Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Yobu 2:1-13

Yobu 2:1-13 Biblia Habari Njema (BHN)

Ikatokea tena siku nyingine, malaika wa Mungu walikwenda kukutana mbele ya Mwenyezi-Mungu, naye Shetani akajitokeza pia pamoja nao. Mwenyezi-Mungu akamwuliza Shetani, “Umetoka wapi wewe?” Naye Shetani akamjibu Mwenyezi-Mungu, “Nimetoka kutembeatembea na kuzungukazunguka duniani.” Mwenyezi-Mungu akamwambia Shetani, “Je, umemwangalia mtumishi wangu Yobu? Duniani hakuna mwingine aliye kama yeye. Yeye ni mtu mnyofu, mcha Mungu na mwenye kujiepusha na uovu. Yeye yuko imara katika unyofu wake, ingawa wewe umenichochea nimwangamize bure.” Shetani akamjibu Mwenyezi-Mungu, “Ngozi kwa ngozi! Mtu hutoa kila kitu alicho nacho ili aokoe uhai wake. Lakini sasa hebu nyosha mkono wako umguse mwili wake; nakuambia atakutukana waziwazi.” Basi, Mwenyezi-Mungu akamwambia Shetani, “Haya! Waweza kumfanya utakavyo, walakini usimuue.” Hapo Shetani akaondoka mbele ya Mwenyezi-Mungu, akamtesa Yobu kwa madonda mabaya tangu wayo wa mguu wake mpaka utosini mwake. Yobu akatwaa kigae, akajikuna nacho na kuketi kwenye majivu. Mkewe akamwambia, “Bado tu ungali ukishikilia unyofu wako? Mtukane Mungu, ufe.” Yobu akamjibu mkewe, “Wewe unaongea kama wanawake wapumbavu. Tukipokea mema kutoka kwa Mungu, kwa nini tukatae kupokea pia mabaya kutoka kwake?” Katika mambo hayo yote, Yobu hakutamka neno lolote la kumkosea Mungu. Marafiki watatu wa Yobu: Elifazi kutoka Temani, Bildadi kutoka Shua na Sofari kutoka Naamathi, walisikia juu ya maafa yote yaliyompata Yobu. Basi, wakaamua kwa pamoja waende kumpa pole na kumfariji. Walipomwona kwa mbali hawakumtambua. Basi, wakaanza kupaza sauti na kulia; waliyararua mavazi yao, wakarusha mavumbi angani na juu ya vichwa vyao. Kisha wakaketi udongoni pamoja na Yobu kwa siku saba, mchana na usiku, bila kumwambia neno lolote kwani waliyaona mateso yake kuwa makubwa mno.

Shirikisha
Soma Yobu 2

Yobu 2:1-13 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Tena ilitukia siku moja hao wana wa Mungu walipokwenda kujiweka mbele za BWANA, Shetani naye akaenda kati yao, ili kujiweka mbele za BWANA. BWANA akamwuliza Shetani, Umetoka wapi? Shetani akamjibu BWANA, na kusema, Natoka katika kuzungukazunguka duniani, na katika kutembea huku na huku humo. BWANA akamwuliza Shetani, Je! Umemwangalia huyo mtumishi wangu Ayubu? Kwa kuwa hakuna hata mmoja aliye kama yeye duniani, mtu mkamilifu na mwelekevu, mwenye kumcha Mungu na kuepukana na uovu; naye hata sasa anashikamana na utimilifu wake, ijapokuwa ulinichochea juu yake, ili nimwangamize pasipokuwa na sababu. Shetani akamjibu BWANA, na kusema, Ngozi kwa ngozi, naam, yote aliyo nayo mtu atayatoa kwa ajili ya uhai wake. Lakini sasa nyosha mkono wako, uuguse mfupa wake na nyama yake, naye atakukufuru mbele za uso wako. BWANA akamwambia Shetani, Tazama, yeye yumo mkononi mwako; lakini tunza tu uhai wake. Basi Shetani akatoka mbele za uso wa BWANA, akampiga Ayubu na majipu mabaya tangu wayo wa mguu hadi utosi wa kichwa. Naye akashika kigae cha kujikunia; akaketi majivuni. Ndipo mkewe akamwambia, Je! Wewe hata sasa washikamana na utimilifu wako? Mkufuru Mungu, ufe. Lakini yeye akamwambia, Wewe wanena kama mmoja wa hao wanawake wapumbavu anenavyo. Je! Tupate mema mkononi mwa Mungu, nasi tusipate na mabaya? Katika mambo hayo yote Ayubu hakufanya dhambi kwa midomo yake. Basi ikawa hao marafiki watatu wa Ayubu walipopata habari ya mabaya hayo yote yaliyomfikia, wakaja kila mtu kutoka mahali pake; nao ni Elifazi Mtemani, na Bildadi Mshuhi, na Sofari Mnaamathi; wakapatana pamoja ili waende kumfariji Ayubu na kumtuliza moyo. Basi walipoinua macho yao, wakiwa bado kwa mbali, wasimtambue, wakainua sauti zao na kulia; kila mmoja akararua joho lake, wakarusha mavumbi juu ya vichwa vyao kuelekea mbinguni. Kisha wakaketi ardhini pamoja naye muda wa siku saba, mchana na usiku, wala hapana mmoja aliyenena naye neno lolote; kwa maana waliona ya kuwa mashaka yake aliyo nayo ni makuu mno.

