Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Yobu 6:1-30

Yobu 6:1-30 Biblia Habari Njema (BHN)

Yobu akamjibu Elifazi: “Laiti mahangaiko yangu yangepimwa uzani wake, mateso yangu yote yakawekwa katika mizani! Yangekuwa mazito kuliko mchanga wa pwani. Ndio maana maneno yangu ni ya kuropoka! Naam, mishale ya Mungu Mwenye Nguvu imenichoma; nafsi yangu imekunywa sumu yake. Vitisho vya Mungu vimenikabili. Je, pundamwitu hulia akiwa na majani, au ng'ombe akiwa na malisho? Je, kitu kisicho na ladha chaweza kuliwa bila chumvi? Je ute wa yai una utamu wowote? Sina hamu ya kuvigusa vyakula hivyo, hivyo ni vyakula vyangu vichukizavyo.” “Laiti ningejaliwa ombi langu, Mungu akanipatia kile ninachotamani: Kwamba angekuwa radhi kunipondaponda, angenyosha mkono wake anikatilie mbali! Hiyo ingekuwa faraja yangu, ningefurahi katika maumivu yasiyo na huruma. Lakini sina nguvu ya kuweza kuendelea; sijui mwisho wangu utakuwaje, nipate kuvumilia. Je, nguvu zangu ni kama za mawe? Au mwili wangu kama shaba? Kweli kwangu hamna cha kunisaidia; msaada wowote umeondolewa kwangu. “Anayekataa kumhurumia rafiki yake, anakataa kumcha Mungu mwenye nguvu. Rafiki zangu wamenidanganya kama kijito, wamenihadaa kama mitaro isiyo na maji. Ambayo imejaa barafu, na theluji imejificha ndani yake. Lakini wakati wa joto hutoweka, wakati wa hari hubaki mito mikavu. Misafara hupotea njia wakitafuta maji, hupanda nyikani na kufia huko. Misafara ya Tema hutafuta tafuta, wasafiri wa Sheba hutumaini. Huchukizwa kwa kutumaini bure, hufika kwenye vijito hivyo na kuudhika. Nyinyi mmekuwa kama vijito hivyo, mwaona balaa yangu na kuogopa. Je, nimesema mnipe zawadi? Au mnitolee rushwa kwa mali zenu? Au mniokoe makuchani mwa adui? Au mnikomboe mkononi mwa wadhalimu? “Nifundisheni, nami nitanyamaza. Nielewesheni jinsi nilivyokosea. Maneno ya kweli yana nguvu kubwa! Lakini makaripio yenu yananikosoa nini? Je, mnadhani kwamba mwaweza kuyakosoa maneno? Maneno ya mtu aliyekata tamaa ni upepo tu. Nyinyi mnathubutu hata kuwapigia yatima kura; mnawapigia bei hata marafiki zenu! Lakini sasa niangalieni tafadhali. Mimi sitasema uongo mbele yenu. Acheni tafadhali, kusiwe na uovu; acheni sasa, kwani mimi ni mnyofu. Je, mnadhani kwamba nimesema uovu? Je, mnafikiri mimi siyatambui machungu?

