Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Yobu 20:1-29

Yobu 20:1-29 Biblia Habari Njema (BHN)

Kisha Sofari, Mnaamathi, akajibu: “Fikira zangu zanifanya nikujibu, wala siwezi kujizuia tena. Nasikia maonyo nisiyoweza kuvumilia, lakini akili yangu yanisukuma nijibu. “Wewe labda umesahau jambo hili: Kwamba tangu zamani Mungu alipomuumba mtu duniani, mwovu atajiona ameshinda kwa muda tu, furaha yake asiyemcha Mungu ni ya muda mfupi tu! Mwovu aweza kufana hata kufikia mbingu, kichwa chake kikafika kwenye mawingu, lakini atatupiliwa mbali kama mavi yake. Waliopata kumjua watajiuliza: ‘Yuko wapi?’ Atatoweka kama ndoto, asionekane tena, atafutika kama maono ya usiku. Aliyemwona, hatamwona tena, wala pale alipoishi hapatatambuliwa tena. Yeye mwenyewe itambidi kurudisha mali yake yote, watoto wake wataomba huruma kwa maskini. Japo alijisikia amejaa nguvu za ujana, lakini zote zitalala pamoja naye mavumbini. “Mdomoni mwake uovu ni mtamu kama sukari, anauficha chini ya ulimi wake; hataki kabisa kuuachilia, bali anaushikilia kinywani mwake. Lakini ufikapo tumboni huwa mchungu, mkali kama sumu ya nyoka. Mwovu humeza mali haramu na kuitapika; Mungu huitoa tumboni mwake. Anachonyonya mtu mwovu ni sumu ya nyoka; atauawa kwa kuumwa na nyoka. Hataishi kuiona mitiririko ya fanaka, wala vijito vya mafanikio na utajiri. Matunda ya jasho lake atayaachilia, hatakuwa na uwezo wa kuyaonja, kwa sababu amewaangamiza maskini na kuwaacha, amenyakua nyumba ambazo hakuzijenga. “Kwa vile ulafi wake hauna mwisho, hataweza kuokoa chochote anachothamini. Baada ya kula hakuacha hata makombo, kwa hiyo fanaka yake yote haitadumu. Kileleni mwa fanaka dhiki itamvamia, balaa itamkumba kwa nguvu zote. Akiwa anajishughulisha kushibisha tumbo, Mungu atamletea ghadhabu yake imtiririkie kama chakula chake. Labda ataweza kuepa upanga wa chuma, kumbe atachomwa na upanga wa shaba. Mshale utachomolewa kutoka mwilini mwake; ncha yake itatolewa mgongoni mwake ikingaa, vitisho vya kifo vitamvamia. Hazina zake zitaharibiwa, moto wa ajabu utamteketeza; kilichobaki nyumbani mwake kitateketezwa. Mbingu zitaufichua uovu wake, dunia itajitokeza kumshutumu. Mali zake zitanyakuliwa katika siku ya ghadhabu ya Mungu. Hicho ndicho apewacho mtu mwovu kutoka kwa Mungu, ndicho mwovu alichopangiwa na Mungu.”

