Yoeli 2:1-17
Yoeli 2:1-17 Biblia Habari Njema (BHN)
Pigeni tarumbeta huko Siyoni; pigeni baragumu juu ya mlima mtakatifu! Tetemekeni enyi wakazi wa Yuda, maana siku ya Mwenyezi-Mungu inakuja, naam, siku hiyo iko karibu! Hiyo ni siku ya giza na huzuni; siku ya mawingu na giza nene. Jeshi kubwa la nzige linakaribia kama giza linalotanda milimani. Namna hiyo haijapata kuweko kamwe wala haitaonekana tena katika vizazi vyote vijavyo. Kama vile moto uteketezavyo jeshi hilo laharibu kila kitu mbele yake na kuacha nyuma kila kitu kinateketezwa; kabla hawajapita, nchi ni kama bustani ya Edeni, lakini wakisha pita, ni jangwa tupu. Hakuna kiwezacho kuwaepa! Wanaonekana kama farasi, wanashambulia kama farasi wa vita, Wanaporukaruka kwenye vilele vya milima, wanarindima kama magari ya farasi, wanavuma kama mabua makavu motoni. Wamejipanga kama jeshi kubwa tayari kabisa kufanya vita. Wakaribiapo, watu hujaa hofu, nyuso zao zinawaiva. Wanashambulia kama mashujaa wa vita; kuta wanazipanda kama wanajeshi. Wote wanakwenda mbele moja kwa moja, bila hata mmoja wao kubadilisha njia. Hakuna amsukumaye mwenziwe; kila mmoja anafuata mkondo wake. Wanapita kati ya vizuizi vya silaha, wala hakuna kiwezacho kuwazuia. Wanauvamia mji, wanapiga mbio ukutani; wanaziparamia nyumba na kuingia, wanapenya madirishani kama wezi. Nchi inatetemeka mbele yao, mbingu zinatikisika. Jua na mwezi vyatiwa giza, nazo nyota zinaacha kuangaza. Mwenyezi-Mungu anaamuru jeshi lake kwa sauti; askari wake ni wengi mno, wanaomtii hawahesabiki. 2Siku ya Mwenyezi-Mungu kweli ni kuu na ya kutisha sana! Nani atakayeweza kuistahimili? “Lakini hata sasa,” nasema mimi Mwenyezi-Mungu, “Nirudieni kwa moyo wote, kwa kufunga, kulia na kuomboleza. Msirarue mavazi yenu kuonesha huzuni bali nirudieni kwa moyo wa toba.” Mrudieni Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu; yeye amejaa neema na huruma; hakasiriki upesi, ni mwingi wa fadhili; daima yu tayari kuacha kuadhibu. Huenda Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, atabadili nia na kuwapeni baraka ya mazao, mkamtolea sadaka za nafaka na kinywaji. Pigeni tarumbeta huko Siyoni! Toeni amri watu wafunge; itisheni mkutano wa kidini. Wakusanyeni watu wote, wawekeni watu wakfu. Waleteni wazee, wakusanyeni watoto, hata watoto wanyonyao. Bwana arusi na bibi arusi na watoke vyumbani mwao. Kati ya madhabahu na lango la hekalu, makuhani, wahudumu wa Mwenyezi-Mungu, walie na kuomba wakisema: “Wahurumie watu wako, ee Mwenyezi-Mungu. Usiyaache mataifa mengine yatudharau na kutudhihaki yakisema, ‘Yuko wapi basi Mungu wao?’”