Shirikisha
Soma Yobu 6

Yobu 6:1-30 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Ndipo Ayubu akajibu na kusema, Laiti uchungu wangu ungepimwa, Na msiba wangu kutiwa katika mizani pamoja! Kwa kuwa sasa ungekuwa mzito kuliko mchanga wa bahari; Kwa hiyo maneno yangu yamekuwa ya haraka. Kwa kuwa mishale ya huyo Mwenyezi iko ndani yangu, Na roho yangu inainywa sumu yake; Vitisho vya Mungu vimejipanga juu yangu. Je! Huyo punda mwitu hulia akiwa na majani? Au, ng'ombe hulia akiwa malishoni? Je! Kitu kisicho na ladha chaweza kulika bila chumvi? Au je, uto wa yai una tamu iwayo yote? Roho yangu inakataa hata kuvigusa; Kwangu mimi ni kama chakula kichukizacho. Laiti ningepewa haja yangu, Naye Mungu angenipa neno hilo ninalolitamani sana! Kwamba Mungu angekuwa radhi kuniponda; Kwamba angeulegeza mkono wake na kunikatilia mbali! Hapo ndipo ningefarijika hata sasa; Naam, ningejikuza katika maumivu yasiyoniacha; Kwa kuwa sikuyakana maneno yake Mtakatifu. Nguvu zangu ni zipi, hata ningoje? Na mwisho wangu ni nini, hata nisubiri? Je! Nguvu zangu ni nguvu za mawe? Au mwili wangu, je! Ni shaba? Je! Si kwamba sina msaada ndani yangu. Tena kwamba kufanikiwa kumeondolewa mbali nami? Kwake huyo atakaye kuzima roho inapasa atendewe mema na rafiki; Hata kwake huyo aachaye kumcha Mwenyezi. Ndugu zangu wametenda udanganyifu kama kijito cha maji. Mfano wa fumbi la vijito vipitavyo. Vilivyokuwa vyeusi kwa sababu ya barafu, Ambamo theluji hujificha. Wakati vipatapo moto hutoweka; Kukiwako joto, hukoma mahali pao. Misafara isafiriyo kwa njia yao hugeuka; Hukwea kwenda barani, na kupotea. Misafara ya Tema huvitazama, Majeshi ya Sheba huvingojea. Wameudhika kwa sababu walitumaini; Wakaja huku, nao walifadhaika. Kwani sasa ninyi mmekuwa hivyo; Mnaona maafa yangu, na kuogopa. Je! Nilisema, Nipeni? Au, Nitoleeni toleo katika mali yenu? Au, Niokoeni na mkono wa adui? Au, Nikomboeni na mikono ya hao waoneao? Nifunzeni, nami nitanyamaa kimya; Mkanijulishe ni jambo gani nililokosa. Jinsi yafaavyo maneno ya uelekevu! Lakini shutuma zenu, je! Zimeonya nini? Je! Mwafikiri kuyakemea maneno? Maana maneno ya huyo aliyekata tamaa ni kama upepo. Naam, mwapenda kuwapigia kura hao mayatima, Na kufanya biashara ya rafiki yenu. Sasa basi iweni radhi kuniangalia; Kwani hakika sitanena uongo usoni penu. Rudini, nawasihi, lisiwe neno la udhalimu; Naam, rudini tena, neno langu ni la haki. Je! Mna udhalimu ulimini mwangu? Je! Makaakaa yangu hayatambui mambo ya madhara?

Shirikisha
Soma Yobu 6

Yobu 6:1-30 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Ndipo Ayubu akajibu na kusema, Laiti uchungu wangu ungepimwa, Na msiba wangu kutiwa katika mizani pamoja! Kwa kuwa sasa ungekuwa mzito kuliko mchanga wa bahari; Kwa hiyo maneno yangu yamekuwa ya haraka. Kwa kuwa mishale ya huyo Mwenyezi i ndani yangu, Na roho yangu inainywa sumu yake; Vitisho vya Mungu vimejipanga juu yangu. Je! Huyo punda-mwitu hulia akiwa na majani? Au, ng’ombe hulia malishoni? Je! Kitu kisicho na ladha yumkini kulika pasipo chumvi? Au je, uto wa yai una tamu iwayo yote? Roho yangu inakataa hata kuvigusa; Kwangu mimi ni kama chakula kichukizacho. Laiti ningepewa haja yangu, Naye Mungu angenipa neno hilo ninalolitamani sana! Kwamba Mungu angekuwa radhi kuniseta; Kwamba angeulegeza mkono wake na kunikatilia mbali! Hapo ndipo ningefarijika hata sasa; Naam, ningejikuza katika maumivu yasiyoniacha; Kwa kuwa sikuyakana maneno yake Mtakatifu. Nguvu zangu ni zipi, hata ningoje? Na mwisho wangu ni nini, hata nisubiri? Je! Nguvu zangu ni nguvu za mawe? Au mwili wangu, je! Ni shaba? Je! Si kwamba sina msaada ndani yangu. Tena kwamba kufanikiwa kumeondolewa mbali nami? Kwake huyo atakaye kuzima roho inapasa atendewe mema na rafiki; Hata kwake huyo aachaye kumcha Mwenyezi. Ndugu zangu wametenda udanganyifu kama kijito cha maji. Mfano wa fumbi la vijito vipitavyo. Vilivyokuwa vyeusi kwa sababu ya barafu, Ambamo theluji hujificha. Wakati vipatapo moto hutoweka; Kukiwako hari, hukoma mahali pao. Misafara isafiriyo kwa njia yao hugeuka; Hukwea kwenda barani, na kupotea. Misafara ya Tema huvitazama, Majeshi ya Sheba huvingojea. Wametahayari kwa sababu walitumaini; Wakaja huku, nao walifadhaika. Kwani sasa ninyi mmekuwa vivyo; Mwaona jambo la kutisha, mkaogopa. Je! Nilisema, Nipeni? Au, Nitoleeni toleo katika mali yenu? Au, Niokoeni na mkono wa adui? Au, Nikomboeni na mikono ya hao waoneao? Nifunzeni, nami nitanyamaa kimya; Mkanijulishe ni jambo gani nililokosa. Jinsi yafaavyo maneno ya uelekevu! Lakini kuhoji kwenu, je! Kumeonya nini? Je! Mwafikiri kuyakemea maneno? Maana maneno ya huyo aliyekata tamaa ni kama upepo. Naam, mwapenda kuwapigia kura hao mayatima, Na kufanya biashara ya rafiki yenu. Sasa basi iweni radhi kuniangalia; Kwani hakika sitanena uongo usoni penu. Rudini, nawasihi, lisiwe neno la udhalimu; Naam, rudini tena, neno langu ni la haki. Je! Mna udhalimu ulimini mwangu? Je! Makaakaa yangu hayatambui mambo ya madhara?

