Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Yoshua 10:1-27

Yoshua 10:1-27 Biblia Habari Njema (BHN)

Mfalme Adoni-sedeki wa Yerusalemu alipata habari juu ya jinsi Yoshua alivyouteka mji wa Ai na kuuharibu kabisa akiutendea mji huo na mfalme wake kama alivyoutendea Yeriko na mfalme wake. Pia alipata habari kwamba wakazi wa Gibeoni walikuwa wamefanya mkataba wa amani na Waisraeli na kwamba sasa wanaishi miongoni mwao. Habari hizo zilisababisha hofu kubwa huko Yerusalemu kwa sababu mji wa Gibeoni ulikuwa maarufu miongoni mwa miji ya kifalme. Isitoshe, mji huu ulikuwa maarufu kuliko Ai na wanaume wake wote walikuwa askari hodari mno. Basi, Mfalme Adoni-sedeki akapeleka ujumbe kwa mfalme Hohamu wa Hebroni, mfalme Piramu wa Yarmuthi, mfalme Yafia wa Lakishi na mfalme Debiri wa Egloni, akawaambia, “Njoni mnisaidie tuwaangamize Wagibeoni, maana wamefanya mkataba wa amani na Yoshua pamoja na Waisraeli.” Kisha wafalme hao watano wa Waamori: Mfalme wa Yerusalemu, mfalme wa Hebroni, mfalme wa Yarmuthi, mfalme wa Lakishi na mfalme wa Egloni, wakaunganisha majeshi yao, wakaenda nayo mpaka Gibeoni; wakapiga kambi kuuzingira mji huo, wakaushambulia. Wagibeoni wakapeleka ujumbe kwa Yoshua huko kambini Gilgali, wakamwambia, “Tafadhali, usitutupe sisi watumishi wako; njoo upesi utusaidie na kutuokoa kwa maana wafalme wote wa Waamori kutoka nchi ya milimani wamekuja kutushambulia.” Basi, Yoshua pamoja na jeshi lake lote na mashujaa wakaondoka Gilgali. Mwenyezi-Mungu akamwambia Yoshua, “Usiwaogope hata kidogo maana nimewatia mikononi mwako, wala hakuna hata mmoja atakayeweza kukukabili.” Baada ya kutembea kutoka Gilgali usiku kucha, Yoshua akawatokea ghafla. Naye Mwenyezi-Mungu akawatia hofu kuu mbele ya Waisraeli ambao waliwaua watu wengi huko Gibeoni wakiwakimbiza kwenye njia ya mteremko wa Beth-horoni mpaka Azeka na Makeda ambako pia waliwaua watu wengi sana. Walipokuwa wakiwakimbia Waisraeli kwenye mteremko wa Beth-horoni, Mwenyezi-Mungu akawanyeshea mvua ya mawe makubwa kutoka mbinguni wakiwa njiani mpaka Azeka hata waliouawa kwa mawe hayo wakawa wengi kuliko waliouawa kwa silaha za Waisraeli. Wakati Mwenyezi-Mungu alipowatia Waamori mikononi mwa Waisraeli, Yoshua alimwomba Mwenyezi-Mungu mbele ya Waisraeli wote, akasema, “Wewe jua, simama kimya juu ya Gibeoni, wewe mwezi, katika bonde la Aiyaloni.” Jua likasimama kimya na mwezi ukasimama mpaka taifa la Israeli lilipolipiza kisasi maadui wake. Kama alivyoandika katika kitabu cha Yashari, jua lilisimama kimya katikati ya mbingu, likakatiza safari yake ya kwenda kutua kwa siku nzima. Siku kama hiyo haijawahi kuwako kamwe wala haijapata kuonekana tena, siku ambayo Mwenyezi-Mungu amemwitikia binadamu kwa namna hiyo; maana Mwenyezi-Mungu mwenyewe aliwapigania Waisraeli. Kisha Yoshua akarudi kambini huko Gilgali pamoja na Waisraeli wote. Wale wafalme watano walikimbia na kujificha katika pango la Makeda. Yoshua akapata habari kwamba wafalme hao wamegunduliwa walikojificha katika pango la Makeda. Yoshua akasema, “Vingirisheni mawe makubwa mlangoni mwa pango na kuweka walinzi hapo. Lakini nyinyi msikae huko, bali muwafuatie adui zenu. Muwapige kutoka upande wa nyuma, wala musiwaache waingie