Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Yoshua 10:16-43

Yoshua 10:16-43 Biblia Habari Njema (BHN)

Wale wafalme watano walikimbia na kujificha katika pango la Makeda. Yoshua akapata habari kwamba wafalme hao wamegunduliwa walikojificha katika pango la Makeda. Yoshua akasema, “Vingirisheni mawe makubwa mlangoni mwa pango na kuweka walinzi hapo. Lakini nyinyi msikae huko, bali muwafuatie adui zenu. Muwapige kutoka upande wa nyuma, wala musiwaache waingie mijini mwao, maana Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, amewatia mikononi mwenu.” Yoshua pamoja na Waisraeli waliwapiga na kuwaangamiza wote, na wachache wao walionusurika walikimbilia kwenye miji yao yenye ngome. Baada ya hayo Waisraeli wote walirudi salama kwa Yoshua huko kambini Makeda; na hakuna tena mtu aliyethubutu kusema lolote dhidi ya Waisraeli. Kisha Yoshua akasema, “Fungueni mlango wa pango mniletee kutoka humo wale wafalme watano.” Wakafanya hivyo, wakamletea Yoshua wale wafalme watano: Mfalme wa Yerusalemu, mfalme wa Hebroni, mfalme wa Yarmuthi, mfalme wa Lakishi na mfalme wa Egloni. Wafalme hao walipoletwa, Yoshua akawaita Waisraeli wote na wakuu wa majeshi waliokwenda naye vitani, akawaambia, “Njoni karibu mwakanyage wafalme hawa shingoni mwao.” Nao wakasogea na kuwakanyaga shingoni. Yoshua akawaambia “Msiogope, wala msiwe na wasiwasi, muwe imara na hodari, maana hivi ndivyo Mwenyezi-Mungu atakavyowatendea adui zenu ambao mtapigana nao. Kwa hiyo, muwe imara na hodari.” Baadaye, Yoshua aliwanyonga kwa kuwaangika kwenye miti mitano ambako walitundikwa mpaka jioni. Wakati jua lilipokuwa karibu kutua, Yoshua aliamuru waondolewe juu ya miti walipokuwa wameangikwa na kutupwa pangoni walimokuwa wamejificha. Kisha wakaweka mawe makubwa kwenye mlango wa pango, nayo mawe hayo yako huko mpaka leo. Siku hiyo Yoshua alipouteka mji wa Makeda, alimuua mfalme wake na wakazi wake wote bila kumbakiza hata mtu mmoja. Alimtendea mfalme wa Makeda kama vile alivyomtendea mfalme wa Yeriko. Kutoka Makeda, Yoshua pamoja na Waisraeli wote walikwenda Libna wakaushambulia. Mwenyezi-Mungu akautia mji huo pamoja na mfalme wao mikononi mwa Waisraeli, wakawaua wakazi wake bila kumbakiza hata mtu mmoja. Walimtendea mfalme wa Libna kama walivyomtendea mfalme wa Yeriko. Kisha kutoka Libna Yoshua na Waisraeli wote walikwenda Lakishi, wakauzingira na kuushambulia. Naye Mwenyezi-Mungu akautia mji huo mikononi mwa Waisraeli, wakauteka mnamo siku ya pili. Waliwaua wakazi wote wa mji huo kama walivyofanya kule Libna. Hapo, mfalme Horamu wa Gerezi akaamua kuja kuwasaidia watu wa Lakishi. Lakini Yoshua alimuua pamoja na watu wake wote, hakumbakiza hata mtu mmoja. Kisha kutoka Lakishi, Yoshua na Waisraeli wote walikwenda mpaka Egloni, wakauzingira na kuushambulia. Wakauteka siku hiyohiyo na kuwaua wakazi wake wote kama walivyofanya kule Lakishi. Halafu kutoka Egloni Yoshua na