote ya Yairi, iliyo katika Bashani, miji sitini; na nusu ya Gileadi, na Ashtarothi, na Edrei, hiyo miji ya ufalme wa Ogu katika Bashani, ilikuwa ni ya wana wa Makiri mwana wa Manase maana, kwa hiyo nusu ya wana wa Makiri sawasawa na jamaa zao. Hizi ndizo mirathi ambazo Musa alizigawanya katika nchi tambarare za Moabu, ng’ambo ya pili ya Yordani, kukabili Yeriko, upande wa mashariki.
Yoshua 13:1-32 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Yoshua alipokuwa mzee, umri wake ukiwa umesogea sana, BWANA akamwambia, “Wewe ni mzee sana, na bado imesalia sehemu kubwa sana ya nchi ambayo haijatwaliwa. “Nchi iliyosalia ni hii: “maeneo yote ya Wafilisti na Wageshuri: kutoka Mto Shihori ulioko mashariki mwa Misri, kuelekea kaskazini kwenye eneo la Ekroni, ambayo yote ilihesabika kama ya Wakanaani, maeneo yale matano ya watawala wa Wafilisti, ambayo ni Gaza, Ashdodi, Ashkeloni, Gathi na Ekroni; nchi ya Waavi kuanzia kusini; nchi yote ya Wakanaani, kuanzia Ara ambayo ni ya Wasidoni, ikienea hadi Afeki, na eneo la Waamori, eneo la Wagebali; na Lebanoni yote kuelekea mashariki, kuanzia Baal-Gadi chini ya Mlima Hermoni hadi Lebo-Hamathi. “Na kuhusu wakaaji wote katika maeneo ya milima, kuanzia Lebanoni hadi Misrefoth-Maimu, pamoja na eneo lote la Wasidoni, mimi mwenyewe nitawafukuza, niwaondoe kwa ajili ya Waisraeli. Hakikisha umegawa nchi hii kwa Israeli kuwa urithi, kama nilivyokuagiza, sasa basi, ligawanye eneo hili kwa yale makabila tisa na ile nusu ya kabila la Manase kuwa urithi.” Ile nusu nyingine ya Manase, Wareubeni na Wagadi, walishapokea urithi Musa aliokuwa amewapa mashariki mwa Yordani, sawasawa na mtumishi wa BWANA alivyowagawia. Eneo lao lilienea toka Aroeri, iliyo ukingoni mwa Bonde la Arnoni, kuanzia mji ulio katikati ya bonde, likijumlisha nchi ya uwanda wa juu wote wa Medeba hadi Diboni, nayo miji yote ya Sihoni mfalme wa Waamori, aliyetawala Heshboni, hadi mpakani mwa Waamoni. Vilevile ilijumlisha Gileadi, eneo la Wageshuri na Wamaaka, mlima wote wa Hermoni na Bashani yote ikienea hadi Saleka: yaani ufalme wote wa Ogu katika Bashani, aliyekuwa ametawala katika Ashtarothi na Edrei, na ndiye pekee alisalia kwa Warefai. Musa alikuwa amewashinda na kuteka nchi yao. Lakini Waisraeli hawakuwafukuza Wageshuri na Wamaaka, kwa hiyo wanaendelea kuishi miongoni mwa Waisraeli hadi leo. Lakini kwa kabila la Lawi, Musa hakupeana urithi, kwa kuwa sadaka za kuteketezwa kwa moto zilizotolewa kwa BWANA, Mungu wa Israeli, ndizo zilikuwa urithi wao, kama alivyowaahidi. Haya ndio maeneo ambayo Musa alikuwa amewapa kabila la Reubeni kufuatana na koo zao: Eneo la Aroeri lililo ukingoni mwa Bonde la Arnoni, na kuanzia mji ulio katikati ya bonde, pia uwanda wote wa juu kupita Medeba hadi Heshboni na miji yake yote kwenye uwanda wa juu, ikijumlishwa miji ya Diboni, Bamoth-Baali, Beth-Baal-Meoni, Yahasa, Kedemothi, Mefaathi, Kiriathaimu, Sibma, Sereth-Shahari juu ya kilima kilicho katika bonde, Beth-Peori, miteremko ya Pisga na Beth-Yeshimothi: miji yote ya uwanda wa juu na eneo lote la utawala wa Sihoni mfalme wa Waamori, aliyetawala katika Heshboni. Musa alikuwa amemshinda Sihoni, pia watawala wakuu wa Wamidiani, ambao ni Evi, Rekemu, Suri, Huri na Reba, waliokuwa wameungana na Sihoni, ambao waliishi katika nchi ile. Pamoja na wale waliouawa katika vita, Waisraeli walikuwa wamemuua kwa upanga Balaamu mwana wa Beori aliyekuwa mwaguzi. Mpaka wa Wareubeni ulikuwa ni ukingo wa Mto Yordani. Miji hii na vijiji vyake ilikuwa urithi wa Wareubeni kufuatana na koo zao. Haya ndio maeneo ambayo Musa alikuwa amewapa kabila la Gadi, kufuatana na koo zao: Nchi ya Yazeri, miji yote ya Gileadi na nusu ya nchi ya Amoni iliyoenea hadi Aroeri, karibu na Raba; na kuanzia Heshboni hadi Ramath-Mispa na Betonimu, na kutoka Mahanaimu hadi eneo la Debiri; na katika bonde, Beth-Haramu, Beth-Nimra, Sukothi na Safoni na sehemu iliyobaki ya eneo la utawala wa Sihoni mfalme wa Heshboni (upande wa mashariki mwa Mto Yordani, eneo inayoishia kwenye Bahari ya Kinerethi). Miji hii na vijiji vyake ilikuwa urithi wa kabila la Gadi kufuatana na koo zao. Haya ndio maeneo ambayo Musa alikuwa amewapa nusu ya kabila la Manase, yaani kwa nusu ya jamaa ya uzao wa Manase, kufuatana na koo zao: Eneo lililoenea kuanzia Mahanaimu, na kujumlisha Bashani yote, ufalme wote wa Ogu mfalme wa Bashani, makazi yote ya Yairi huko Bashani, miji sitini, nusu ya Gileadi, na Ashtarothi na Edrei (miji ya kifalme ya Ogu katika Bashani). Hii ilikuwa kwa ajili ya wazao wa Makiri mwana wa Manase, kwa ajili ya nusu ya wana wa Makiri, kufuatana na koo zao. Huu ndio urithi Musa alipeana alipokuwa katika tambarare za Moabu, ngʼambo ya Yordani, mashariki mwa Yeriko.