mijini mwao, maana Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, amewatia mikononi mwenu.” Yoshua pamoja na Waisraeli waliwapiga na kuwaangamiza wote, na wachache wao walionusurika walikimbilia kwenye miji yao yenye ngome. Baada ya hayo Waisraeli wote walirudi salama kwa Yoshua huko kambini Makeda; na hakuna tena mtu aliyethubutu kusema lolote dhidi ya Waisraeli. Kisha Yoshua akasema, “Fungueni mlango wa pango mniletee kutoka humo wale wafalme watano.” Wakafanya hivyo, wakamletea Yoshua wale wafalme watano: Mfalme wa Yerusalemu, mfalme wa Hebroni, mfalme wa Yarmuthi, mfalme wa Lakishi na mfalme wa Egloni. Wafalme hao walipoletwa, Yoshua akawaita Waisraeli wote na wakuu wa majeshi waliokwenda naye vitani, akawaambia, “Njoni karibu mwakanyage wafalme hawa shingoni mwao.” Nao wakasogea na kuwakanyaga shingoni. Yoshua akawaambia “Msiogope, wala msiwe na wasiwasi, muwe imara na hodari, maana hivi ndivyo Mwenyezi-Mungu atakavyowatendea adui zenu ambao mtapigana nao. Kwa hiyo, muwe imara na hodari.” Baadaye, Yoshua aliwanyonga kwa kuwaangika kwenye miti mitano ambako walitundikwa mpaka jioni. Wakati jua lilipokuwa karibu kutua, Yoshua aliamuru waondolewe juu ya miti walipokuwa wameangikwa na kutupwa pangoni walimokuwa wamejificha. Kisha wakaweka mawe makubwa kwenye mlango wa pango, nayo mawe hayo yako huko mpaka leo.

Shirikisha
Soma Yoshua 10

Yoshua 10:1-27 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Basi ikawa hapo Adoni-sedeki, mfalme wa Yerusalemu, aliposikia jinsi Yoshua alivyouteka mji wa Ai na kuuharibu kabisa; kama alivyoufanyia mji wa Yeriko na mfalme wake, akaufanya hivyo Ai na mfalme wake; na jinsi wenyeji waliokaa Gibeoni walivyofanya amani na Israeli, na ya kwamba walikuwa kati yao; ndipo wakaogopa mno, kwa sababu Gibeoni ulikuwa ni mji mkubwa, kama ilivyo miji ya kifalme mmojawapo, tena kwa sababu ulikuwa ni mji mkubwa kupita Ai, tena watu wake wote walikuwa ni mashujaa. Basi kwa hiyo Adoni-sedeki, mfalme wa Yerusalemu, akatuma ujumbe kwa Hohamu, mfalme wa Hebroni, na kwa Piramu, mfalme wa Yarmuthi, na kwa Yafia, mfalme wa Lakishi, na kwa Debiri, mfalme wa Egloni, akiwaambia, Haya, kweeni mje kwangu, mnisaidie, tuupige Gibeoni; kwa sababu umefanya mapatano ya amani pamoja na Yoshua na wana wa Israeli. Ndipo hao wafalme watano wa Waamori, mfalme wa Yerusalemu, na mfalme wa Hebroni na mfalme wa Yarmuthi na mfalme wa Lakishi, na mfalme wa Egloni, wakakutana pamoja, kisha wakakwea, wao na majeshi yao yote, na kupiga kambi yao kinyume cha Gibeoni, na kuupiga vita. Ndipo watu wa Gibeoni wakatuma wajumbe kwenda kwa Yoshua huko Gilgali kambini, wakamwambia, Usiulegeze mkono wako hata ukatuacha sisi watumishi wako; njoo kwetu upesi, utuokoe, na kutusaidia; kwa sababu wafalme wote wa Waamori wakaao katika nchi ya vilima wamekutana pamoja juu yetu. Basi Yoshua akakwea kutoka Gilgali, yeye, na watu wa vita wote pamoja naye, na mashujaa wote wenye uwezo. BWANA akamwambia Yoshua, Usiwaogope watu hao; kwa kuwa mimi nimekwisha kuwatia mikononi mwako; hapana mtu awaye yote miongoni mwao atakayesimama mbele yako. Basi Yoshua akawatokea ghafla; kwani alikwea kutoka Gilgali kwenda usiku kucha. BWANA naye akawatapanya mbele ya