Waisraeli wote wakaenda mpaka Hebroni, wakaushambulia na kuuteka. Wakawaua wakazi wake wote pamoja na mfalme wao; waliiharibu kabisa miji mingine iliyouzunguka, wakawaua wakazi wake wote kama walivyofanya kule Egloni. Kisha, Yoshua na Waisraeli wote wakarudi Debiri, wakaushambulia. Waliuteka mji huo na mfalme wake pamoja na miji mingine yote iliyouzunguka na kuwaangamiza wote waliokuwamo bila kumbakiza hata mtu mmoja. Waliutendea mji huo kama walivyoutendea mji wa Hebroni na mji wa Libna na wafalme wao. Basi, Yoshua aliiteka nchi yote; aliwashinda wafalme wa sehemu za milimani, eneo la Negebu, na sehemu za nchi tambarare na miteremko. Hakuacha chochote chenye uhai ila aliangamiza kila kitu kama Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, alivyoamuru. Yoshua aliwashinda watu wote kutoka Kadesh-barnea mpaka Gaza, na kutoka Gosheni mpaka Gibeoni. Aliweza kuitwaa nchi hii yote kwa sababu Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, aliwapigania Waisraeli. Basi, Yoshua akarudi mpaka kambini huko Gilgali pamoja na Waisraeli wote.

Shirikisha
Soma Yoshua 10

Yoshua 10:16-43 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Na hawa wafalme watano wakakimbia, wakajificha ndani ya pango la Makeda. Kisha Yoshua aliambiwa habari hiyo, ya kwamba, Hao wafalme watano wameonekana, nao wamejificha ndani ya pango ya Makeda Basi Yoshua akasema, Haya, vingirisheni mawe makubwa mdomoni mwa lile pango, kisha wekeni watu hapo ili kuwalinda; lakini msikae ninyi; wafuatieni adui zenu, mwapige hao walio nyuma; msiwaache wakaingia ndani ya miji yao; kwa kuwa BWANA, Mungu wenu, amewatia mikononi mwenu. Kisha ikawa, hapo Yoshua, na wana wa Israeli, walipokuwa wamekwisha kuwaua watu wengi mno, hata wakaangamizwa, na hayo mabaki yao yaliyowasalia walipokuwa wamekwisha ingia katika miji yao yenye boma, ndipo hao watu wote wakamrudia Yoshua kambini huko Makeda salama; hakuna mtu awaye yote aliyetoa ulimi kinyume cha hao wana wa Israeli hata mmojawapo. Kisha Yoshua akasema, Haya, funua mdomo wa pango, mniletee hao wafalme watano hapa nje ya pango. Nao wakafanya hivyo, wakamletea hao wafalme watano hapo nje ya pango, yaani, mfalme wa Yerusalemu, na mfalme wa Hebroni, na mfalme wa Yarmuthi, na mfalme wa Lakishi, na mfalme wa Egloni. Kisha ikawa hapo walipomletea Yoshua hao wafalme watano hapo nje, Yoshua akawaita wanaume wote wa Israeli, akawaambia majemadari wa watu wa vita waliokwenda naye, Haya, jongeeni karibu, mweke nyayo za miguu yenu katika shingo za wafalme hawa. Nao wakajongea karibu, wakatia nyayo zao katika shingo zao. Yoshua akawaambia, Msiogope, wala msifadhaike; iweni hodari na wa mioyo ya ushujaa; kwa kuwa ndivyo BWANA atakavyowafanyia adui zenu wote ambao mnapigana nao. Baadaye Yoshua akawapiga, na kuwaua, akawatundika katika miti mitano; nao wakawa wametundikwa katika hiyo miti hadi jioni. Kisha wakati wa kuchwa jua, Yoshua