Yona 4:1-11
Yona 4:1-11 Biblia Habari Njema (BHN)
Lakini jambo hilo halikumpendeza Yona hata kidogo, akakasirika sana. Kwa hiyo akaomba, “Mwenyezi-Mungu, je, hayo si mambo yaleyale niliyowaza utayafanya nilipokuwa nyumbani? Ndio maana nilifanya haraka kukimbilia Tarshishi. Nilijua kwamba wewe u Mungu wa upendo na huruma. Hukasiriki upesi, daima u mwema na u tayari kubadili nia yako wakati wowote ili usiadhibu. Basi, sasa ee Mwenyezi-Mungu, nakusihi uniondolee uhai wangu, maana, kwangu mimi ni afadhali kufa kuliko kuishi.” Naye Mwenyezi-Mungu akamjibu Yona: “Unadhani wafanya vema kukasirika?” Ndipo Yona akatoka nje ya mji, akajikalia upande wa mashariki wa mji huo. Hapo, akajijengea kibanda, akaketi kivulini mwake huku anangojea apate kuona litakaloupata mji wa Ninewi. Mungu, Mwenyezi-Mungu akaamuru mmea uote na kukua. Akauotesha ili kumpatia Yona kivuli cha kumpunguzia taabu aliyokuwa nayo. Yona akaufurahia sana mmea huo. Lakini siku ya pili, kulipopambazuka, Mungu akaamuru mdudu auharibu mmea huo, ukanyauka. Jua lilipochomoza, Mungu akaleta upepo wa hari kutoka mashariki, jua likamchoma sana Yona kichwani, karibu azirai. Yona akasema, “Afadhali kufa kuliko kuishi!” Lakini Mungu akamwambia Yona, “Je, unadhani wafanya vema kuukasirikia mmea huo?” Yona akajibu, “Ndiyo, nafanya vema kukasirika – kukasirika hata kufa!” Hapo Mungu akamwambia, “Mmea huu uliota na kukua kwa usiku mmoja, na usiku uliofuata ukanyauka. Wewe hukuufanyia kitu chochote, wala hukuuotesha. Mbona unauhurumia? Je, haifai kwangu kuuhurumia mji wa Ninewi, ule mji mkuu wenye watu 120,000, wasioweza kupambanua jema na baya, na pia wanyama wengi?”
Yona 4:1-11 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Lakini jambo hili lilimchukiza Yona sana, naye akakasirika. Akamwomba BWANA, akasema, Nakuomba, Ee BWANA; sivyo hivyo nilivyosema, hapo nilipokuwa katika nchi yangu? Hii ndiyo sababu nilifanya haraka kukimbilia Tarshishi; kwa maana nilijua ya kuwa wewe u Mungu mwenye neema, umejaa huruma, si mwepesi wa hasira, u mwingi wa rehema, nawe waghairi mabaya. Basi, sasa, Ee BWANA, nakuomba, uniondolee uhai wangu; maana ni afadhali nife mimi kuliko kuishi. Naye BWANA akasema, Je! Unatenda vema kukasirika? Ndipo Yona akatoka mjini, akaketi upande wa mashariki wa mji, akajitengenezea kibanda huko, akakaa chini yake uvulini, hadi aone mji ule utakuwaje. Na BWANA Mungu aliutayarisha mtango, akaufanya ukue juu ya Yona, ili uwe kivuli juu ya kichwa chake, na kumponya katika hali yake mbaya. Basi Yona akafurahi sana kwa sababu ya ule mtango. Lakini siku ya pili kulipopambazuka, Mungu akatayarisha buu, nalo likautafuna ule mtango, ukakatika. Basi ikawa, jua lilipopanda juu, Mungu akatayarisha upepo wa mashariki, wenye joto jingi; jua likampiga Yona kichwani, hata akazimia, naye akajitakia kufa, akasema, Ni afadhali nife mimi kuliko kuishi. Mungu akamwambia Yona, Je! Unatenda vema kukasirika kwa ajili ya mtango? Naye akasema, Ndiyo, natenda vema kukasirika hata kufa. Bwana akamwambia, Wewe umeuhurumia mtango, ambao hukuufanyia kazi, wala kuuotesha; uliomea katika usiku mmoja, na kuangamia katika usiku mmoja; na mimi, je! Haikunipasa kuuhurumia Ninawi, mji ule mkubwa; ambao ndani yake wamo watu zaidi ya elfu mia moja na ishirini, wasioweza kupambanua katika mkono wao wa kulia na mkono wao wa kushoto; tena wamo wanyama wa kufugwa wengi sana?
