Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Yobu 3:1-26

Yobu 3:1-26 Biblia Habari Njema (BHN)

Hatimaye Yobu aliamua kuongea, akailaani siku aliyozaliwa. Yobu akasema: “Ilaaniwe siku ile niliyozaliwa; usiku ule iliposemwa, ‘Mwana amechukuliwa mimba’ Siku hiyo na iwe giza! Mungu juu asijishughulishe nayo! Wala nuru yoyote isiiangaze! Mauzauza na giza nene yaikumbe, mawingu mazito yaifunike. Giza la mchana liitishe! Usiku huo giza nene liukumbe! Usihesabiwe katika siku za mwaka, wala usitiwe katika idadi ya siku za mwezi. Naam, usiku huo uwe tasa, sauti ya furaha isiingie humo. Walozi wa siku waulaani, watu stadi wa kuligutua dude Lewiyathani waulaani! Nyota zake za pambazuko zififie, utamani kupata mwanga, lakini usipate, wala usione nuru ya pambazuko. Maana usiku huo haukulifunga tumbo la mama, wala kuficha taabu nisizione. Mbona sikufa nilipozaliwa, nikatoka tumboni na kutoweka? Kwa nini mama yangu alinizaa? Kwa nini nikapata kunyonya? Maana ningekuwa nimezikwa, kimya; ningekuwa nimelazwa na kupumzika, pamoja na wafalme na watawala wa dunia, waliojijengea upya magofu yao; ningekuwa pamoja na wakuu waliokuwa na dhahabu, waliojaza nyumba zao fedha tele. Au, mbona sikuwa kama mimba iliyoharibika, naam, kama mtoto aliyezaliwa mfu? Huko kwa wafu waovu hawamsumbui mtu, huko wachovu hupumzika. Huko wafungwa hustarehe pamoja, hawaisikii kamwe sauti ya mnyapara. Wakubwa na wadogo wako huko, nao watumwa wamepata uhuru mbali na bwana zao. Ya nini kumjalia nuru yule aliye taabuni; na uhai yule aliye na huzuni moyoni? Mtu atamaniye kifo lakini hafi; hutafuta kifo kuliko hazina iliyofichika. Mtu kama huyo atashangilia mno na kufurahi, atafurahi atakapokufa na kuzikwa! Ya nini kumjalia uhai mtu ambaye njia zake zimefungwa, mtu ambaye Mungu amemwekea kizuizi? Kwa maana kusononeka ndio mkate wangu, kupiga kite kwangu kunatiririka mithili ya maji. Kile ninachokiogopa kimenipata, ninachokihofia ndicho kilichonikumba. Sina amani wala utulivu; sipumziki, taabu imenijia.”

Shirikisha
Soma Yobu 3

Yobu 3:1-26 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Baada ya hayo Ayubu akafunua kinywa chake, na kuilaani siku yake. Ayubu akajibu, na kusema; Na ipotelee mbali ile siku niliyozaliwa mimi, Na ule usiku uliosema, Mtoto wa kiume ametungishwa mimba. Siku hiyo na iwe giza; Mungu asiiangalie toka juu, Wala mwanga usiiangazie. Ishikwe na giza, giza tupu, kuwa yake; Wingu na likae juu yake; Chote kiifanyacho siku kuwa giza na kiitishe. Tena usiku huo, na ushikwe na giza kuu; Usihesabiwe katika siku za mwaka; Wala kutiwa katika hesabu ya miezi. Tazama, usiku huo na uwe tasa; Wala isiwe ndani yake sauti ya shangwe. Na waulaani hao waulaanio mchana, Hao walio tayari kumwamsha huyo Lewiathani. Nyota za mapambazuko yake na ziwe giza; Na utafute mwanga lakini usiupate; Wala usiyaone mapambazuko; Kwa sababu haukuifunga milango ya tumbo la mamangu. Wala kunifichia taabu machoni. Mbona mimi sikufa wakati nikizaliwa? Mbona nisitoe roho hapo nilipotoka tumboni? Mbona pawe na magoti ya kunipokea? Au hayo maziwa, hata nikanyonya? Maana hapo ningelala na kutulia; Ningelala usingizi; na kupata kupumzika; Pamoja na wafalme na washauri wa dunia, Hao waliojijengea maganjoni; Au pamoja na wakuu wenye dhahabu, Waliozijaza nyumba zao fedha; Au, mbona kuzikwa kama mimba iliyoharibika, nisingekuwako; Kama wachanga wasiouona mwanga kabisa. Huko waovu huacha kusumbua; Huko nako hao waliochoka wanapumzika. Huko wafungwa wanastarehe pamoja; Hawaisikii sauti yake msimamizi. Wakuu na wadogo wako huko; Mtumishi yuko huru kwa bwana wake. Mbona yeye aliye mashakani kupewa mwanga, Na hao wenye uchungu rohoni kupewa uhai; Ambao wangojea mauti, lakini hawayapati; Na kuyachimbulia kuliko watafutavyo hazina iliyostirika; Ambao wafurahi mno, Na kushangilia watakapoliona kaburi? Kwa nini mtu aliyezibiwa njia kupewa mwanga, Ambaye Mungu amemzingira kwa ukigo? Kwani kuugua kwangu kwaja kana kwamba ni chakula, Na kunguruma kwangu kumemiminika kama maji. Maana jambo hilo nichalo hunipata, Nalo linitialo hofu hunijia. Mimi sioni raha, wala situlii, wala kupumzika; Lakini taabu huja.