akatoa amri, nao wakawateremsha katika hiyo miti, na kuwatupa katika lile pango ambamo walikuwa walijificha kisha wakatia mawe makubwa mdomoni mwa pango, hata hivi leo. Siku hiyo Yoshua akautwaa mji wa Makeda, akaupiga kwa makali ya upanga, na mfalme wake; akawaangamiza kabisa na wote pia waliokuwamo ndani yake, hakumwacha hata mmoja aliyesalia; naye akamfanyia huyo mfalme wa Makeda kama alivyomfanyia huyo mfalme wa Yeriko. Kisha Yoshua akapita kutoka hapo Makeda, mpaka Libna, na Israeli wote pamoja naye, nao wakapiga Libna; BWANA akautia na mji huo pia pamoja na mfalme wake mkononi mwa Israeli; naye akaupiga kwa makali ya upanga, na wote pia waliokuwamo ndani yake; hakumwacha hata mmoja aliyesalia ndani yake; naye akamtenda mfalme wake kama alivyomtenda huyo mfalme wa Yeriko. Kisha Yoshua akapita kutoka hapo Libna, na Israeli wote pamoja naye, wakafika Lakishi, wakapiga kambi mbele yake na kupigana nao; BWANA akautia huo mji wa Lakishi mkononi mwa Israeli, naye akautwaa siku ya pili, akaupiga kwa makali ya upanga, na wote pia waliokuwamo ndani yake, sawasawa na hayo yote aliyoutenda Libna. Wakati huo Horamu, mfalme wa Gezeri, akakwea ili kuusaidia Lakishi, lakini Yoshua akampiga yeye na watu wake, hata asimsazie hata mtu mmoja. Kisha Yoshua akapita kutoka hapo Lakishi, na Israeli wote pamoja naye, hadi wakafika Egloni; nao wakauzingira na kuushambulia; siku iyo hiyo wakautwaa, nao wakaupiga kwa makali ya upanga, na wote pia waliokuwamo ndani yake akawaangamiza kabisa siku hiyo, sawasawa na hayo yote aliyoufanyia mji wa Lakishi. Kisha Yoshua akakwea kutoka hapo Egloni, na Israeli wote pamoja naye, hadi wakafika Hebroni; nao wakapigana nao; wakautwaa, na kuupiga kwa makali ya upanga, na mfalme wake, na miji yake yote, na wote waliokuwamo ndani yake; hakumwacha aliyesalia hata mtu mmoja, sawasawa na hayo yote aliyoufanyia huo mji wa Egloni; lakini akauangamiza kabisa, na wote pia waliokuwamo ndani yake. Kisha Yoshua akarudi, na Israeli wote pamoja naye, hata Debiri; nao wakapigana nao; kisha akautwaa, na mfalme wake, na miji yake yote; nao wakawapiga kwa makali ya upanga, wakawaangamiza kabisa wote pia waliokuwamo ndani yake; hakumwacha hata mmoja aliyesalia; kama alivyoufanyia Hebroni aliufanyia na Debiri vivyo hivyo, na mfalme wake; kama alivyoufanyia Libna, na mfalme wake. Basi Yoshua akaipiga nchi hiyo yote, nchi ya vilima, na nchi ya Negebu, na nchi ya Shefela, na nchi ya materemko, na wafalme wake wote; hakumwacha aliyesalia hata mmoja; lakini akawaharibu kabisa wote waliokuwa hai, kama BWANA, Mungu wa Israeli, alivyoamuru. Yoshua akawapiga kutoka Kadesh-barnea mpaka Gaza, na nchi yote ya Gosheni, hata Gibeoni. Na wafalme hao wote na nchi zao Yoshua akatwaa kwa wakati mmoja, kwa sababu yeye BWANA, Mungu wa Israeli, alipigana kwa ajili ya Israeli, Kisha Yoshua akarudi, na Israeli wote pamoja naye, hata kambi yao huko Gilgali.