Israeli, naye Israeli akawaua uuaji ulio mkuu hapo Gibeoni, akawafukuza waikimbilie hiyo njia ya kukwelea kwenda Beth-horoni, na kuwapiga hadi kufikia Azeka, tena hadi kufikia Makeda. Kisha ikawa, hapo walipokuwa wakikimbia mbele ya Israeli, hapo walipokuwa wakiteremka Beth-horoni, ndipo BWANA alipowatupia mawe makubwa kutoka mbinguni juu yao hadi kufikia Azeka, nao wakafa; hao waliokufa kwa kuuawa na hayo mawe ya barafu walikuwa ni wengi kuliko hao waliouawa na wana wa Israeli kwa upanga. Ndipo Yoshua akanena na BWANA katika siku hiyo ambayo BWANA aliwatoa Waamori mbele ya wana wa Israeli; akasema mbele ya macho ya Israeli, Wewe Jua, simama kimya juu ya Gibeoni; Na wewe Mwezi, simama katika bonde la Aiyaloni. Ndipo jua likasimama, na mwezi ukatulia, Hadi hilo taifa lilipokuwa limekwisha jilipiza kisasi juu ya adui zao. Hayo, je! Hayakuandikwa ndani ya kitabu cha Yashari? Basi jua likasimama kimya katikati ya mbingu, wala halikufanya haraka kuchwa kama muda wa siku nzima. Haikuwapo siku nyingine mfano wa siku hiyo katika siku zilizotangulia mbele yake wala katika hizo zilizofuata baada yake, hata ikawa yeye BWANA kuisikia sauti ya binadamu; kwa kuwa BWANA alipiga vita kwa ajili ya Israeli. Basi Yoshua akarudi, na Israeli wote wakarudi pamoja naye, mpaka kambini hapo Gilgali. Na hawa wafalme watano wakakimbia, wakajificha ndani ya pango la Makeda. Kisha Yoshua aliambiwa habari hiyo, ya kwamba, Hao wafalme watano wameonekana, nao wamejificha ndani ya pango ya Makeda Basi Yoshua akasema, Haya, vingirisheni mawe makubwa mdomoni mwa lile pango, kisha wekeni watu hapo ili kuwalinda; lakini msikae ninyi; wafuatieni adui zenu, mwapige hao walio nyuma; msiwaache wakaingia ndani ya miji yao; kwa kuwa BWANA, Mungu wenu, amewatia mikononi mwenu. Kisha ikawa, hapo Yoshua, na wana wa Israeli, walipokuwa wamekwisha kuwaua watu wengi mno, hata wakaangamizwa, na hayo mabaki yao yaliyowasalia walipokuwa wamekwisha ingia katika miji yao yenye boma, ndipo hao watu wote wakamrudia Yoshua kambini huko Makeda salama; hakuna mtu awaye yote aliyetoa ulimi kinyume cha hao wana wa Israeli hata mmojawapo. Kisha Yoshua akasema, Haya, funua mdomo wa pango, mniletee hao wafalme watano hapa nje ya pango. Nao wakafanya hivyo, wakamletea hao wafalme watano hapo nje ya pango, yaani, mfalme wa Yerusalemu, na mfalme wa Hebroni, na mfalme wa Yarmuthi, na mfalme wa Lakishi, na mfalme wa Egloni. Kisha ikawa hapo walipomletea Yoshua hao wafalme watano hapo nje, Yoshua akawaita wanaume wote wa Israeli, akawaambia majemadari wa watu wa vita waliokwenda naye, Haya, jongeeni karibu, mweke nyayo za miguu yenu katika shingo za wafalme hawa. Nao wakajongea karibu, wakatia nyayo zao katika shingo zao. Yoshua akawaambia, Msiogope, wala msifadhaike; iweni hodari na wa mioyo ya ushujaa; kwa kuwa ndivyo BWANA atakavyowafanyia adui zenu wote ambao mnapigana nao. Baadaye Yoshua akawapiga, na kuwaua, akawatundika katika miti mitano; nao wakawa wametundikwa katika hiyo miti hadi jioni. Kisha wakati wa kuchwa jua, Yoshua akatoa amri, nao wakawateremsha katika hiyo miti, na kuwatupa katika lile pango ambamo walikuwa walijificha kisha wakatia mawe makubwa mdomoni mwa pango, hata hivi leo.

