Yoeli 1:1-20
Yoeli 1:1-20 Biblia Habari Njema (BHN)
Neno la Mwenyezi-Mungu lililomjia Yoeli, mwana wa Pethueli: Sikilizeni kitu hiki enyi wazee; tegeni sikio wakazi wote wa Yuda! Je, jambo kama hili limewahi kutokea maishani mwenu, au nyakati za wazee wenu? Wasimulieni watoto wenu jambo hili, nao wawasimulie watoto wao, na watoto wao wakisimulie kizazi kifuatacho. Nzige, makundi kwa makundi, wameivamia mimea; kilichoachwa na nzige kimeliwa na tunutu, kilichoachwa na tunutu kimeliwa na parare, kilichoachwa na parare kimeliwa na matumatu. Enyi walevi, levukeni na kulia; pigeni yowe, enyi walevi wa divai; zabibu zote za kutengeneza divai mpya zimeharibiwa. Jeshi la nzige limeivamia nchi yetu; lina nguvu na ni kubwa ajabu; meno yake ni kama ya simba, na magego yake ni kama ya simba jike. Limeiharibu mizabibu yetu, na kuitafuna mitini yetu. Limeyabambua magamba yake na kuyatupa chini, na matawi yake yameachwa meupe. Lieni kama msichana aliyevaa vazi la gunia akiombolezea kifo cha mchumba wake. Sadaka za nafaka na kinywaji zimetoweka nyumbani kwa Mwenyezi-Mungu. Makuhani, wahudumu wa Mwenyezi-Mungu, wanaomboleza. Mashamba yamebaki matupu; nchi inaomboleza, maana nafaka imeharibiwa, divai imetoweka, mafuta yamekosekana. Ombolezeni enyi wakulima; pigeni yowe enyi watunza mizabibu. Ngano na shayiri zimeharibika, mavuno yote shambani yameangamia. Mizabibu imenyauka; mitini imedhoofika; mikomamanga, mitende na mitofaa imekauka, naam miti yote shambani imekauka. Furaha imetoweka miongoni mwa watu. Enyi makuhani, jivikeni magunia kuomboleza, lieni enyi wahudumu wa madhabahu. Ingieni hekaluni mkaomboleze usiku kucha! Sadaka za nafaka na kinywaji zimetoweka nyumbani kwa Mungu. Toeni amri watu wafunge; itisheni mkutano wa kidini. Kusanyeni wazee na wakazi wote wa nchi, nyumbani kwa Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, na humo mkamlilie Mwenyezi-Mungu. Ole wetu kwa ile siku ya Mwenyezi-Mungu, siku hiyo ya Mwenyezi-Mungu inakaribia; inakuja pamoja na maangamizi, kutoka kwa Mungu Mkuu. Mazao yetu yameharibiwa huku tunatazama. Furaha na kicheko vimetoweka nyumbani kwa Mungu wetu. Mbegu zinaoza udongoni; ghala za nafaka ni ukiwa mtupu, ghala zimeharibika, kwa kukosa nafaka ya kuhifadhi. Tazama wanyama wanavyolia kwa huzuni! Makundi ya ng'ombe yanahangaika, kwa sababu yamekosa malisho; hata makundi ya kondoo yanateseka. Ninakulilia wewe, ee Mwenyezi-Mungu, moto umemaliza malisho nyikani, miali ya moto imeteketeza miti mashambani. Hata wanyama wa porini wanakulilia wewe, maana, vijito vya maji vimekauka, moto umemaliza malisho nyikani.