Shirikisha
Soma Yoshua 10

Yoshua 10:16-43 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Na hawa wafalme watano wakakimbia, wakajificha ndani ya pango la Makeda. Kisha Yoshua aliambiwa habari hiyo, ya kwamba, Hao wafalme watano wameonekana, nao wa hali ya kujificha ndani ya pango la Makeda Basi Yoshua akasema, Haya, vingirisheni mawe makubwa mdomoni mwa lile pango, kisha wekeni watu hapo ili kuwalinda; lakini msikae ninyi; wafuatieni adui zenu, mwapige hao walio nyuma; msiwaache wakaingia ndani ya miji yao; kwa kuwa BWANA, Mungu wenu, amewatia mikononi mwenu. Kisha ikawa, hapo Yoshua, na wana wa Israeli, walipokuwa wamekwisha kuwaua watu wengi mno, hata wakaangamizwa, na hayo mabaki yao yaliyowasalia walipokuwa wamekwisha ingia katika miji yao yenye boma, ndipo hao watu wote wakamrudia Yoshua maragoni huko Makeda salama; hakuna mtu awaye yote aliyetoa ulimi kinyume cha hao wana wa Israeli hata mmojawapo. Kisha Yoshua akasema, Haya, funua mdomo wa pango, mniletee hao wafalme watano hapa nje ya pango. Nao wakafanya, wakamletea hao wafalme watano hapo nje ya pango, yaani, mfalme wa Yerusalemu, na mfalme wa Hebroni, na mfalme wa Yarmuthi, na mfalme wa Lakishi, na mfalme wa Egloni. Kisha ikawa hapo walipomletea Yoshua hao wafalme watano hapo nje, Yoshua akawaita wanaume wote wa Israeli, akawaambia majemadari wa watu wa vita waliokwenda naye, Haya, jongeeni karibu, mweke nyayo za miguu yenu katika shingo za wafalme hawa. Nao wakajongea karibu, wakatia nyayo zao katika shingo zao. Yoshua akawaambia, Msiche, wala msifadhaike; iweni hodari na wa mioyo ya ushujaa; kwa kuwa ndivyo BWANA atakavyowafanyia adui zenu wote ambao mwapigana nao. Baadaye Yoshua akawapiga, na kuwaua, akawatundika katika miti mitano; nao wakawa wakitundikwa katika hiyo miti hata jioni. Kisha wakati wa kuchwa jua, Yoshua akatoa amri, nao wakawatelemsha katika hiyo miti, na kuwatupa katika lile pango ambamo walikuwa walijificha kisha wakatia mawe makubwa mdomoni mwa pango, hata hivi leo. Siku hiyo Yoshua akautwaa mji wa Makeda, akaupiga kwa makali ya upanga, na mfalme wake; akawaangamiza kabisa na wote pia waliokuwamo ndani yake, hakumwacha hata mmoja aliyesalia; naye akamfanyia huyo mfalme wa Makeda kama alivyomfanyia huyo mfalme wa Yeriko. Kisha Yoshua akapita kutoka hapo Makeda, mpaka Libna, na Israeli wote pamoja naye, nao wakapiga Libna; BWANA akautia na mji huo pia pamoja na mfalme wake mkononi mwa Israeli; naye akaupiga kwa makali ya upanga, na wote pia waliokuwamo ndani yake; hakumwacha hata mmoja aliyesalia ndani yake; naye akamtenda mfalme wake kama alivyomtenda huyo mfalme wa Yeriko. Kisha Yoshua akapita kutoka hapo Libna, na Israeli wote pamoja naye, wakafika Lakishi, wakapanga marago mbele yake na kupigana nao; BWANA akautia huo mji wa Lakishi mkononi mwa Israeli, naye akautwaa siku ya pili, akaupiga kwa makali ya upanga, na wote pia waliokuwamo ndani yake, sawasawa na hayo yote aliyoutenda Libna. Wakati huo Horamu, mfalme wa Gezeri, akakwea