Yona 4:1-11 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Lakini jambo hili lilimchukiza Yona sana, naye akakasirika. Akamwomba BWANA, akasema, Nakuomba, Ee BWANA; sivyo hivyo nilivyosema, hapo nilipokuwa katika nchi yangu? Hii ndiyo sababu nalifanya haraka kukimbilia Tarshishi; kwa maana nalijua ya kuwa wewe u Mungu mwenye neema, umejaa huruma, si mwepesi wa hasira, u mwingi wa rehema, nawe waghairi mabaya. Basi, sasa, Ee BWANA, nakuomba, uniondolee uhai wangu; maana ni afadhali nife mimi kuliko kuishi. Naye BWANA akasema, Je! Unatenda vema kukasirika? Ndipo Yona akatoka mjini, akaketi upande wa mashariki wa mji, akajifanyia kibanda huko, akakaa chini yake uvulini, hata aone mji ule utakuwaje. Na BWANA Mungu aliweka tayari mtango, akaufanya ukue juu ya Yona, ili uwe kivuli juu ya kichwa chake, na kumponya katika hali yake mbaya. Basi Yona akafurahi sana kwa sababu ya ule mtango. Lakini siku ya pili kulipopambazuka, Mungu akaweka tayari buu, nalo likautafuna ule mtango, ukakatika. Basi ikawa, jua lilipopanda juu, Mungu akaweka tayari upepo wa mashariki, wenye hari nyingi; jua likampiga Yona kichwani, hata akazimia, naye akajitakia kufa, akasema, Ni afadhali nife mimi kuliko kuishi. Mungu akamwambia Yona, Je! Unatenda vema kukasirika kwa ajili ya mtango? Naye akasema, Ndiyo, natenda vema kukasirika hata kufa. Bwana akamwambia, Wewe umeuhurumia mtango, ambao hukuufanyia kazi, wala kuuotesha; uliomea katika usiku mmoja, na kuangamia katika usiku mmoja; na mimi, je! Haikunipasa kuuhurumia Ninawi, mji ule mkubwa; ambao ndani yake wamo watu zaidi ya mia na ishirini elfu, wasioweza kupambanua katika mkono wao wa kulia na mkono wao wa kushoto; tena wamo wanyama wa kufugwa wengi sana?
Yona 4:1-11 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Lakini Yona alichukizwa sana akakasirika. Akamwomba BWANA, “Ee BWANA, hili si lile nililolisema nilipokuwa ningali nyumbani? Hii ndiyo sababu niliharakisha kukimbilia Tarshishi. Nikifahamu kuwa wewe ni Mungu mwenye neema na huruma, si mwepesi wa hasira na umejaa upendo, ni Mungu ambaye hughairi katika kupeleka maafa. Sasa, Ee BWANA, niondolee uhai wangu, kwa kuwa ni afadhali mimi nife kuliko kuishi.” Lakini BWANA akamjibu, “Je unayo haki yoyote kukasirika?” Yona akatoka nje akaketi mahali upande wa mashariki wa mji. Hapo akajitengenezea kibanda, akaketi kwenye kivuli chake na kungojea ni nini kitakachotokea katika mji. Ndipo BWANA Mungu akaweka tayari mzabibu na kuufanya uote, kumpa Yona kivuli kilichomfunika kichwa ili kuondoa taabu yake, naye Yona akafurahi sana kwa ajili ya ule mzabibu. Lakini kesho yake asubuhi na mapema Mungu akaamuru buu, autafune mzabibu huo nao ukanyauka. Jua lilipochomoza, Mungu akautuma upepo wa hari wa mashariki, nalo jua likawaka juu ya kichwa cha Yona hadi akazimia. Akatamani kufa, naye akasema, “Ni afadhali mimi nife kuliko kuishi.” Lakini Mungu alimwambia Yona, “Je, unayo haki kukasirika kuhusu mzabibu huo?” Akasema, “Ndiyo, ninayo haki. Nimekasirika kiasi cha kufa.” Lakini BWANA akamwambia, “Wewe unakasirika kwa ajili ya mzabibu huu, nawe hukuusababisha kuota wala kuutunza. Uliota usiku mmoja, nao ukafa usiku mmoja. Lakini Ninawi ina zaidi ya watu elfu mia moja na ishirini ambao hawawezi kupambanua kulia au kushoto, pamoja na ngʼombe wengi. Je, hainipasi kufikiri kuhusu mji ule mkubwa?”