Shirikisha
Soma Yoshua 10

Yoshua 10:1-27 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Basi ikawa hapo Adoni-sedeki, mfalme wa Yerusalemu, aliposikia jinsi Yoshua alivyoushika mji wa Ai na kuuharibu kabisa; kama alivyoufanyia mji wa Yeriko na mfalme wake, akaufanya vivyo Ai na mfalme wake; na jinsi wenyeji waliokaa Gibeoni walivyofanya amani na Israeli, na ya kwamba walikuwa kati yao; ndipo wakacha mno, kwa sababu Gibeoni ulikuwa ni mji mkubwa, kama ilivyo miji ya kifalme mmojawapo, tena kwa sababu ulikuwa ni mji mkubwa kupita Ai, tena watu wake wote walikuwa ni mashujaa. Basi kwa hiyo Adoni-sedeki, mfalme wa Yerusalemu, akatuma ujumbe kwa Hohamu, mfalme wa Hebroni, na kwa Piramu, mfalme wa Yarmuthi, na kwa Yafia, mfalme wa Lakishi, na kwa Debiri, mfalme wa Egloni, akiwaambia, Haya, kweeni mje kwangu, mnisaidie, tuupige Gibeoni; kwa sababu umefanya mapatano ya amani pamoja na Yoshua na wana wa Israeli. Ndipo hao wafalme watano wa Waamori, mfalme wa Yerusalemu, na mfalme wa Hebroni na mfalme wa Yarmuthi na mfalme wa Lakishi, na mfalme wa Egloni, wakakutana pamoja, kisha wakakwea, wao na jeshi zao zote, na kupanga marago yao kinyume cha Gibeoni, na kuupiga vita. Ndipo watu wa Gibeoni wakatuma wajumbe kwenda kwa Yoshua huko Gilgali maragoni, wakamwambia, Usiulegeze mkono wako hata ukatuacha sisi watumishi wako; uje kwetu kwa upesi, utuokoe, na kutusaidia; kwa sababu wafalme wote wa Waamori wakaao katika nchi ya vilima wamekutana pamoja juu yetu. Basi Yoshua akakwea kutoka Gilgali, yeye, na watu wa vita wote pamoja naye, na mashujaa wenye uwezo pia wote. BWANA akamwambia Yoshua, Usiwache watu hao; kwa kuwa mimi nimekwisha kuwatia mikononi mwako; hapana mtu awaye yote miongoni mwao atakayesimama mbele yako. Basi Yoshua akawafikilia ghafula; kwani alikwea kutoka Gilgali kwenda usiku kucha. BWANA naye akawatapanya mbele ya Israeli, naye Israeli akawaua uuaji ulio mkuu hapo Gibeoni, akawafukuza waikimbilie hiyo njia ya kukwelea kwenda Beth-horoni, na kuwapiga hata kufikilia Azeka, tena hata kufikilia Makeda. Kisha ikawa, hapo walipokuwa wakimbia mbele ya Israeli, hapo walipokuwa katika kutelemkia Beth-horoni, ndipo BWANA alipowatupia mawe makubwa kutoka mbinguni juu yao hata kufikilia Azeka, nao wakafa; hao waliokufa kwa kuuawa na hayo mawe ya barafu walikuwa ni wengi kuliko hao waliouawa na wana wa Israeli kwa upanga. Ndipo Yoshua akanena na BWANA katika siku hiyo ambayo BWANA aliwatoa Waamori mbele ya wana wa Israeli; akasema mbele ya macho ya Israeli, Wewe Jua, simama kimya juu ya Gibeoni; Na wewe Mwezi, simama katika bonde la Aiyaloni. Ndipo jua likasimama, na mwezi ukatulia, Hata hilo taifa lilipokuwa limekwisha jipatiliza juu ya adui zao. Hayo, je! Hayakuandikwa ndani ya kitabu cha Yashari? Basi jua likasimama kimya katikati ya mbingu, wala halikufanya haraka kuchwa kama muda wa siku nzima. Haikuwapo siku nyingine mfano wa siku hiyo katika siku zilizotangulia mbele yake wala katika hizo zilizoandama baada yake, hata ikawa yeye BWANA kuisikia sauti ya binadamu; kwa kuwa BWANA alipiga vita kwa ajili ya Israeli. Basi Yoshua akarudi, na Israeli wote wakarudi