Yoeli 1:1-20 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Neno la BWANA lililomjia Yoeli, mwana wa Pethueli. Sikieni haya, enyi wazee; Sikilizeni, enyi wenyeji wote wa nchi. Je! Mambo haya yamekuwako katika siku zenu, Au katika siku za baba zenu? Waambieni watoto wenu habari yake, Watoto wenu wakawaambie watoto wao, Na watoto wao wakakiambie kizazi kingine. Yaliyosazwa na tunutu yameliwa na nzige; na yaliyosazwa na nzige yameliwa na parare; na yaliyosazwa na parare yameliwa na madumadu. Levukeni, enyi walevi, mkalie; Pigeni yowe, ninyi nyote mnywao divai; Kwa sababu ya divai mpya; Maana umekatiliwa mbali na vinywa vyenu. Maana taifa limepanda juu ya nchi yangu, Lenye nguvu, tena halina hesabu; Meno yake ni kama meno ya simba, Naye ana magego ya simba mkubwa. Ameuharibu mzabibu wangu; ameuvunja mtini wangu; ameyaambua magamba yake kabisa; ameuangusha chini; matawi yake yamefanywa kuwa meupe. Omboleza kama mwanamwali avaaye magunia Kwa ajili ya mume wa ujana wake. Sadaka ya unga na sadaka ya kinywaji Zimekatiliwa mbali na nyumba ya BWANA; Hao makuhani, wahudumu wa BWANA, wanaomboleza. Shamba limeharibika, nchi inaomboleza; maana nafaka imeharibika, divai mpya imekauka, mafuta yamepunguka. Tahayarini, enyi wakulima; Pigeni yowe, enyi watunzaji wa mizabibu; Kwa ajili ya ngano na shayiri, Maana mavuno ya mashamba yamepotea. Mzabibu umesinyaa, mtini nao umevia; Nao mkomamanga na mtende na mtofaa; Naam, miti yote ya mashamba imekauka; Maana furaha imetoweka kwa wanadamu. Jikazeni mkaomboleze, enyi makuhani; Pigeni yowe, enyi wahudumu wa madhabahu; Njooni mlale usiku kucha katika magunia, Enyi wahudumu wa Mungu wangu; Kwa kuwa sadaka ya unga na sadaka ya kinywaji Zimezuiwa katika nyumba ya Mungu wenu. Takaseni saumu, iteni kusanyiko la dini, Wazee na wakusanye wenyeji wote wa nchi; Waende nyumbani kwa BWANA, Mungu wenu, Na kumlilia BWANA, Ole wake siku hii! Kwa maana siku ya BWANA inakaribia, nayo itakuja kama maangamizi yatokayo kwake aliye Mwenyezi. Je! Chakula hakikukatiliwa mbali mbele ya macho yetu? Naam, furaha na kicheko mbali na nyumba ya Mungu wetu? Mbegu zinaoza chini ya udongo wake; mabohari yameachwa ukiwa; ghala zimeharibika; kwa maana nafaka imekauka. Jinsi wanyama wanavyougua! Makundi ya ng'ombe yamefadhaika, kwa sababu hawana malisho; naam, makundi ya kondoo yamehangaika. Ee BWANA, nakulilia wewe; Kwa maana moto umeyala malisho ya nyikani, Na miali ya moto imeteketeza miti yote ya mashamba. Naam, hata wanyama pori wanakulilia wewe; Kwa maana vijito vya maji vimekauka, Na moto umeyateketeza malisho ya nyikani.
Yoeli 1:1-20 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Neno la BWANA lililomjia Yoeli, mwana wa Pethueli. Sikieni haya, enyi wazee; Sikilizeni, enyi wenyeji wote wa nchi. Je! Mambo haya yamekuwako katika siku zenu, Au katika siku za baba zenu? Waarifuni watoto wenu habari yake, Watoto wenu wakawaambie watoto wao, Na watoto wao wakakiambie kizazi kingine. Yaliyosazwa na tunutu yameliwa na nzige; na yaliyosazwa na nzige yameliwa na parare; na yaliyosazwa na parare yameliwa na madumadu. Levukeni, enyi walevi, mkalie; Pigeni yowe, ninyi nyote mnywao divai; Kwa sababu ya divai mpya; Maana umekatiliwa mbali na vinywa vyenu. Maana taifa limepanda juu ya nchi yangu, Lenye nguvu, tena halina hesabu; Meno yake ni kama meno ya simba, Naye ana magego ya simba mkubwa. Ameuharibu mzabibu wangu; ameuvunja mtini wangu; ameyaambua magamba yake kabisa; ameuangusha chini; matawi yake yamefanywa kuwa meupe. Ombolea kama mwanamwali avaaye magunia Kwa ajili ya mume wa ujana wake. Sadaka ya unga na sadaka ya kinywaji Zimekatiliwa mbali na nyumba ya BWANA; Hao makuhani, wahudumu wa BWANA, wanaomboleza. Shamba limeharibika, nchi inaomboleza; maana nafaka imeharibika, divai mpya imekauka, mafuta yamepunguka. Tahayarini, enyi wakulima; Pigeni yowe, enyi watunzaji wa mizabibu; Kwa ajili ya ngano na shayiri, Maana mavuno ya mashamba yamepotea. Mzabibu umesinyaa, mtini nao umevia; Nao mkomamanga na mtende na mtofaa; Naam, miti yote ya mashamba imekauka; Maana furaha imekauka katika wanadamu. Jikazeni mkaomboleze, enyi makuhani; Pigeni yowe, enyi wahudumu wa madhabahu; Njoni mlale usiku kucha katika magunia, Enyi wahudumu wa Mungu wangu; Kwa kuwa sadaka ya unga na sadaka ya kinywaji Zimezuiwa katika nyumba ya Mungu wenu. Takaseni saumu, iteni kusanyiko la dini, Wazee na wakusanye wenyeji wote wa nchi; Waende nyumbani kwa BWANA, Mungu wenu, Na kumlilia BWANA, Ole wake siku hii! Kwa maana siku ya BWANA inakaribia, nayo itakuja kama uangamivu utokao kwake aliye Mwenyezi. Je! Chakula hakikukatiliwa mbali mbele ya macho yetu? Naam, furaha na kicheko mbali na nyumba ya Mungu wetu? Mbegu zinaoza chini ya udongo wake; ghala zimeachwa ukiwa; mabanda yamevunjika; kwa maana nafaka imekauka. Jinsi wanyama wanavyougua! Makundi ya ng’ombe yamefadhaika, kwa sababu hawana malisho; naam, makundi ya kondoo yamepata mateso. Ee BWANA, nakulilia wewe; Kwa maana moto umeyala malisho ya nyikani, Na miali ya moto imeteketeza miti yote ya mashamba. Naam, wanyama wa mashamba wanakutwetea wewe; Kwa maana vijito vya maji vimekauka, Na moto umeyateketeza malisho ya nyikani.