ili kuusaidia Lakishi, lakini Yoshua akampiga yeye na watu wake, hata asimsazie hata mtu mmoja. Kisha Yoshua akapita kutoka hapo Lakishi, na Israeli wote pamoja naye, hata wakafikilia Egloni; nao wakapanga marago mbele yake, na kupigana nao; siku iyo hiyo wakautwaa, nao wakaupiga kwa makali ya upanga, na wote pia waliokuwamo ndani yake akawaangamiza kabisa siku hiyo, sawasawa na hayo yote aliyoufanyia mji wa Lakishi. Kisha Yoshua akakwea kutoka hapo Egloni, na Israeli wote pamoja naye, hata wakafikilia Hebroni; nao wakapigana nao; wakautwaa, na kuupiga kwa makali ya upanga, na mfalme wake, na miji yake yote, na wote waliokuwamo ndani yake; hakumwacha aliyesalia hata mtu mmoja, sawasawa na hayo yote aliyoufanyia huo mji wa Egloni; lakini akauangamiza kabisa, na wote pia waliokuwamo ndani yake. Kisha Yoshua akarudi, na Israeli wote pamoja naye, hata Debiri; nao wakapigana nao; kisha akautwaa, na mfalme wake, na miji yake yote; nao wakawapiga kwa makali ya upanga, wakawaangamiza kabisa wote pia waliokuwamo ndani yake; hakumwacha hata mmoja aliyesalia; kama alivyoufanyia Hebroni aliufanyia na Debiri vivyo, na mfalme wake; kama alivyoufanyia Libna, na mfalme wake. Basi Yoshua akaipiga nchi hiyo yote, nchi ya vilima, na nchi ya Negebu, na nchi ya Shefela, na nchi ya matelemko, na wafalme wake wote; hakumwacha aliyesalia hata mmoja; lakini akawaharibu kabisa wote waliokuwa wavuta pumzi, kama BWANA, Mungu wa Israeli, alivyoamuru. Yoshua akawapiga kutoka Kadesh-barnea mpaka Gaza, na nchi yote ya Gosheni, hata Gibeoni. Na wafalme hao wote na nchi zao Yoshua akatwaa, wakati huo, kwa sababu yeye BWANA, Mungu wa Israeli, alipigana kwa ajili ya Israeli, Kisha Yoshua akarudi, na Israeli wote pamoja naye, hata marago yao huko Gilgali.

Shirikisha
Soma Yoshua 10

Yoshua 10:16-43 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)

Basi wale wafalme watano wakawa wamekimbia kujificha kwenye pango huko Makeda. Yoshua alipoambiwa kuwa wafalme hao watano wamekutwa wakiwa wamejificha ndani ya pango huko Makeda, akasema, “Vingirisheni mawe makubwa kwenye mlango wa pango, tena mweke walinzi wa kulilinda. Lakini msiwaache! Wafuatieni adui zenu, washambulieni kutoka nyuma, wala msiwaache wafike kwenye miji yao, kwa kuwa BWANA Mungu wenu amewatia mkononi mwenu.” Hivyo Yoshua pamoja na Waisraeli wakawaangamiza, isipokuwa wachache waliosalia walifika kwenye miji yao yenye ngome. Basi jeshi lote likarudi salama kwa Yoshua kule kambini Makeda, na hakuna yeyote aliyetoa neno kinyume cha Waisraeli. Ndipo Yoshua akasema, “Haya fungueni mdomo wa pango, mniletee hao wafalme watano.” Kwa hiyo wakawatoa hao wafalme watano nje ya pango: wafalme wa Yerusalemu, Hebroni, Yarmuthi, Lakishi na Egloni. Walipokuwa wamewaleta hawa wafalme kwa Yoshua, akawaita wanaume wote wa Israeli, na kuwaambia majemadari wa vita walioenda pamoja naye, “Njooni hapa mweke nyayo zenu juu ya shingo za hawa wafalme.” Basi wakaja wakaweka nyayo zao shingoni. Yoshua