pamoja naye, mpaka maragoni hapo Gilgali. Na hawa wafalme watano wakakimbia, wakajificha ndani ya pango la Makeda. Kisha Yoshua aliambiwa habari hiyo, ya kwamba, Hao wafalme watano wameonekana, nao wa hali ya kujificha ndani ya pango la Makeda Basi Yoshua akasema, Haya, vingirisheni mawe makubwa mdomoni mwa lile pango, kisha wekeni watu hapo ili kuwalinda; lakini msikae ninyi; wafuatieni adui zenu, mwapige hao walio nyuma; msiwaache wakaingia ndani ya miji yao; kwa kuwa BWANA, Mungu wenu, amewatia mikononi mwenu. Kisha ikawa, hapo Yoshua, na wana wa Israeli, walipokuwa wamekwisha kuwaua watu wengi mno, hata wakaangamizwa, na hayo mabaki yao yaliyowasalia walipokuwa wamekwisha ingia katika miji yao yenye boma, ndipo hao watu wote wakamrudia Yoshua maragoni huko Makeda salama; hakuna mtu awaye yote aliyetoa ulimi kinyume cha hao wana wa Israeli hata mmojawapo. Kisha Yoshua akasema, Haya, funua mdomo wa pango, mniletee hao wafalme watano hapa nje ya pango. Nao wakafanya, wakamletea hao wafalme watano hapo nje ya pango, yaani, mfalme wa Yerusalemu, na mfalme wa Hebroni, na mfalme wa Yarmuthi, na mfalme wa Lakishi, na mfalme wa Egloni. Kisha ikawa hapo walipomletea Yoshua hao wafalme watano hapo nje, Yoshua akawaita wanaume wote wa Israeli, akawaambia majemadari wa watu wa vita waliokwenda naye, Haya, jongeeni karibu, mweke nyayo za miguu yenu katika shingo za wafalme hawa. Nao wakajongea karibu, wakatia nyayo zao katika shingo zao. Yoshua akawaambia, Msiche, wala msifadhaike; iweni hodari na wa mioyo ya ushujaa; kwa kuwa ndivyo BWANA atakavyowafanyia adui zenu wote ambao mwapigana nao. Baadaye Yoshua akawapiga, na kuwaua, akawatundika katika miti mitano; nao wakawa wakitundikwa katika hiyo miti hata jioni. Kisha wakati wa kuchwa jua, Yoshua akatoa amri, nao wakawatelemsha katika hiyo miti, na kuwatupa katika lile pango ambamo walikuwa walijificha kisha wakatia mawe makubwa mdomoni mwa pango, hata hivi leo.

Shirikisha
Soma Yoshua 10

Yoshua 10:1-27 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)

Baada ya haya Adoni-Sedeki mfalme wa Yerusalemu alisikia kuwa Yoshua alikuwa ameteka mji wa Ai na kuuangamiza kabisa, tena alikuwa ameua mfalme wake, kama alivyofanya huko Yeriko na mfalme wake, tena ya kuwa watu wa Gibeoni walikuwa wamefanya mapatano ya amani na Waisraeli, na walikuwa wakiishi karibu yao. Yeye na watu wake wakataharuki mno kwa kuwa Gibeoni ulikuwa mji mkubwa kama mmoja wa miji ya kifalme; ulikuwa mkubwa kuliko Ai, na watu wake wote walikuwa mashujaa wa vita. Hivyo Adoni-Sedeki mfalme wa Yerusalemu akaomba msaada kwa Hohamu mfalme wa Hebroni, Piramu mfalme wa Yarmuthi, Yafia mfalme wa Lakishi, na Debiri mfalme wa Egloni. Akawaambia, “Njooni mnisaidie kuipiga Gibeoni, kwa sababu imefanya mkataba wa amani na Yoshua na Waisraeli.” Ndipo hao wafalme watano wa Waamori, ambao ni wafalme wa Yerusalemu, Hebroni, Yarmuthi, Lakishi na Egloni, wakaunganisha majeshi yao. Wakapanda na vikosi vyao vyote, nao wakajipanga dhidi ya Gibeoni na kuishambulia. Nao Wagibeoni wakatuma ujumbe kwa Yoshua kwenye kambi ya Gilgali na kumwambia, “Usiwatelekeze watumishi