Yobu 32:1-10
Yobu 32:1-10 Biblia Habari Njema (BHN)
Basi hawa watu watatu: Elifazi, Bildadi na Sofari, wakaacha kumjibu Yobu kwa vile alijiona kuwa mwema. Ndipo Elihu, mwana wa Barakeli, wa kabila la Buzi wa ukoo wa Rama, akakasirika. Alimkasirikia Yobu kwa sababu Yobu alijiona yeye mwadilifu na sio Mungu. Pia, aliwakasirikia rafiki watatu wa Yobu kwa sababu hawakuwa na la kumjibu Yobu, na hivyo kuonesha kwamba Mungu amekosa. Elihu alikuwa amekaa kimya wakati hao wazee waliposema na Yobu kwa kuwa yeye alikuwa kijana kuliko wao. Lakini alipoona hao watu watatu wameshindwa kumjibu Yobu, aliwaka hasira. Basi, Elihu mwana wa Barakeli, wa kabila la Buzi akaanza kusema: “Mimi ni kijana, nyinyi ni wazee zaidi; kwa hiyo niliogopa kuwaambieni mawazo yangu. Nilisema moyoni: ‘Waache wenye siku nyingi waseme, wenye miaka mingi wafundishe hekima.’ Lakini hiyo roho iliyomo ndani ya mtu, hiyo pumzi ya Mungu Mwenye Nguvu, ndio inayomwezesha mwanadamu kufahamu. Si lazima kuwa mzee ili uwe na hekima wala wazee siyo wenye kufahamu lililo sawa. Kwa hiyo nasema, ‘Nisikilizeni, acheni nami nitoe maoni yangu.’
Yobu 32:1-10 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Basi hao watu watatu wakaacha kumjibu Ayubu, kwa sababu alikuwa mwenye haki machoni pake mwenyewe. Ndipo zikawaka hasira za huyo Elihu mwana wa Barakeli, Mbuzi, katika jamaa ya Ramu, juu ya Ayubu, kwa sababu alikuwa amejipa haki mwenyewe zaidi ya Mungu. Tena hasira zake ziliwaka juu ya hao rafiki zake watatu kwa sababu hawakupata jawabu, lakini wamemhukumia Ayubu makosa. Basi huyo Elihu alikuwa anangoja ili anene na Ayubu, kwa sababu hao wengine walikuwa wazee kuliko yeye. Hata Elihu alipoona kuwa hapana jawabu katika vinywa vya watu hao watatu, hasira zake ziliwaka. Basi Elihu mwana wa Barakeli, Mbuzi, akajibu, na kusema, Mimi ni kijana, na ninyi ni wazee sana; Kwa hiyo nilijizuia, nisithubutu kuwaonesha nionavyo. Nilisema, Yafaa siku ziseme, Na wingi wa miaka ufundishe hekima. Lakini hakika imo roho ndani ya mwanadamu, Na pumzi ya Mwenyezi ndiyo impayo ufahamu. Sio wakuu walio wenye hekima, Wala sio wazee watambuao haki. Basi nilisema, Nisikilizeni mimi; Mimi nami nitawaonesha nionavyo.
Yobu 32:1-10 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Basi hao watu watatu wakaacha kumjibu Ayubu, kwa sababu alikuwa mwenye haki machoni pake mwenyewe. Ndipo zikawaka hasira za huyo Elihu mwana wa Barakeli, Mbuzi, katika jamaa ya Ramu, juu ya Ayubu, kwa sababu alikuwa amejipa haki mwenyewe zaidi ya Mungu. Tena hasira zake ziliwaka juu ya hao rafiki zake watatu kwa sababu hawakupata jawabu, lakini wamemhukumia Ayubu makosa. Basi huyo Elihu alikuwa anangoja ili anene na Ayubu, kwa sababu hao wengine walikuwa wazee kuliko yeye. Hata Elihu alipoona kuwa hapana jawabu katika vinywa vya watu hao watatu, hasira zake ziliwaka. Basi Elihu mwana wa Barakeli, Mbuzi, akajibu, na kusema, Mimi ni kijana, na ninyi ni wazee sana; Kwa hiyo nilijizuia, nisithubutu kuwaonyesha nionavyo. Nilisema, Yafaa siku ziseme, Na wingi wa miaka ufundishe hekima. Lakini imo roho ndani ya mwanadamu, Na pumzi za Mwenyezi huwapa akili. Sio wakuu walio wenye akili, Wala sio wazee watambuao hukumu. Basi nilisema, Nisikilizeni mimi; Mimi nami nitawaonyesha nionavyo.
Yobu 32:1-10 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Basi watu hawa watatu wakaacha kumjibu Ayubu, kwa kuwa alikuwa mwadilifu machoni pake mwenyewe. Lakini Elihu mwana wa Barakeli, wa kabila la Buzi wa jamaa ya Ramu, akamkasirikia sana Ayubu, kwa sababu ya kujihesabia haki mwenyewe badala ya Mungu. Pia aliwakasirikia hao rafiki watatu wa Ayubu, kwa sababu hawakuweza kupata njia ya kuthibitisha ya kuwa hayo maneno ya Ayubu hayakuwa ya kweli, nao bado walikuwa wamemlaumu. Basi Elihu alikuwa amesubiri kwanza waongee na Ayubu, kwa sababu walikuwa na umri mkubwa kuliko yeye. Lakini alipoona watu hao watatu hawakuwa na kitu zaidi cha kusema, hasira yake ikaamka. Basi Elihu mwana wa Barakeli wa kabila la Buzi akasema: “Mimi ni mdogo kwa umri, nanyi ni wazee; ndiyo sababu niliogopa, sikuthubutu kuwaambia kile ninachojua. Nilifikiri, ‘Yafaa umri useme, nao wingi wa miaka ungefundisha hekima.’ Lakini ni Roho iliyo ndani ya mwanadamu, pumzi ya Mwenyezi, ndiyo impayo ufahamu. Sio wazee peke yao walio na hekima, sio wenye umri mkubwa peke yao wanaofahamu lililo sawa. “Kwa hiyo nasema: Nisikilizeni; mimi nami nitawaambia ninalolijua.