Yoeli 2:18-32
Yoeli 2:18-32 Biblia Habari Njema (BHN)
Ndipo Mwenyezi-Mungu akaipenda nchi yake akawahurumia watu wake. Alisikiliza, akajibu sala zao; akasema, “Sasa nitawapeni tena nafaka, sitawafanya mdharauliwe tena na mataifa. Nitawaondoa hao adui watokao kaskazini, nitawafukuza mpaka jangwani; askari wa mbele nitawatupa katika Bahari ya Chumvi na wale wa nyuma katika Bahari ya Mediteranea. Watatoa uvundo na harufu mbaya, hao ambao wamefanya maovu makubwa. “Usiogope, ewe nchi, bali furahi na kushangilia, maana Mwenyezi-Mungu ametenda makuu. Msiogope, enyi wanyama. malisho ya nyikani yamekuwa mazuri, miti inazaa matunda yake, mizabibu na mitini zinazaa kwa wingi. “Furahini, enyi watu wa Siyoni, shangilieni kwa sababu ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, maana amewapeni mvua za masika, amewapeni mvua ya kutosha: Mvua za masika na mvua za vuli kama hapo awali. Mahali pa kupuria patajaa nafaka, mashinikizo yatafurika divai na mafuta. Nitawarudishia miaka ile iliyoliwa na nzige, kila kitu kilicholiwa na tunutu, parare na matumatu, hilo jeshi kubwa nililowaletea! Mtapata chakula kingi na kutosheka; mtalisifu jina la Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, aliyewatendea mambo ya ajabu. Watu wangu, kamwe hawatadharauliwa tena. Mtatambua kwamba mimi nimo miongoni mwenu, enyi Waisraeli; kwamba mimi Mwenyezi-Mungu, ndimi Mungu wenu wala hakuna mwingine. Watu wangu, kamwe hawatadharauliwa tena. “Kisha hapo baadaye nitaimimina roho yangu juu ya binadamu wote. Watoto wenu wa kike na wa kiume watatabiri, wazee wenu wataota ndoto, na vijana wenu wataona maono. Hata juu ya watumishi wa kiume na wa kike, nitaimimina roho yangu wakati huo. “Nitatoa ishara mbinguni na duniani; kutakuwa na damu, moto na minara ya moshi. Jua litatiwa giza, na mwezi utakuwa mwekundu kama damu, kabla ya kufika siku ya Mwenyezi-Mungu, siku iliyo kuu na ya kutisha. Hapo watu wote watakaoomba kwa jina la Mwenyezi-Mungu wataokolewa. Maana katika mlima Siyoni na Yerusalemu, watakuwako watu watakaosalimika, kama nilivyosema mimi Mwenyezi-Mungu.
Yoeli 2:18-32 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Hapo ndipo BWANA alipoona wivu kwa ajili ya nchi yake, akawahurumia watu wake. BWANA akajibu, akawaambia watu wake; Tazameni, nitawaletea nafaka, na divai, na mafuta, nanyi mtashiba kwa vitu hivyo; wala sitawafanya tena kuwa aibu kati ya mataifa; lakini jeshi lililotoka kaskazini nitaliondolea mbali nanyi, nami nitalifukuza mpaka nchi ya ukame na ukiwa; sehemu yake iliyo mbele itaingia katika bahari ya mashariki, na sehemu yake iliyo nyuma itaingia katika bahari ya magharibi; na uvundo wake utapanda juu, na harufu yake mbaya itapanda juu, kwa sababu ametenda mambo makubwa. Ee nchi, usiogope; furahi na kushangilia; kwa kuwa BWANA ametenda mambo makuu. Msiogope, enyi wanyama wa porini; maana malisho ya jangwani yanatoa miche, na huo mti unazaa matunda yake, mtini na mzabibu inatoa nguvu zake. Furahini, basi, enyi wana wa Sayuni, mkamfurahie BWANA, Mungu wenu; kwa kuwa yeye huwapa ninyi mvua ya masika, kwa kipimo cha haki, naye huwanyeshea mvua, mvua ya masika, na mvua ya vuli, kama awali. Na sakafu za kupepetea zitajaa ngano, na mashinikizo yatafurika kwa divai na mafuta. Nami nitawarudishia hiyo miaka iliyoliwa na nzige, na parare, na madumadu, na tunutu, jeshi langu kubwa nililotuma kati yenu. Nanyi mtakula chakula tele na kushiba, na kulihimidi jina la BWANA, Mungu wenu, aliyewatendea mambo ya ajabu; na watu wangu hawatatahayari kamwe. Nanyi mtajua ya kuwa mimi ni katikati ya Israeli, na ya kuwa mimi ndimi BWANA, Mungu wenu, wala hakuna mwingine; na watu wangu hawatatahayari kamwe. Hata itakuwa, baada ya hayo, ya kwamba nitamimina roho yangu juu ya wote wenye mwili; na wana wenu, wa kiume na wa kike, watatabiri, wazee wenu wataota ndoto, na vijana wenu wataona maono; tena juu ya watumishi wenu, wanaume kwa wanawake, katika siku zile, nitamimina roho yangu. Nami nitaonesha mambo ya ajabu katika mbingu na katika dunia, damu, na moto, na minara ya moshi. Jua litageuzwa kuwa giza, na mwezi kuwa damu, kabla haijaja hiyo siku ya BWANA iliyo kuu na itishayo. Na itakuwa ya kwamba mtu awaye yote atakayeliita jina la BWANA ataponywa; kwa kuwa katika mlima Sayuni na katika Yerusalemu watakuwako watu watakaookoka, kama BWANA alivyosema; na katika mabaki, hao awaitao BWANA.