wako. Panda haraka uje kwetu utuokoe! Tusaidie, kwa sababu wafalme wote wa Waamori wanaokaa nchi ya vilima wameunganisha majeshi yao pamoja dhidi yetu.” Basi Yoshua akaondoka Gilgali pamoja na jeshi lake lote, wakiwepo mashujaa wote. BWANA akamwambia Yoshua, “Usiwaogope watu hao, nimewatia mkononi mwako. Hakuna yeyote atakayeweza kushindana nawe.” Baada ya Yoshua kutembea usiku kucha kutoka Gilgali, akawashambulia ghafula. BWANA akawafadhaisha mbele ya Waisraeli, naye Yoshua na Waisraeli wakawashinda kwa ushindi mkuu huko Gibeoni. Waisraeli wakawafukuza kwa njia inayopanda kwenda Beth-Horoni, huku wakiwaua hadi kufikia Azeka na Makeda. Walipokuwa wanawakimbia Waisraeli kwenye barabara inayoteremka kutoka Beth-Horoni hadi Azeka, BWANA akawavurumishia mawe makubwa kama mvua kutoka mbinguni, na wengi wao walikufa kwa mawe kuliko wale waliokufa kwa panga za Waisraeli. Siku ile BWANA alipowakabidhi Waamori kwa Waisraeli, Yoshua akanena na BWANA akiwa mbele ya Waisraeli, akasema: “Wewe jua, simama juu ya Gibeoni, wewe mwezi, tulia juu ya Bonde la Aiyaloni.” Hivyo jua likasimama, nao mwezi ukatulia, hadi taifa hilo lilipokwisha kujilipizia kisasi kwa adui zake, kama ilivyoandikwa katika Kitabu cha Yashari. Jua likasimama katikati ya mbingu, likachelewa kuzama muda wa siku nzima. Hakujakuwa na siku nyingine kama hiyo kabla au baada, siku ambayo BWANA alimsikiliza mwanadamu. Hakika BWANA alikuwa akiwapigania Israeli. Ndipo Yoshua akarudi kambini huko Gilgali pamoja na Israeli yote. Basi wale wafalme watano wakawa wamekimbia kujificha kwenye pango huko Makeda. Yoshua alipoambiwa kuwa wafalme hao watano wamekutwa wakiwa wamejificha ndani ya pango huko Makeda, akasema, “Vingirisheni mawe makubwa kwenye mlango wa pango, tena mweke walinzi wa kulilinda. Lakini msiwaache! Wafuatieni adui zenu, washambulieni kutoka nyuma, wala msiwaache wafike kwenye miji yao, kwa kuwa BWANA Mungu wenu amewatia mkononi mwenu.” Hivyo Yoshua pamoja na Waisraeli wakawaangamiza, isipokuwa wachache waliosalia walifika kwenye miji yao yenye ngome. Basi jeshi lote likarudi salama kwa Yoshua kule kambini Makeda, na hakuna yeyote aliyetoa neno kinyume cha Waisraeli. Ndipo Yoshua akasema, “Haya fungueni mdomo wa pango, mniletee hao wafalme watano.” Kwa hiyo wakawatoa hao wafalme watano nje ya pango: wafalme wa Yerusalemu, Hebroni, Yarmuthi, Lakishi na Egloni. Walipokuwa wamewaleta hawa wafalme kwa Yoshua, akawaita wanaume wote wa Israeli, na kuwaambia majemadari wa vita walioenda pamoja naye, “Njooni hapa mweke nyayo zenu juu ya shingo za hawa wafalme.” Basi wakaja wakaweka nyayo zao shingoni. Yoshua akawaambia, “Msiogope, wala msivunjike moyo. Kuweni hodari na wenye ushujaa. Hili ndilo BWANA atakalowatendea adui zenu wote mnaoenda kupigana nao.” Ndipo Yoshua akawapiga na kuwaua wale wafalme na kuwatundika juu ya miti mitano, nao wakaachwa wakiningʼinia juu ya ile miti hadi jioni. Wakati wa kuzama jua Yoshua akaamuru, nao wakawashusha kutoka ile miti na kuwatupa kwenye lile pango ambalo walikuwa wamejificha. Wakaweka mawe makubwa kwenye mlango wa pango, ambayo yapo hadi leo.

Shirikisha
Soma Yoshua 10