Shirikisha
Soma Yobu 2

Yobu 2:1-13 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Tena kulikuwa na siku hao wana wa Mungu walipokwenda kujihudhurisha mbele za BWANA, Shetani naye akaenda kati yao, ili kujihudhurisha mbele za BWANA. BWANA akamwuliza Shetani, Umetoka wapi? Shetani akamjibu BWANA, na kusema, Natoka katika kuzunguka-zunguka duniani, na katika kutembea huku na huku humo. BWANA akamwuliza Shetani, Je! Umemwangalia huyo mtumishi wangu Ayubu? Kwa kuwa hapana mmoja aliye kama yeye duniani, mtu mkamilifu na mwelekevu, mwenye kumcha Mungu na kuepukana na uovu; naye hata sasa anashikamana na utimilifu wake, ujapokuwa ulinichochea juu yake, ili nimwangamize pasipokuwa na sababu. Shetani akamjibu BWANA, na kusema, Ngozi kwa ngozi, naam, yote aliyo nayo mtu atayatoa kwa ajili ya uhai wake. Lakini sasa nyosha mkono wako, uuguse mfupa wake na nyama yake, naye atakukufuru mbele za uso wako. BWANA akamwambia Shetani, Tazama, yeye yumo mkononi mwako; lakini tunza tu uhai wake. Basi Shetani akatoka mbele za uso wa BWANA, akampiga Ayubu na majipu mabaya tangu wayo wa mguu hata utosi wa kichwa. Naye akashika kigae cha kujikunia; akaketi majivuni. Ndipo mkewe akamwambia, Je! Wewe hata sasa washikamana na utimilifu wako? Umkufuru Mungu, ukafe. Lakini yeye akamwambia, Wewe wanena kama mmoja wa hao wanawake wapumbavu anenavyo. Je! Tupate mema mkononi mwa Mungu, nasi tusipate na mabaya? Katika mambo hayo yote Ayubu hakufanya dhambi kwa midomo yake. Basi ikawa hao rafikize Ayubu watatu walipopata habari ya mabaya hayo yote yaliyomfikilia, wakaja kila mtu kutoka mahali pake; nao ni Elifazi Mtemani, na Bildadi Mshuhi, na Sofari Mnaamathi; wakapatana pamoja ili waende kumlilia Ayubu na kumtuliza moyo. Basi walipovua macho yao, nao wakali mbali, wasimtambue, wakainua sauti zao na kulia; kila mmoja akararua joho yake, wakarusha mavumbi juu ya vichwa vyao kuelekea mbinguni. Kisha wakaketi nchi pamoja naye muda wa siku saba, mchana na usiku, wala hapana mmoja aliyenena naye neno lo lote; kwa maana waliona ya kuwa mashaka yake aliyo nayo ni makuu mno.

Shirikisha
Soma Yobu 2

Yobu 2:1-13 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)

Siku nyingine wana wa Mungu walienda kujionesha mbele za BWANA. Shetani naye akaja pamoja nao kujionesha mbele zake. BWANA akamwambia Shetani, “Umetoka wapi?” Shetani akamjibu BWANA, “Natoka kuzunguka duniani, nikitembea huku na huko.” BWANA akamwambia Shetani, “Je, umemwangalia huyo mtumishi wangu Ayubu? Hakuna mtu mwingine duniani aliye kama yeye, mtu asiye na hatia, ni mnyofu, mwenye kumcha Mungu na kuepukana na uovu. Naye bado anadumisha uadilifu wake, ingawa ulinichochea dhidi yake, ili nimwangamize pasipo sababu.” Shetani akamjibu BWANA, “Ngozi kwa ngozi! Mwanadamu atatoa vyote alivyo navyo kwa ajili ya uhai wake. Lakini nyoosha mkono wako na kuipiga nyama yake na mifupa yake, naye kwa hakika atakulaani mbele za uso wako.” BWANA akamwambia Shetani, “Vema sana; kwa hiyo, yeye yumo mikononi mwako, lakini lazima umwachie uhai wake.” Basi Shetani akatoka mbele za BWANA, naye akampiga Ayubu kwa majipu mabaya tangu nyayo za miguu yake hadi utosi wa kichwa. Ndipo Ayubu akachukua kigae na kujikuna nacho, huku akiketi kwenye majivu. Mke wake akamwambia, “Je, bado unashikamana na uadilifu wako? Mlaani Mungu nawe ukafe!” Akamjibu, “Unazungumza kama mwanamke mpumbavu. Je, tupokee mema kutoka kwa Mungu, bali tusipokee mabaya?” Katika mambo haya yote, Ayubu hakutenda dhambi katika kusema kwake. Basi rafiki watatu wa Ayubu, ndio Elifazi Mtemani, na Bildadi Mshuhi na Sofari Mnaamathi, waliposikia kuhusu taabu yote iliyompata Ayubu, wakajipanga kutoka nyumbani mwao, wakakutana ili kwenda kumtuliza katika taabu hiyo na kumfariji. Walipomwona kwa mbali, ilikuwa vigumu kumtambua. Wakaanza kulia kwa sauti kubwa, wakayararua majoho yao na kujirushia mavumbi juu ya vichwa vyao. Kisha wakaketi chini kwenye udongo pamoja na Ayubu kwa siku saba usiku na mchana. Hakuna yeyote aliyesema naye neno, kwa sababu waliona jinsi mateso yake yalivyokuwa makubwa.

Shirikisha
Soma Yobu 2