Yoshua 1:10-18
Yoshua 1:10-18 Biblia Habari Njema (BHN)
Kisha Yoshua akawaamuru viongozi wa watu, “Piteni katika kambi na kuwaamrisha watu watayarishe chakula, kwa kuwa baada ya siku tatu mtavuka mto Yordani, kwenda kuimiliki nchi ambayo Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu anawapeni iwe mali yenu.” Yoshua akawaambia watu wa kabila la Reubeni na Gadi na nusu ya kabila la Manase: “Kumbukeni lile jambo ambalo Mose, mtumishi wa Mwenyezi-Mungu, aliwaamuru akisema, ‘Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, atawapa mahali pa kupumzika, na atawapa nchi hii’. Wake zenu, watoto wenu na wanyama wenu wa kufugwa watabaki katika nchi hiyo ambayo Mose aliwapeni, ngambo ya mto Yordani. Lakini wanaume wote hodari wakiwa na silaha watavuka mto na kuwatangulia ndugu zenu. Mtawasaidia mpaka Mwenyezi-Mungu atakapowapa ndugu zenu pia mahali pa kupumzikia, kama alivyowapa nyinyi, nao pia wamiliki nchi ambayo wanapewa na Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu. Kisha mtarudi katika nchi ambayo ni mali yenu na kuimiliki, nchi ambayo mlipewa na Mose, mtumishi wa Mwenyezi-Mungu, mashariki ya mto Yordani.” Wakamjibu Yoshua, “Mambo yote uliyotuamuru tutayafanya, na popote utakapotutuma tutakwenda. Kama vile tulivyomtii Mose katika mambo yote, ndivyo tutakavyokutii wewe; Mwenyezi-Mungu, Mungu wako na awe pamoja nawe kama alivyokuwa pamoja na Mose. Mtu yeyote atakayeasi amri yako au kukataa kutii maneno yako au jambo lolote unalomwamuru, atauawa. Wewe, lakini, uwe na nguvu na kuwa hodari.”
Yoshua 1:10-18 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ndipo Yoshua akawaamuru viongozi wa watu, akisema, Piteni katika kambi, mkawaamuru hao watu, mkisema, Tayarisheni vyakula; kwa maana baada ya siku tatu mtavuka mto huu wa Yordani, ili kuingia na kuimiliki nchi awapayo BWANA, Mungu wenu, mpate kuimiliki. Tena Yoshua akawaambia Wareubeni, na Wagadi, na hao wa nusu ya kabila la Manase, akasema, Likumbukeni neno lile alilowaamuru Musa mtumishi wa BWANA, akisema, BWANA, Mungu wenu, anawapa ninyi raha, naye atawapa nchi hii. Wake zenu, na watoto wenu, na makundi yenu, watakaa katika nchi aliyowapa Musa ng'ambo ya Yordani; bali ninyi mtawatangulia ndugu zenu kuvuka, mkiwa mmevaa silaha zenu, watu wote wenye nguvu, na ushujaa, ili mpate kuwasaidia; hadi BWANA atakapowapa ndugu zenu raha, kama alivyowapa ninyi, na wao pia wamepata kuimiliki nchi awapayo BWANA, Mungu wenu; ndipo mtakapoirudia nchi ya milki yenu na kuimiliki, ambayo Musa mtumishi wa BWANA aliwapeni ng'ambo ya Yordani upande wa maawio ya jua. Wakamjibu Yoshua, wakasema, Hayo yote uliyotuamuru tutayafanya, na kila mahali utakakotutuma tutakwenda. Kama vile tulivyomsikiliza Musa katika mambo yote, ndivyo tutakavyokusikiliza wewe; BWANA, Mungu wako, na awe pamoja nawe tu, kama alivyokuwa pamoja na Musa. Kila mtu atakayeiasi amri yako, asiyasikilize maneno yako katika mambo yote utakayomwamuru, atauawa. Uwe hodari na moyo wa ushujaa, hilo tu.
