Yoshua 10:7-14
Yoshua 10:7-14 Biblia Habari Njema (BHN)
Basi, Yoshua pamoja na jeshi lake lote na mashujaa wakaondoka Gilgali. Mwenyezi-Mungu akamwambia Yoshua, “Usiwaogope hata kidogo maana nimewatia mikononi mwako, wala hakuna hata mmoja atakayeweza kukukabili.” Baada ya kutembea kutoka Gilgali usiku kucha, Yoshua akawatokea ghafla. Naye Mwenyezi-Mungu akawatia hofu kuu mbele ya Waisraeli ambao waliwaua watu wengi huko Gibeoni wakiwakimbiza kwenye njia ya mteremko wa Beth-horoni mpaka Azeka na Makeda ambako pia waliwaua watu wengi sana. Walipokuwa wakiwakimbia Waisraeli kwenye mteremko wa Beth-horoni, Mwenyezi-Mungu akawanyeshea mvua ya mawe makubwa kutoka mbinguni wakiwa njiani mpaka Azeka hata waliouawa kwa mawe hayo wakawa wengi kuliko waliouawa kwa silaha za Waisraeli. Wakati Mwenyezi-Mungu alipowatia Waamori mikononi mwa Waisraeli, Yoshua alimwomba Mwenyezi-Mungu mbele ya Waisraeli wote, akasema, “Wewe jua, simama kimya juu ya Gibeoni, wewe mwezi, katika bonde la Aiyaloni.” Jua likasimama kimya na mwezi ukasimama mpaka taifa la Israeli lilipolipiza kisasi maadui wake. Kama alivyoandika katika kitabu cha Yashari, jua lilisimama kimya katikati ya mbingu, likakatiza safari yake ya kwenda kutua kwa siku nzima. Siku kama hiyo haijawahi kuwako kamwe wala haijapata kuonekana tena, siku ambayo Mwenyezi-Mungu amemwitikia binadamu kwa namna hiyo; maana Mwenyezi-Mungu mwenyewe aliwapigania Waisraeli.
Yoshua 10:7-14 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Basi Yoshua akakwea kutoka Gilgali, yeye, na watu wa vita wote pamoja naye, na mashujaa wote wenye uwezo. BWANA akamwambia Yoshua, Usiwaogope watu hao; kwa kuwa mimi nimekwisha kuwatia mikononi mwako; hapana mtu awaye yote miongoni mwao atakayesimama mbele yako. Basi Yoshua akawatokea ghafla; kwani alikwea kutoka Gilgali kwenda usiku kucha. BWANA naye akawatapanya mbele ya Israeli, naye Israeli akawaua uuaji ulio mkuu hapo Gibeoni, akawafukuza waikimbilie hiyo njia ya kukwelea kwenda Beth-horoni, na kuwapiga hadi kufikia Azeka, tena hadi kufikia Makeda. Kisha ikawa, hapo walipokuwa wakikimbia mbele ya Israeli, hapo walipokuwa wakiteremka Beth-horoni, ndipo BWANA alipowatupia mawe makubwa kutoka mbinguni juu yao hadi kufikia Azeka, nao wakafa; hao waliokufa kwa kuuawa na hayo mawe ya barafu walikuwa ni wengi kuliko hao waliouawa na wana wa Israeli kwa upanga. Ndipo Yoshua akanena na BWANA katika siku hiyo ambayo BWANA aliwatoa Waamori mbele ya wana wa Israeli; akasema mbele ya macho ya Israeli, Wewe Jua, simama kimya juu ya Gibeoni; Na wewe Mwezi, simama katika bonde la Aiyaloni. Ndipo jua likasimama, na mwezi ukatulia, Hadi hilo taifa lilipokuwa limekwisha jilipiza kisasi juu ya adui zao. Hayo, je! Hayakuandikwa ndani ya kitabu cha Yashari? Basi jua likasimama kimya katikati ya mbingu, wala halikufanya haraka kuchwa kama muda wa siku nzima. Haikuwapo siku nyingine mfano wa siku hiyo katika siku zilizotangulia mbele yake wala katika hizo zilizofuata baada yake, hata ikawa yeye BWANA kuisikia sauti ya binadamu; kwa kuwa BWANA alipiga vita kwa ajili ya Israeli.