Shirikisha
Soma Yobu 6

Yobu 6:1-30 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)

Kisha Ayubu akajibu: “Laiti uchungu wangu ungeweza kupimwa, nayo taabu yangu yote ingewekwa kwenye mizani! Kwa kuwa hakika ingekuwa nzito kuliko mchanga wa bahari zote, kwa hiyo si ajabu maneno yangu yamekuwa ya haraka. Mishale ya Mwenyezi iko ndani yangu, roho yangu inakunywa sumu yake; vitisho vya Mungu vimejipanga dhidi yangu. Je, punda-mwitu hulia akiwa na majani, au fahali hulia akiwa na chakula? Je, chakula kisicho na ladha huliwa bila chumvi, au upo utamu katika ute mweupe wa yai? Ninakataa kuvigusa; vyakula vya aina hii hunichukiza. “Laiti ningepata haja yangu, kwamba Mungu angenijalia hilo nililotarajia, kwamba Mungu angekuwa radhi kuniponda, kuuachia mkono wake na kunikatilia mbali! Ndipo bado ningekuwa na hii faraja, furaha yangu katika maumivu makali: kwamba sikuwa nimeyakana maneno yake yeye Aliye Mtakatifu. “Nina nguvu gani, hata niendelee kutumaini? Matazamio yangu ni nini, hata niendelee kuwa mvumilivu? Je, mimi nina nguvu za jiwe? Je, mwili wangu ni shaba? Je, ninao uwezo wowote wa kujisaidia mimi mwenyewe, wakati mafanikio yamefukuziwa mbali nami? “Mtu anayekata tamaa angetazamia moyo wa kujitoa wa rafiki zake, hata akiacha uchaji wa Mwenyezi. Lakini ndugu zangu sio wa kutegemewa, ni kama vijito vya msimu, ni kama vijito ambavyo hufurika wakati vimefunikwa barafu iyeyukayo, ambavyo hujazwa na theluji inayoyeyuka, lakini hukauka majira ya ukame, na wakati wa hari hutoweka katika mikondo yake. Misafara hugeuka kutoka njia zake; hukwea kwenda kwenye nchi ya ukiwa na kuangamia. Misafara ya Tema inatafuta maji, wafanyabiashara wa Sheba wanaosafiri hutazama kwa matarajio. Wamedhikika, kwa sababu walikuwa na matumaini; wanafika huko, lakini wanahuzunika kwa kukosa walichotarajia. Sasa nanyi mmethibitika kwamba hamna msaada wowote; mnaona jambo la kutisha, nanyi mnaogopa. Je, nimewahi kusema, ‘Toeni kitu kwa ajili yangu, au mnilipie fidia kutoka mali yenu, au niokoeni mikononi mwa adui, au nikomboeni kutoka makucha ya wasio na huruma’? “Nifundisheni, nami nitakaa kimya; nionesheni nilikokosea. Tazama yalivyo ya kuumiza maneno ya kweli! Lakini mabishano yenu yanathibitisha nini? Je, mna maana ya kuyasahihisha ninayosema, na kuyafanya maneno ya mtu anayekata tamaa kama upepo? Mngeweza hata kupiga kura kwa ajili ya yatima, na kubadilishana rafiki yenu na mali. “Lakini sasa kuweni na huruma mkaniangalie mimi. Je, ningeweza kusema uongo mbele zenu? Tulizeni hasira, msiwe wadhalimu; angalieni tena, kwa maana nimehatarisha uadilifu wangu. Je, pana uovu wowote mdomoni mwangu? Je, kinywa changu hakiwezi kupambanua hila?

Shirikisha
Soma Yobu 6