Shirikisha
Soma Yobu 20

Yobu 20:1-29 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Ndipo Sofari, Mnaamathi, akajibu, na kusema, Kwa hiyo mawazo yangu hunipa jawabu, Kwa ajili ya haraka niliyo nayo ndani yangu. Nimesikia maonyo yanayonitahayarisha, Nayo roho ya ufahamu wangu hunijibu. Je! Hujui neno hili tangu zamani za kale, Tangu wanadamu kuwekwa juu ya nchi, Ya kuwa shangwe ya waovu ni kwa muda kidogo, Na furaha ya wapotovu ni ya dakika moja tu? Ujapopanda ukuu wake mpaka mbinguni, Na kichwa chake kufikia mawinguni; Hata hivyo ataangamia milele kama mavi yake mwenyewe; Hao waliomwona watasema, Yuko wapi? Ataruka mfano wa ndoto, asionekane; Naam, atafukuzwa kama maono ya usiku, Jicho lililomwona halitamwona tena; Wala mahali pake hapatamtazama tena. Watoto wake watataka fadhili kwa maskini, Na mikono yake itarudisha mali yake. Mifupa yake imejaa ujana wake, Lakini utalala nchi naye mavumbini. Ingawa uovu ni mtamu kinywani mwake, Ingawa auficha chini ya ulimi wake; Ingawa hawataki kuuachilia uende zake. Naye huushikilia kinywani mwake; Hata hivyo chakula chake matumboni mwake kinabadilika, Kimekuwa ni nyongo za majoka ndani yake. Amemeza mali, naye atayatapika tena; Mungu atayatoa tumboni mwake. Atanyonya sumu ya majoka; Na ulimi wa fira utamwua. Hataiangalia hiyo mito ya maji, Vile vijito vilivyojaa asali na siagi. Aliyoyataabikia kazi atayarudisha, asiyameze; Kwa mali aliyoyapata, hatafurahi. Kwa maana amewaonea na kuwaacha maskini; Amenyang'anya nyumba kwa jeuri, wala hataijenga. Kwa sababu hakujua utulivu ndani yake, Hataokoa chochote kutoka hicho alichokifurahia. Hakikusalia kitu asichokula; Kwa hiyo kufanikiwa kwake hakutadumu. Katika kujaa kwa wingi wake atakuwa katika dhiki; Mkono wa kila anayesumbuliwa utamjia. Hapo atakapo kulijaza tumbo lake, Mungu atamtupia ukali wa ghadhabu zake, Na kuunyesha juu yake akiwa anakula. Ataikimbia silaha ya chuma, Na uta wa shaba utamchoma. Yeye autoa, nao watoka mwilini mwake; Naam, ncha ing'aayo yatoka katika nyongo yake; Vitisho viko juu yake. Giza lote linawekwa kwa ajili ya hazina zake; Moto ambao haukuvuviwa na mtu utamla; Utayateketeza yaliyosalia hemani mwake. Mbingu zitafunua wazi uovu wake, Nayo nchi itainuka kinyume chake. Mali ya nyumba yake yatanyakuliwa, Yatamwagika mbali katika siku ya ghadhabu zake. Hii ndiyo sehemu ya mtu mwovu itokayo kwa Mungu, Na urithi aliowekewa na Mungu.

Shirikisha
Soma Yobu 20

Yobu 20:1-29 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Ndipo Sofari, Mnaamathi, akajibu, na kusema, Kwa hiyo mawazo yangu hunipa jawabu, Kwa ajili ya haraka niliyo nayo ndani yangu. Nimesikia maonyo yanayonitahayarisha, Nayo roho ya ufahamu wangu hunijibu. Je! Hujui neno hili tangu zamani za kale, Tangu wanadamu kuwekwa juu ya nchi, Ya kuwa shangwe ya waovu ni kwa muda kidogo, Na furaha ya wapotovu ni ya dakika moja tu? Ujapopanda ukuu wake mpaka mbinguni, Na kichwa chake kufikilia mawinguni; Hata hivyo ataangamia milele kama mavi yake mwenyewe; Hao waliomwona watasema, Yuko wapi? Ataruka mfano wa ndoto, asionekane; Naam, atafukuzwa kama maono ya usiku, Jicho lililomwona halitamwona tena; Wala mahali pake hapatamtazama tena. Watoto wake watataka fadhili kwa maskini, Na mikono yake itarudisha mali yake. Mifupa yake imejaa ujana wake, Lakini utalala nchi naye mavumbini. Ingawa uovu una tamu kinywani mwake, Ingawa auficha chini ya ulimi wake; Ingawa auhurumia, asikubali kuuacha uende zake. Lakini akaushika vivyo kinywani mwake; Hata hivyo chakula chake matumboni mwake kinabadilika, Kimekuwa ni nyongo za majoka ndani yake. Amemeza mali, naye atayatapika tena; Mungu atayatoa tumboni mwake. Ataamwa sumu ya majoka; Na ulimi wa fira utamwua. Hataiangalia hiyo mito ya maji, Vile vijito vilivyojaa asali na siagi. Aliyoyataabikia kazi atayarudisha, asiyameze; Kwa mali aliyoyapata, hatafurahi. Kwa maana amewaonea na kuwaacha maskini; Amenyang’anya nyumba kwa jeuri, wala hataijenga. Kwa sababu hakujua utulivu ndani yake, Hataponya cho chote katika hicho alichokifurahia. Hakikusalia kitu asichokula; Kwa hiyo kufanikiwa kwake hakutadumu. Katika kujaa kwa wingi wake atakuwa katika dhiki; Mkono wa kila anayesumbuliwa utamjia. Hapo atakapo kulijaza tumbo lake, Mungu atamtupia ukali wa ghadhabu zake, Na kuunyesha juu yake akiwa anakula. Ataikimbia silaha ya chuma, Na uta wa shaba utamchoma kwa pili. Yeye autoa, nao watoka mwilini mwake; Naam, ncha ing’aayo yatoka katika nyongo yake; Vitisho viko juu yake. Giza lote linawekwa kwa ajili ya hazina zake; Moto ambao haukuvuviwa na mtu utamla; Utayateketeza yaliyosalia hemani mwake. Mbingu zitafunua wazi uovu wake, Nayo nchi itainuka kinyume chake. Maongeo ya nyumba yake yataondoka, Yatamwagika mbali katika siku ya ghadhabu zake. Hii ndiyo sehemu ya mtu mwovu itokayo kwa Mungu, Na urithi aliowekewa na Mungu.