Yoeli 2:1-17 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Pigeni tarumbeta katika Sayuni, Pigeni na kelele katika mlima wangu mtakatifu; Wenyeji wote wa nchi na watetemeke; Kwa maana siku ya BWANA inakuja. Kwa sababu inakaribia; siku ya giza na huzuni, siku ya mawingu na giza kuu. Kama mapambazuko yakitandazwa juu ya milima, hao ni wakuu, tena wenye nguvu, mfano wao haukuwako kamwe, wala hautakuwako baada ya hao, hata katika miaka ya vizazi vingi. Moto unaunguza vikali mbele yao; na nyuma yao miali ya moto inateketeza; hiyo nchi inafanana na bustani ya Edeni mbele yao, na nyuma yao imekuwa jangwa tupu; naam, hakuna aliyeokoka asipatikane nao. Kuonekana kwao ni kama kuonekana kwa farasi; na kama wapanda farasi ndivyo wanavyopiga mbio. Kama mshindo wa magari ya vita juu ya vilele vya milima, ndivyo warukavyo; kama mshindo wa miali ya moto iunguzapo mabua makavu, kama mashujaa waliopangwa tayari kwa vita. Mbele yao watu wanahangaika; nyuso zote zimegeuka kuwa nyeupe kwa hofu. Hupiga mbio kama mashujaa; huupanda ukuta kama watu wa vita; nao huendelea mbele kila mmoja katika njia zake, wala hawapotoshi safu zao. Wala hapana mmoja amsukumaye mwenzake; huendelea mbele kila mmoja katika njia yake; hujifanyia njia kwa nguvu kati ya silaha, wala hawaachi kuifuata njia yao. Huurukia mji; hupiga mbio juu ya ukuta; hupanda na kuingia ndani ya nyumba; huingia madirishani kama aingiavyo mwizi. Nchi inatetemeka mbele yao; mbingu zinatetemeka; jua na mwezi hutiwa giza, na nyota huacha kuangaza; naye BWANA anatoa sauti yake mbele ya jeshi lake; maana matuo yake ni makubwa sana; kwa maana yeye ni hodari atekelezaye neno lake; kwa kuwa siku ya BWANA ni kuu, yenye kitisho sana; naye ni nani awezaye kuistahimili? Lakini hata sasa, asema BWANA, nirudieni mimi kwa mioyo yenu yote, na kwa kufunga, na kwa kulia, na kwa kuomboleza; rarueni mioyo yenu, wala si mavazi yenu, mkamrudie BWANA, Mungu wenu; kwa maana yeye ndiye mwenye neema, amejaa huruma; si mwepesi wa hasira, ni mwingi wa rehema, naye hughairi kuadhibu. Ni nani ajuaye kwamba hatarudi na kugeuka, na kutuachia baraka nyuma yake, naam, sadaka ya unga, na sadaka ya kinywaji, kwa BWANA, Mungu wenu? Pigeni tarumbeta katika Sayuni, Takaseni saumu, kusanyeni kusanyiko kuu; Kusanyeni watu, litakaseni kusanyiko, Kusanyeni wazee, kusanyeni watoto, Na hao wanyonyao maziwa; Bwana arusi na atoke chumbani mwake, Na bibi arusi katika hema yake. Hao makuhani, wahudumu wa BWANA, na walie Kati ya patakatifu na madhabahu, Na waseme, Uwaachilie watu wako, Ee BWANA, Wala usiutoe urithi wako upate aibu, Hata mataifa watawale juu yao; Kwa nini waseme kati ya watu, Yuko wapi Mungu wao?
Yoeli 2:1-17 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Pigeni tarumbeta katika Sayuni, Pigeni na kelele katika mlima wangu mtakatifu; Wenyeji wote wa nchi na watetemeke; Kwa maana siku ya BWANA inakuja. Kwa sababu inakaribia; siku ya giza na weusi, siku ya mawingu na giza kuu. Kama mapambazuko yakitandazwa juu ya milima, hao ni wakuu, tena wenye nguvu, mfano wao haukuwako kamwe, wala hautakuwako baada ya hao, hata katika miaka ya vizazi vingi. Moto unakula mbele yao; na nyuma yao miali ya moto inateketeza; hiyo nchi inafanana na bustani ya Adeni mbele yao, na nyuma yao imekuwa jangwa tupu; naam, hakuna aliyeokoka asipatikane nao. Kuonekana kwao ni kama kuonekana kwa farasi; na kama wapanda farasi ndivyo wanavyopiga mbio. Kama mshindo wa magari ya vita juu ya vilele vya milima, ndivyo warukavyo; kama mshindo wa miali ya moto ilapo mabua makavu, kama mashujaa waliopangwa tayari kwa vita. Mbele yao watu wanahangaika; nyuso zote zimegeuka kuwa nyeupe kwa hofu. Hupiga mbio kama mashujaa; huupanda ukuta kama watu wa vita; nao huendelea mbele kila mmoja katika njia zake, wala hawapotoshi safu zao. Wala hapana mmoja amsukumaye mwenzake; huendelea mbele kila mmoja katika njia yake; hujifanyizia njia kwa nguvu kati ya silaha, wala hawaachi kuifuata njia yao. Huurukia mji; hupiga mbio juu ya ukuta; hupanda na kuingia ndani ya nyumba; huingia madirishani kama aingiavyo mwivi. Nchi inatetemeka mbele yao; mbingu zinatetemeka; jua na mwezi hutiwa giza, na nyota huacha kuangaza; naye BWANA anatoa sauti yake mbele ya jeshi lake; maana matuo yake ni makubwa sana; kwa maana yeye ni hodari atekelezaye neno lake; kwa kuwa siku ya BWANA ni kuu, yenye kitisho sana; naye ni nani awezaye kuistahimili? Lakini hata sasa, asema BWANA, nirudieni mimi kwa mioyo yenu yote, na kwa kufunga, na kwa kulia, na kwa kuombolea; rarueni mioyo yenu, wala si mavazi yenu, mkamrudie BWANA, Mungu wenu; kwa maana yeye ndiye mwenye neema, amejaa huruma; si mwepesi wa hasira, ni mwingi wa rehema, naye hughairi mabaya. N’nani ajuaye kwamba hatarudi na kugeuka, na kutuachia baraka nyuma yake, naam, sadaka ya unga, na sadaka ya kinywaji, kwa BWANA, Mungu wenu? Pigeni tarumbeta katika Sayuni, Takaseni saumu, kusanyeni kusanyiko kuu; Kusanyeni watu, litakaseni kusanyiko, Kusanyeni wazee, kusanyeni watoto, Na hao wanyonyao maziwa; Bwana arusi na atoke chumbani mwake, Na bibi arusi katika hema yake. Hao makuhani, wahudumu wa BWANA, na walie Kati ya patakatifu na madhabahu, Na waseme, Uwaachilie watu wako, Ee BWANA, Wala usiutoe urithi wako upate aibu, Hata mataifa watawale juu yao; Kwani waseme kati ya watu, Yuko wapi Mungu wao?