Yoeli 2:18-32 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Hapo ndipo BWANA alipoona wivu kwa ajili ya nchi yake, akawahurumia watu wake. BWANA akajibu, akawaambia watu wake; Tazameni, nitawaletea nafaka, na divai, na mafuta, nanyi mtashiba kwa vitu hivyo; wala sitawafanya tena kuwa aibu kati ya mataifa; lakini jeshi lililotoka kaskazini nitaliondolea mbali nanyi, nami nitalifukuza mpaka nchi ya ukame na ukiwa; sehemu yake iliyo mbele itaingia katika bahari ya mashariki, na sehemu yake iliyo nyuma itaingia katika bahari ya magharibi; na uvundo wake utapanda juu, na harufu yake mbaya itapanda juu, kwa sababu ametenda mambo makubwa. Ee nchi, usiogope; furahi na kushangilia; kwa kuwa BWANA ametenda mambo makuu. Msiogope, enyi wanyama wa kondeni; maana malisho ya jangwani yanatoa miche, na huo mti unazaa matunda yake, mtini na mzabibu inatoa nguvu zake. Furahini, basi, enyi wana wa Sayuni, mkamfurahie BWANA, Mungu wenu; kwa kuwa yeye huwapa ninyi mvua ya masika, kwa kipimo cha haki, naye huwanyeshea mvua, mvua ya masika, na mvua ya vuli, kama kwanza. Na sakafu za kupepetea zitajaa ngano, na mashinikizo yatafurika kwa divai na mafuta. Nami nitawarudishia hiyo miaka iliyoliwa na nzige, na parare, na madumadu, na tunutu, jeshi langu kubwa nililotuma kati yenu. Nanyi mtakula chakula tele na kushiba, na kulihimidi jina la BWANA, Mungu wenu, aliyewatendea mambo ya ajabu; na watu wangu hawatatahayari kamwe. Nanyi mtajua ya kuwa mimi ni katikati ya Israeli, na ya kuwa mimi ndimi BWANA, Mungu wenu, wala hakuna mwingine; na watu wangu hawatatahayari kamwe. Hata itakuwa, baada ya hayo, ya kwamba nitamimina roho yangu juu ya wote wenye mwili; na wana wenu, waume kwa wake, watatabiri, wazee wenu wataota ndoto, na vijana wenu wataona maono; tena juu ya watumishi wenu, wanaume kwa wanawake, katika siku zile, nitamimina roho yangu. Nami nitaonyesha mambo ya ajabu katika mbingu na katika dunia, damu, na moto, na minara ya moshi. Jua litageuzwa kuwa giza, na mwezi kuwa damu, kabla haijaja hiyo siku ya BWANA iliyo kuu na itishayo. Na itakuwa ya kwamba mtu awaye yote atakayeliita jina la BWANA ataponywa; kwa kuwa katika mlima Sayuni na katika Yerusalemu watakuwako watu watakaookoka, kama BWANA alivyosema; na katika mabaki, hao awaitao BWANA.
Yoeli 2:18-32 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Kisha BWANA atakuwa na wivu kwa ajili ya nchi yake na kuwa na huruma juu ya watu wake. BWANA atawajibu: “Ninawapelekea nafaka, mvinyo mpya na mafuta, vya kuwatosha ninyi hadi mridhike kabisa; kamwe sitawafanya tena kitu cha kudharauliwa na mataifa. “Nitafukuza jeshi la kaskazini likae mbali nanyi, nikilisukuma ndani ya jangwa, askari wa safu za mbele wakienda ndani ya bahari ya mashariki na wale wa safu za nyuma katika bahari ya magharibi. Uvundo wake utapaa juu; harufu yake itapanda juu.” Hakika ametenda mambo makubwa. Usiogope, ee nchi; furahi na kushangilia. Hakika BWANA ametenda mambo makubwa. Msiogope, enyi wanyama pori, kwa kuwa mbuga za malisho yenu zinarudia ubichi. Miti nayo inazaa matunda, mtini na mzabibu inatoa utajiri wake. Furahini, enyi watu wa Sayuni, shangilieni katika BWANA Mungu wenu, kwa kuwa amewapa mvua za vuli kwa kipimo cha haki. Anawapelekea mvua nyingi, mvua ya vuli na ya masika, kama mwanzoni. Sakafu za kupuria zitajaa nafaka, mapipa yatafurika mvinyo mpya na mafuta. “Nitawalipa kwa ajili ya miaka ile iliyoliwa na nzige: parare, madumadu na tunutu, jeshi langu kubwa ambalo nililituma kati yenu. Mtakuwa na wingi wa vyakula hadi mshibe, na mtalisifu jina la BWANA Mungu wenu, ambaye amefanya maajabu kwa ajili yenu; kamwe watu wangu hawataaibishwa tena. Ndipo mtajua kuwa mimi niko katika Israeli, kuwa mimi ndimi BWANA Mungu wenu, na kwamba hakuna mwingine; kamwe watu wangu hawataaibika tena. BWANA “Hata itakuwa, baada ya hayo, nitamimina Roho wangu juu ya wote wenye mwili. Wana wenu wa kiume na wa kike watatabiri, wazee wenu wataota ndoto, na vijana wenu wataona maono. Hata juu ya watumishi wangu, wanaume kwa wanawake, katika siku zile nitamimina Roho wangu. Nami nitaonesha maajabu katika mbingu na duniani: damu, moto na mawimbi ya moshi. Jua litageuzwa kuwa giza na mwezi kuwa mwekundu kama damu, kabla ya kuja siku ya BWANA ile kuu na ya kutisha. Na kila mtu atakayeliitia jina la BWANA ataokolewa. Kwa maana juu ya Mlima Sayuni na katika Yerusalemu kutakuwa na wokovu, kama BWANA alivyosema, miongoni mwa walionusurika ambao BWANA awaita.