Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Yobu 22:1-30

Yobu 22:1-30 Biblia Habari Njema (BHN)

Kisha Elifazi, Mtemani, akajibu Yobu: “Je, binadamu anafaa chochote kwa Mungu? Kwa kweli mwenye hekima anajifaidi mwenyewe tu. Je, unadhani wamfurahisha Mungu kwa kuwa mnyofu? Au anapata faida gani kama huna hatia? Unadhani anakurudi na kukuhukumu kwa sababu wewe unamheshimu? La! Uovu wako ni mkubwa mno! Ubaya wako hauna mwisho! Wewe umemnyanganya ndugu yako nguo ya rehani; umemchukulia nguo hiyo moja aliyokuwa nayo. Umewanyima maji wale waliokuwa wamechoka; umewanyima chakula wale walio na njaa. Umemruhusu mwenye cheo kuchukua ardhi yote; umemwacha anayependelewa aishi humo. Umewaacha wajane waende mikono mitupu; umewanyima yatima uwezo wao. Kwa hiyo mitego imekuzunguka pande zote, hofu ya ghafla imekuvamia. Giza limekuangukia usione kitu; mafuriko ya maji yamekufunika. Twajua Mungu yuko huko juu mbinguni. Tazama nyota za juu kabisa zilivyo mbali! Lakini wewe wasema: ‘Mungu ajua nini? Je, aweza kupenya mawingu akatoa hukumu? Mawingu mazito yamemzunguka asipate kuona yeye hutembea nje ya anga la dunia!’ “Je, umeamua kufuata njia za zamani ambazo watu waovu wamezifuata? Hao walifagiliwa kabla ya wakati wao, misingi yao ilikumbwa mbali na maji. Hao ndio waliomwambia Mungu, ‘Achana nasi!’ Na ‘Wewe Mungu Mwenye Nguvu waweza nini juu yetu?’ Lakini Mungu ndiye aliyejaza nyumba zao fanaka, lakini walimweka mbali na mipango yao! Wanyofu huona na kufurahi, wasio na hatia huwacheka na kuwadharau, Wanasema ama kweli maadui zetu wameangamizwa, na walichobakiza kimeteketezwa kwa moto. “Sasa, Yobu, kubaliana na Mungu uwe na amani, na hapo mema yatakujia. Pokea mafundisho kutoka kwake; na yaweke maneno yake moyoni mwako. Ukimrudia Mungu na kunyenyekea, ukiondoa uovu mbali na makao yako, ukitupilia mbali mali yako, ukaitupa dhahabu ya Ofiri ukingoni mwa kijito, Mungu Mwenye Nguvu akawa ndio dhahabu yako, na fedha yako ya thamani; basi, ndipo utakapomfurahia Mungu mwenye nguvu na kutazama kwa matumaini; utamwomba naye atakusikiliza, nawe utazitimiza nadhiri zako. Chochote utakachoamua kitafanikiwa, na mwanga utaziangazia njia zako. Maana, Mungu huwaporomosha wenye majivuno, lakini huwaokoa wanyenyekevu. Yeye humwokoa mtu asiye na hatia; wewe utaokolewa kwa matendo yako mema.”

