Yoshua 11:1-15
Yoshua 11:1-15 Biblia Habari Njema (BHN)
Mfalme Yabini wa mji wa Hazori alipopata habari hizo, alipeleka ujumbe kwa mfalme Yobabu wa Madoni, mfalme wa Shimroni na mfalme wa Akshafi, na kwa wafalme waliokuwa katika milima ya kaskazini, waliokuwa Araba ambayo ilikuwa kusini mwa Kinerethi, kwenye tambarare na waliokuwa Nafath-dori katika upande wa magharibi. Pia, alipeleka ujumbe kwa Wakanaani waliokuwa pande za mashariki na magharibi, kwa Waamori, Wahiti, Waperizi, Wayebusi ambao walikaa milimani na kwa Wahivi ambao walikaa chini ya mlima Hermoni katika nchi ya Mizpa. Basi, wakatoka wote na majeshi yao makubwa. Nao walikuwa wengi kama mchanga wa pwani pamoja na magari mengi na farasi wengi sana. Wafalme hawa wote wakaungana na kupiga kambi yao katika chemchemi ya Meromu ili wapigane na Waisraeli. Mwenyezi-Mungu akamwambia Yoshua, “Usiwaogope hao, maana kesho, wakati kama huu, nitawaangamiza wote kwa kuwatia mikononi mwa Waisraeli; nanyi mtakata mishipa ya farasi wao na kuteketeza magari yao kwa moto.” Basi, ghafla kwenye chemchemi ya Meromu Yoshua pamoja na jeshi lake lote akawatokea na kuwashambulia. Mwenyezi-Mungu akawatia mikononi mwa Waisraeli, nao wakawachapa na kuwafukuza mpaka Sidoni Kuu na Misrefoth-maimu, hadi upande wa mashariki katika bonde la Mizpa. Waisraeli wakawapiga na kuwaua wote. Yoshua aliwakatakata mishipa farasi wao wote na kuyateketeza magari yao kwa moto, kama Mwenyezi-Mungu alivyomwagiza. Yoshua alipokuwa anarudi, akauteka mji wa Hazori. Alimuua mfalme wake maana ndiye aliyekuwa kiongozi wa falme hizo zote. Kisha akauteketeza mji wa Hazori kwa moto na kuwaua wakazi wake wote, asimwache hata mtu mmoja. Pia aliiteketeza miji ile mingine yote kwa moto na kuwaua wafalme wao wote kama Mose, mtumishi wa Mwenyezi-Mungu, alivyomwamuru. Lakini Waisraeli hawakuiteketeza miji iliyokuwa vilimani, isipokuwa tu mji wa Hazori ambao Yoshua aliuteketeza. Waisraeli wakachukua vitu vyote walivyoteka nyara na wanyama wa miji hiyo; lakini waliwaua wakazi wake wote, wala hawakumwacha hata mtu mmoja. Amri hii alipewa Mose, mtumishi wa Mwenyezi-Mungu, naye Mose akamwamuru Yoshua ambaye aliitekeleza. Yoshua alitimiza kila jambo Mwenyezi-Mungu alilomwamuru Mose.
Yoshua 11:1-15 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Kisha ikawa, hapo huyo Yabini, mfalme wa Hazori, aliposikia habari ya mambo hayo, akatuma mjumbe aende kwa Yobabu, mfalme wa Madoni, na kwa mfalme wa Shimroni, na mfalme wa Akshafu, na hao wafalme waliokuwa upande wa kaskazini, katika nchi ya vilima, na katika Araba upande wa kusini wa Kinerethi, na katika Shefela, na katika nchi tambarare za Dori upande wa magharibi, na kwa Mkanaani upande wa mashariki, na upande wa magharibi, na kwa Mwamori, na Mhiti, na Mperizi na Myebusi katika nchi ya vilima, na kwa Mhivi pale chini ya Hermoni katika nchi ya Mispa. Nao wakatoka nje, wao na mjeshi yao yote pamoja nao, watu wengi mno, kama mchanga ulio ufuoni mwa bahari kwa wingi, pamoja na farasi na magari mengi sana. Wafalme hao wote wakakutana pamoja; wakaenda na kupanga mahema yao pamoja hapo penye maji ya Meromu, ili kupigana na Israeli. BWANA akamwambia Yoshua, Wewe usiogope kwa ajili ya hao; kwani kesho wakati kama huu nitawatoa wakiwa wameuawa wote mbele ya Israeli; utawakata farasi wao, na magari yao utayateketeza kwa moto. Basi Yoshua akaenda, na watu wote wa vita pamoja naye, ili kupigana nao hapo penye maji ya Meromu ghafla; wakawashambulia. BWANA akawatia mkononi mwa Israeli, nao wakawapiga, na kuwafukuza mpaka kufikia Sidoni ulio mkuu, tena hadi kufika Misrefoth-maimu, tena hata kufikia bonde la Mispa upande wa mashariki; wakawaua wote, wasibakize hata mtu mmoja Yoshua akawafanyia vile vile kama BWANA alivyomwamuru; akawakata farasi wao, na kuteketeza magari