akawaambia, “Msiogope, wala msivunjike moyo. Kuweni hodari na wenye ushujaa. Hili ndilo BWANA atakalowatendea adui zenu wote mnaoenda kupigana nao.” Ndipo Yoshua akawapiga na kuwaua wale wafalme na kuwatundika juu ya miti mitano, nao wakaachwa wakiningʼinia juu ya ile miti hadi jioni. Wakati wa kuzama jua Yoshua akaamuru, nao wakawashusha kutoka ile miti na kuwatupa kwenye lile pango ambalo walikuwa wamejificha. Wakaweka mawe makubwa kwenye mlango wa pango, ambayo yapo hadi leo. Siku ile Yoshua akateka Makeda. Akamuua kila mmoja katika ule mji, pamoja na mfalme wake kwa upanga. Hakubakiza mtu yeyote. Akamfanyia mfalme wa Makeda kama vile alivyokuwa amemfanyia mfalme wa Yeriko. Ndipo Yoshua akaondoka Makeda akiwa pamoja na Israeli yote hadi mji wa Libna na kuushambulia. BWANA pia akautia huo mji wa Libna pamoja na mfalme wake mikononi mwa Israeli. Yoshua akaangamiza ule mji na kila mtu aliyekuwa ndani yake kwa upanga. Hakubakiza huko mtu yeyote. Akamfanyia mfalme wa Libna kama alivyokuwa amemfanyia mfalme wa Yeriko. Kisha Yoshua akaondoka Libna kwenda Lakishi akiwa pamoja na Israeli yote; wakajipanga dhidi yake na kuushambulia. BWANA akautia Lakishi mikononi mwa Israeli, hivyo Yoshua akauteka siku ya pili. Yoshua akauangamiza mji na kila kilichokuwa ndani yake kwa upanga, kama tu vile alivyokuwa ameufanyia mji wa Libna. Wakati huo huo, Horamu mfalme wa Gezeri alikuwa amepanda ili kusaidia Lakishi, lakini Yoshua akamshinda pamoja na jeshi lake, hadi hapakubakia mtu yeyote. Ndipo Yoshua akaondoka Lakishi kwenda Egloni akiwa pamoja na Israeli yote; wakajipanga dhidi yake na kuushambulia. Wakauteka mji huo siku ile ile, wakaupiga kwa upanga na kumwangamiza kila mmoja aliyekuwa ndani yake, kama vile walivyokuwa wameufanyia Lakishi. Kisha Yoshua na Waisraeli wote wakapanda kutoka Egloni hadi Hebroni, na kuushambulia. Wakauteka mji na kuupiga kwa upanga, pamoja na mfalme wake, vijiji vyake na kila mmoja aliyekuwa ndani yake. Hawakubakiza mtu yeyote. Kama vile huko Egloni, waliuangamiza kabisa pamoja na kila mmoja aliyekuwa ndani yake. Ndipo Yoshua na Waisraeli wote wakageuka na kushambulia Debiri. Wakauteka mji, mfalme wake na vijiji vyake, na kuupiga kwa upanga. Kila mmoja aliyekuwa ndani yake wakamwangamiza kabisa. Hawakubakiza mtu yeyote. Wakaufanyia Debiri na mfalme wake kama vile walivyokuwa wameifanyia miji ya Libna na Hebroni na wafalme wao. Hivyo Yoshua akalishinda eneo hilo lote, ikiwa ni pamoja na nchi ya vilima, na Negebu, na Shefela, miteremko ya milima, pamoja na wafalme wake wote. Hakubakiza mtu yeyote. Akaangamiza kabisa kila kitu chenye pumzi, kama vile BWANA, Mungu wa Israeli, alivyokuwa ameamuru. Yoshua akawashinda kuanzia Kadesh-Barnea hadi Gaza na kutoka eneo lote la Gosheni hadi Gibeoni. Wafalme hawa wote pamoja na nchi zao Yoshua aliwashinda kwa wakati mmoja, kwa sababu BWANA, Mungu wa Israeli, aliwapigania Israeli. Ndipo Yoshua akarudi pamoja na Israeli yote kwenye kambi huko Gilgali.

Shirikisha
Soma Yoshua 10