Shirikisha
Soma Yobu 22

Yobu 22:1-30 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Ndipo huyo Elifazi Mtemani akajibu, na kusema, Je! Yumkini mtu awaye yote kumfaa Mungu? Hakika yeye aliye na hekima hujifaa mwenyewe. Je! Mwenyezi hupata furaha katika wewe kuwa mwenye haki? Au je, ni faida kwake, kwamba wafanya njia zako kuwa timilifu? Je! Ni kwa wewe kumcha yeye anakukemea? Na kuingia hukumuni nawe? Je! Uovu wako si mkuu? Wala maovu yako hayana mwisho. Kwa kuwa umetwaa dhamana kwa nduguyo bure, Na kuwavua nguo zao walio uchi. Hukumpa maji ya kunywa huyo aliyechoka, Nawe umemnyima chakula huyo mwenye njaa. Lakini huyo shujaa, nchi ilikuwa yake; Na huyo mwenye kusifiwa, yeye aliikaa. Umewafukuza wanawake wajane bila chochote, Na mikono ya mayatima imevunjwa. Kwa hiyo umezungukwa na mitego, Na hofu ya ghafla yakutaabisha, Au je! Huoni giza, Na maji mengi yanayokufunika? Je! Mungu hayuko mbinguni juu? Tena tazama umbali wa nyota, jinsi zilivyo juu! Nawe wasema, Mungu anajua nini? Je! Aweza kuamua kati ya giza kuu? Mawingu mazito ni kifuniko chake, hata asione; Naye yuatembea juu ya kuba ya mbingu. Je! Utaifuata njia ya zamani Waliyoikanyaga watu waovu? Ambao walinyakuliwa kabla ya wakati wao, Msingi wao ulimwagika kama kijito cha maji; Waliomwambia Mungu, Tuondokee; Tena, Huyo Mwenyezi aweza kutufanyia nini? Naye ndiye aliyezijaza nyumba zao vitu vyema; Lakini mashauri ya waovu na yawe mbali nami. Wenye haki huyaona hayo wakafurahi; Nao wasio na hatia huwacheka; Wasema, Hakika hao waliotuinukia wamekatiliwa mbali, Na mabaki yao moto umeyateketeza. Mjue sana Mungu, ili uwe na amani; Ndivyo mema yatakavyokujia. Uyapokee, tafadhali, mafunzo yatokayo kinywani mwake, Na maneno yake yaweke moyoni mwako. Ukimrudia Mwenyezi, utajengwa; Ukiuondoa udhalimu mbali na hema yako. Nawe hazina zako ziweke mchangani, Na dhahabu ya Ofiri iweke kati ya mawe ya vijito; Naye Mwenyezi atakuwa hazina yako, Atakuwa ni fedha ya thamani kwako. Kwani ndipo utakapojifurahisha katika Mwenyezi, Na kuinua uso wako kumwelekea Mungu. Utamwomba yeye naye atakusikia; Nawe utazitimiliza nadhiri zako. Nawe utakusudia neno, nalo litathibitika kwako; Na mwanga utaziangazia njia zako. Hapo watakapokuangusha, utasema, Kuna kuinuka tena; Naye mnyenyekevu Mungu atamwokoa. Atamwokoa na huyo asiye na hatia; Naam, utaokolewa kwa sababu ya usafi wa mikono yako.

Shirikisha
Soma Yobu 22

Yobu 22:1-30 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Ndipo huyo Elifazi Mtemani akajibu, na kusema, Je! Yumkini mtu awaye yote kumfaa Mungu? Hakika yeye aliye na hekima hujifaa mwenyewe. Je! Mwenyezi hupata furaha katika wewe kuwa mwenye haki? Au je, ni faida kwake, kwamba wafanya njia zako kuwa timilifu? Je! Ni kwa wewe kumcha yeye anakukemea? Na kuingia hukumuni nawe? Je! Uovu wako si mkuu? Wala maovu yako hayana mwisho. Kwa kuwa umetwaa dhamana kwa nduguyo bure, Na kuwavua nguo zao walio uchi. Hukumpa maji ya kunywa huyo aliyechoka, Nawe umemnyima chakula huyo mwenye njaa. Lakini huyo shujaa, nchi ilikuwa yake; Na huyo mwenye kusifiwa, yeye aliikaa. Umewafukuza wanawake wajane hali ya utupu, Na mikono ya mayatima imevunjwa. Kwa hiyo umezungukwa na mitego, Na hofu ya ghafula yakutaabisha, Au je! Huoni giza, Na maji mengi yanayokufunika? Je! Mungu hayuko mbinguni juu? Tena tazama umbali wa nyota, jinsi zilivyo juu! Nawe wasema, Mungu anajua nini? Je! Aweza kuamua kati ya giza kuu? Mawingu mazito ni kifuniko chake, hata asione; Naye yuatembea juu ya kuba ya mbingu. Je! Utaiandama njia ya zamani Waliyoikanyaga watu waovu? Ambao walinyakuliwa kabla ya wakati wao, Msingi wao ulimwagika kama kijito cha maji; Waliomwambia Mungu, Tuondokee; Tena, Huyo Mwenyezi aweza kutufanyia nini? Naye ndiye aliyezijaza nyumba zao vitu vyema; Lakini mashauri ya waovu na yawe mbali nami. Wenye haki huyaona hayo wakafurahi; Nao wasio na hatia huwacheka; Wasema, Hakika hao waliotuinukia wamekatiliwa mbali, Na mabaki yao moto umeyateketeza. Mjue sana Mungu, ili uwe na amani; Ndivyo mema yatakavyokujia. Uyapokee, tafadhali, mafunzo yatokayo kinywani mwake, Na maneno yake yaweke moyoni mwako. Ukimrudia Mwenyezi, utajengwa; Ukiuondoa udhalimu mbali na hema yako. Nawe hazina zako ziweke mchangani, Na dhahabu ya Ofiri iweke kati ya mawe ya vijito; Naye Mwenyezi atakuwa hazina yako, Atakuwa ni fedha ya thamani kwako. Kwani ndipo utakapojifurahisha katika Mwenyezi, Na kuinua uso wako kumwelekea Mungu. Utamwomba yeye naye atakusikia; Nawe utazitimiliza nadhiri zako. Nawe utakusudia neno, nalo litathibitika kwako; Na mwanga utaziangazia njia zako. Hapo watakapokuangusha, utasema, Kuna kuinuka tena; Naye mnyenyekevu Mungu atamwokoa. Atamwokoa na huyo asiye na hatia; Naam, utaokolewa kwa sababu ya usafi wa mikono yako.

