Yona 1:4-9
Yona 1:4-9 Biblia Habari Njema (BHN)
Lakini Mwenyezi-Mungu akavumisha upepo mkali baharini, ikatokea dhoruba kali, meli ikawa karibu kabisa kuvunjika. Mabaharia wakajawa na hofu, kila mmoja akaanza kumlilia mungu wake; wakatupa baharini shehena ya meli ili kupunguza uzito wake. Wakati huo, Yona alikuwa ameteremkia sehemu ya ndani ya meli, akawa amelala usingizi mzito. Nahodha akamwendea, akamwambia, “Wawezaje wewe kulala? Amka umwombe Mungu wako; labda Mungu wako atatuhurumia, tusiangamie.” Mabaharia wakasemezana: “Tupige kura tujue balaa hili limetupata kwa kosa la nani.” Basi, wakapiga kura; kura ikamwangukia Yona. Hapo wakaanza kumhoji: “Haya, sasa tuambie! Kwa nini balaa hili linatupata? Unafanya kazi gani? Umetoka wapi? U kabila gani?” Yona akawajibu, “Mimi ni Mwebrania; namcha Mwenyezi-Mungu, Mungu wa mbingu, muumba wa bahari na nchi kavu.”
Yona 1:4-9 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Lakini BWANA alituma upepo mkuu baharini, ikawa tufani kubwa baharini, hata merikebu ikawa karibu kuvunjika. Basi wale mabaharia wakaogopa, kila mtu akamwomba mungu wake; nao wakatupa baharini shehena iliyokuwa merikebuni, ili kuupunguza uzito wake. Lakini Yona alikuwa ameshuka hadi pande za ndani za merikebu; akajilaza, akapata usingizi. Basi nahodha akamwendea, akamwambia, Una nini, Ewe ulalaye usingizi? Amka, ukamwombe Mungu wako; labda Mungu huyo atatukumbuka, tusipotee. Wakasemezana kila mtu na mwenzake, Haya, na tupige kura, tupate kujua mabaya haya yametupata kwa sababu ya nani. Basi wakapiga kura, nayo kura ikamwangukia Yona. Ndipo wakamwambia, Tafadhali utuambie, wewe ambaye mabaya haya yametupata kwa sababu yako; kazi yako ni kazi gani? Nawe umetoka wapi? Nchi yako ni nchi ipi? Nawe u mtu wa kabila gani? Akawaambia, Mimi ni Mwebrania; nami namcha BWANA, Mungu wa mbingu, aliyeziumba bahari na nchi kavu.
Yona 1:4-9 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Lakini BWANA alituma upepo mkuu baharini, ikawa tufani kubwa baharini, hata merikebu ikawa karibu na kuvunjika. Basi wale mabaharia wakaogopa, kila mtu akamwomba mungu wake; nao wakatupa baharini shehena iliyokuwa merikebuni, ili kuupunguza uzito wake. Lakini Yona alikuwa ameshuka hata pande za ndani za merikebu; akajilaza, akapata usingizi. Basi nahodha akamwendea, akamwambia, Una nini, Ewe ulalaye usingizi? Amka, ukamwombe Mungu wako; labda Mungu huyo atatukumbuka, tusipotee. Wakasemezana kila mtu na mwenzake, Haya, na mpige kura, mpate kujua mabaya haya yametupata kwa sababu ya nani. Basi wakapiga kura, nayo kura ikamwangukia Yona. Ndipo wakamwambia, Tafadhali utuambie, wewe ambaye mabaya haya yametupata kwa sababu yako; kazi yako ni kazi gani? Nawe umetoka wapi? Nchi yako ni nchi ipi? Nawe u mtu wa kabila gani? Akawaambia, Mimi ni Mwebrania; nami namcha BWANA, Mungu wa mbingu, aliyeziumba bahari na nchi kavu.
Yona 1:4-9 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Ndipo BWANA akatuma upepo mkali baharini, nayo dhoruba kali sana ikavuma hata meli ikawa hatarini ya kuvunjika. Mabaharia wote waliogopa na kila mmoja akamlilia mungu wake mwenyewe. Nao wakatupa mizigo baharini ili meli ipungue uzito. Lakini Yona alikuwa ameteremkia chumba cha ndani ya meli, ambapo alilala na kupatwa na usingizi mzito. Nahodha akamwendea na kusema, “Wewe unawezaje kulala? Amka ukamwite mungu wako! Huenda akatuangalia, tusiangamie.” Kisha mabaharia wakasemezana wao kwa wao, “Njooni, tupige kura tumtafute anayehusika na maafa haya.” Wakapiga kura, nayo kura ikamwangukia Yona. Kwa hiyo walimuuliza, “Tuambie, ni nani anayehusika kwa kutuletea tatizo hili lote? Unafanya kazi gani? Umetoka wapi? Nchi yako ni ipi? Wewe ni kutoka taifa lipi?” Akajibu, “Mimi ni Mwebrania, nami namwabudu BWANA, Mungu wa Mbinguni, aliyeumba bahari na nchi kavu.”