Shirikisha
Soma Yobu 20

Yobu 20:1-29 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)

Ndipo Sofari Mnaamathi akajibu: “Mawazo yanayonisumbua yananisukuma kujibu, kwa sababu nimehangaika sana. Ninasikia makaripio ambayo yananivunjia heshima, nao ufahamu wangu unanisukuma kujibu. “Hakika unajua jinsi ilivyokuwa tangu zamani, tangu zamani mwanadamu alipowekwa duniani, macheko ya mtu mwovu ni ya muda mfupi, nayo furaha ya wasiomcha Mungu hudumu kwa kitambo tu. Ingawa kujikweza kwake hufikia mbinguni na kichwa chake hugusa mawingu, ataangamia milele kama mavi yake mwenyewe. Wale waliomwona watauliza, ‘Yuko wapi?’ Kama ndoto hutoweka, wala hapatikani tena, amefukuziwa mbali kama maono ya usiku. Jicho lililomwona halitamwona tena; mahali pake hapatamwona tena. Watoto wake watalipa yote baba yao aliyowadhulumu maskini, nayo mikono yake itarudisha mali yote aliyonyangʼanya watu. Nguvu za ujana zilizoijaza mifupa yake, zitalala naye mavumbini. “Ingawa uovu ni mtamu kinywani mwake naye huuficha chini ya ulimi wake, ingawa hawezi kukubali kuuachia uende, lakini huuweka kinywani mwake. Hata hivyo chakula chake kitakuwa kichungu tumboni mwake, nacho kitakuwa sumu kali ya nyoka ndani yake. Atatema mali alizozimeza; Mungu atalifanya tumbo lake kuzitapika. Atanyonya sumu za majoka; meno ya nyoka mwenye sumu kali yatamuua. Hatafurahia vijito, mito inayotiririsha asali na siagi. Vile alivyovitaabikia atavirudisha bila kuvila; hatafurahia faida itokanayo na biashara yake. Kwa kuwa aliwadhulumu maskini na kuwaacha bila kitu; amenyangʼanya kwa nguvu nyumba asizozijenga. “Hakika hatakuwa na amani katika kutamani kwake; hawezi kujiokoa mwenyewe kwa hazina zake. Hakuna chochote kitakachosalia kwa ajili yake ili ale; kufanikiwa kwake hakutadumu. Katikati ya wingi wa ustawi wake, dhiki itampata; taabu itamjia kwa nguvu zote. Atakapokuwa amelijaza tumbo lake, Mungu ataionesha ghadhabu kali dhidi yake, na kumnyeshea mapigo juu yake. Ijapokuwa aikimbia silaha ya chuma, mshale wa shaba utamchoma. Atauchomoa katika mgongo wake, ncha inayongʼaa kutoka ini lake. Vitisho vitakuja juu yake; giza nene linavizia hazina zake. Moto usiopepewa na mtu utamteketeza, na kuangamiza yaliyosalia nyumbani mwake. Mbingu zitaweka wazi hatia yake, nayo nchi itainuka kinyume chake. Mafuriko yataichukua nyumba yake, maji yaendayo kasi katika siku ya ghadhabu ya Mungu. Hili ndilo fungu Mungu alilowagawia waovu, urithi uliowekwa kwa ajili yao na Mungu.”

Shirikisha
Soma Yobu 20