Yoeli 2:1-17 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Pigeni tarumbeta katika Sayuni; pigeni mbiu katika mlima wangu mtakatifu. Wote wanaoishi katika nchi na watetemeke, kwa kuwa siku ya BWANA inakuja. Iko karibu, siku ya giza na huzuni, siku ya mawingu na utusitusi. Kama mapambazuko yanavyosambaa toka upande huu wa milima hata upande mwingine, jeshi kubwa na lenye nguvu linakuja. Jambo kama hili halijakuwepo tangu zamani, wala halitakuwepo tena kamwe kwa vizazi vijavyo. Mbele yao moto unateketeza, nyuma yao miali ya moto inawaka kwa nguvu. Mbele yao nchi iko kama bustani ya Edeni, nyuma yao ni jangwa lisilofaa: hakuna kitu kinachowaepuka. Wanaonekana kama farasi; wanaenda mbio kama askari wapanda farasi. Wanatoa sauti kama magari ya vita, wanaporukaruka juu ya vilele vya milima, kama mlio wa miali ya moto ilayo mabua, kama jeshi kubwa lililojipanga kwa ajili ya vita. Wanapoonekana, mataifa yanakuwa katika maumivu makuu; kila uso unabadilika rangi. Wanashambulia kama mashujaa; wanapanda kuta kama askari. Wote wanatembea katika safu, hawapotoshi safu zao. Hakuna anayemsukuma mwenzake; kila mmoja anaenda mbele moja kwa moja. Wanapita katika vizuizi bila kuharibu safu zao. Wanaenda kasi kuingia mjini; wanakimbia ukutani. Wanaingia ndani ya nyumba; kwa kuingilia madirishani kama wezi. Mbele yao dunia inatikisika, anga linatetemeka, jua na mwezi vinatiwa giza, na nyota hazitoi mwanga wake tena. BWANA anatoa mshindo wa ngurumo mbele ya jeshi lake; majeshi yake hayana idadi, ni wenye nguvu nyingi wale ambao hutii agizo lake. Siku ya BWANA ni kuu, ni ya kutisha. Ni nani anayeweza kuistahimili? “Hata sasa,” asema BWANA, “nirudieni kwa mioyo yenu yote, kwa kufunga, kwa kulia na kuomboleza.” Rarueni mioyo yenu na siyo mavazi yenu. Mrudieni BWANA Mungu wenu, kwa maana yeye ndiye mwenye neema na mwingi wa huruma, si mwepesi wa hasira, ni mwingi wa upendo, huona huruma, hujizuia kuleta maafa. Ni nani ajuaye? Yeye aweza kugeuka na kuwa na huruma na kuacha baraka nyuma yake: sadaka za nafaka na sadaka za vinywaji kwa ajili ya BWANA Mungu wenu. Pigeni tarumbeta katika Sayuni, tangazeni saumu takatifu, liiteni kusanyiko takatifu. Wakusanyeni watu, wekeni wakfu kusanyiko; waleteni pamoja wazee, wakusanyeni watoto, wale wanyonyao maziwa. Bwana arusi na atoke chumbani mwake na bibi arusi naye atoke katika chumba chake. Makuhani, ambao wanahudumu mbele za BWANA, na walie katikati ya ukumbi wa Hekalu na madhabahu. Waseme, “Wahurumie watu wako, Ee BWANA. Usifanye urithi wako kitu cha kudharauliwa, neno la dhihaka kati ya mataifa. Kwa nini wasemezane miongoni mwao, ‘Yuko wapi Mungu wao?’ ”