Yoeli 3:1-4
Yoeli 3:1-4 Biblia Habari Njema (BHN)
“Wakati huo na siku hizo nitakapoirekebisha hali ya Yuda na Yerusalemu, nitayakusanya mataifa yote, niyapeleke katika bonde liitwalo, ‘Mwenyezi-Mungu Ahukumu. Huko nitayahukumu mataifa hayo, kwa mambo yaliyowatendea watu wangu Israeli, hao walio mali yangu mimi mwenyewe. Maana waliwatawanya miongoni mwa mataifa, waligawa nchi yangu na kugawana watu wangu kwa kura. Waliwauza wavulana ili kulipia malaya, na wasichana ili kulipia divai. “Mnataka kunifanya nini enyi Tiro na Sidoni na maeneo yote ya Filistia? Je, mna kisasi nami mnachotaka kulipiza? Kama mnalipiza kisasi, mimi nitawalipizeni mara moja!
Yoeli 3:1-4 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Kwa maana, angalieni, siku zile, na wakati ule, nitakapowarudisha mateka wa Yuda na Yerusalemu, nitakusanya mataifa yote, nami nitawaleta chini katika bonde la Yehoshafati, na huko nitawahukumu kwa ajili ya watu wangu, na kwa ajili ya urithi wangu, Israeli, ambao wamewatawanya kati ya mataifa, na kuigawanya nchi yangu. Nao wamewapigia kura watu wangu; na mvulana wamemwuza ili kupata kahaba, na msichana wamemwuza ili kupata divai, wapate kunywa. Naam, na ninyi ni kitu gani kwangu, enyi Tiro, na Sidoni, na nchi zote za Filisti? Je! Mtanirudishia malipo? Au mtanitenda neno lolote? Upesi na kwa haraka nitawarudishia malipo yenu juu ya vichwa vyenu wenyewe.
Yoeli 3:1-4 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Kwa maana, angalieni, siku zile, na wakati ule, nitakapowarudisha mateka wa Yuda na Yerusalemu, nitakusanya mataifa yote, nami nitawaleta chini katika bonde la Yehoshafau, na huko nitawahukumu kwa ajili ya watu wangu, na kwa ajili ya urithi wangu, Israeli, ambao wamewatawanya kati ya mataifa, na kuigawanya nchi yangu. Nao wamewapigia kura watu wangu; na mtoto mwanamume wamemtoa ili kupata kahaba, na mtoto mwanamke wamemwuza ili kupata divai, wapate kunywa. Naam, na ninyi ni kitu gani kwangu, enyi Tiro, na Sidoni, na nchi zote za Filisti? Je! Mtanirudishia malipo? Au mtanitenda neno lo lote? Upesi na kwa haraka nitawarudishia malipo yenu juu ya vichwa vyenu wenyewe.
Yoeli 3:1-4 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
“Katika siku hizo na wakati huo, nitakaporejesha neema ya Yuda na Yerusalemu, nitayakusanya mataifa yote na kuyaleta katika Bonde la Yehoshafati. Hapo nitaingia kwenye hukumu dhidi yao kuhusu urithi wangu, watu wangu Israeli, kwa kuwa waliwatawanya watu wangu miongoni mwa mataifa na kuigawa nchi yangu. Waliwapigia kura watu wangu na kuwauza wavulana ili kupata makahaba; waliwauza wasichana ili wapate kunywa mvinyo. “Sasa una nini dhidi yangu, ee Tiro na Sidoni, nanyi nchi zote za Ufilisti? Je, mnanilipiza kwa yale niliyoyafanya? Kama mnalipa, mimi nitalipiza juu ya vichwa vyenu kwa kasi na kwa haraka yale mliyoyatenda.