Yoshua 10:7-14 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Basi Yoshua akakwea kutoka Gilgali, yeye, na watu wa vita wote pamoja naye, na mashujaa wenye uwezo pia wote. BWANA akamwambia Yoshua, Usiwache watu hao; kwa kuwa mimi nimekwisha kuwatia mikononi mwako; hapana mtu awaye yote miongoni mwao atakayesimama mbele yako. Basi Yoshua akawafikilia ghafula; kwani alikwea kutoka Gilgali kwenda usiku kucha. BWANA naye akawatapanya mbele ya Israeli, naye Israeli akawaua uuaji ulio mkuu hapo Gibeoni, akawafukuza waikimbilie hiyo njia ya kukwelea kwenda Beth-horoni, na kuwapiga hata kufikilia Azeka, tena hata kufikilia Makeda. Kisha ikawa, hapo walipokuwa wakimbia mbele ya Israeli, hapo walipokuwa katika kutelemkia Beth-horoni, ndipo BWANA alipowatupia mawe makubwa kutoka mbinguni juu yao hata kufikilia Azeka, nao wakafa; hao waliokufa kwa kuuawa na hayo mawe ya barafu walikuwa ni wengi kuliko hao waliouawa na wana wa Israeli kwa upanga. Ndipo Yoshua akanena na BWANA katika siku hiyo ambayo BWANA aliwatoa Waamori mbele ya wana wa Israeli; akasema mbele ya macho ya Israeli, Wewe Jua, simama kimya juu ya Gibeoni; Na wewe Mwezi, simama katika bonde la Aiyaloni. Ndipo jua likasimama, na mwezi ukatulia, Hata hilo taifa lilipokuwa limekwisha jipatiliza juu ya adui zao. Hayo, je! Hayakuandikwa ndani ya kitabu cha Yashari? Basi jua likasimama kimya katikati ya mbingu, wala halikufanya haraka kuchwa kama muda wa siku nzima. Haikuwapo siku nyingine mfano wa siku hiyo katika siku zilizotangulia mbele yake wala katika hizo zilizoandama baada yake, hata ikawa yeye BWANA kuisikia sauti ya binadamu; kwa kuwa BWANA alipiga vita kwa ajili ya Israeli.
Yoshua 10:7-14 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Basi Yoshua akaondoka Gilgali pamoja na jeshi lake lote, wakiwepo mashujaa wote. BWANA akamwambia Yoshua, “Usiwaogope watu hao, nimewatia mkononi mwako. Hakuna yeyote atakayeweza kushindana nawe.” Baada ya Yoshua kutembea usiku kucha kutoka Gilgali, akawashambulia ghafula. BWANA akawafadhaisha mbele ya Waisraeli, naye Yoshua na Waisraeli wakawashinda kwa ushindi mkuu huko Gibeoni. Waisraeli wakawafukuza kwa njia inayopanda kwenda Beth-Horoni, huku wakiwaua hadi kufikia Azeka na Makeda. Walipokuwa wanawakimbia Waisraeli kwenye barabara inayoteremka kutoka Beth-Horoni hadi Azeka, BWANA akawavurumishia mawe makubwa kama mvua kutoka mbinguni, na wengi wao walikufa kwa mawe kuliko wale waliokufa kwa panga za Waisraeli. Siku ile BWANA alipowakabidhi Waamori kwa Waisraeli, Yoshua akanena na BWANA akiwa mbele ya Waisraeli, akasema: “Wewe jua, simama juu ya Gibeoni, wewe mwezi, tulia juu ya Bonde la Aiyaloni.” Hivyo jua likasimama, nao mwezi ukatulia, hadi taifa hilo lilipokwisha kujilipizia kisasi kwa adui zake, kama ilivyoandikwa katika Kitabu cha Yashari. Jua likasimama katikati ya mbingu, likachelewa kuzama muda wa siku nzima. Hakujakuwa na siku nyingine kama hiyo kabla au baada, siku ambayo BWANA alimsikiliza mwanadamu. Hakika BWANA alikuwa akiwapigania Israeli.