Yoshua 1:1-5
Yoshua 1:1-5 Biblia Habari Njema (BHN)
Baada ya kifo cha Mose, mtumishi wa Mwenyezi-Mungu, Mwenyezi-Mungu alimwambia Yoshua mwana wa Nuni, mtumishi wa Mose: “Mtumishi wangu Mose amefariki, sasa vukeni mto Yordani, wewe pamoja na Waisraeli wote hadi kwenye nchi ile ambayo ninawapa. Kila mahali mtakapokanyaga nimewapeni kama nilivyomwahidi Mose. Mipaka ya nchi yenu itakuwa hivi: Kusini ni jangwa, kaskazini ni milima ya Lebanoni, mashariki ni mto ule mkubwa Eufrate, kupitia nchi yote ya Wahiti hadi bahari ya Mediteranea upande wa magharibi. Hakuna mtu atakayekushinda siku zote za maisha yako. Nitakuwa pamoja nawe kama nilivyokuwa pamoja na Mose. Daima nitakuwa nawe wala sitakuacha kamwe.
Yoshua 1:1-5 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Baada ya kufa kwake Musa, mtumishi wa BWANA, BWANA akamwambia Yoshua, mwana wa Nuni, mtumishi wa Musa, akasema, Musa mtumishi wangu amefariki; sasa ondoka, vuka mto huu wa Yordani; wewe na watu hawa wote, mkaende hadi nchi niwapayo wana wa Israeli. Kila mahali zitakapopakanyaga nyayo za miguu yenu, nimewapa ninyi, kama nilivyomwapia Musa. Toka jangwa hili na mlima huu, Lebanoni, mpaka mto ule mkubwa, mto wa Frati, nchi yote ya Wahiti, tena mpaka bahari ile kubwa upande wa machweo ya jua, hapo ndipo patakapokuwa mpaka wenu. Hakuna mtu yeyote atakayeweza kusimama mbele yako siku zote za maisha yako; kama nilivyokuwa pamoja na Musa, ndivyo nitakavyokuwa pamoja na wewe; sitakupungukia wala sitakuacha.
Yoshua 1:1-5 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ikawa baada ya kufa kwake Musa, mtumishi wa BWANA, BWANA akamwambia Yoshua, mwana wa Nuni, mtumishi wa Musa, akasema, Musa mtumishi wangu amekufa; haya basi, ondoka, vuka mto huu wa Yordani; wewe na watu hawa wote, mkaende hata nchi niwapayo wana wa Israeli. Kila mahali zitakapopakanyaga nyayo za miguu yenu, nimewapa ninyi, kama nilivyomwapia Musa. Tangu jangwa hili na mlima huu, Lebanoni, mpaka mto ule mkubwa, mto wa Frati, nchi yote ya Wahiti, tena mpaka bahari ile kubwa upande wa machweo ya jua, hapo ndipo patakapokuwa mpaka wenu. Hapatakuwa mtu ye yote atakayeweza kusimama mbele yako siku zote za maisha yako; kama nilivyokuwa pamoja na Musa, ndivyo nitakavyokuwa pamoja na wewe; sitakupungukia wala sitakuacha.
Yoshua 1:1-5 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Baada ya kifo cha Musa mtumishi wa BWANA, BWANA akamwambia Yoshua mwana wa Nuni, msaidizi wa Musa: “Mtumishi wangu Musa amekufa. Sasa basi, wewe na watu wote hawa jiandaeni kuvuka Mto Yordani kuingia nchi nitakayowapa Waisraeli karibuni. Kila mahali nyayo za miguu yenu zitakapokanyaga nimewapa, kama vile nilivyomwahidi Musa. Nchi yenu itaenea kuanzia jangwa hili hadi Lebanoni, tena kuanzia mto mkubwa wa Frati, yaani nchi yote ya Wahiti, hadi Bahari ile Kubwa iliyo upande wa magharibi. Hakuna mtu yeyote atakayeweza kushindana na wewe siku zote za maisha yako. Kama vile nilivyokuwa pamoja na Musa, ndivyo nitakavyokuwa pamoja na wewe, sitakuacha wala sitakupungukia.