Shirikisha
Soma Yobu 22

Yobu 22:1-30 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)

Ndipo Elifazi Mtemani akajibu: “Je, mwanadamu aweza kuwa wa faida kwa Mungu? Je, hata mtu mwenye hekima aweza kumfaidi? Je, Mwenyezi angefurahia nini kama ungekuwa mwadilifu? Au je, yeye angepata faida gani kama njia zako zingekuwa kamilifu? “Je, ni kwa ajili ya utaua wako ndiyo maana anakukemea na kuleta mashtaka dhidi yako? Je, uovu wako si mkuu? Dhambi zako si hazina mwisho? Umedai dhamana kwa ndugu zako bila sababu; umewavua watu nguo zao, ukawaacha uchi. Hukumpa maji aliyechoka, nawe ulimnyima chakula mwenye njaa, ingawa ulikuwa mtu mwenye uwezo ukimiliki nchi: mtu uliyeheshimiwa, ukiishi ndani yake. Umewafukuza wajane mikono mitupu na kuzivunja nguvu za yatima. Ndiyo sababu mitego imekuzunguka pande zote, hatari ya ghafula inakutia hofu, ndiyo sababu ni giza sana huwezi kuona, tena ndiyo sababu mafuriko ya maji yamekufunika. “Je, Mungu hayuko katika mbingu za juu? Juu kuliko nyota zilizo juu sana! Hivyo wewe wasema, ‘Mungu anajua nini?’ Je, yeye huhukumu katika giza kama hilo? Mawingu mazito ni pazia lake, hivyo hatuoni sisi atembeapo juu ya anga la dunia. Je, utaifuata njia ya zamani, ambayo watu waovu waliikanyaga? Waliondolewa kabla ya wakati wao, misingi yao ikachukuliwa na mafuriko. Walimwambia Mungu, ‘Tuache sisi! Huyo Mwenyezi aweza kutufanyia nini?’ Lakini ndiye alizijaza nyumba zao na vitu vizuri, hivyo ninajitenga mbali na mashauri ya waovu. “Wenye haki wanaona maangamizi yao na kufurahi, nao wasio na hatia huwadhihaki, wakisema, ‘Hakika adui zetu wameangamizwa, nao moto umeteketeza mali yao.’ “Mjue sana Mungu ili uwe na amani, ndipo mema yatakapokujia. Uyapokee mafundisho toka kinywani mwake, na maneno yake uyaweke moyoni mwako. Ukimrudia Mwenyezi, utarudishwa upya: Ukiuondoa uovu uwe mbali na hema lako, kama dhahabu yako ukiihesabu kama mavumbi, dhahabu yako ya Ofiri kama miamba ya mabondeni, ndipo Mwenyezi atakuwa dhahabu yako, naye atakuwa fedha yako iliyo bora. Hakika ndipo utakapojifurahisha kwa Mwenyezi, nawe utamwinulia Mungu uso wako. Utamwomba yeye, naye atakusikia, nawe utazitimiza nadhiri zako. Utakusudia jambo nalo litatendeka, nao mwanga utaangazia njia zako. Watu watakaposhushwa, nawe ukasema, ‘Wainue!’ ndipo atamwokoa aliyevunjika moyo. Atamwokoa hata yule ambaye ana hatia, ataokolewa kwa sababu ya usafi wa mikono yako.”

Shirikisha
Soma Yobu 22