yao kwa moto. Yoshua akarudi wakati huo na kuutwaa Hazori, akampiga mfalme wa Hazori kwa upanga; kwa kuwa Hazori hapo awali ulikuwa ni kichwa cha falme hizo zote. Nao wakawapiga wote pia waliokuwamo ndani ya Hazori kwa makali ya upanga, wakawaangamiza kabisa; hakubakizwa hata mmoja akiwa hai; kisha akauteketeza Hazori kwa moto. Tena miji yote ya wafalme hao, na wafalme wake wote, Yoshua akawatwaa, akawapiga kwa makali ya upanga, na kuwaangamiza kabisa; vile vile kama huyo Musa mtumishi wa BWANA alivyomwamuru. Lakini katika habari ya miji hiyo iliyosimama katika vilima vyao, Israeli hakuteketeza kwa moto miji hiyo, isipokuwa ni mji wa Hazori tu; mji huo Yoshua aliuteketeza kwa moto. Tena nyara zote za miji hiyo, na wanyama wa miji, wana wa Israeli walitwaa kuwa nyara zao wenyewe; lakini kila mtu wakampiga kwa makali ya upanga, hadi walipokuwa wamewaangamiza wote, wala hawakumsaza mmoja mwenye kuvuta pumzi. Vile vile kama BWANA alivyomwamuru Musa mtumishi wake, ndivyo Musa alivyomwamuru Yoshua; naye Yoshua akafanya hivyo; hakukosa kufanya neno lolote katika hayo yote BWANA aliyomwamuru Musa.
Yoshua 11:1-15 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Kisha ikawa, hapo huyo Yabini, mfalme wa Hazori, aliposikia habari ya mambo hayo, akatuma mjumbe aende kwa Yobabu, mfalme wa Madoni, na kwa mfalme wa Shimroni, na mfalme wa Akshafu, na hao wafalme waliokuwa upande wa kaskazini, katika nchi ya vilima, na katika Araba upande wa kusini wa Kinerethi, na katika Shefela, na katika nchi zilizoinuka za Dori upande wa magharibi, na kwa Mkanaani upande wa mashariki, na upande wa magharibi, na kwa Mwamori, na Mhiti, na Mperizi na Myebusi katika nchi ya vilima, na kwa Mhivi pale chini ya Hermoni katika nchi ya Mispa. Nao wakatoka nje, wao na jeshi zao zote pamoja nao, watu wengi mno, kama mchanga ulio ufuoni mwa bahari kwa wingi, pamoja na farasi na magari mengi sana. Wafalme hao wote wakakutana pamoja; wakaenda na kupanga mahema yao pamoja hapo penye maji ya Meromu, ili kupigana na Israeli. BWANA akamwambia Yoshua, Usiche wewe kwa ajili ya hao; kwani kesho wakati kama huu nitawatoa hali wameuawa wote mbele ya Israeli; utawatema farasi zao, na magari yao utayapiga moto. Basi Yoshua akaenda, na watu wote wa vita pamoja naye, ili kupigana nao hapo penye maji ya Meromu ghafula; wakawaangukia. BWANA akawatia mkononi mwa Israeli, nao wakawapiga, na kuwafukuza hata kufikilia Sidoni ulio mkuu, na hata kufikilia Misrefoth-maimu, tena hata kufikilia bonde la Mispa upande wa mashariki; wakawapiga hata wasiwasaze hata mtu mmoja aliyesalia. Yoshua akawafanyia vile vile kama BWANA alivyomwamuru; akawatema farasi zao, na magari yao akayapiga moto. Yoshua akarudi wakati huo na kuutwaa Hazori, akampiga mfalme wa Hazori kwa upanga; kwa kuwa Hazori hapo kwanza ulikuwa ni kichwa cha falme hizo zote. Nao wakawapiga wote pia waliokuwamo ndani ya Hazori kwa makali ya upanga, wakawaangamiza kabisa; hakusazwa hata mmoja aliyevuta pumzi; kisha akauteketeza Hazori kwa moto. Tena miji yote ya wafalme hao, na wafalme wake wote, Yoshua akawatwaa, akawapiga kwa makali ya upanga, na kuwaangamiza kabisa; vile vile kama huyo Musa mtumishi wa BWANA alivyomwamuru. Lakini katika habari ya miji hiyo iliyosimama katika vilima vyao, Israeli hawakuipiga moto miji hiyo, isipokuwa ni mji wa Hazori tu; mji huo Yoshua aliupiga moto. Tena nyara zote za miji hiyo, na wanyama wa miji, wana wa Israeli walitwaa kuwa nyara zao wenyewe; lakini kila mtu wakampiga kwa makali ya upanga, hata walipokuwa wamewaangamiza wote, wala hawakumsaza mmoja mwenye kuvuta pumzi. Vile vile kama BWANA alivyomwamuru Musa mtumishi wake, ndivyo Musa alivyomwamuru Yoshua; naye Yoshua akafanya vivyo; hakukosa kufanya neno lo lote katika hayo yote BWANA aliyomwamuru Musa.