Yoeli 1:1-20 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Neno la BWANA ambalo lilimjia Yoeli mwana wa Pethueli. Sikilizeni hili, enyi wazee; sikilizeni, ninyi nyote mnaoishi katika nchi. Je, jambo kama hili lilishawahi kutokea katika siku zenu au katika siku za babu zenu? Waelezeni watoto wenu, na watoto wenu wawaambie watoto wao, na watoto wao kwa kizazi kitakachofuata. Kilichosazwa na kundi la tunutu nzige wakubwa wamekula, kilichosazwa na nzige wakubwa parare wamekula, kilichosazwa na parare madumadu wamekula. Amkeni, enyi walevi, mlie! Pigeni yowe enyi wanywaji wote wa mvinyo, pigeni yowe kwa sababu ya mvinyo mpya, kwa kuwa mmenyangʼanywa kutoka midomoni mwenu. Taifa limevamia nchi yangu, lenye nguvu tena lisilo na idadi; lina meno ya simba, magego ya simba jike. Limeharibu mizabibu yangu na kuangamiza mitini yangu. Limebambua magome yake na kuyatupilia mbali, likayaacha matawi yake yakiwa meupe. Omboleza kama bikira aliyevaa gunia akimwomboleza mume wa ujana wake. Sadaka za nafaka na sadaka za kinywaji zimekatiliwa mbali kutoka nyumba ya BWANA. Makuhani wanaomboleza, wale wanaohudumu mbele za BWANA. Mashamba yameharibiwa, ardhi imekauka; nafaka imeharibiwa, mvinyo mpya umekauka, mafuta yamekoma. Kateni tamaa, enyi wakulima, lieni, enyi mlimao mizabibu; huzunikeni kwa ajili ya ngano na shayiri, kwa sababu mavuno ya shambani yameharibiwa. Mzabibu umekauka na mtini umenyauka; mkomamanga, mtende na mtofaa, miti yote shambani, imekauka. Hakika furaha yote ya mwanadamu imeondoka. Vaeni gunia, enyi makuhani, muomboleze; pigeni yowe, enyi mnaohudumu madhabahuni. Njooni, vaeni gunia usiku kucha, enyi mnaohudumu mbele za Mungu wangu; kwa kuwa sadaka za nafaka na sadaka za kinywaji zimezuiliwa kufika katika nyumba ya Mungu wenu. Tangazeni saumu takatifu; liiteni kusanyiko takatifu. Waiteni wazee na wote wanaoishi katika nchi waende katika nyumba ya BWANA Mungu wenu, wakamlilie BWANA. Ole kwa siku hiyo! Kwa kuwa siku ya BWANA iko karibu; itakuja kama uharibifu kutoka kwa Mwenyezi. Je, chakula hakikukatiliwa mbali mbele ya macho yetu: furaha na shangwe kutoka nyumba ya Mungu wetu? Mbegu zinakauka chini ya mabonge ya udongo. Maghala yameachwa katika uharibifu, maghala ya nafaka yamebomolewa, kwa maana hakuna nafaka. Jinsi gani ngʼombe wanavyolia! Makundi ya mifugo yanahangaika kwa sababu hawana malisho; hata makundi ya kondoo yanateseka. Kwako, Ee BWANA, naita, kwa kuwa moto umeteketeza malisho ya mbugani na miali ya moto imeunguza miti yote shambani. Hata wanyama pori wanakuonea shauku; vijito vya maji vimekauka, na moto umeteketeza malisho yote ya mbugani.