Yoshua 1:10-18 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ndipo Yoshua akawaamuru maakida wa watu, akisema, Piteni katikati ya matuo, mkawaamuru hao watu, mkisema, Fanyeni tayari vyakula; kwa maana baada ya siku tatu mtavuka mto huu wa Yordani, ili kuingia na kuimiliki nchi awapayo BWANA, Mungu wenu, mpate kuimiliki. Tena Yoshua akawaambia Wareubeni, na Wagadi, na hao wa nusu ya kabila ya Manase, akasema, Likumbukeni neno lile alilowaamuru Musa mtumishi wa BWANA, akisema, BWANA, Mungu wenu, anawapa ninyi raha, naye atawapa nchi hii. Wake zenu, na watoto wenu, na makundi yenu, watakaa katika nchi aliyowapa Musa ng’ambo ya Yordani; bali ninyi mtavuka mbele ya ndugu zenu, hali mmevikwa silaha zenu, watu wote wenye nguvu, na ushujaa, ili mpate kuwasaidia; hata BWANA atakapowapa ndugu zenu raha, kama alivyowapa ninyi, na wao pia wamepata kuimiliki nchi awapayo BWANA, Mungu wenu; ndipo mtakapoirudia nchi ya milki yenu na kuimiliki, ambayo Musa mtumishi wa BWANA aliwapeni ng’ambo ya Yordani upande wa maawio ya jua. Wakamjibu Yoshua, wakasema, Hayo yote uliyotuamuru tutayafanya, na kila mahali utakakotutuma tutakwenda. Kama vile tulivyomsikiliza Musa katika mambo yote, ndivyo tutakavyokusikiliza wewe; BWANA, Mungu wako, na awe pamoja nawe tu, kama alivyokuwa pamoja na Musa. Kila mtu atakayeiasi amri yako, asiyasikilize maneno yako katika mambo yote utakayomwamuru, atauawa. Uwe hodari na moyo wa ushujaa, hilo tu.
Yoshua 1:10-18 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Ndipo Yoshua akawaagiza maafisa wa watu akisema, “Pitieni katika kambi yote mkawaambie watu, ‘Tayarisheni vyakula vyenu. Siku tatu kuanzia sasa mtavuka Yordani ili kuingia na kuimiliki nchi ambayo BWANA Mungu wenu anawapa iwe yenu.’ ” Lakini kwa Wareubeni, Wagadi na nusu ya kabila la Manase, Yoshua akasema, “Kumbukeni agizo lile Musa mtumishi wa BWANA alilowapa: ‘BWANA Mungu wenu anawapa ninyi utulivu kwa kuwapa nchi hii.’ Wake zenu, watoto wenu na mifugo yenu watakaa katika nchi ambayo Musa aliwapa mashariki mwa Yordani, lakini wapiganaji wenu wote, wakiwa wamejiandaa kwa vita, lazima wavuke mbele ya ndugu zenu. Imewapasa kuwasaidia ndugu zenu, hadi BWANA awape nao utulivu, kama alivyowatendea ninyi, hadi wao pia watakapokuwa wamemiliki nchi ile BWANA Mungu wenu anayowapa. Baada ya hilo, mwaweza kurudi na kuimiliki nchi yenu wenyewe, ambayo Musa mtumishi wa BWANA aliwapa mashariki mwa Yordani kuelekea linakochomoza jua.” Ndipo wakamjibu Yoshua, “Chochote ambacho umetuagiza tutafanya na popote utakapotutuma tutaenda. Kama vile tulivyomtii Musa kikamilifu, ndivyo tutakavyokutii wewe. BWANA Mungu wako na awe pamoja nawe tu kama vile alivyokuwa pamoja na Musa. Yeyote atakayeasi neno lako na kuacha kuyatii maneno yako, au chochote utakachowaamuru, atauawa. Uwe imara na hodari tu!”