Yona 1:9-16
Yona 1:9-16 Biblia Habari Njema (BHN)
Yona akawajibu, “Mimi ni Mwebrania; namcha Mwenyezi-Mungu, Mungu wa mbingu, muumba wa bahari na nchi kavu.” Kisha Yona akawaeleza kwamba alikuwa anamkwepa Mwenyezi-Mungu. Kusikia hayo, mabaharia hao wakazidi kujawa na hofu, wakamwambia, “Umefanya nini wewe!” Wakati huo wote, bahari ilikuwa inazidi kuchafuka. Basi, wakamwuliza Yona, “Tukufanye nini ili bahari itulie?” Yona akawajibu, “Nichukueni mkanitupe baharini, nayo bahari itatulia, maana naona wazi kwamba dhoruba hii imewapata kwa sababu yangu mimi.” Mabaharia hao wakajaribu bado kupiga makasia wapate kuifikisha meli yao pwani, lakini hawakufanikiwa kwa maana bahari ilizidi kuwachafukia. Basi, wakamlilia Mwenyezi-Mungu wakisema, “Ee Mwenyezi-Mungu, twakusihi usituangamize kwa kuutoa uhai wa mtu huyu, wala usitupatilize kwa kumwaga damu ya mtu asiye na hatia. Wewe, ee Mwenyezi-Mungu, umefanya upendavyo.” Basi, wakamchukua Yona, wakamtupa baharini, na papo hapo bahari ikatulia. Mabaharia hao wakamwogopa sana Mwenyezi-Mungu, wakamtolea sadaka na kuweka nadhiri.
Yona 1:9-16 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Akawaambia, Mimi ni Mwebrania; nami namcha BWANA, Mungu wa mbingu, aliyeziumba bahari na nchi kavu. Ndipo watu wale wakaogopa mno, wakamwambia, Ni jambo gani hili ulilolitenda! Kwa maana watu wale walijua ya kuwa amekimbia, ajiepushe na uso wa BWANA, kwa sababu alikuwa amewaambia. Basi wakamwambia, Tukutende nini, ili bahari itulie? Kwa maana bahari ilikuwa inazidi kuchafuka. Naye akawaambia, Nikamateni, mnitupe baharini; kisha bahari itatulia; kwa maana najua ya kuwa ni kwa ajili yangu tufani hii imewapata. Lakini wale watu wakavuta makasia kwa nguvu, ili wapate kurudi pwani, wasiweze; kwa maana bahari ilizidi kuwachafukia sana. Basi wakamlilia BWANA, wakasema, Twakuomba, Ee BWANA, twakuomba, tusiangamie kwa ajili ya uhai wa mtu huyu, wala usitupatilize kwa ajili ya damu isiyo na hatia; kwa maana wewe, BWANA, umefanya kama ulivyopenda. Basi wakamkamata Yona, wakamtupa baharini, nayo bahari ikaacha kuchafuka. Ndipo wale watu wakamwogopa BWANA mno, wakamtolea BWANA sadaka, na kuweka nadhiri.
Yona 1:9-16 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Akawaambia, Mimi ni Mwebrania; nami namcha BWANA, Mungu wa mbingu, aliyeziumba bahari na nchi kavu. Ndipo watu wale wakaogopa mno, wakamwambia, Ni jambo gani hili ulilolitenda! Kwa maana watu wale walijua ya kuwa amekimbia, ajiepushe na uso wa BWANA, kwa sababu alikuwa amewajulisha. Basi wakamwambia, Tukutende nini, ili bahari itulie? Kwa maana bahari ilikuwa inazidi kuchafuka. Naye akawaambia, Nikamateni, mnitupe baharini; basi bahari itatulia; kwa maana najua ya kuwa ni kwa ajili yangu tufani hii imewapata. Lakini wale watu wakavuta makasia kwa nguvu, ili wapate kurudi pwani, wasiweze; kwa maana bahari ilizidi kuwachafukia sana. Basi wakamlilia BWANA, wakasema, Twakuomba, Ee BWANA, twakuomba, tusiangamie kwa ajili ya uhai wa mtu huyu, wala usitupatilize kwa ajili ya damu isiyo na hatia; kwa maana wewe, BWANA, umefanya kama ulivyopenda. Basi wakamkamata Yona, wakamtupa baharini, nayo bahari ikaacha kuchafuka. Ndipo wale watu wakamwogopa BWANA mno, wakamtolea BWANA sadaka, na kuweka nadhiri.
Yona 1:9-16 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Akajibu, “Mimi ni Mwebrania, nami namwabudu BWANA, Mungu wa Mbinguni, aliyeumba bahari na nchi kavu.” Hili liliwaogopesha nao wakamuuliza, “Umefanya nini?” (Walijua alikuwa anamkimbia BWANA, kwa sababu alishawaambia hivyo.) Bahari ilikuwa inazidi kuchafuka. Kwa hiyo walimuuliza, “Tukutendee nini ili kufanya bahari itulie kwa ajili yetu?” Akawajibu, “Niinueni mnitupe baharini, nayo itakuwa shwari. Ninajua mawimbi haya makubwa yamewatokea kwa ajili ya kosa langu.” Badala yake, wale watu walijitahidi kupiga makasia walivyoweza ili wapate kurudi pwani. Lakini hawakuweza, kwa kuwa bahari ilizidi kuchafuka kuliko mwanzo. Ndipo wakamlilia BWANA, “Ee BWANA, tafadhali usituue kwa kumuua mtu huyu. Usituhesabie hatia kwa kumuua mtu asiyekuwa na hatia, kwa kuwa wewe, Ee BWANA, umefanya kama ilivyokupendeza.” Kisha wakamchukua Yona, wakamtupa baharini, nayo bahari iliyokuwa imechafuka ikatulia. Katika jambo hili watu wakamwogopa BWANA sana, wakamtolea BWANA dhabihu na kumwekea nadhiri.