Shirikisha
Soma Yobu 3

Yobu 3:1-26 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Baada ya hayo Ayubu akafunua kinywa chake, na kuilaani siku yake. Ayubu akajibu, na kusema; Na ipotelee mbali ile siku niliyozaliwa mimi, Na ule usiku uliosema, Mtoto mume ametungishwa mimba. Siku hiyo na iwe giza; Mungu asiiangalie toka juu, Wala mwanga usiiangazie. Ishikwe na giza, giza tupu, kuwa yake; Wingu na likae juu yake; Chote kiifanyacho siku kuwa giza na kiitishe. Tena usiku huo, na ushikwe na giza kuu; Usihesabiwe katika siku za mwaka; Wala kutiwa katika hesabu ya miezi. Tazama, usiku huo na uwe tasa; Wala isiwe ndani yake sauti ya shangwe. Na waulaani hao waulaanio mchana, Hao walio tayari kumwamsha huyo lewiathani. Nyota za mapambazuko yake na ziwe giza; Na utafute mwanga lakini usiupate; Wala usiyaone makope ya asubuhi; Kwa sababu haukuifunga milango ya tumbo la mamangu. Wala kunifichia taabu machoni. Mbona si kufa mimi tokea mimbani? Mbona nisitoe roho hapo nilipotoka tumboni? Mbona hayo magoti kunipokea? Au hayo maziwa, hata nikanyonya? Maana hapo ningelala na kutulia; Ningelala usingizi; na kupata kupumzika; Pamoja na wafalme na washauri wa dunia, Hao waliojijengea maganjoni; Au pamoja na wakuu wenye dhahabu, Waliozijaza fedha nyumba zao; Au, kama kuzikwa mimba iliyoharibika, nisingekuwako; Kama wachanga wasiouona mwanga kabisa. Huko waovu huacha kusumbua; Huko nako hao waliochoka wapumzika Huko wafungwa waona raha pamoja; Hawaisikii sauti yake msimamizi. Wakuu na wadogo wako huko; Mtumishi yu huru kwa bwana wake. Mbona yeye aliye mashakani kupewa mwanga, Na hao wenye uchungu rohoni kupewa uhai; Ambao wangojea mauti, lakini hawayapati; Na kuyachimbulia zaidi ya kutafuta hazina iliyostirika; Ambao wafurahi mno, Na kushangilia watakapoliona kaburi? Kwa nini mtu aliyezibiwa njia kupewa mwanga, Ambaye Mungu amemzingira kwa ukingo? Kwani kuugua kwangu kwaja kana kwamba ni chakula, Na kunguruma kwangu kumemiminika kama maji. Maana jambo hilo nichalo hunipata, Nalo linitialo hofu hunijilia. Mimi sioni raha, wala situlii, wala kupumzika; Lakini huja taabu.

Shirikisha
Soma Yobu 3

Yobu 3:1-26 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)

Baada ya jambo hili, Ayubu akafumbua kinywa chake na kuilaani siku ya kuzaliwa kwake. Kisha akasema: “Siku ya kuzaliwa kwangu na ipotelee mbali, na usiku ule iliposemekana, ‘Mtoto wa kiume amezaliwa!’ Siku ile na iwe giza; Mungu juu na asiiangalie; nayo nuru isiiangazie. Giza na kivuli kikuu viikalie tena; wingu na likae juu yake; weusi na uifunike nuru yake. Usiku ule na ushikwe na giza nene; usihesabiwe katika siku za mwaka, wala usihesabiwe katika siku za mwezi wowote. Usiku ule na uwe tasa; sauti ya furaha na isisikike ndani yake. Wale wanaozilaani siku na wailaani hiyo siku, wale walio tayari kumwamsha Lewiathani. Nyota zake za alfajiri na ziwe giza; nao ungojee mwanga bila mafanikio, wala usiione miali ya mapambazuko, kwa sababu huo usiku haukunifungia mlango wa tumbo la mama yangu, ili kuyaficha macho yangu kutokana na taabu. “Kwa nini sikuangamia wakati wa kuzaliwa? Kwa nini sikufa nilipokuwa ninatoka tumboni? Kwa nini pakawa na magoti ya kunipokea na matiti ili nipate kunyonyeshwa? Kwa maana sasa ningekuwa nimepumzika kwa amani. Ningekuwa nimelala na kupumzika pamoja na wafalme na washauri wa dunia, waliojijengea mahali ambapo sasa ni magofu, pamoja na watawala waliokuwa na dhahabu, waliozijaza nyumba zao kwa fedha. Au kwa nini sikufichwa ardhini kama mtoto aliyezaliwa mfu, kama mtoto mchanga ambaye kamwe hakuuona mwanga? Huko waovu huacha kusumbua na huko waliochoka hupumzika. Wafungwa nao hufurahia utulivu wao, hawasikii tena sauti ya kukemea ya kiongozi wa watumwa. Wadogo kwa wakubwa wamo humo, na mtumwa ameachiwa huru kutoka kwa bwana wake. “Mbona nuru inawaangazia wale walio taabuni, na hao wenye uchungu kupewa uhai, wale wanaotamani kifo ambacho hakiji, wale wanaotafuta kufa zaidi ya kutafuta hazina iliyofichwa, ambao hujawa na furaha, na hushangilia wanapofika kaburini? Kwa nini uhai hupewa mtu ambaye njia yake imefichika, ambaye Mungu amemzingira? Kwa maana kulia kwangu kwa uchungu kwanijia badala ya chakula; kusononeka kwangu kunamwagika kama maji. Lile nililokuwa nikiogopa limenijia; lile nililokuwa nikihofia limenipata. Sina amani, wala utulivu; sina pumziko, bali taabu tu.”

Shirikisha
Soma Yobu 3