Yoshua 11:1-15 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Yabini mfalme wa Hazori aliposikia habari hizo, akatuma ujumbe kwa Yobabu mfalme wa Madoni, na kwa mfalme wa Shimroni, na kwa mfalme wa Akshafu, na pia kwa wafalme wa upande wa kaskazini wale waliokuwa milimani, katika Araba upande wa kusini mwa Kinerethi, katika Shefela, na katika miinuko ya Nafoth-Dori upande wa magharibi; kwa Wakanaani upande wa mashariki na magharibi; kwa Waamori, Wahiti, Waperizi na Wayebusi katika nchi ya vilima; na kwa Wahivi chini ya Hermoni katika eneo ya Mispa. Wakaja na vikosi vyao vyote na idadi kubwa ya farasi na magari ya vita: jeshi kubwa, kama wingi wa mchanga ulio pwani ya bahari. Wafalme hawa wote wakaunganisha majeshi yao na kupiga kambi pamoja kwenye Maji ya Meromu, ili kupigana dhidi ya Israeli. BWANA akamwambia Yoshua, “Usiwaogope, kwa sababu kesho saa kama hii nitawatia wote mikononi mwa Israeli, wakiwa wameuawa. Utakata mishipa ya nyuma ya miguu ya farasi wao na kuyachoma moto magari yao ya vita.” Hivyo Yoshua na jeshi lake lote wakaja dhidi yao ghafula kwenye Maji ya Meromu na kuwashambulia, naye BWANA akawatia mikononi mwa Israeli. Wakawashinda na kuwafukuza hadi Sidoni Kuu na kuwafikisha Misrefoth-Maimu, hadi Bonde la Mispa upande wa mashariki, hata pakawa hakuna yeyote aliyebaki. Yoshua akawatendea kama BWANA alivyoamuru. Akakata mishipa ya nyuma ya miguu ya farasi wao na kuchoma moto magari yao ya vita. Wakati huo Yoshua akarudi na kuuteka mji wa Hazori na kumuua mfalme wake kwa upanga. (Hazori ulikuwa mji mkuu wa falme hizo zote.) Kila aliyekuwa ndani yake wakamuua kwa upanga. Wakawaangamiza kabisa, wala hawakusaza chochote chenye pumzi, na akauchoma Hazori kwa moto. Yoshua akaiteka hii miji yote ya kifalme pamoja na wafalme wake, na akawaua kwa upanga. Akawaangamiza kabisa wote, jinsi Musa mtumishi wa BWANA alivyowaagiza. Lakini Israeli hawakuichoma moto hata mojawapo ya miji iliyojengwa katika vilima vyao vidogo, isipokuwa mji wa Hazori, ambao Yoshua aliuchoma kwa moto. Waisraeli wakajichukulia nyara zote na mifugo yote ya miji hii, bali waliwaua watu wote kwa upanga hadi walipowaangamiza kabisa, pasipo kumbakiza yeyote mwenye pumzi. Kama vile BWANA alivyomwagiza Musa mtumishi wake, vivyo hivyo Musa alimwagiza Yoshua, naye Yoshua akafanya vivyo hivyo; hakukosa kufanya lolote katika yale yote BWANA aliyomwagiza Musa.